YANGA: Yaingia Kambini Kuiwinda KMC

Kikosi cha vinara wa ligi kuu ya Tanzania Bara Yanga kinaingia kambini leo katika Hotel ya Nefaland kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya KMC

Mchezo huo utapigwa keshokutwa Jumapili, March 10 2019 saa kumi kamili jioni katika uwanja wa Taifa

Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh amesema wachezaji 20 wanatarajiwa kuingia kambini leo jioni kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo huo

Tangu irejee kutoka Mwanza ambako iliichapa Alliance Fc bao 1-0, Yanga imekuwa ikijifua kwenye uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar es salaam

DISMAS TEN: Afunguka kuhusu Usajili wa NDEMLA

Kwa siku za karibuni kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Msemaji wa klabu ya Yanga Dismas Ten amekuwa akimposti kiungo wa Simba Said Khamis Ndemla huku akiweka jumbe zinazoashiria kuwa huenda mabingwa hao wa kihistoria wanaiwania sahihi ya kiungo huyo kwa ajili ya msimu ujao

Ndemla nusura asajiliwe na Yanga katika usajili wa mwanzoni mwa msimu huu kabla hajaamua kubaki Simba kwa kuongeza mkataba wa mwaka mmoja

Jana Ten alifunguka kuhusu tetesi za Yanga kumuwania Ndemla ambapo amekiri kuwa kiungo huyo ana uwezo mkubwa lakini ana bahati mbaya hapati nafasi katika klabu yake ya Simba

“Ndemla ni mchezaji mzuri sana. Mtu yeyote ukimuuliza katika wachezaji wa Tanzania wenye vipaji hawezi kukosa kumtaja Ndemla,” amesema Ten

“Ndemla mimi ni rafiki yangu, suala la kusajili au kutosajiliwa na Yanga hilo linahusu benchi la ufundi na Kamati yetu ya usajili. “

“Yote yanaweza kusemwa mwisho wa msimu lakini kwa sasa hivi huwezi kuzungumza lolote lakini anabaki kuwa ni mchezaji mwenye kipaji na kila mtu anaona”

“Amekuwa ni mchezaji mwenye mwenendo mzuri licha ya kuwa sasa hapati nafasi kwenye timu yake”

Wakati msimu ukielekea ukingoni tayari timu zimeanza ‘kupigana vikumbo’ kuwania wachezajia ambao mikataba yao inaelekea ukingoni

ZAHERA: Michango ya Wanayanga Ipo SALAMA

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amewahakikishia wapenzi, mashabiki na Wanachama wa klabu ya Yanga kuwa pesa wanazoichangia timu yao ziko salama na wapuuze taarifa zinazosambazwa zinazodai kuwa kuna fedha zimetolewa ‘kinyemela’

Akizungumza mapema leo katika mazoezi ya Yanga yanayofanyika uwanja wa chuo cha Polisi, Kurasini jijini Dar es salaam, Zahera amesema wanaotoa taarifa hizo wana lengo la kuwavunja moyo Wana Yanga ili wasiendelee kuichangia timu yao

“Nawaambia watu wengi wanapenda timu yetu iharibike. Kuna watu wanafanya matangazo mengi ya kusema kama mchango unaofanyika viongozi wanakula pesa”

“Wanasema kuna viongozi wanakula milioni tatu, ni uongo. Hakuna hata elfu moja, senti moja ambayo inatoka katika pesa hiyo ambayo watu wanachangia.” amesema Zahera

“Hakuna hata kiongozi mmoja ambaye ana ruhusa ya kugusa iyo pesa”

Naye nahodha wa Yanga Ibrahim Ajib amesema hakuna namna yoyote ambayo fedha hiyo inaweza kutolewa bila kuidhinishwa na watia saini watatu ambao ni yeye(Ajib), Kocha Mwinyi Zahera na Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh

“Kama fedha inatakiwa kutolewa ni lazima wote watatu tusaini, hivyo taarifa inayosambazwa ni uongo kwani jambo hilo haliwezekani”

Jana kupitia Redio One, mtu aliyejitambulisha kama mwanachama wa Yanga Suleiman Kato alidai kiasi cha pesa milioni tatu zilizochangwa na mashabiki wa Yanga kupitia mitandao ya simu zilitolewa kwenye mtandao husika na kuhamishiwa kwenye Bank moja iliyopo Kariakoo ambapo aliwatuhumu Kaimu katibu Omary Kaaya pamoja na Mhasibu na baadhi ya viongozi kushirikiana katika hujuma hiyo

Breaking News: Ephraim KIBONDE wa CloudsFm Amefariki Dunia Leo

Taarifa iliyotufikia muda huu ni kwamba Mtangazaji wa Clouds FM, Ephraim Kibonde amefariki dunia leo Machi 7, 2019.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amethibitisha kwamba Kibonde amefariki akiwa Mwanza, alianza kusumbuliwa na Presha toka Bukoba kwenye msiba wa Ruge Mutahaba na kuhamishiwa Mwanza.


Aidha, siku chache zilizopita, Clouds Media iliondokewa na mkurugenzi wake wa vipindi, Ruge Mutahaba aliyezikwa nyumbani kwao wilayani Bukoba mkoa wa Kagera.

Soka Updates inatoa pole kwa CLOUDS MEDIA GROUP.

Amunike kutangaza kikosi cha Stars kesho

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itachuana na Uganda March 24 2019 katika mchezo wa kusaka tiketi ya kutinga fainali za michuano ya AFCON 2019 itakayofanyika mwezi Juni nchini Misri

Kocha Mkuu wa Stars Emmanuel Amunike kesho Ijumaa March 08 anatarajiwa kutangaza kikosi cha Stars

Hatuwahofii Alliance Fc, tukutane Mwanza -Dismas Ten

Misimu miwili iliyopita Yanga ilitolewa kwenye michuano ya kombe la Azam (ASFC) na Mbao Fc katika hatua ya nusu fainali ambapo mchezo ulipigwa dimba la CCM Kirumba

Yanga itarudi tena Mwanza katika uwanja huohuo kuikabili Alliance Fc lakini ikiwa ni mchezo wa hatua ya robo fainali

Afisa Habari wa Yanga Dismas Ten amesema hawana hofu ya kuikabili Alliance Fc kwa mara nyingine na watajiandaa kikamilifu ili waweze kushinda mchezo huo na kutinga hatua ya nusu fainali

Baada ya kukosa ushindi kwa misimu kadhaa kwenye dimba la CCM Kirumba, msimu huu Yanga imetakata katika dimba hilo kwa kufanikiwa kuzifunga Mbao Fc na Alliance

“Tunafahamu Mwanza ni pagumu, ili kupata ushindi kwenye uwanja wa CCM Kirumba unapaswa kuwa umejiandaa kwelikweli,” amesema Ten

“Msimu huu tumefanya vizuri katika michezo yote miwili tuliocheza Mwanza, naamini tunao uwezo wa kupata matokeo kwa mara nyingine”

“Tunaiheshimu Alliance, tunafahamu ni timu nzuri lakini kucheza na Yanga ni kitu tofauti”

Kama Yanga itashinda mchezo huo utakaopigwa kati ya March 25-28, kwenye hatua ya nusu fainali itachuana na mshindi kati ya Lipuli Fc dhidi ya Singida United, mchezo ambao utakuwa wa ugenini

Mchezo wa fainali utapigwa uwanja wa Ilulu mkoani Lindi mwishoni mwa msimu