Wadau wa Simba Morogoro wapongezwa kwa ukarabati uwanja wa Jamhuri

Simba itaweka makazi ya muda mkoani Morogoro ikitumia uwanja wa Jamhuri kwa baadhi ya michezo yake ya ligi wakati wote ambao uwanja wa Taifa utakuwa umefungwa

Katika kuhakikisha uwanja huo unakuwa na hali nzuri, wanachama na mashabiki wa klabu ya Simba mkoani Morogoro walijitolea kuufanyia ukarabati

Ukarabati uliofanywa ni pamoja na kun’goa magugu, kujaza vifusi sehemu zenye mashimo na kuotesha nyasi pamoja na kumwagilia katika kipindi cha wiki tatu zilizopita

Pia ukarabati umefanywa kwenye vyoo na vyumba vya kubadilishia nguo

Meneja wa uwanja huo John Simkoko amewapongeza Wanasimba kwa jitihada zao za kuuboresha uwanja huo

Simba itaanza rasmi kuutumia uwanja wa Jamhuri kama uwanja wake wa nyumbani kesho Jumapili itakapochuana na Mbao Fc katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara

FT : Alliance 1-1 Yanga, mikwaju ya penati 4-3 yaipeleka Yanga nusu fainali

Mabingwa wa kihistoria Tanzania, Yanga wametinga nusu fainali ya kombe la FA (ASFC) baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penati 4-3 kufuatia matokeo ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Alliance Fc

Yanga ilitangulia kupata bao la kuongoza kwenye dakika ya 39 likiwekwa kambani na Heritier Makambo kwa kombora la nje ya 18

Alliance Fc iliyokuwa kwenye kiwango bora ilisawazisha bao hilo kwenye dakika ya 62 kupitia kwa Joseph James

Baada ya kumalizika kwa dakika 90 huku matokeo yakiwa 1-1, changamoto ya mikwaju ya penati ikatumika kuamua mshindi

Deus Kaseke, Paulo Godfrey, Thabani Kamusoko na Haruna Moshi ndio waliofunga penati za Yanga wakati Kelvin Yondani na Mrisho Ngasa walikosa

Yanga sasa itachuana na Lipuli Fc kwenye mchezo wa nusu fainali

Niyonzima ampagawisha Aussems, aapa kumbakisha Simba

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema anajivunia uwepo wa kiungo Haruna Niyonzima katika kikosi chake na amesisitiza kiungo huyo hatauzwa

Katika siku za karibuni Niyonzima ameonekana kufanya vyema hali inayoashiria amerejea katika kiwango chake cha zamani

Ukizungumzia ushindi wa mabao 2-1 iliyopata Simba dhidi ya AS Vita na kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, ni lazima utaje jina la Niyonzima kwani alikuwa miongoni mwa wachezaji waliojituma zaidi katika mchezo huo

Aussems amefichua kuwa wakati alipokutana na Niyonzima kwa mara ya kwanza baada ya kuanza kuinoa Simba, alibaini kiungo huyo alikuwa amekata tamaa

Aussems amesema alifanya kazi ya ziada kumrejesha nahodha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Rwanda katika kiwango chake baada ya kubaini ni mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu

Anaamini uongozi wa Simba utamuongezea mkataba kwani ni miongoni mwa wachezaji anaowahitaji kwa ajili ya msimu ujao

Yanga yajifua Mwanza tayari kuikabili Alliance Fc

Kikosi cha Yanga jana jioni kilifanya mazoezi kwenye uwanja wa Chuo cha Ualimu Butimba kujiandaa na mchezo wa robo fainali kombe la FA (ASFC) dhidi ya Alliance Fc

Mchezo huo utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa CCM Kirumba

Vinara hao wa ligi kuu ya Tanzania Bara walitua jana asubuhi jijini Mwanza wakiongozwa na kocha Mwinyi Zahera

Jioni ya leo Ijumaa Yanga inatarajiwa kufanya mazoezi yake ya mwisho kwenye dimba la CCM Kirumba tayari kwa mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na wakazi wa jiji la Mwanza na maeneo ya jirani

Robo fainali ya tatu kombe la FA kupigwa leo, Yanga kesho

Michuano ya kombe la FA (ASFC) hatua ya robo fainali inaendelea leo kwa mchezo kati ya Kagera Sugar dhidi ya Azam FC utakaopigwa uwanja Kaitaba

Huo utakuwa mchezo wa tatu wa robo fainali baada ya juzi kuzishuhudia Lipuli Fc na KMC kutinga nusu fainali baada ya kushinda michezo yao

Kesho Jumamosi Yanga itakamilisha hatua hiyo ya robo fainali kwa kuumana na Alliance Fc katika mchezo utakaopigwa dimba la CCM Kirumba

Mshindi wa mchezo kati ya Kagera Sugar dhidi ya Azam Fc atachuana na KMC kwenye mchezo wa nusu fainali wakati mshindi wa mchezo wa kesho kati ya Alliance Fc dhidi ya Yanga, ataumana na Lipuli Fc kwenye mchezo wa nusu fainali

Simba yaifuata Mbao Fc Morogoro

Msafara wa kikosi cha Simba umeondoka jijini Dar es salaam asubuhi ya leo Ijumaa, kuelekea Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mbao FC ambao utapigwa siku ya Jumapili kwenye uwanja wa Jamhuri

Leo jioni Simba inatarajiwa kufanya mazoezi yake ya kwanza katika uwanja wa Jamhuri ambao uongozi wa timu hiyo uliufanyia ukarabati wa sehemu ya kuchezea ‘pitch’

Baada ya mchezo dhidi ya Mbao Fc, Simba itaendelea kubaki mkoani Morogoro kuendelea na maandalizi ya mchezo wa robo fainali ligi ya mabingwa dhidi ya TP Mazembe