Nyota wapya yanga wajifua na kikosi cha yanga

Uongozi wa Yanga tayari umewapokea nyota wanne wa kigeni wanaotarajiwa kusajiliwa na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema anatarajia kukamilisha usajili wa nyota sita wa kigeni pamoja na wazawa wawili kabla ya kuondoka kwenda DR Congo kujiunga na kambi ya timu ya Taifa

Nyota wa kigeni waliohudhuria mazoezi ya Yanga jana ni pamoja na kiungo mwenye umri wa miaka 20 raia wa Nigeria Victor Patrick Akpan aliyekuwa akikipiga na JKU ya Zanzibar

Akpan yuko kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Nigeria umri chini ya miaka 23

Wengine ni beki wa kati Mohammed Ali Camara mwenye umri wa miaka 21 kutoka klabu ya Horoya AC ya Guinea.

Camara aliitumikia timu ya Taifa ya Guinea U20 na tayari ameitumikia timu ya wakubwa mara moja

Wengine ni mshambuliaji Shehu Magaji Bulama raia wa Nigeria na kiungo Allex Komenan kutoka nchini Ivory Coast

Bulama na Komenan watafanyiwa majaribio na Zahera kabla kuidhinisha kama wasajiliwe au la

TEN: Awaaga AJIBU, MAKAMBO: Amkaribisha KOUKPO

Heritrier Makambo na Ibrahim Ajib wamebakisha wiki moja tu ya kuitumikia Yanga kwani baada ya mchezo dhidi ya Azam Fc, wachezaji hao hawatakuwa mali ya Yanga

Wakati Makambo akisubiri kutimkia Horoya AC, Ajib anaelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujiunga na mabingwa wa nchi hiyo, TP Mazembe

Afisa Habari wa Yanga Dismas amewatakia kila la kheri wachezaji hao waliokuwa na mchango mkubwa kwa kikosi cha Yanga msimu huu

Wakati Makambo akifunga mabao 17, Ajib amehusika katika mabao 23, akitengeneza 17 na kufunga sita

Ten amesema wawili hao wangetengeneza ‘combination’ ya hatari na Marcellin Koukpo ambaye anatajwa kusajiliwa na Yanga

“Simba kuna utatu wa Kagere, Bocco na Okwi nawaza sijui ingekuwaje kama nasi tungepata utatu wa Ajib, Makambo na Koukpo”

“Simaanishi kwamba waliokuwepo hawawezi, lakini wakati mwingine si vibaya kuwaza kwa mafanikio ya mwingine. Kikubwa kila timu ijenge kikosi imara ili tuwe na ligi ya ushindani kweli mwakani” amendika Ten kwenye ukurasa wake wa Instagram

Yanga itamkumbuka Ajib kwa mchango wake aliotoa kwa klabu hiyo tangu alipojiunga kutoka Simba misimu miwili iliyopita, wakati Makambo amecheza Yanga kwa msimu mmoja lakini atakumbukwa kwa uhodari wake wa ‘kuzijaza’ mabao timu pinzani

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera ana kazi ya kusaka wachezaji watakaoziba nafasi zao.

Mwenyewe amewatoa hofu mashabiki wa Yanga akiwahakikishia kuwa atasajili wachezaji wenye uwezo sawa au zaidi yao

Majembe ya nje yanayoshuka yanga ni ya KIMATAIFA

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema wachezaji wa kigeni wanaotarajiwa kusajiliwa na timu hiyo wote wanacheza katika timu zao za Taifa

Zahera amesema usajili wa wachezaji wa kigeni umezingatia umuhimu wa kusajili wachezaji ambao wataongeza ushindani na kuinua kiwango cha wachezaji wa ndani

“Miongoni mwa wachezaji tutakaowasajili, sita au saba ni wachezaji wa kigeni. Wageni wote wanaokuja Yanga wanacheza timu za Taifa. Watasaidia kuongeza ushindani wa kikosi chetu na kuinua viwango vya wachezaji wazawa,” amesema

Kuhusu usajili wa wachezaji wa ndani, Zahera amesema hawatafanya usajili mkubwa wa wachezaji wa ndani

