KENNY ALLY: Huru Kutua Jangwani #YANGA

Kiungo wa Singida United Kenny Ally ni miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwaniwa na Yanga kwa ajili ya msimu ujao

Kenny anaweza kutua Yanga akiwa mchezaji huru kwani mkataba wake na Singida United unamalizika mwishoni mwa msimu huu

Uongozi wa Singida United umesema hauna pingamizi kwa kiungo huyo kama atapenda kujiunga na Yanga kwa kuwa maamuzi ni yake, mkataba wake uko ukingoni

“Kenny atakuwa huru kujiunga na timu yeyote baada ya ligi kumalizika, hivyo kama Yanga wanamuhitaji wazungumze nae,” amesema Cales Katemana ambaye ni msemaji wa Singida United

Yanga imedhamiria kuunda kikosi cha ushindani kwa ajili ya msimu ujao

Tayari michakato ya usajili imeanza kimyakimya

TETESI ZA USAJILI YANGA LEO JUMATATU

KUNA kila dalii kwamba, endapo straika Heritier Makambo wa Yanga atakamilisha dili lake la kujiunga na klabu ya Horoya FC ya nchini Guinea, basi mkali mwingine raia wa Ghana ataziba nafasi yake.
Anayetajwa kuziba nafasi hiyo ni Mnamibia anayekipiga katika klabu ya Lusaka Dynamos ya Zambia, Petrus Shitembi, anayetajwa kuwa hatari katika nafasi ya kiungo mshambuliaji.

Kiungo huyo alisajiliwa na Lusaka Dynamos siku chake baada ya Clatous Chama kusajiliwa na Simba ili kuziba pengo lake kutokana na uwezo mkubwa alionao.

Simba walimsajili Chama kutoka klabu hiyo na kwa haraka nao hawakulaza damu, wakamchukua Shitembi ambaye naye ameingia kwenye rada za Yanga.

Kigogo mmoja wa Yanga amefunguka kuwa kiungo huyo ambaye ana uwezo mkubwa wa kutoa pasi za uhakika na kufunga mabao muhimu, ameshaingia kwenye 18 zao na kilichobakia ni kumalizana tu.
“Ni kweli Makambo ameondoka lakini hiyo haimaanishi kwamba Yanga inakufa. Tumeshaanza harakati za usajili na muda si mrefu tutamalizana na kiungo kutoka Namibia.
“Ni moja ya viungo wazuri na yeye hana tabu yoyote kuja Yanga. Nadhani ataungana na wachezaji wengine ambao tutawasajili kwani dhamira yetu ni kuisuka klabu yetu upya ili msimu unaokuja tuwakate kilimilimi wapinzani wetu,” alisema.
Alisema kiungo huyo ni moja ya wachezaji wanane wa kigeni ambao kocha wao mkuu, Mwinyi Zahera, alidai atawasajili, huku akisema kuna mastraika wengine watatu kutoka nchi tofauti.

“Wapo pia mastraika watatu tunaendelea na mazungumzo nao, hiyo kazi inafanywa na kocha wetu, nadhani baada ya kuondoka Makambo, tutashusha mashine nyingine hatari zaidi,” alisema.
Kiungo huyo alianza soka katika timu ya Rundu Chiefs ya nchini kwao Namibia kabla ya kwenda Afrika Kusini ambako alijiunga na University Of Pretoria na baadaye kwenda Ghana kuichezea Ashanti Gold kabla ya kurudi tena na kuzichezea Amazulu FC na Stellenbosch FC na baada ya kuondoka Chama akasajiliwa Lusaka Dynamos kuziba pengo lake.

