Kagera Sugar vs Simba, mchezo wa kisasi leo

Simba mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara, leo Jumamosi saa kumi kamili jioni watashuka kwenye uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera kuikabili Kagera Sugar katika mchezo muhimu kwa kila timu

Wakati Simba ikihitaji alama tatu kuendelea kusogea kileleni katika mpango wake wa kutetea ubingwa, Kagera Sugar iko katika hatari ya kuteremka daraja

Lakini pia, ukiachana na mazingira hayo, kwa misimu miwili iliyopita, Kagera Sugar ilihusika katika kuvuruga mipango ya Simba

Msimu wa 2016/17 Kagera Sugar iliisababishia Simba isitwae ubingwa baada ya kunyan’ganywa alama tatu ambazo walikuwa wamepewa awali na Bodi ya Ligi kufuatia Kagera Sugar kumchezesha mchezaji aliyekuwa na kadi tatu za njano katika mchezo ambao Kagera Sugar ilishinda 2-1

Tukio hilo lilisababisha uongozi wa Simba kupeleka malalamiko FIFA, malalamiko ambayo yalitupiliwa mbali

Aidha mwaka jana wakati Simba ikiwa tayari imetangaza ubingwa, Kagera Sugar ikatibua tena siku muhimu kwa mabingwa hao ambayo walikuwa wakikabidhiwa kombe na Rais Dk John Magufuli kwa kuwachapa bao 1-0 kwenye uwanja wa Taifa

Kagera Sugar ndiyo timu pekee iliyopata ushindi dhidi ya Simba msimu uliopita

Msimu huu Simba imejipambanua kwa kuwa na kikosi bora zaidi ikiwa imeshinda michezo yote 11 iliyopita kwenye ligi na kuweka rekodi mpya

Ushindi katika mchezo wa leo utakuwa wa 12

Kocha Patrick Aussems amesema vijana wake wako tayari kuelekea mchezo huo na wamedhamiria kuondoka na alama zote tatu kama walivyofanya katika michezo 11 iliyopita

Simba kusaka ushindi wa 12 mfululizo Bukoba

Msafara wa wachezaji 18 wa kikosi cha Simba unaondoka leo Ijumaa asubuhi kuelekea Kagera tayari kuwakabili wenyeji wao Kagera Sugar kwenye mchezo utakaopigwa uwanja wa Kaitaba kesho Jumamosi

Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu amesema wachezaji wengine wanne watasafiri kesho kuungana na wenzao wanaoondoka leo

Ni beki Paschal Wawa pekee ambaye hakujumishwa kwenye safari hiyo ya kanda ya ziwa kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya nyonga

Baada ya kushinda michezo yote 11 iliyopita na kuweka rekodi mpya kwenye ligi, Simba itakuwa inasaka ushindi wa 12 dhidi ya Kagera Sugar ambayo msimu uliopita ndio timu pekee iliyopata ushindi dhidi ya Simba

Kesho Simba itaingia dimba la Kaitaba ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa bao 1-0 kwenye mchezo ambao ulishuhudiwa na Rais Magufuli msimu uliopita

Ratiba haiwezi kutukosesha ubingwa – Aussems

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wamedhamiria kutetea ubingwa wa ligi kuu walioutwaa msimu uliopita hivyo wako tayari kukabiliana na ratiba ngumu ya viporo waliyopangiwa na Bodi ya Ligi

Baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 juzi dhidi ya Coastal Union, kesho Jumamosi Simba itashuka tena uwanjani kumenyana na Kagera Sugar katika mchezo utakaopigwa dimba la Kaitaba mkoani Kagera

Simba imewasili Bukoba mapema leo tayari kwa mchezo huo

Aussems amekosoa mpangilio wa ratiba ikiwemo kupangiwa kucheza saa nane mchana. Hata hivyo amesisitiza kuwa kikosi chake kiko tayari hata wakipangiwa kucheza saa nne asubuhi

