OKWI : Atoa neno kuelekea Mechi SIMBA vs AS VITA

Mshambuliaji hatari wa Simba Emmanuel Okwi amewaita mashabiki uwanja wa Taifa kuiunga mkono Simba itakapokuwa ikichuana na Vita Club katika mchezo utakaopigwa saa moja jioni baadae leo Jumamosi

“Tunawaomba mashabiki wetu mje kwa wingi uwanjani ili kutuunga mkono.

“Siku zote tumekuwa pamoja na sapoti yenu imekuwa msaada mkubwa kwetu katika michezo iliyopita,” amesema Okwi

“Tunataka tufanye hii siku pamoja. Tunaomba mje tupambane pamoja ili tukifuzu iwe tumefuzu wote pamoja”

“Njooni uwanjani tuandike historia wote. Tumejiandaa vya kutosha na tuko tayari kuipeleka Simba hatua ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa”

Manara amtahadharisha Zahera

Afisa Habari wa Simba Haji Manara amesema wamebaini kocha wa Yanga Mwinyi Zahera hajasafiri na timu yake ambayo kesho inamchezo dhidi ya Lipuli Fc akibaki jijini Dar es salaam kuipokea AS Vita Club

Zahera ameonekana akiambatana na viongozi wa timu ya Vita Club itakayochuana na Simba hapo kesho

“Hii ni mechi ya kitaifa na ya kimataifa, tunaiwakilisha nchi, kuna kocha yeye kazi yake imekuwa ni kuzunguka na Vita tu na aliaga anaenda kwao Congo hata Iringa hajaenda.

“Hii ni mechi ambayo nchi inajua, Rais anajua, sasa ole wake aendelee kutuharibia mipango,” amesema Manara kwenye mahojiano yake na eFM radio

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Manara amesema kikosi kiko tayari, ari na morali ya wachezaji iko juu kuelekea mchezo huo

Amewataka mashabiki kuwahi mapema uwanja wa Taifa hapo kesho ili wawe sehemu ya historia ambayo Simba imepania kuiandika

Aussems ataja sababu ya Juuko kuikosa AS Vita

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema beki wa Kimataifa wa Uganda Juuko Murshidi hatakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kitakachoikabili AS Vita Club kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa utakaopigwa katika dimba la Taifa kesho.

Aussems amesema Juuko alipata majeraha na atahitaji kupumzika zaidi ili aweze kuwa sawa kabla ya kuanza kumtumia

“Juuko alipata majeraha, anahitaji kupumzika mpaka Jumatatu. Hivyo hakuna uwezekano wa kumtumia katika mchezo huo wa kesho,” amesema Aussems

Hata hivyo Aussems amethibitisha kuwa kiraka Erasto Nyoni yuko fit kuelekea mchezo huo

“Nyoni alianza mazoezi wiki iliyopita. Hatukusafiri nae kwenda Algeria ili kumpa muda zaidi wa kufanya mazoezi ili aweze kuwa fit”

“Tumefanya nae mazoezi siku hizi mbili, bila shaka atakuwepo Jumamosi”

Nyoni na Okwi walijiunga katika mazoezi ya kikosi cha Simba juzi ambapo wanatarajiwa kujumuishwa katika kikosi kitakachoikabili AS Vita

Kiungo Jonas Mkude ataukosa mchezo huo akitumikia adhabu ya kadi mbili za njano

Aussems afunguka utayari wa kikosi cha Simba kuelekea mchezo wa kesho

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema vijana wake wako tayari kuwakabili AS Vita Club na hawana wasiwasi wowote kuelekea mchezo huo

Jana jioni Simba ilijifua katika uwanja wa Taifa yakiwa ni maandalizi yake ya mwisho katika uwanja huo kabla ya mchezo hapo kesho

Aussems amesema licha ya kuwa tayari wamefikia malengo ya msimu huu ya kutinga hatua ya makundi, lakini wana nafasi adimu ya kutinga robo fainali kama watashinda mchezo huo utakaopigwa mbele ya mashabiki wake takribani elfu 60

“Mimi nipo sawa na hata wachezaji wangu wapo vizuri, ni mechi yenye msisimko sana tunajua tukishinda tutaingia robo fainali na tumesubiri jambo hili kwa miezi 7 sasa,” amesema

“Hata kama matarajio hayakuwa makubwa sisi kufika mbali kwenye ligi ya mabingwa Afrika, lakini bado tuna nafasi kwa hiyo hatuna presha, zaidi presha ipo kwao (AS Vita) kwa sababu ni wanafainali wa kombe la shirikisho mwaka jana na kama hawatafuzu itakuwa jambo baya sana kwao.”

“Hatupo katika hali inayofanana, chochote kitakachotokea ni ziafa kwetu, tuna nafasi adimu ya kucheza mchezo huu muhimu mbele ya mashabiki 60,000 kwa hiyo itakuwa mechi nzuri na wachezaji wapo tayari.”