Dk Msolla Atangaza kusaka kocha msaidizi – YANGA

Habari njema kwa Wanajangwani ni kuwa uongozi wa Yanga umetangaza kuanza mchakato wa kutafuta kocha Msaidizi Mzawa ambaye atasaidiana na kocha Mwinyi Zahera kukinoa kikosi cha Yanga

Tangu alipoanza kazi mwishoni mwa msimu uliopita, kocha Zahera hakuwa na Msaidizi zaidi ya Noel Mwandila ambaye amekuwa akikaimu nafasi hiyo licha ya kuajiriwa Yanga kama kocha mtaalamu wa viungo

Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshondo Msolla ambaye kitaalam ni kocha, amesema kuna umuhimu kwa benchi la Ufundi kuongezewa nguvu kwa kuajiri kocha Msaidizi mzawa ambaye atakuwa sambamba na Zahera

“Benchi la ufundi linahitaji kuwa na kocha msaidizi mwenye kiwango kizuri ili kuongeza nguvu ndani ya kikosi chetu, tutaangalia zaidi kocha mzawa ili aweze kuwa sambamba na kocha Zahera kufanya kazi,” amesema

ZAHERA APEWA MAJUKUMU HAYA YANGA

Katika kuhakikisha timu zote za Yanga zinakuwa imara, uongozi wa timu hiyo umemtangaza Mwinyi Zahera kuwa msimamizi Mkuu wa timu zote

Akizungumza kwenye hafla ya Iftar Gala Dinner iliyofanyika Hotel ya Serena jijini Dar es salaam usiku wa kuamkia leo, Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla amesema Zahera ambaye ni kocha wa kikosi cha kwanza, pia atasimamia timu ya Vijana (Yanga B) na timu ya Wanawake (Yanga Princess)

“Kwa sababu ya masuala ya ufundi, natangaza mbele yenu, timu zote zitakuwa chini ya kocha Mwinyi Zahera,” alisema Dk Msolla

“Ni lazima kama timu tuwe na filosofia moja. Hivyo tumeona filosofia inayotumiwa kwenye kikosi cha kwanza ni lazima ikafuatwa na makundi yote. Zahera atakuwa msimamizi Mkuu”

ASISITIZA KUVUNJWA MAKUNDI

Dk Msolla amewataka Wanayanga kudumisha umoja ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea

Aidha amesema ahadi walizotoa wakati wa kampeni watazitimiza ambapo ameahidi kushirikiana na waliokuwa wagombea wengine wa nafasi mbalimbali lakini bahati mbaya kura hazikutosha

“La kwanza lilikuwa kuleta mshikamano na kuirudisha timu kwa Wananchi”

“La pili lilikuwa kubadilisha mfumo na uendeshaji wa timu. Nawaahidi mbele yenu hili tutalifanya ndani ya mwaka mmoja au chini ya hapo”

“La tatu muhimu tutasaidia miradi inayoendelea klabuni sasa ambayo ni ujenzi wa uwanja, ukarabati wa jengo na miradi mipya”

“Nafurahi Igangula hapa amesema yuko tayari kutoa ushirikiano, niliona randama yake wakati wa kampeni, nawaahidi tutashirikiana nae na tutahakikisha atakuwa sehemu ya uongozi wetu”

“Dk Tiboroha ameshindwa kufika hapa kutokana na kuchelewa kutoka safarini Arusha lakini ameahidi kuchangia Tsh Milioni Moja kwa ajili ya shughuli mbalimbali za klabu, na yeye tuko nae pamoja”

“Muhimu nimeomba sote tuvunje makundi yetu baada ya uchaguzi. Umoja na Ushirikiano wetu utatusaidia kusonga mbele kwa haraka”

UTAWALA BORA

Dk Msolla amesema katika uongozi wake watahakikisha wanafuata utawala bora na watakuwa makini katika usimamizi wa fedha

“Maeneo ya ukaguzi wa ndani na nje tutakuwa wakali sana. Tutakuwa tayari kutumia gharama kuwapata wakaguzi wanaoheshimika Kimataifa na tutakuwa tukitoa ripoti wazi kwenye vyombo vya habari kuhusu mapato na matumizi ya klabu kama zinavyofanya taasisi nyingine”

