FT : Lipuli Fc 1-3 Simba

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba leo wamewaadhibu vikali Lipuli Fc katika uwanja wao wa nyumbani kwa kuwafumua mabao 3-1 kwenye mchezo wa ligi kuu uliopigwa dimba la Samora

Baada ya Lipuli Fc kunusurika katika michezo mitatu iliyopita, leo Simba imepata matokeo stahili baada ya kuwabana vilivyo vijana hao wa Selemani Matola ambaye kabla ya mchezo alitamba kuwa hataki sare

Clatous Chama aliitanguliza Simba mapema tu kwenye dakika ya tano kwa kufunga bao safi kabla Lipuli Fc hawajasawazisha kupitia kwa Paul Nonga kwenye dakika ya 18

Chama tena akaongeza la pili dakika chache kabla ya kwenda mapumziko na Meddie Kagere aliye katika kiwango bora kabisa cha kupachika mabao , akafunga bao la tatu kwenye dakika ya 58

Ushindi huo umeendelea kuisogeza Simba kileleni baada ya kufikisha alama 48, sasa ikiwa nyuma ya Azam Fc kwa tofauti ya alama mbili

Kituo kinachofuata ni Shinyanga ambapo Jumapili, March 03 Simba itachuana na Stand United katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Kambarage

FT : Simba yaitunga Mbao Fc 5-3 kwa matuta baada ya sare

Simba imefanikiwa kumaliza nafasi ya tatu kwenye michuano ya SportPesa Cup baada ya kupata ushindi wa penati 5-3 kufuatia matokeo ya 0-0 dhidi ya Mbao Fc katika mchezo uliopigwa uwanja Taifa

Simba iliutawala mchezo huo kwa muda mwingi ikikosa nafasi kadhaa huku mlinda lango wa Mbao Fc Metacha Mnata akiibuka nyota wa mchezo baada ya kuikoa timu yake na kipigo

Aidha, Haikuwa siku nzuri kwa mshambuliaji Sadney Urikhob aliye kwenye majaribio katika kikosi cha Simba kwani alikosa nafasi kadhaa za kufunga leo
Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wachezaji wake walicheza vizuri leo lakini walishindwa kufunga kutokana na kukosa umakini kwa washambuliaji wake huku akimsifia mlinda lango wa Mbao Fc Metacha kwa kuzuia michomo mingi iliyoelekezwa langoni kwake
Simba imejinyakulia kitita cha dola 7,500 baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu huku Mbao Fc ikipata dola 5,000

FT : Simba 1-2 Bandari

Simba imeaga michuano ya SportPesa Cup baada ya kulazwa mabao 2-1 na Bandari Fc kwenye mchezo wa nusu fainali uliopigwa uwanja wa Taifa

Simba ilitangulia kupata bao la kuongoza kwenye dakika ya 45 mfungaji akiwa Meddie Kagere aliyeachia shuti kali akiwa ndani na 18

Hata hivyo Bandari Fc ilirejea mchezoni kwenye kipindi cha pili ikisawazisha kupitia mkwaju wa penati kwenye dakika ya 59 baada ya Mzamiru Yassin kumfanyia madhambi Abdallah Khamis ndani ya eneo la hatari

Mzamiru alilazimika kukimbizwa Hospitalini kwa matibabu zaidi baada ya kuumia kwenye tukio hilo

Bandari Fc ilifunga bao la pili kwenye dakika ya 72 kupitia kwa Lugogo

Simba haikuwa kwenye kiwango bora leo, pengine muda wa saa nane uliopigwa mchezo huo haukuwa rafiki kwa wachezaji kutokana na joto la jijini Dar es salaam

Hata hivyo hiyo haiwezi kutumika kama sababu ya kufungwa kwa kuwa hata Bandari Fc ilicheza katika mzingira hayo hayo

Simba sasa itacheza kusaka nafasi ya tatu ikitarajiwa kuchuana na timu itakayopoteza kwenye mchezo wa pili wa nusu fainali kati ya Mbao Fc dhidi ya K Sharks

FT : Simba 2-1 AFC Leopards

Simba imetinga nusu fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup baada ya kuilaza AFC Leopards mabao 2-1 katika mchezo wa robo fainali uliopigwa uwanja wa Taifa leo

Mabao ya Simba yalipatikana katika kila kipindi yakifungwa na Emmanuel Okwi na Clatous Chama

Okwi aliifungia Simba bao la kuongoza kwenye dakika ya 13 akimalizia kwa ufundi kabisa krosi ya Zana Coulibaly

