SIMBA : Kuelekea Shinyanga Leo

Mshambuliaji wa Simba Emmanuel Okwi alipata majeraha kwenye mchezo dhidi ya Lipuli Fc na kulazimika kurejea jijini Dar es salaam kwa ajili ya matibabu zaidi

Hata hivyo Okwi bado anaweza kuungana na kikosi cha Simba kwa ajili ya mchezo dhidi ya Stand United utakaopigwa keshokutwa katika uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga

Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amesema hatma yake itategemea na ripoti ya Daktari wa timu hiyo Dk Yassin Gembe

Wakati huo huo Simba inaondoka mkoani Singida leo kuelekea Shinyanga tayari kwa mchezo dhidi ya Stand United utakaopigwa Jumapili

FT : Lipuli Fc 1-3 Simba

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba leo wamewaadhibu vikali Lipuli Fc katika uwanja wao wa nyumbani kwa kuwafumua mabao 3-1 kwenye mchezo wa ligi kuu uliopigwa dimba la Samora

Baada ya Lipuli Fc kunusurika katika michezo mitatu iliyopita, leo Simba imepata matokeo stahili baada ya kuwabana vilivyo vijana hao wa Selemani Matola ambaye kabla ya mchezo alitamba kuwa hataki sare

Clatous Chama aliitanguliza Simba mapema tu kwenye dakika ya tano kwa kufunga bao safi kabla Lipuli Fc hawajasawazisha kupitia kwa Paul Nonga kwenye dakika ya 18

Chama tena akaongeza la pili dakika chache kabla ya kwenda mapumziko na Meddie Kagere aliye katika kiwango bora kabisa cha kupachika mabao , akafunga bao la tatu kwenye dakika ya 58

Ushindi huo umeendelea kuisogeza Simba kileleni baada ya kufikisha alama 48, sasa ikiwa nyuma ya Azam Fc kwa tofauti ya alama mbili

Kituo kinachofuata ni Shinyanga ambapo Jumapili, March 03 Simba itachuana na Stand United katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Kambarage

FT : Azam Fc 1-3 Simba

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba wameendeleza wimbi la ushindi kwenye ligi hiyo baada ya leo kuifumua Azam Fc mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa dimba la Taifa

Mapema tu katika dakika ya nne, Meddie Kagere aliifungia Simba bao la kuongoza akimalizia mpira uliokuwa umegonga mwamba ambao ulipigwa na John Bocco

Muda mfupi uliopita, Razak Abarora, mlinda lango wa Azam Fc alinusurika kuokata mpira kimiani baada ya shuti la Clatous Chama kumponyoka mikononi na kuuokota mpira huo katika mstari wakati ukielekea nyavuni

Bocco aliiongezea Simba bao la pili kwenye dakika ya 38 akimalizia kwa kichwa krosi murua ya Zana Coulibaly

Zana ameendelea kun’gara katika kikosi cha Simba, baada ya kuanza kwa kusuasua, sasa uwezo wake unadhihiri

Simba ilikwenda mapumziko ikiongoza kwa mabao 2-0

Katika kipindi cha pili Simba ilipunguza kasi na kuwapa nafasi Azam Fc kutawala mchezo huku vijana wa Aussems wakitumia mashambulizi ya kushitukiza

Kagere aliiongezea Simba bao la tatu kwenye dakika ya 78 akiachia shuti akiwa ndani ya 18

Hilo lilikuwa bao la 11 kwa Kagere sasa akiwa nyuma kwa bao moja dhidi ya vinara wa mabao kwenye ligi Salim Aiyee na Heritier Makambo wenye mabao 12

Bao la kufutia machozi kwa upande wa Azam Fc lilifungwa na Frank Domayo kwenye dakika ya 81

Ushindi huo umeifanya Simba ifikishe alama 45, alama tano nyuma ya Azam Fc inayoshika nafasi ya pili ikiwa na alama 50

