Wachezaji Simba kujaa Manoti wakaiito MBABANE SWALLOWS

Simba imetua salama Manzini, Eswatini na leo Jumatatu jioni inatarajia kupasha moto kwenye Uwanja wa Mavuso tayari kwa mchezo wake wa kesho Jumanne dhidi ya Mbabane Swallows, huku nyota wake wakijazwa mamilioni.

Msafara wa watu 26 wakiwamo wachezaji 20 ulipaa alfajiri ya jana Jumapili kuelekea Eswatini, lakini nyota wake wakiwamo Meddie Kagere, John Bocco na wengine wakiwekewa mezani mzigo wa maana ili kuwahamasisha waifumue tena Mbabane.

Juzi kabla ya kikosi hakijaanza safari ya kwenda Uwanja wa Ndege ili kukwea pipa kuelekea Eswatini, mabosi wa Simba wakishirikiana na bilionea wao, Mohammed ‘MO’ Dewji, waliwakalisha chini wachezaji wakiwaeleza wanataka ushindi ugenini.

Lakini ili kuhakikisha ushindi huo utakaowavusha hadi raundi ya kwanza unapatikana kirahisi, mastaa hao wakaambiwa; “Mkiachana na posho na bonasi zenu za kawaida za ushindi wa mechi za nyumbani, kuna mzigo wa maana mtaubeba kama mtashinda ugenini kama motisha kwenu.”

Kauli hiyo iliwafanya wachezaji kutabasamu na kuahidi lazima Mbabane ife, baada ya kuifumua jijini Dar es Salaam kwa mabao 4-1, kwa vile wanahitaji fedha hasa ikizingatiwa hiki ni kipindi cha kuelekea sikukuu za kuuaga mwaka 2018.

Wanene wa Msimbazi waliposikia ahadi hiyo ya ushindi kwa vijana wao wakawaambia wakipata matokeo ya kusonga mbele basi kila aliyecheza atavuna Sh 2 milioni nje ya mshahara na posho zao za kawaida.

Kama Kocha Patrick Aussems atawatumia nyota wote 20 katika mechi hiyo maana yake Simba itamwaga Sh 40 milioni kwa vijana, wale ambao hawatapata nafasi ya kucheza lakini wakavaa jezi nao watafutwa jasho.

Inaelezwa mshiko huo unajumuisha mchezo wa kwanza na huo wa kesho Manzini, hivyo kama kuna aliyecheza mechi ya Dar lakini akakosa mchezo wa Eswatini atapata nusu ya fedha watakazopewa wenzao ili iwaongeze motisha wapambane wapate nafasi ya kucheza.

Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi alisema kama viongozi wamejipanga kuweka motisha kwa wachezaji wao ili wapambane na kupata matokeo mazuri ya kusonga mbele kwani timu zote dunia zinafanya vizuri kwa kuweka motisha kama hizo.

“Kama uongozi tumeanza na posho hizi ambazo nina imani katika mechi za mbele ugumu wa mashindano utaongezeka na hata posho zitakuwa kubwa zaidi ya hizi ambazo tutawapatia wakati huu,” alisema.

“Tunafanya yote haya ili kuhakikisha Simba inafanya vizuri msimu huu katika mashindano ya kimataifa ili kutimiza malengo ya kwenda kucheza hatua ya makundi,” alisema Mkwabi.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema; “Tutakuwa tunawapatia matosha wachezaji wetu tofauti na zile za kwenye ligi na tutawapatia kile ambacho tutakuwa tunawahidi kwani viongozi huo tunakutana kujadili suala hilo.”

KWASI, JUUKO WATEMWA

Katika hatua nyingine mabeki, Asante Kwasi na Juuko Murshid wameachwa kwenye safari hiyo kama ilivyokuwa kwa Haruna Niyonzima aliyekwama kwa sababu ya viza.

Kiungo Haruna Niyonzima alitakiwa kuondoka Ijumaa usiku lakini akakwama sambamba na Nicholas Gyan ambaye alfajiri ya jana alisepa na msafara huo wa Simba ukiongozwa na Mtendaji Mkuu, Crescentius Magori sambamba na Mwenyekiti Mkwabi.

Kwasi na Juuko wameachwa kwa vile hawajawa fiti na Niyonzima alikiri kuachwa kwa sababu ya viza, licha alikuwa kwenye mipango ya kuwahishwa mapema na wenzake Rashid Juma na Gyan.

