YANGA YAUTUMIA UWANJA WA UHURU VIZURI, YAICHAPA RUVU SHOOTING BAO 1-0

Yanga imerejea kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru


Bao pekee la Yanga lilifungwa na Papi Tshishimbi aliyemalizia pasi murua ya Deus Kaseke kwenye dakika ya 16
Hilo lilikuwa bao la nne kwa Tshishimbi kwenye ligi msimu huu

Yanga ilikuwa bora kwenye kipindi cha kwanza na ilistahili kwenda mapumziko na angalau mabao mawili kama Raphael Daud asingekosa nafasi ya wazi
Ushindi huo umeifanya Yanga ifikishe alama 83 na kuiondoa Simba kileleni mwa msimamo wa ligi

Simba itacheza na Mtibwa Sugar keshokutwa Alhamisi katika mchezo ambao kama haitapata ushindi huenda ikafufua matumaini ya Yanga kwenye mbio za ubingwa

SIKU CHACHE BAADA YA UCHAGUZI…BILIONEA MPYA AIBUKA YANGA

BILIONEA maarufu hapa nchini, Rostam Azizi imeelezwa kuwa amekusudia kuisaidia Yanga kwa kuipa misaada ya kifedha pale inapowezekana. Hii inakuja siku chache tu baada ya Yanga kufanya uchaguzi na kupata viongozi wapya chini ya mwenyekiti, Dk Mshindo Msolla na makamu wake, Frederick Mwakalebela aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Rostam amekuwa akitajwa mara nyingi na baadhi ya wadau wa soka kuwa anatarajia kuwekeza ndani ya Klabu ya Yanga baada ya kuondoka aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji. Klabu ya Yanga kwa sasa ipo katika mikakati ya kuboresha kikosi chake ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ndani ya klabu hiyo ili kuifanya timu hiyo iwe ya kisasa zaidi, ikiwemo suala zima la usajili.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Katibu wa Rostam, Abbas Gulamali (huyu ni mtu mwingine, siyo yule marehemu), amesema kuwa, bilionea huyo alikuwa na mpango wa kuwekeza ndani ya klabu hiyo lakini muingiliano wa watu wengi uliojitokeza ndani ya klabu ndiyo uliosababisha kumrudisha nyuma.

“Kweli Rostam alikuwa anahitaka kuwekeza ndani ya Klabu ya Yanga, lakini aliamua kuachana na suala hilo baada ya kuona kuna muingiliano wa watu wengi, hivyo ameamua kukaa pembeni. “Lakini atakuwa anatoa misaada kama kawaida watakayokuwa wakiihitaji Yanga, hakutakuwa na shida yoyote, na yeye ni mwanachama halali wa Klabu ya Yanga,” alisema Gulamali.
Tangu kuondoka kwa Manji kumekuwa na anguko kubwa la kiuchumi ndani ya Yanga hadi kufikia hatua ya kuanza kutembeza bakuli lakini inaonekana uongozi mpya uliochaguliwa Jumapili iliyopita, umekuja na neema.

Kwa mamilioni ya msaada ambayo Rostam anatarajiwa kuyatoa kwa Yanga, inawezekana kabisa ukawa ni mwisho wa Yanga kujiendesha kwa mtindo wa kutembeza bakuli. Rostam Novemba 2018 aliweka wazi mbele ya Rais John Pombe Magufuli kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa Yanga.
Rostam ni bilionea mwenye mchango mkubwa sana katika michezo na mambo yake mengi amekuwa akiyafanya kimyakimya bila kutaka kujulikana.
Chanzo: CHAMPIONI ( GPL )

Yanga kuivaa Ruvu Shooting kesho, Chikupe kukosa

Mabingwa wa kihistoria Yanga kesho Jumanne watashuka kwenye uwanja wa Uhuru kuikabili Ruvu Shooting katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara hatua za lala salama


Baada ya kupoteza michezo miwili iliyopita dhidi ya Lipuli Fc (FA) na Biashara United, vijana wa Mwinyi Zahera wamepania kuondoka na alama zote tatu dhidi ya Ruvu Shooting

Kwenye mchezo wa kesho Yanga itamkosa beki wake Andrew Vicent mwenye kadi tatu za njano
Hata hivyo Yanga haina hofu ya kukosekana kwake kwani beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ yupo

Yanga imebakisha michezo mitatu ya kumaliza msimu na yote itapigwa kwenye uwanja wa Uhuru

