YANGA YAUTUMIA UWANJA WA UHURU VIZURI, YAICHAPA RUVU SHOOTING BAO 1-0

Yanga imerejea kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru


Bao pekee la Yanga lilifungwa na Papi Tshishimbi aliyemalizia pasi murua ya Deus Kaseke kwenye dakika ya 16
Hilo lilikuwa bao la nne kwa Tshishimbi kwenye ligi msimu huu

Yanga ilikuwa bora kwenye kipindi cha kwanza na ilistahili kwenda mapumziko na angalau mabao mawili kama Raphael Daud asingekosa nafasi ya wazi
Ushindi huo umeifanya Yanga ifikishe alama 83 na kuiondoa Simba kileleni mwa msimamo wa ligi

Simba itacheza na Mtibwa Sugar keshokutwa Alhamisi katika mchezo ambao kama haitapata ushindi huenda ikafufua matumaini ya Yanga kwenye mbio za ubingwa

Mo Simba awards kutolewa May 30 2019

Hafla ya utoaji Tuzo za Mo Simba 2019 itafanyika siku ya Ijumaa Mei 30, 2019 katika hoteli ya Hyatt Regency, The Kilimanjaro iliyopo Jijini Dar es Salaam

Tuzo za mwaka huu zitahusisha wachezaji na mashabiki wa Simba ambao juhudi zao zimesaidia kupatikana kwa mafanikio makubwa msimu huu

Tuzo hizo zitakuwa na vipengele 11 ambavyo ni Mchezaji Bora, Goli Bora, Golikipa Bora, Beki Bora, Kiungo Bora na Mshambuliaji Bora

Nyingine ni Mchezaji Bora Mwanamke, Mchezaji Bora Mdogo, Shabiki Bora, Tuzo ya Heshima na Mhamasishaji Bora katika mitandao ya kijamii

Simba kurejea dimba la Uhuru Alhamisi, kuikabili Mtibwa Sugar

Baada ya kulazimishwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya Azam Fc jana, Simba itarejea tena uwanja wa Uhuru keshokutwa Alhamisi, May 16 kuikabili Mtibwa Sugar

Katika michezo miwili iliyopita Simba imepoteza alama tano, mabingwa hao watetezi wanahitaji kushinda mchezo huo

Simba haikuwa imecheza na Mtibwa Sugar msimu huu, huo utakuwa mchezo wa duru ya kwanza na timu hizo zitarudiana May 28 siku ya kuhitimisha ligi kuu msimu huu

Katika michezo mitano iliyobaki, miwili ni dhidi ya Mtibwa na mingine mitatu ni dhidi ya Biashara United (nyumbani), Ndanda Fc (nyumbani) na Singida United (ugenini)

Simba inahitaji kukusanya angalau alama nane kuweza kutetea ubingwa wake

Sare dhidi ya Azam Fc haikubadili mipango yetu – Aussems

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema licha ya timu yake kulazimishwa suluhu ya bila kufungana na Azam Fc, hakuna kilichobadilika juu ya mpango wa kutetea ubingwa

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya mchezo, Aussems alisema timu yake ilifanya jitihada zote za kusaka ushindi kwenye mchezo huo lakini walikosa bahati

Aidha amekosoa mbinu waliyotumia Azam FC kuwa hawakuwa na lengo la kushinda

“Tumejaribu kila mbinu kuweza kupata ushindi lakini imeshindikana. Sisi tulihitaji kushinda mchezo huu lakini mwenzetu walikuja kusaka alama moja na wameipata,” amesema

“Hata hivyo matokeo haya hayabadili chochote katika mipango yetu ya kutetea ubingwa”

Simba imeendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imefikisha alama 82

Bado hesabu za ubingwa ziko upande wao kwani wanahitaji alama nane tu ili kutawazwa mabingwa kwa msimu wa pili mfululizo

Simba imebakisha michezo mitano

SIKU CHACHE BAADA YA UCHAGUZI…BILIONEA MPYA AIBUKA YANGA

BILIONEA maarufu hapa nchini, Rostam Azizi imeelezwa kuwa amekusudia kuisaidia Yanga kwa kuipa misaada ya kifedha pale inapowezekana. Hii inakuja siku chache tu baada ya Yanga kufanya uchaguzi na kupata viongozi wapya chini ya mwenyekiti, Dk Mshindo Msolla na makamu wake, Frederick Mwakalebela aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Rostam amekuwa akitajwa mara nyingi na baadhi ya wadau wa soka kuwa anatarajia kuwekeza ndani ya Klabu ya Yanga baada ya kuondoka aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji. Klabu ya Yanga kwa sasa ipo katika mikakati ya kuboresha kikosi chake ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ndani ya klabu hiyo ili kuifanya timu hiyo iwe ya kisasa zaidi, ikiwemo suala zima la usajili.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Katibu wa Rostam, Abbas Gulamali (huyu ni mtu mwingine, siyo yule marehemu), amesema kuwa, bilionea huyo alikuwa na mpango wa kuwekeza ndani ya klabu hiyo lakini muingiliano wa watu wengi uliojitokeza ndani ya klabu ndiyo uliosababisha kumrudisha nyuma.

“Kweli Rostam alikuwa anahitaka kuwekeza ndani ya Klabu ya Yanga, lakini aliamua kuachana na suala hilo baada ya kuona kuna muingiliano wa watu wengi, hivyo ameamua kukaa pembeni. “Lakini atakuwa anatoa misaada kama kawaida watakayokuwa wakiihitaji Yanga, hakutakuwa na shida yoyote, na yeye ni mwanachama halali wa Klabu ya Yanga,” alisema Gulamali.
Tangu kuondoka kwa Manji kumekuwa na anguko kubwa la kiuchumi ndani ya Yanga hadi kufikia hatua ya kuanza kutembeza bakuli lakini inaonekana uongozi mpya uliochaguliwa Jumapili iliyopita, umekuja na neema.

Kwa mamilioni ya msaada ambayo Rostam anatarajiwa kuyatoa kwa Yanga, inawezekana kabisa ukawa ni mwisho wa Yanga kujiendesha kwa mtindo wa kutembeza bakuli. Rostam Novemba 2018 aliweka wazi mbele ya Rais John Pombe Magufuli kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa Yanga.
Rostam ni bilionea mwenye mchango mkubwa sana katika michezo na mambo yake mengi amekuwa akiyafanya kimyakimya bila kutaka kujulikana.
Chanzo: CHAMPIONI ( GPL )

SIMBA YASHINDWA KUFURUKUTA MBELE YA AZAM FC WATOKA SARE TASA

Mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya Simba dhidi ya Azam Fc umemalizika kwa timu hizo kugawana pointi baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana


Simba ilitawala mchezo huo hata hivyo Azam Fc waliotumia mbinu ya kujihami zaidi, walikuwa imara katika kujilinda
Ni matokeo ambayo bado yanaiweka Simba kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama mbili dhidi ya Yanga

Simba imefikisha alama 82 wakati Yanga ina alama 80 na Azam Fc ikifikisha alama 69
Simba inahitaji alama nane katika michezo mitano iliyobaki ili kuweza kutetea ubingwa