“Nadhani viongozi hawakufahamu kama nilitakiwa kuwa na viza ili niweze kuingia Eswatini ndio maana nimeshindwa kupata ruhusa ya kusafiri na nipo Dar naendelea na ratiba ya mazoezi,” alisema Niyonzima.

Wachezaji wengine walioachwa nchini ni Yusuf Mlipili, Marcel Kaheza, Mohammed Rashid, Ally Salim, Said Mohammed ‘Nduda’ na Abdul Selemani, huku 20 waliosafiri ni pamoja na Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Clatous Chama, James Kotei, John Bocco, Meddie Kagere na Hassan Dilunga.

Wengine Deogratius ‘Dida’, Shiza Kichuya, Emmanuel Okwi, Mohammed Ibrahim, Adam Salamba, Said Ndemla, Rashid Juma, Poul Bukaba, Mzamiru Yasin.

Mwanaspoti

KAIZER CHIEF YAMNYEMELEA OKWII

Wachezaji waandamizi wa kikosi cha Simba wameanza kunyemelewa kwa kasi na timu vigogo barani Afrika kutokana na kiwango kikubwa wanachoonyesha sasa.

Baada ya klabu za AS Vital na Zamalek kujitosa kumuwania Meddie Kagere, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini nayo imejitosa kumuwania Emmanuel Okwi kulingana na Mwanaspoti

Chiefs ambayo iko visiwani Zanzibar kurudiana na Zimamoto kwenye mchezo wa kombe la Shirikisho, inadaiwa kutuma ofa ikitaka kumsajili kinara huyo wa mabao wa kikosi cha Simba

Okwi alirejea Simba msimu uliopita na katika msimu wake wa kwanza alifanikiwa kuwa mfungaji bora baada ya kufunga mabao 20.

Msimu huu tayari ameifungia Simba mabao saba akiwa nyuma ya Eliudi Ambokile wa Mbeya City anayeongoza na mabao tisa.

Uongozi wa Simba utakazimikia kufanya kazi ya ziada kuhakikisha washambuliaji wake hawachukuliwi na timu nyingine

Kwani ili kuweza kufikia malengo ya kuifanya Simba kuwa bingwa wa Afrika inahitaji kuwa na wachezaji hawa ambao tayari wameonyesha uwezo usio na shaka

Simba yapaa kuwafuata MBABANE

Kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba kimeondoka leo Jumapili kuelekea nchini Afrika Kusini ambako kitaunganisha kwenda Eswatini kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa ligi ya mabingwa barani Afrika.

Msafara wa mabingwa hao wa kihistoria umejumuisha wachezaji 20 na viongozi nane wa benchi la Ufundi.

Mchezo dhidi ya Mbabane Swallows utapigwa siku ya Jumatano, Disemba 05 huko eSwatini (zamani Swaziland)

Afisa Habari wa Simba Haji Manara amesema wanakwenda kuivaa Mbabane Swallows kwa tahadhari kubwa huku wakifahamu wanahitaji kufuzu kwenda raundi inayofuata.

Jumatano Simba itashuka dimbani ikiwa na faida ya ushindi wa mabao 4-1 iliyopata mapema wiki hii kwenye dimba la Taifa.

Coulibaly Amwaga Wino MSIMBAZI

Klabu ya Simba imekamilisha usajili wa beki wa kulia Zana Coulibaly kutoka klabu ya Asec Mimosas ya ivory Coast.

Coulibaly aliyefuzu vipimo vya afya jana amesaini mkataba wa miaka miwili kuwatumikia mabingwa hao wa Tanzania Bara.

Coulibaly raia wa Burkina Faso amesajiliwa rasmi leo Ijumaa mchana na alikabidhiwa uzi wa Simba na kocha Mkuu Patrick Aussems mbele ya Mkurugenzi Mtendaji wa Simba Cresentius Magori

Kocha SIMBA: Ajipanga kuwaua Mbabane Kwao

Kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki hii kwenda Eswatini kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa ligi ya mabingwa dhidi ya Mbabane Swallows.

Mchezo huo utapigwa Jumatano ijayo huko Swaziland Simba ikiwa mbele kwa mabao 4-1 kufuatia ushindi iliyopata uwanja wa taifa juzi.

Kocha Mkuu wa timu hiyo Patrick Aussems ameendelea na maandalizi ya kuelekea mchezo huo unaotarajiwa kuwa mgumu.