TETESI ZA USAJILI YANGA: Makambo atengewa Sh228 million

SAWA msimu ujao wa kimataifa, Yanga ni kama haina chake vile kwani tayari tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika ilishaipoteza mbele ya Lipuli Iringa, ila hilo halijaufanya uongozi wa klabu hiyo kuacha kujipanga kukisuka upya kikosi chake kwa msimu ujao wa michuano ya ndani.
Lakini katika ya mipango yake hiyo ya kufanya usajili mzito habari mbaya ni kwamba moja kati ya klabu za Afrika kuhitaji saini ya straika wake matata, Heritier Makambo na kama kocha wake, Mwinyi Zahera atakubali, basi jamaa hatabaki Jangwani.
Taarifa ambazo uongozi wa Yanga unazifanya kuwa siri kubwa ni juu ya ofa hiyo ambayo imetua klabuni hapo hivi karibuni ikimtaka mshambuliaji huyo raia wa DR Congo, lakini Mwanaspoti limefanikiwa kupenyezewa bila chenga juu ya mchongo huo.
Bosi mmoja wa Yanga ameliambia Mwanaspoti, Makambo ana ofa ya sio kwenda kujaribiwa, bali ni kuuzwa, huku klabu hiyo (ikifichwa jina lake) ikitaka kutoa kiasi kisichopungua Dola 100,000 (zaidi ya Sh.228 milioni).

Dau hilo sasa lipo mezani kwa Yanga likisubiri kujua kipi kitaamuliwa na Kocha Zahera ambaye ndiye aliyemshusha nchini mwishoni mwa msimu uliopita akitokea kwao, DR Congo.

Hata hivyo, kitu pekee ambacho Zahera na mabosi wa klabu hiyo wanaweza kukitumia ni kusalia kwa mkataba wa mwaka mmoja ambapo kama wataendelea kuitingisha klabu hiyo inaweza kuongeza mzigo zaidi.
Bosi huyo (jina tunalo) alisema haoni kama Yanga itapata hasara kwa kuchukua kiasi hicho kutokana na klabu hiyo kutumia kiasi kidogo kumpata mshambuliaji huyo aliyetokea DC Motema Pembe baada ya kuvunja mkataba.

“Makambo anatakiwa na klabu moja sitaki kukutajia kwa sasa kwa vile mambo hayajakamilika na iko tayari kutoa kiasi cha Dola 100,000” alisema bosi huyo ambaye alihusika kwa kiasi kikubwa katika usajili wake.

“Tunachosubiri ni jibu na uamuzi wa Kocha Zahera ambaye kimsingi ndiye mwamuzi kiufundi, lakini kwa kiasi hicho au hata zaidi sioni kama ni shida kwa Yanga naona ni faida kwa kuwa tulimpata kwa bei rahisi kupitia mpango wetu wa kuepuka usajili wa gharama kubwa.
“Kwa sasa uamuzi upo kwa Zahera na hata uongozi mpya chini ya Mwenyekiti Dk. Mshindo Msolla kama watakubaliana sawa.”
Hata hivyo, aliongeza, licha ya ofa hiyo ambayo ipo wazi zaidi lakini wakala wa mchezaji huyo ambaye anaishi Afrika Kusini ana ofa tatu za majaribio za mshambuliaji huyo.
“Hiyo ni ofa ambayo imejitosheleza na tuliwaambia wasubiri kwanza amalize ligi kwa kuwa hatukutaka achanganyikiwe wakati ule tulipokuwa tunacheza mechi muhimu za Kombe la FA.
“Unajua wachezaji wa Kikongomani wanaposikia wanahitajika sehemu ni habari kubwa kwao, unaweza kuona hata uwezo wake uwanjani unapungua sasa tusubiri kuona kipi kitaamuliwa na uongozi.”

Makambo tangu atue Yanga msimu huu amefanikiwa kuifungia timu yake mabao 16 katika Ligi Kuu, huku akifunga mengine manne katika michuano ya Kombe la FA ambapo Vijana wa Jangwani waling’olewa hatua ya nusu fainali za Lipuli FC katika Uwanja wa Samora, Iringa.

Straika huyo pia ameweza kunyakua tuzo mbili mfululizo za Mchezaji Bora wa Miezi ya Novemba na Desemba na kuisaidia Yanga kukaa kileleni kwa muda mrefu kabla ya juzi Jumatano kushushwa na Simba.

YANGA YAKUBALI KICHAPO CHA BAO 1-0 DHIDI YA BIASHARA

Yanga imeshindwa kutamba mbele ya Biashara United leo baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara uliopigwa uwanja wa Karume


Bao pekee la Biashara United lilifungwa kwenye dakika ya 8 na Tariq Kiakal baada ya kuwazidi maarifa walinzi wa Yanga waliokuwa wakidhani ameotea
Ulikuwa ni mchezo uliotawaliwa na Biashara United kwa muda mwingi huku mazingira ya uwanja wa Karume yakitajwa kuwa kikwazo kikubwa kwa Yanga

Aidha mvua iliyonyesha wakati mchezo huo ukiendelea iiufanya uwanja uwe na mazingira magumu zaidi mpira kuchezeka kwa upande wa Yanga huku wenyeji wao wakionekana kuzoea hali hiyo
Baada ya mchezo huo Yanga inarejea jijini Dar es salaam kumalizia michezo mitatu iliyobaki