“Tumetoka katika kibarua kigumu cha michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tumekuja kwenye kazi ngumu ya kutetea ubingwa wetu. Tutakabiliana na ratiba tuliyopangiwa hata tukitakiwa kucheza saa nne asubuhi” amesema

“Kuchukua ubingwa si jambo la kuzungumza kwa mdomo, bali linahitaji matendo yenye uthubutu, ikiwa ni pamoja na mipango yake ndani ya kikosi”

Simba inakabiliwa kucheza michezo minne kanda ya ziwa dhidi ya Kagera Sugar, KMC, Alliance Fc na Biashara United kabla ya kuelekea mkoani Mbeya kuzikabili Tanzania Prisons na Mbeya City

HAJI MANARA vs ZAHERA

MICHEZO || Afisa Habari wa klabu ya Simba Sc Haji Manara alitaka shirikisho la soka nchini Tanzania TFF kumchukulia hatua kocha Mkuu wa klabu ya Yanga Sc Mwinyi Zahera kwa makosa ya kuituhumu Simba Sc na TFF kuwa wanaihujumu klabu yake ya Yanga Sc kwa kuiibia point zao la Ligi kuu Tanzania bara bila kutaja kuwa hizo point wanaiba vipi.

Marefa wa Tanzania watoswa AFCON 2019

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetoa orodha ya marefa 27 na marefa wasaidizi 29 kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu nchini Misri, lakini hakuna Mtanzania hata mmoja.

Waamuzi hao wameteuliwa kushiriki kozi maalum kuanzia Aprili 28 hadi Mei 5 mwaka huu mjini Rabat, Morocco kunolewa kwa ajili ya Fainali za Misri mwezi Juni.

Marefa hao wanatoka nchi 33 na wataingia kwenye kambi maalum ya mafunzo itakayosaidia uteuzi wa orodha ya mwisho ya marefa watakaochezesha fainali za mwaka huu zitakazoanza Juni 21 hadi Julai 19 katika miji ya Alexandria, Cairo, Ismailia na Suez

Bodi ya ligi yatahadharishwa mechi za saa nane

Mtaalamu wa misuli ya mwili wa binadamu Dk Kitambi Mganga ameishauri Bodi ya ligi kuu kuwa makini na utaratibu wa kupanga michezo ya ligi kuu saa nane mchana wakati wa jua kali

Dk Mganga amesema kitaalam, muda huo sio mzuri kwani unaweza ukasababisha madhara makubwa kwa wachezaji yakiwemo matukio ya vifo

“Wachezaji wanapocheza wakati wa jua kali wanakuwa katika hali ya kukausha maji mwilini kwa haraka na hivyo kuwepo na hatari ya kupatwa na shambulio la moyo au kuziba moyo na misuli kukakamaa,” amesema

“Shambulio la moyo linatokana na mwili kulazimishwa kufanya kazi ngumu wakati wa jua kali, moyo unaziba, ulimi unatoka nje, misuri inashindwa kufanya kazi ni hatari kubwa mchezaji anaweza kupoteza maisha uwanjani kama hakutakuwa na mtaalamu mwenye kujua atoe huduma gani”

Dk Mganga ambaye ni Daktari wa Coastal Union, amesema kama kuna ulazima wa kuchezesha mechi hizo katika muda huo basi mwamuzi anaweza kutenga hata dakika moja ya kuwapa nafasi wachezaji kunywa maji utaratibu ambao hutumika kote duniani ambapo mchezo husimamishwa kwenye dakika ya 25-30 kuwapa nafasi wachezaji kunywa maji

Msimu huu baadhi ya michezo ya ligi kuu imekuwa ikipigwa saa nane mchana ili kutoa nafasi kwa michezo mingi kuonyeshwa ‘mbashara’ na Azam TV

Michezo ya ligi iliyopigwa jana ambayo ilihusisha Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga na Coastal Union dhidi ya Simba, ilipigwa saa nane mchana ili kuepusha muingiliano wa ratiba na michuano ya AFCON U17 inayoendelea jijini Dar es salaam