Aussems amesema anakiandaa kikosi chake kuweza kupambana na mazingira watakayokutana nayo ugenini ili kuweza kulinda ushindi na hata kushinda ugenini.

“Ushindi tuliopata hapa nyumbani umetuweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele. Lakini bado tunapaswa kuamini kazi bado hatujaimaliza,” amesema Aussems

“Tunakwenda ugenini tukiwa na faida ya mabao matatu, tunajiandaa kikamilifu kuhakikisha tunapata matokeo ugenini yatakayo-tuhakikishia kufuzu hatua inayofuata”

Matokeo ya sare, ushindi au hata kufungwa chini ya mabao matatu yataiwezesha Simba kuitinga raundi ya kwanza ambapo itachuana na mshindi kati ya Nkana Fc dhidi ya UD Songo.

Beki Mpya wa SIMBA Afanyiwa Vipimo

Mlinzi wa pembeni kutoka klabu ya Asec Mimosas Zana Coulibaly leo amefanyiwa vipimo vya afya Hospitali ya Muhimbili tayari kusaini mkataba wa kuitumikia Simba

Zana aliyetua jana, inaelezwa amefuzu vipimo hivyo na anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba

Beki huyo mwenye ‘mapafu ya mbwa’ amesajiliwa ili kuziba pengo la Shomari Kapombe aliyeumia mwezi uliopita wakati akiitumikia timu ya Taifa

Kapombe anaendelea na matibabu nchini Afrika Kusini.

Zana anatarajiwa kutumika kwenye ligi tu kwa kuwa atakuwa amechelewa usajili wa CAF.

Hata hivyo mchezaji huyo ataweza kuongezwa kwenye kikosi cha Simba kinachoshiriki michuano hiyo kama mabingwa hao wa Tanzania Bara watafuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo ya CAF

USAJILI: Simba yamsajili beki huyu

Simba imemnasa beki wa kulia wa klabu ya Asec Mimosas Zana Coulibaly.

Mchezaji huyo atawasili nchini leo kwa ajili ya kukamilisha taratibu za usajili.

Beki huyo anatarajiwa kuziba pengo la Shomari Kapombe ambaye atakuwa nje kwa muda mrefu baada ya kupata majeraha wakati akiitumikia timu ya Taifa

“Tunapenda kuwatangazia kwamba beki Zana Coulibaly kutoka ASEC Mimosas ya Ivory Coast leo atawasili nchini kwa ajili kukamilisha taratibu za mwisho kujiunga na timu yetu ili kuziba pengo la beki Shomari Kapombe ambaye siku za karibuni alipata majeraha,” imesema taarifa ya Simba

USAJILI: Simba kumsajili mchezaji huyu?

Mapema leo katika ukurasa rasmi wa klabu ya Simba mtandao wa Instagram iliwekwa picha ya beki kutoka klabu ya Asec Mimosas, Zana Oumar Coulibaly

Coulibaly ni mlinzi wa kulia anayetarajiwa kusajili na Simba kuziba pengo la Shomari Kapombe

Hiyo ni habari njema kwa mashabiki wa Simba kwani Coulibaly huenda akawa njiani kutua Msimbazi.

Ingawa picha hiyo haikuwa na maelezo mengi, ni dhahiri uongozi wa Simba utakuwa umemalizana na mkali huyo.

OKWI: Kuongeza mzuka kikosi cha Simba

Licha ya kuchelewa kujiunga na kambi ya Simba kutokana na kukabiliwa na majukumu ya timu ya Taifa, mshambuliaji hatari Emmanuel Okwi jana aliwasili nchini sambamba na beki Juuko Murshidi.

Baada ya kuwasili, moja kwa moja wachezaji hao walielekea kambini kujiunga na wachezaji wengine tayari kwa mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Mbabane Swallows kesho.

Okwi alishiriki mazoezi ya jana jioni ya kikosi cha Simba na uwepo wake uliongeza ‘mzuka’ kwa mashabiki waliojawa na furaha baada ya kumuona.

Kurejea kwake pia kumeimarisha utimamu wa safu ya ushambuliaji ya Simba ambayo sasa ina uhakika wa kuwavaa Mbabane Swallows ikiwa na majembe yake yote matatu Okwi, Kagere na Bocco.

Kocha Patrick Aussems amesema atamtumia Okwi kwenye mchezo wa kesho kwani katika mazoezi ya jana ameonyesha kuwa yuko ‘fit’