“Nafikiri tutasajili wachezaji watatu au wanne wa ndani. Tunao wachezaji wazuri ambao tutawaimarisha ili msimu ujao wawe bora zaidi”

Kuhusu wachezaji wanaoachwa, Zahera amesema wataachana na wachezaji 10 ambao majina yao yatafahamika baada ya kumalizika kwa mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa Jumanne, May 28 2019

Mkwasa Amkumbuka Msuva Yanga – Atakwa mbadala wake Utaftwe

Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga Charles Mkwasa anaamini timu hiyo inahitaji maboresha katika baadhi ya nafasi ili iweze kuchuana na Simba msimu ujao katika kuwania ubingwa wa ligi kuu

Mkwasa aliyejiuzulu uongozi Yanga mwaka jana baada ya kupata maradhi ya moyo, amesema lazima Yanga iimarishwe ili iweze kurudisha makali yake ya zamani

Mkwasa ametaka kusajiliwa kwa wachezaji ambao watarudisha utamaduni wa timu hiyo ambao ni kushambulia kupitia pembeni akimtaja Simon Msuva kuwa aliondoka na makali yake

Tangu kuondoka kwa Simon Msuva, Yanga haikuweza kuziba pengo lake na hivyo kujikuta ikikosa makali ya kushambulia kupitia pembeni

Mabao mengi ya Yanga msimu huu yamefungwa kupitia krosi au mipira iliyokufa, kiungo Ibrahim Ajib akihusika kutengeneza mabao 17 huku mwenyewe akifunga mabao sita

“Yanga inahitaji kusajili washambuliaji wa pembeni waliokuwa na uwezo kama wa Msuva au zaidi,” amesema

Mkwasa pia amependekeza maboresho kwenye safu ya ulinzi akiamini timu hiyo inahitaji angalau walinzi wawili wapya watakaoboresha eneo hilo

Eneo la mlindalango pia limempa mashaka nahodha huyo wa zamani wa Yanga ambapo amependekeza kusajiliwa kipa mwengine mwenye ubora zaidi ya waliopo

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema wako katika mazungumzo na wachezaji wengi wanaotarajiwa kusajiliwa na timu hiyo

Zahera amesema kabla ya wiki ijayo kukamilika, watakamilisha usajili wa wachezaji nane

ZAHERA: amefichua kuwa aliwasiliana na viongozi wa TP Mazembe wiki tatu zilizopita kuhusu usajili wa kiungo Ibrahim Ajib

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amefichua kuwa aliwasiliana na viongozi wa TP Mazembe wiki tatu zilizopita kuhusu usajili wa kiungo Ibrahim Ajib

Zahera amesema kwa uwezo alioonyesha kwenye kikosi cha Yanga, Ajib anaweza kufanikiwa kukipiga TP Mazembe lakini ni lazima abadilike

“Nilisimulia na TP Mazembe wiki tatu zilizopita juu ya Ajib,” amesema Zahera

“Sina wasiwasi na yeye kusajiliwa TP Mazembe sababu nafahamu ni mchezaji mzuri sana”

“Lakini inafaa akajitume sana ili kuweza kupata namba TP Mazembe”

“Mpira wa TP Mazembe ni mpira wa nguvu mingi, yafaa akatumike sana ili aweze kucheza”

MAKAMBO: “Nitawakumbuka Mashabiki wa Yanga”

Mshambuliaji wa Yanga Heritier Makambo jana aliwashukuru mashabiki wa timu hiyo kwa kumuunga mkono katika kipindi chote alichokuwa hapa nchini

Makambo aliyefunga bao pekee la Yanga katika mchezo dhidi ya Mbeya City, anatarajiwa kuondoka mwishoni mwa msimu kujiunga na Horoya AC

“Nawashukuru mashabiki kwa kuniunga mkono. Ligi haikuwa rahisi kwetu lakini mashabiki walikuwa nasi kwa kipindi chote,” amesema Makambo

“Tayari nimeshakamilisha kila kitu na Horoya hivyo nasubiri ligi imalizike nielekee Guinea nikaanze changamoto mpya”