KUIMARISHA KIKOSI CHA YANGA

Dk Msolla amesema kwa ushirikiano ulioonyeshwa na makundi mbalimbali ya Yanga, ndani ya wiki mbili au tatu, zoezi la kukiboresha kikosi litakuwa limeanza

“Nawaahidi ndani ya wiki mbili au tatu zijazo, tutaanza kutengeneza kikosi imara chini ya usimamizi wa kocha Mwinyi Zahera”

MAKAMBO : Kawapa Somo Wachezaji Wa YANGA SC

Kuna wakati kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera alifichua kuwa mshambuliaji Heritier Makambo alifukuzwa Hotelini alikokuwa amepanga kutokana na uongozi wa Yanga kushindwa kulipa kodi ya pango

Makambo alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Yanga wenye madai ya fedha za mishahara hadi miezi minne achilia mbali malimbikizo ya bonasi na fedha za usajili

Lakini changamoto hizo hazikumuondoa katika majukumu yake, alijituma kwa moyo mmoja kuhakikisha Yanga inafanya vizuri

Dili nono alilopata klabu ya Horoya AC ni matunda ya uvumilivu na kujituma kwake katika klabu ya Yanga

Hili ni somo kwa wachezaji wengine Yanga hasa wale wenye malengo ya kufika mbali

Migomo na ‘kususa’ kucheza haviwezi kuwasaidia kufikia malengo hayo

Nakumbuka mwanzoni mwa msimu Zahera alikaa na wachezaji wote na kuwaeleza umuhimu wa wao kuifanya kazi kwa bidii bila ya kujali changamoto zinazowakabili

Bila shaka hawa akina Makambo walimuelewa vizuri na ndio maana walifanya kazi kwa bidii, leo wameona matunda yake

Wachezaji wa Kitanzania wajenge utamaduni wa kuwa na malengo ya kufika mbali

Leo hii ukimuangalia Beno Kakolanya alichokipata baada ya kuigomea Yanga utamsikitikia tu

Kama Beno angeendelea kucheza Yanga pengine leo angekuwa kipa namba moja wa kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’

Beno aliigomea Yanga wakati kiwango chake kikiwa juu sana na tayari alishaitwa kikosi cha timu ya Taifa

Angecheza michuano ya AFCON 2019 na kuwa na nafasi kubwa ya kuonekana Kimataifa na kujiongezea nafasi ya kupata timu nje ya nchi

Hawa akina Makambo wawe somo kwa wachezaji wetu.

Wawe makini katika kufanya maamuzi, wajitambue, wawe wavumilivu na kuwa na malengo ya kufika mbali

Muhimu zaidi watafute Wasimamizi ambao wanaweza kuwasaidia kufikia malengo yao

ZAHERA : Asaka Mrithi wa MAKAMBO

Baada ya kusambaa kwa taarifa za mshambuliaji wa Yanga Heritier Makambo kusajiliwa na Horoya AC ya Guinea kwa mkataba wa miaka mitatu, Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla alifafanua kuwa dili hilo limeihusisha klabu yake na Makambo aliondoka nchini na Kocha Mwinyi Zahera

Hata hivyo imefahamika Zahera alilekea nchini Bennin ambako amekwenda kufanya mazungumzo na mshambuliaji mwingine

Halitakuwa jambo la kushangaza kama mshambuliaji huyo atakuwa Marcellin Koukpo ambaye alikuja msimu uliopita lakini usajili wake kukwamishwa na wajanja wachache waliokuwa wakitaka ‘ten percent’

Koukpo mshambuliaji wa Kimataifa wa Benin, alikaa nchini kwa zaidi ya wiki mbili kabla ya kuamua kuondoka baada ya kupishana na viongozi wa Yanga

Mshambuliaji huyo alipendekezwa na aliyekuwa kocha wa Yanga msimu uliopita, George Lwandamina na alifanyiwa majaribio na kocha Mwinyi Zahera kabla ya kuibuliwa taarifa za ‘uzushi’ kuwa ameshindwa majaribio

