Mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Baraka Igangula amesema kama atachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, atahitaji miezi mitatu tu kukamilisha ukarabati wa uwanja wa Kaunda ambao unamilikiwa na Yanga
Aidha Igangula anayechuana na Dk Mshindo Msolla, Dr Jonas Tiboroha na Elias Mwanjala kuwania uwenyekiti wa Yanga, amesema kutokana na uzoefu mkubwa aliyokuwa nao kwenye uongozi wa Yanga, ana lengo la kuifanyia timu hiyo mambo makubwa na kamwe hataweka mbele maslahi binafsi
“Tutakuwa na mpango wa muda mfupi ambao tutaukarabati uwanja wetu pale klabuni, huku tukiwa na mpango wa muda mrefu wa kujenga uwanja nje ya mji, hata ikiwezekana Kibaha, Pwani ambao utakuwa na hosteli, maduka na ofisi mbalimbali,” amesema Igangula
Igangula pia ameunga mkono mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa Yanga akiahidi kulikamilisha zoezi hilo haraka
“Nitasimamia mchakato wa mabadiliko na kuhakikisha unakamiliki punde tu nitakapoingia madarakani. Nitaajiri wataalamu wenye ujuzi wa masuala ya kampuni ili tuachane na utaratibu huu wa kuendesha klabu kwa mazoea”
Ahadi nyingine alizotoa Igangula ni kuanzisha bima ya afya itakayowalenga wanachama, saccos, vicoba na mfuko wa kufa na kuzikana, kama sehemu ya kuimarisha umoja, upendo na mshikamano baina ya wanachama na viongozi wa Yanga
Pia atahakikisha wachezaji na benchi la ufundi wanalipwa mishahara kwa wakati, kusimamia mikataba na mapato ili kudhibiti ufisadi
Uchaguzi wa Yanga utafanyika Jumapili, May 05 ukumbi wa bwalo la Polisi, Osterbay jijini Dar es salaam