Zana Coulibaly

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems leo anaweza kumtumia beki mpya wa kulia wa timu hiyo Zana Coulibaly kwenye mchezo dhidi ya KMC baada ya kibali chake kuwasili.

Coulibaly alitua Simba mwishoni mwa mwezi Novemba akitokea klabu ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast

Amekuwa akijifua katika kikosi cha Simba akisubiri kibali hicho cha uhamisho wa Kimataifa (ITC) ambapo uongozi wa Simba umethibitisha tayari kimewasili

“Zana Oumar Coulibaly anayo ruhusa kwa sasa kucheza Ligi kuu na kocha Patrick Aussems anayo nafasi ya kumpanga leo dhidi ya KMC ikimpendeza,” ilisema taarifa ya msemaji wa Simba, Haji Manara

Simba 1-2 Nkana FC : Full Time

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba wameanza kwa kupoteza mchezo wa awali wa michuano ya ligi ya mabingwa raundi ya kwanza baada ya kufungwa mabao 2-1 na Nkana FC.

Bao muhimu la ugenini la Simba lilifungwa kwa mkwaju wa penati na nahodha John Bocco kwenye dakika ya 73 baada ya Meddie Kagere kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari

Simba sasa inahitaji ushindi wa bao 1-0 nyumbani ili iweze kutinga hatua ya makundi.

Nkana Fc wamecheza vyema kwenye uwanja wao wa nyumbani na kufanikiwa kuibuka na ushindi huo.

Sasa ni zamu ya Simba nayo kuutumia vyema uwanja wa Taifa kwenye mchezo wa marudiano wiki ijayo.

Hakuna kisichowezekana, hii ni nafasi adimu kwa Simba kutinga hatua ya makundi ya michuano hii mikubwa kabisa barani Afrika katika ngazi ya vilabu

SIMBA yaendelea na Mazoezi Zambia

Kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba leo kimeendelea na mazoezi nchini Zambia kujiandaa na mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Nkana Fc utakaopigwa Jumamosi.

Mabingwa hao wa kihistoria wa soka Afrika Mashariki wameendelea kujifua katika uwanja wa Dynamos walioanza kuutumia jana.

Kesho Simba inatarajiwa kujifua kwenye uwanja wa Nkana utakaotumika katika mchezo wa keshokutwa.

Simba Yapewa tahadhari juu ya NKANA FC

Simba imetinga raundi ya kwanza ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika kibabe kwa kuifumua Mbabane Swallows jumla ya mabao 8-1 katika michezo miwili ya hatua ya awali.

Ushindi huo umeongeza mzuka na kujiamini kwa kikosi cha Simba ambacho kimedhamiria kutinga hatua ya makundi.

Simba itachuana na Nkana Fc ya Zambia katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo ambapo itaanzia ugenini mjini Kitwe wiki ijayo Disemba 14 2018.

Kuelekea mchezo huo wadau na wachambuzi mbalimbali wa soka nchini wameitahadharisha Simba kuwa ni lazima ijipange sawasawa kuweza kuiondosha Nkana Fc kwani timu hiyo sio ya kubezwa.

Pia historia baina ya timu hizo inafanya mchezo baina yao kuwa na ushindani wa aina yake. Nkana ilianzishwa mwaka 1935 wakati Simba ilianzishwa mwaka 1936

Timu zote zinatumia jezi za rangi nyeupe na nyekundu.

Mwaka 1990 Nkana Fc ilitinga fainali za michuano ya ligi ya mabingwa wakati Simba ilitinga fainali za michuano ya kombe la Washindi mwaka 1993

“Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Simba na Nkana kukutana kwenye michuano mikubwa barani Afrika,” amesema Ally Mayay mmoja wa wachambuzi wa soka katika runinga ya Azam

“Simba na Nkana zilishawahi kukutana miaka iliyopita. Ifahamike kuwa Nkana ilishafika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1990, lakini pia ina wachezaji wengi kutoka nchi zilizoendelea kisoka tofauti na Simba,” amesema

“Ili Simba waweze kushinda mbele ya Nkana, ni lazima wajipange upya kwa kurekebisha makosa ambayo yalijitokeza hususan kwenye safu ya ulinzi ambayo licha ya kutofungwa kwenye mechi za kwanza, lakini inahitaji maboresho kwani wangekutana na timu nzuri wasingefika walipo sasa”

Naye Kenny Mwaisabula amesema Simba inapaswa itambue kila wanaposonga mbele katika michuano hiyo ndio ugumu unaongezeka hivyo wanapaswa kujipanga.

