Wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika klabu ya Yanga leo wanahitimisha zoezi la kampeni kuelekea uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo utakaofanyika kesho Jumapili ukumbi wa Bwalo la Polisi, Osterbay jijini Dar es salaam
Wagombea walianza kunadi sera zao kwa Wanachama Jumanne iliyopita
Nafasi ya Mwenyekiti wa Yanga inawaniwa na wagombea watatu Barak Igangula, Dk Jonas Tiboroha na Dk Mshindo Msolla wakati nafasi ya Makamu Mwenyekiti inawaniwa na wagombea wanne ambao ni Fredrick Mwakalebela, Janeth Mbene, Titus Osoro na Yono Kevela
Aidha wagombea 21 wanawania nafasi nane za wajumbe wa Kamati ya Utendaji
Wanachama wa Yanga wametakiwa kutofanya makosa kwenye uchaguzi wa kesho kwa kuwachagua viongozi ambao wataweza kuipeleka Yanga mbele
Suala la Mabadiliko limekuwa kilio cha Wanayanga. Wagombea wote wameahidi kufanya mabadiliko, ni jukumu la Wanachama kujiridhisha na uwezo wao na ahadi walizotoa katika kutatua changamoto zinazoikabili Yanga
Wanachama wameaswa kutochagua viongozi kwa mazoea badala yake wachague viongozi ambao wana upeo mkubwa
Ni vyema kiongozi atakayechaguliwa awe na uwezo wa kutengeneza mikakati ya kuipeleka Yanga kule ambako kila mdau anahitaji kuona klabu ikielekea
Huu sio wakati wa kujaribu viongozi, Wanachama wawaweke madarakani ‘watu wa kazi’
Wanachama wasichague viongozi kwa papara, mihemko na makundi, kila mmoja afanye uamuzi kwa maslahi ya klabu kwa kuchagua viongozi wenye tija
Yanga ikipata viongozi wazuri, utakuwa mwanzo wa kutengeneza Yanga imara ambayo itagombewa na wawekezaji na kuifanya timu hiyo kongwe zaidi Tanzania kuondokana na dimbwi la ‘umasikini’