Hata hivyo Simba ina michezo saba ya viporo

Mchezo unaofuta ni dhidi ya Lipuli Fc utakaopigwa Jumanne ijayo, Februari 26 mkoani Iringa

FT : African Lyon 0-3 Simba

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara, Simba wameendeleza moto wao wa ushindi leo wakiwafumua African Lyon mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa dimba la Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha

Nahodha John Bocco alifunga mabao mawili kwenye mchezo huo huku Adam Salamba naye akifunga bao muhimu ambalo bila shaka litamuongezea kujiamini

Bocco amefikisha mabao sita akiendelea kusogea juu katika kinyan’ganyiro cha kuwania kiatu cha dhahabu

Katika mchezo wa leo kocha Patrick Aussems alifanya mabadiliko ya kikosi chake kwa kuwapumzisha baadhi ya wachezaji huku washambuliaji Emmanuel Okwi na Meddie Kagere wakikosa mchezo huo wakitumikia adhabu ya kadi tatu za njano

Simba imeendelea ikisogea kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha alama 42 baada ya ushindi huo

Kikosi cha Simba kinatarajiwa kurejea jijini Dar es salaam kesho kujiandaa na mchezo unaofuata dhidi ya Azam Fc utakaopigwa Ijumaa, Februari 22 2019

FT : Yanga 0-1 Simba

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba wameendeleza ubabe wao dhidi ya Yanga baada ya kuondoka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo baina ya timu hizo uliopigwa leo uwanja wa Taifa

Ulikuwa ni mchezo ambao mzani ulielemea upande wa Simba hata kabla mchezo huo haujapigwa kutokana na ubora wa kikosi cha Simba

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa timu hizo kutofungana licha ya Simba kutawala kwa muda mwingi

Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Patrick Aussems kwa kumtoa Chama na kumuingiza Dilunga kwenye kipindi cha pili yaliongeza umakini kwa wekundu wa Msimbazi na Dilunga ndiye aliyesaidia kupatikana kwa bao la Simba

Bao hilo pekee lilifungwa na Meddie Kagere katika dakika ya 72 akimalizia pasi murua ya nahodha John Bocco

Hilo lilikuwa bao la tisa kwa Kagere kwenye ligi msimu huu

Ushindi huo umeiweka Simba katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wake dhidi ya wapinzani wao Yanga

Imefikisha alama 39 na kuchupa mpaka nafasi ya tatu.

Kama Simba itashinda michezo yake yote ya viporo itakuwa na uhakika wa kuwazidi alama tano wapinzani wao Yanga.

FT : Al Ahly 5-0 Simba

Simba imepoteza mchezo wa pili wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika baada ya kukubali kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa Al Ahly katika mchezo wa mzunguuko wa tatu, kundi D

Al Ahly ilitumia dakika 40 kufunga mabao yake yote matano wakitumia makosa ya safu ya ulinzi ya Simba iliyokuwa ikijichanganya mara kwa mara

Ni mchezo ambao kiufundi ulimalizika katika kipindi cha kwanza baada ya Al Ahly kufunga mabao hayo matano

Simba imeruhusu mabao 10 katika michezo miwili ya ligi ya mabingwa iliyopita

Kocha Patrick Aussems huenda akahitaji kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza hasa kwenye safu ya ulinzi ili kuweza kufanya vizuri katika michezo miwili ya nyumbani iliyobaki

Mchezo unaofuata utapigwa wiki ijayo katika dimba la Taifa dhidi ya Al Ahly

Licha ya kipigo hicho Simba imeendelea kusalia nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi D ikiwa na alama tatu

Al Ahly imejikita kileleni mwa kundi hilo baada ya kufikisha alama saba

Vita Club inashika nafasi ya pili ikiwa na alama nne baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 nyumbani dhidi ya JS Saoura katika mchezo mwingine wa kundi ambao ulipigwa mapema

JS Saoura inashika nafasi ya nne ikiwa na alama mbili