Baada ya kumuuza Makambo, Yanga inaweza kusajili washambuliaji wawili ambapo mmoja anaweza kuwa huyo Mbenin huku timu hiyo ikihusishwa na mshambuliaji wa Gor Mahia Jacques Tuyisenge na Roderick Matuma raia wa Zimbabwe anayekipiga kunako klabu ya Fc Lupopo

Dirisha la usajili litafunguliwa mwezi ujao ambapo uongozi wa Yanga umepania kukiimarisha kikosi chake wakijipanga kutumia kati ya Bil 1.5 hadi Bil 2

Hata hivyo Yanga imedhamiria kukamilisha masuala ya usajili mapema hasa ikizingatiwa Zahera ndiye msimamizi Mkuu wa mchakato huo

Mwanzoni mwa mwezi wa sita Zahera atarejea kwao Congo kwa ajili ya majukumu ya timu ya Taifa kuelekea fainali za AFCON zitakazofanyika Misri kuanzia Juni 21 2019

BREAKING NEWS: MAKAMBO ATIMKA YANGA, AJIUNGA HOROYA AC

Mshambuliaji wa Yanga Heritier Makambo ametimkia Guinea kujiunga na klabu ya Horoya Fc

Taarifa za Makambo kusajiliwa na Horoya zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii mapema leo ambapo timu hiyo imemtambulisha rasmi
Makambo ndiye kinara wa mabao katika kikosi cha Yanga msimu huu akitupia kambani mabao 16

Kulingana na mtandao wa Kalonews, Makambo amesaini mkataba wa miaka mitatu

“Horoya AC imemsajili mshambuliaji kutoka DR Congo Heritier Makambo aliyekuwa akiichezea Young Africans ya Tanzania,” imesema taarifa ya mtandao huo

“Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 aliyewahi kuichezea Motema Pembe, amefunga mabao 16 kwenye ligi ya Tanzania”
“Amesaini mkataba wa miaka mitatu”

Kuondoka kwa mshambuliaji huyo ni pigo kwa Yanga ambayo iko kwenye mchakato wa kukiimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao

https://play.app.goo.gl/?link=https://play.google.com/store/apps/details?id=com.chumbani.raha&ddl=1&pcampaignid=web_ddl_1

Yanga italazimika kuingia sokoni kusaka washambuliaji wengine wakali

Hata hivyo Yanga itanufaika na mauzo ya mshambuliaji huyo kwani mkataba wake na Yanga ulikuwa bado haujamalizika
Inaelezwa Makambo ameuzwa kwa dau linalokadiriwa kufikia Milioni 230 za Kitanzania




Yanga kukamilisha ukarabati uwanja wa Kaunda

Uongozi wa klabu ya Yanga umeandaa mpango wa muda mfupi ambao utawezesha ukarabati wa uwanja wa Kaunda ili uweze kutumika kwa ajili ya mazoezi

Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema baada ya msimu kumalizika wataanza ukarabati wa sehemu ya kuchezea ‘pitch’ ya uwanja wa Kaunda ili uweze kutumika msimu ujao

“Kwa sasa tutakarabati sehemu ya kuchezea, ni zoezi ambalo litachukua takribani miezi mitatu,” amesema Mwakalebela

“Lengo letu ni kuhakikisha msimu ujao tunakuwa na uwanja wetu wa mazoezi ili kupunguza gharama”

“Gharama tunazotumia kukodi viwanja ni kubwa, pesa hiyo inaweza kutusaidia katika masuala mengine yakiwemo ya usajili”

Kuhusu adha ya mafuriko Jangwani, Mwakalebela amesema kifusi kilichowekwa mwanzo kimepunguza adha hiyo na wanakusudia kuongeza kifusi kingine kabla ya kuanza mchakato wa kupanda nyasi sehemu ya kuchezea