“Simba bado ina kazi kubwa na kila wanavyosonga mbele lazima wajue ndio ugumu wa mashindano unavyoongezeka, hivyo benchi la ufundi linatakiwa kukaa na wachezaji ili kuwaeleza nini kilichopo mbele yao”

“Ni vema Simba wakaenda kucheza mechi hiyo kwa tahadhari kubwa kwani Nkana ni timu nzuri kuliko hata Mbabane, wana uzoefu wa mashindano na wamekuwa wakifanya vema katika mechi nyingi za kimataifa”

Simba itakuwa inasaka ushindi wake wa kwanza dhidi ya Nkana ambayo wamewahi kukutana nayo mara mbili huko nyuma.

Hata hivyo awamu hii Simba imeonekana kuwa na kikosi imara ambacho kinao uwezo wa kuwaondosha Wazambia hao na kutinga hatua ya makundi

SIMBA kuifuata NKANA FC Jumatano

Kikosi cha mabingwa wa Tanzania Bara Simba kinatarajiwa kuondoka Jumatano ijayo Disemba 12 kwenda nchini Zambia kwa ajili ya mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Nkana Fc.

Mchezo huo wa kwanza utapigwa Ijumaa ijayo, Disemba 14 Kitwe Zambia

Baada ya mchezo huo, Simba itarejea nchini tayari kwa mchezo wa marudiano utakaopigwa Disemba 21 katika dimba la Taifa.

Mabingwa hao wa nchi wameendelea kujifua kwenye uwanja wa Boko Veterans wakijiandaa na mchezo huo wa ugenini

Timu hiyo inayonolewa na kocha Patrick Aussems imedhamiria kutinga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu

Italikamilisha hilo kama itaibuka na ushindi wa jumla katika michezo hiyo miwili dhidi ya Nkana

MO Akoleza Moto Ubingwa Africa

Mwekezaji wa klabu ya Simba Mohammed Dewji ‘MO’ amewapongeza wachezaji wa timu hiyo baada ya kufanikiwa kutinga raundi ya kwanza ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.

Simba imeiondosha Mbabane Swallows katika hatua ya awali ya michuano hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-1

MO amesema ushindi wa jana ni ishara kwamba mabingwa hao wa Tanzania Bara wako tayari kupambana na vigogo wengine wa Afrika kuwania ubingwa wa bara hili

“Hongera Simba ya Africa. Sasa tuendelee na maandalizi ya mchezo unaofuatia, Mungu atutangulie. Narudia tena, lengo letu ni kuwa mabingwa wa Africa,” ameandika MO kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram

Mwanzoni mwa msimu uliopita wakati wa tamasha la SIMBA DAY, MO alitoa ahadi ya kuijenga Simba imara itakayokuwa na uwezo wa kushindana sio Tanzania pekee bali Africa nzima

Ahadi hiyo ameikamilisha kwa kiasi kikubwa kwani licha ya usajili wa wachezaji mahiri, Simba imemleta kocha Patrick Aussems ambaye ametengeneza timu imara ambayo imeonyesha kuwa tayari kuchuana na timu yoyote barani Afrika.

FT : SIMBA 4-0 MBABANE SWALLOWS

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba wametinga raundi ya kwanza ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika kibabe baada ya kuifumua Mbabane Swallows mabao 4-0 katika mchezo uliopigwa leo huko Eswatini.

Simba imewaondosha mabingwa hao wa Eswatini kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-1 kufuatia ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo wa kwanza uliopigwa wiki iliyopita jijini Dar es salaam

Mabao mawili ya haraka haraka yaliyofungwa na Clatos Chama ‘CCC’ kwenye kipindi cha kwanza yalitosha kuwaondoa Mbabane mchezoni na kuiwezesha Simba kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0

Licha ya kuwa ugenini, Simba ilitawala mchezo huo na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao.

Okwi na Kagere waliongeza mabao mengine mawili kwenye kipindi cha pili kuihakikishia Simba ushindi muhimu ulioivusha raundi ya kwanza.

Simba sasa inasubiri mpinzani wake wa mchezo wa raundi ya kwanza ambapo mchezo kati ya Nkana FC ya Zambia dhidi ya UD Songo ya Msumbiji utaamua timu itakayochuana na mabingwa hao wa Tanzania katika raundi ya kwanza.

Nkana Fc iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye mchezo wa kwanza baina ya timu hizo uliopigwa nchini Msumbiji.

Nayo Mtibwa Sugar imetinga raundi ya kwanza ya michuano ya kombe la Shirikisho baada ya kuilaza Northen Dynamos kwa bao 1-0

Mtibwa imefuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-1

Kikosi Cha Simba vs Mbabane Swallows Leo

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba muda mfupi ujao wa wanashuka dimbani huko Eswatini kuikabili Mbabane Swallows katika mchezo wa marudiano wa ligi ya mabingwa.
Hiki hapa kikosi cha Simba kinachoanza mchezo huo;
Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba muda mfupi ujao wa wanashuka dimbani huko Eswatini kuikabili Mbabane Swallows katika mchezo wa marudiano wa ligi ya mabingwa.

Hiki hapa kikosi cha Simba kinachoanza mchezo huo;