Mchezo huo utapigwa saa moja usiku sambamba na mchezo kati Al Ahly dhidi ya JS Saoura

Nyoni awaita mashabiki uwanja wa Taifa

Kiraka Erasto Nyoni amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa keshokutwa katika mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya AS Vita Club

Nyoni aliyerejea kikamilifu baada ya kupona majeraha, amesema upande wao wachezaji wanajifua kikamilifu ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo

“Mchezo huu ni fainali kwetu, tunahitaji kushinda ili tuweze kutinga robo fainali. Mawazo yetu yote yako katika mchezo huo,” amesema

“Tunahitaji sana sapoti ya mashabiki wetu. Tunajua wakija kwa wingi wataongeza hamasa kwetu na kutuongezea ari ya kupambana”

Kikosi cha Simba chini ya kocha Patrick Aussems na Msaidizi wake Denis Kitambi leo kimejifua kwenye uwanja wa Taifa ikiwa ni maandalizi yake ya mwisho kwenye uwanja huo kabla ya mchezo keshokutwa

Wapinzani wao AS Vital Club waliwasili jijini Dar es salaam jana ambapo leo wamefanya mazoezi katika viwanja vya Ghymkhana

Timu hiyo itajifua kwenye uwanja wa Taifa kesho

Kamati ya saidia Stars ishinde yakutana Dar

Hivi karibuni Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liliunda Kamati maalum ya kusaidia Taifa Stars ishinde mchezo dhidi ya Uganda utakaopigwa March 24 ili iweze kutinga fainali za AFCON zitakazofanyika nchini Misri baadae mwaka huu

Kamati hiyo inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh Paul Makonda leo ilikutana katika kikao chake cha pili kilichofanyika Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam

Kamati hiyo ina wajumbe 14.

Djuma aitakia kheri Simba

Kocha Mkuu wa AS Kigali inayoshiriki ligi kuu ya Rwanda, Masudi Djuma ameitakia kheri Simba ili iweze kushinda mchezo dhidi ya AS Vita Club na kuweza kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika

Djuma aliyewahi kuhudumu Simba akiwa kocha msaidizi kwa misimu miwili, amesema Simba itakayokuwa nyumbani ina kila sababu ya kushinda mchezo huo Jumamosi

“Timu zinazoshiriki michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu zimetumia vyema viwanja vyao vya nyumbani. Naamini Simba itatumia uwanja wake vizuri pia,” Djuma aliiambia Radio eFM

Djuma aliondolewa Simba mwezi Oktoba mwaka jana baada ya kutofautiana na kocha Mkuu Patrick Aussems.

Nafasi yake tayari imechukuliwa na kocha Denis Kitambi

Djuma anabaki kuwa miongoni mwa makocha waliopita Simba na kukubalika sana na mashabiki wa timu hiyo

Aussems amewapania kwelikweli AS Vita

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wanayo kila sababu ya kushinda mchezo wa keshokutwa dhidi ya AS Vita utakaopigwa saa moja usiku katika uwanja wa Taifa

Aussems ambaye msimu huu ameiongoza Simba kwa mafanikio makubwa kwa kuweza kuipeleka hatua ya makundi, amedhamiria kuvuka malengo kwa kutinga robo fainali

“Mchezo huu muhimu kuchezwa katika uwanja wetu wa nyumbani mbele ya mashabiki wetu, inatuongezea kujiamini.

“Tuko katika nafasi nzuri zaidi ya kupata ushindi kuliko wapinzani wetu,” amesema Aussems

“Nafahamu mchezo hautakuwa mwepesi kwani wapinzani wetu nao wanahitaji ushindi ili wafuzu”

“Lakini sisi tuna faida ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa mashabiki wetu. Ni muhimu mashabiki wakajitokeza kwa wingi uwanjani, wajaze uwanja na watuunge mkono kwa muda wote wa mchezo, ushindi utakuwa upande wetu”

Mshindi wa mchezo kati ya Simba dhidi ya AS Vita atajihakikishia kutinga hatua ya robo fainali na timu itakayoshinda kwenye mchezo kati ya Al Ahly dhidi ya JS Saoura unaopigwa Misri

Matokeo ya sare yatazipa nafasi JS Saoura na Al Ahly kutinga robo fainali

Niko fiti kuwakabili AS Vita – Wawa

Beki kisiki wa Simba Paschal Serge Wawa amesema yuko imara kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya AS Vital utakaopigwa keshokutwa Jumamosi kwenye uwanja wa Taifa

Wawa alipata majeraha ya kifundo cha mguu kwenye mchezo uliopita dhidi ya JS Saoura ambapo Daktari wa Simba Yassin Gembe alisema beki huyo raia wa Ivory Coast pamoja na kiungo Haruna Niyonzima walipata majeraha ya enka kutokana na mazingira ya uwanja wa Agosti 20 ambao una nyasi bandia

Wawa amesema hali yako imeimarika na atacheza mchezo wa Jumamosi

“Niko vizuri sasa, niliumia katika mechi iliyopita kule Algeria, lakini sasa ninaendelea vizuri na nitacheza mechi ya Jumamosi,” amesema

“Naamini tutafanya vizuri kwenye mchezo huo, tutapambana kwa sababu tunataka kuwafurahisha mashabiki wetu na vilevile tunataka kuweka rekodi ya kutinga robo fainali”

Wawa alishiriki mazoezi ya Simba yliyofanyika kwenye uwanja wa Boko Veterans jana jioni