Licha ya AFC Leopards kumiliki mpira kwa muda mwingi lakini ni Simba iliyokuwa hatari zaidi kila ilipokuwa na mpira kwa kupeleka mashambulizi ya kasi langoni kwa Leopards

Okwi aliyekuwa mwiba mkali kwa safu ya ulinzi ya Leopards alisababisha bao la pili lililofungwa na Chama aliyemalizia krosi murua iliyomiminwa na mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Uganda

Leopards ilipata bao la kufutia machozi kwenye dakika ya 61 kupotia kwa Oburo

Katika mchezo huo kocha Patrick Aussems aliwapa nafasi Lamine Moro na mshambuliaji Hunlede Kisimbo walio kwenye majaribio ya kusajiliwa na mabingwa hao wa Tanzania Bara

Baada ya ushindi huo Simba imeungana na Mbao Fc, K. Sharks na Bandari kutinga hatua ya nusu fainali

Michezo ya nusu fainali itapigwa Ijumaa, Januari 25 2019

FT : Azam Fc 2-1 Simba

Azam Fc wamefanikiwa kutwaa taji la kombe la Mapinduzi kwa msimu wa tatu mfululizo baada ya kuichapa Simba mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliopigwa leo kisiwani Pemba.

Azam Fc ilionekana kuwa imara zaidi na ilitangulia kufunga bao la kuongoza kupitia kwa Mdathir Yahya kwenye dakika ya 44 kabla beki Yusufu Mlipili haijairudisha Simba mchezoni kwenye dakika ya 62

Obrey Chirwa ndiye aliyeifungia Azam Fc bao la ushindi kwenye dakika ya 72.

Azam Fc walidhamiria kufanya vizuri katika michuano hiyo wakati Simba imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na ushiriki wake wa michuano ya ligi ya mabingwa kwani haikuwa na wachezaji wake wa kikosi cha kwanza ambao jana waliichapa JS Saoura mabao 3-0

FT : Simba 3-0 JS Saoura

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba wameanza vyema michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika hatua ya makundi baada ya kuilaza JS Saoura mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa

Wakicheza kandanda safi na ya kuvutia vijana wa Aussems waliwapoteza kabisa Saoura waliojikuta muda mwingi wakiusaka mpira ‘kwa tochi’

Simba ilifanya mashambulizi mengi langoni kwa Saoura kwenye kipindi cha kwanza Mganda Emmanuel Okwi akikosa nafasi mbili mapema kabisa

Baada ya kosakosa nyingi, Okwi alisahihisha makosa yake na kuiandikia Simba bao la kuongoza mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa Clatous Chama, Okwi aliwahadaa walinzi wa Saoura kabla ya kuujaza mpira kimiani.

Mabadiliko yaliofanywa na Aussems kwenye dakika ya 35 kwa kumuingiza Meddie Kagere kuchukua nafasi ya Bocco aliyeumia, yalikuwa na faida kwa Simba kwani alikuwa ni Kagere aliyeiongezea Simba mabao mawili katika kipindi cha pili.

Kagere aliifungia Simba bao la pili kwenye dakika ya 52 akimalizia pasi murua ya Okwi aliyevunja mtego wa kuotea.

Katika dakika ya 62 Okwi tena akamuwekea Kagere pasi mpenyezo na bila ajizi Kagere akaweka bao la tatu kimiani.

Ushindi huo ni matokeo stahili kwa Simba kutokana na ubora walioonyesha katika mchezo wa leo.

Simba inaongoza kundi D ikiwa na alama tatu na mabao matatu. AS Vital na Al Ahly vitachuana leo katika mchezo mwingine wa kundi D

Wiki ijayo Simba itasafiri kwenda nchini Congo kuivaa AS Vital katika mchezo mwingine wa raundi ya pili

FT : KMKM 0-1 Simba

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba wameendeleza vipigo kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar baada ya kuilaza KMKM bao 1-0 katika mchezo uliopigwa dimba la Amaan leo Jumapili usiku.

Katika mchezo huo, licha ya kutawala kwa muda mwingi, Simba ililazimika kusubiri hadi dakika ya 84 kupata bao pekee la ushindi lililofungwa na Rashid Juma.

Ushindi huo umeifanya Simba ifikishe alama sita na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.

Nyoni aumia

Aidha, kwenye mchezo huo Simba ilipata pigo baada ya beki wake kiraka Erasto Nyoni kupata majeraha ya goti mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Uongozi wa Simba unatarajiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu majeraha ya mchezaji huyo tegemeo wa kikosi cha kwanza ambacho Jumamosi ijayo kinakabiliwa na mchezo wa ligi ya mabingwa hatua ya makundi dhidi ya JS Sauora

FT : Simba 3-0 Singida United

Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba leo wamerejesha furaha Msimbazi baada ya kuifumua Singida United mabao 3-0 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Taifa.