“Ssitaacha kuwakumbuka mashabiki, wachezaji wenzangu kocha na viongozi wa Yanga kwani tumeshirikiana vizuri”

Makambo tayari amesaini mkataba wa awali klabu ya Horoya AC kinachosubiriwa ni viongozi wa timu hiyo kuja nchini kumalizana na Yanga kabla ya ITC yake kuachiwa

Mwinyi Zahera amewapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City

Licha ya kuwakosa wachezaji saba wanaougua Malaria, kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amewapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City

Zahera amesema katika mchezo wa leo alitumia wachezaji wanne kutoka katika kikosi cha U20

“Tulikosa wachezaji wetu saba wanaumwa Malaria, nimetumia vijana wanne wa U20, nafurahi wachezaji wameweza kutupatia matokeo,” amesema

“Tulitengeneza nafasi nyingi, tulipaswa kufunga mabao zaidi, nafikiri leo hatukuwa na nidhamu ya mchezo”

Kuhusu maoni yake baada ya Simba kutwaa ubingwa jana, Zahera ameshikilia msimamo wake kuwa hawakustahili kutwaa ubingwa kutokana na upindishwaji mkubwa wa sheria uliofanywa kuwawezesha washinde taji hilo

“Simba waliwapa ubingwa jana, maoni yangu mie nilicheza mpira ambao uko na sheria, ule sio ubingwa,” amesema

“Ninapoishi nakaa na watu wa Simba, wananiambia kweli hata kama mpira wetu tunapenda Simba, tunaona kama sio hivyo”

“Tunapata kikombe lakini ukiangalia sheria kabisa mwaka huu hatungepata kikombe”

Wadau mbalimbali wametoa maoni tofauti juu ya ubingwa wa Simba

Wakati wengine wakiamini kuwa Simba ilistahili ubingwa huo, wapo wanaoamini mazingira yaliyotengenezwa na TFF kwa kuiacha timu hiyo isicheze mpaka michezo 12 wakati nyingine zikiendelea na ligi, yameirahisishia timu hiyo kutwaa ubingwa

“Simba walikuwa na michezo 12 ya viporo. Walikuwa wanafahamu matokeo ambayo wanatakiwa wapate ili watwae ubingwa, pengine hali ingekuwa tofauti kama wangecheza sambamba na timu nyingine,” amesema Rajabu Issa kutoka Buguruni

“Umeona wapi na ligi gani duniani ambapo timu moja inakuwa na michezo ya viporo 12? kushiriki ligi ya mabingwa haitoshi kuwa sababu ya kurundikiwa michezo mingi kiasi hicho mbona timu walizokuwa wakishindana nazo zilikuwa zikicheza ligi zao?”

“Hawa Simba baada ya kutolewa kombe la FA walipanga mkakati na TFF kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa ligi kuu kupitia ratiba na hujuma kwa Yanga”

“Angalia mchezo dhidi ya KMC ilikuwa wafungwe lakini refa akawatafutia ushindi kwa nguvu halafu baadae TFF wanatangaza kumfungia mwamuzi wakati mpango umeshakamilishwa”

FT: Yanga 1-0 Mbeya City

Yanga imeendeleza umwamba wake katika dimba la Uhuru baada ya kuichapa Mbeya City bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara mzunguuko wa 37

Bao pekee la Yanga lilipatikana kwenye dakika ya 26 likiwekwa kimiani na Heritier Makambo aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Haji Mwinyi

Hilo ni bao la 17 kwa Makambo, akishika nafasi ya pili sawa na Salim Aiyee katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu nyuma ya Meddie Kagere wa Simba mwenye mabao 23

Licha ya kuwakosa nyota wake wengi ambao ni wagonjwa na majeruhi, Yanga ilitandaza kandanda safi na kutawala mchezo huo kwa muda mwingi

Kiungo kinda Gustapha Simon ameendelea kudhihirisha ubora wake, hakuna shaka msimu ujao atapata nafasi zaidi kwenye kikosi cha Zahera

Yanga imefikisha alama 86 sasa ikibakiwa na mchezo mmoja wa kumaliza msimu dhidi ya Azam Fc

Mchezo huo utapigwa May 28 2019