Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba leo wanarejea ‘mzigoni’ kwa kuikabili Coastal Union katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Mkwakwani, saa nane mchana
Simba iko mkoani Tanga tangu juzi ambapo jana jioni ilifanya mazoezi ya mwisho Mkwakwani kuelekea mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu
Baada ya kuondoshwa katika hatua ya robo fainali michuano ya ligi ya mabingwa, Simba imejizatiti kutetea ubingwa iliyotwaa msimu uliopita ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya hiyo msimu ujao
Ikiwa imeshuka dimbani mara 22 na kuvuna alama 57, ushindi katika mchezo wa leo utaifanya Simba ifikishe alama 60 na kuendelea kuzifukuzia Azam Fc (66) na Yanga (74) ambazo hata hivyo zimecheza michezo tisa zaidi
Kocha Patrick Aussems amesema wachezaji wake wanafahamu umuhimu wa mchezo wa leo na baada ya kupoteza mchezo dhidi ya TP Mazembe, leo watakuwa na nafasi ya kufuta makosa waliyofanya kwenye mchezo huo kwa kuibuka na ushindi mnono
Mchezo utapigwa saa nane mchana ili kuwapa nafasi mashabiki kushuhudia mchezo wa michuano ya AFCON U17 kati ya Tanzania dhidi ya Uganda ambao utaanza saa kumi kamili jioni