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems leo alipanga kikosi cha maangamizi ambacho kwa hakika kimeingamiza Singida United iliyokuwa na wakati mgumu katika mchezo huo.

Shiza Kichuya leo alikuwa nyota wa kikosi cha Simba baada ya kuhusika katika mabao yote yaliyofungwa na washiriki hao wa michuano ya ligi ya mabingwa hatua ya makundi

Katika dakika ya 17 Kichuya alimtengenezea Bocco aliyefunga bao lake la tatu msimu huu huku Kichuya tena akifunga mabao mengine mawili kwenye kipindi cha pili yote yakitengenezwa na Cletous Chama ‘CCC’

Ushindi ni matokeo stahiki kwa Simba iliyochocheza kandanda safi kwa muda wote wa mchezo.

Simba imefikisha alama 33 baada ya ushindi wa leo, imeendelea kusalia katika nafasi ya tatu.

Kama itashinda michezo yake minne ya kiporo, Simba ina uhakika wa kuiengua Azam Fc katika nafasi ya pili.

Leo Azam imepoteza mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar kwa kuchapwa mabao 2-0

Wekundu wa Msimbazi, Simba wametinga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika kwa staili ya aina yake baada ya kuifumua Nkana Fc mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa leo.

Bao la kideo lililoipeleka Simba hatua ya makundi liliwekwa kimiani na kiungo fundi, Clatous Chama kwenye dakika ya 88 akimalizia pasi ya Hassani Dilunga ‘HD’.

Nkana Fc hawatalisahau bao hilo na hakika Wazambia hao hawatamsahau ‘ndugu yao’ Chama kwani leo alikuwa kama hawajui.

Ilikuwa ni Nkana Fc iliyotangulia kufunga bao la kuongoza kupitia kwa Walter Bwalya kwenye dakika ya 17. Bao hilo liliiharibia Simba hesabu kwani awali ilikuwa ikihitaji ushindi wa bao 1-0.

Licha ya kuwa nyuma kwa bao la mapema, mabingwa hao wa Tanzania Bara hawakukata tamaa na walifanikiwa kusawazisha kwenye dakika ya 30 kupitia kwa shuti la Jonas Mkude aliyemalizia pasi ya Chama.

Meddie Kagere akaiongezea Simba bao la pili kwa kichwa dakika chache kabla ya kwenda mapumziko kabla Chama hajafunga bao la ‘usiku’ lililoipeleka Simba hatua ya makundi.

Matokeo hayo ni ushindi mwingine wa kihistoria kwa Simba ambayo sasa imerejea hatua ya makundi baada ya kusubiri ka miaka 15.

Simba 2-1 KMC FC :Full Time


Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara, Simba wamefanikiwa kuondoka na alama zote tatu katika mchezo wake wa kwanza wa kiporo baada ya kuilaza KMC mabao 2-1

Simba ilijipatia mabao yake yote mawili kwenye kipindi cha kwanza yakifungwa na Adam Salamba na Said Khamis Ndemla.

Salamba alitangulia kuifungia Simba bao la kuongoza kwenye dakika ya 11 akiunganisha vyema krosi ya Haruna Niyonzima aliyekuwa nahodha wa Simba kwenye mchezo huo.

Dakika tatu baadae Ndemla aliifungia Simba bao la pili akiachia shuti kali kutoka nje kidogo ya 18.

Simba iliyochezesha wachezaji wengi ambao hawapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza, ilicheza vizuri na kufanya mashambulizi mengi kwenye kipindi cha kwanza

Katika kipindi cha pili mabingwa hao watetezi walipunguza kasi na KMC ikatumia nafasi hiyo kurejea mchezoni na ikafanikiwa kufunga bao la kufutia machozi kwenye dakika ya 67 likifungwa na James Msuva

Kwenye mchezo huo Simba imemtumia kwa mara ya kwanza mlinzi wake mpya Zana Coulibaly aliyetua kutoka klabu ya ASEC Mimosas

Ushindi huo umeongeza hamasa kwa mashabiki wa Simba ambao Jumapili wameapa kufurika kwa wingi kwenye uwanja wa Taifa kuipa sapoti timu yao itakapokuwa ikichuana na Nkana Fc katika mchezo wa ligi ya mabingwa.

Matokeo ya ushindi pia yameifanya Simba ifikishe alama 30 na imeendelea kusalia nafasi ya tatu huku bado ikiwa na michezo mitatu ya viporo