Aidha watani zao Simba nao wameendeleza uteja mbele ya Kagera Sugar baada ya kukabali kipigo cha bao 1-0 kwenye mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru

Sababu ya Ajib kuachwa Dar yatajwa

Kikosi cha Yanga kiko mkoani Mara ambapo kesho kitashuka katika uwanja wa Karume kuikabili Biashara United katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Hata hivyo Yanga ilisafiri bila ya nahodha wake Ibrahim Ajib ambaye aliondolewa kwenye kikosi baada ya kuugua ghafla

Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh amesema Ajib alipata maradhi wakati wakiwa kambini usiku wa kuamkia jana ambapo alipatiwa huduma ya kwanza na Dk Edward Bavu kabla ya kukimbizwa Hospitalini

Hafidh amesema hali ya kiungo huyo kinara wa kutoa pasi za mabao ligi kuu ya Tanzania Bara, inaendelea vizuri

Yanga iliwasili Musoma jana na kupokelewa kwa shangwe na mamia ya mashabiki wa timu hiyo

Makocha Yanga, Stand United na Mbeya City wapelekwa Kamati ya Nidhamu TFF

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imewasilisha malalamiko mbalimbali ya kinidhamu dhidi ya viongozi, makocha na wachezaji kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Walalamikiwa ni kutoka katika klabu za Ligi Kuu ya Tanzania (TPL), na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Makocha waliolalamikiwa ni Athuman Bilal wa Stand United, Mwinyi Zahera (Yanga), Nassoro Mrisho (Geita Gold FC), na Ramadhani Nsanzurwimo (Mbeya City).

Viongozi ni Herry Chibakasa wa Friends Rangers FC, Mohamed Hussein (Kagera Sugar FC),Walter Harrison (KMC) na Hussein Salehe wa Geita Gold FC wakati mchezaji aliyelalamikiwa ni Deus Tulusubya wa Pamba SC.

Kamati ya Nidhamu ya TFF itakutana Mei 12,2019

Fei Toto atakiwa Uingereza

Hivi karibuni kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Emmanuel Amunike alimwagia sifa kiungo wa Yanga Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuwa anaweza kucheza soka barani Ulaya akiitaja FC Barcelona kuwa ni timu ambayo anaweza kucheza kabisa

Inaelezwa klabu ya Yanga imepokea maombi kutoka klabu moja ya Uingereza ambayo inamuhitaji Fei Toto akafanye majaribio

Timu hiyo ambayo haikuwekwa hadharani, imedhamiria kumsajili Fei Toto kama atafuzu majaribio hayo

Fei Toto aliyetua Yanga mwaka jana, amekuwa katika kiwango bora, akijihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Mwinyi Zahera

Inaelezwa Yanga imejipanga kusajili kiungo mwingine ikitokea Fei Toto atafanikiwa kutimkia Uingereza

Tumetolewa FA, tutaendelea kupambana kwenye ligi – Zahera

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema baada ya kupoteza mchezo wa nusu fainali kombe la FA kwa kufungwa mabao 2-0 na Lipuli Fc leo, wanahamishia nguvu zao kwenye ligi kuhakikisha wanashinda michezo minne iliyobaki

Zahera amesema licha ya kutofanikiwa kutinga fainali, msimu huu wamevuka malengo na matarajio ya awali

“Hakuna kitu kitabadilika juu ya mipango yetu, tunahitaji kushinda mechi nne zilizobakia ligi kuu,” amesema Zahera

“Ukiangalia mpaka hapa tumefanikiwa kuliko matarajio. Mwaka huu tulianza ligi tukiomba mungu atusaidie japo tumalize nafasi ya sita au ya saba”

“Tulipaswa kumaliza nafasi ya sita au saba kutokana na changamoto tulizopitia msimu huu. Tulikubaliana tufanye nguvu tusimalize chini ya nafasi ya kumi”

“Mkiangalia tunaongoza ligi tokea mwanzo wa msimu mpaka leo. Malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi na hata kombe la FA yalikuja baada ya kuona tumeweza kufanya vizuri licha ya changamoto zilizokuwa zinatukabili”

“Kazi waliyofanya wachezaji wangu ni nzuri sana. Tutaendelea kupambana kwenye ligi ili tuweze kushinda michezo yote minne iliyobaki”

Aidha akizungumzia mabadiliko aliyofanya kwenye kipindi cha pili amesema ilikuwa ni kazima kuwatoa Ajib na Mohammed Issa na kuwaingiza Tambwe na Juma Abdul ili kwendana na aina ya uchezaji wa Lipuli Fc

“Lipuli walikuwa wengi katikati hivyo nililazimika kumuingiza Tambwe na Abdul ili kutumia mipira ya krosi kupitia pembeni kujaribu kusaka mabao ya kusawazisha”

“Mfumo huo ulitusaidia kwani tulipata karibu nafasi tatu za kuweza kufunga lakini tulikosa bahati”