Uganda, Kenya, Burundi zatangulia AFCON 2019, Stars zamu yetu leo

Timu ya Taifa ya Burundi jana iliandika historia ya kukata tiketi ya kushiriki fainali za AFCON 2019 kwa mara ya kwanza baada ya kutoka sare ya ao 1-1 dhidi ya Togo matokeo ambayo yamewapa nafasi ya kwenda Misri

Burundi imeungana na Uganda na Kenya kuwa timu kutoka Afrika Mashariki ambazo zimefuzu kwa fainali hizo zitakazopigwa mwezi Juni mwaka huu

Leo Tanzania inaweza kuwa timu ya nne kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kufuzu kwa fainali za michuano hiyo kama itapata ushindi dhidi ya Uganda huku ikiomba matokeo mabaya kwa Lesotho

Ni mchezo wa ‘kufa au kupona’ kwa Stars ambayo inajaribu kurudia kile ilichokifanya miaka 39 iliyopita kwa kutinga fainali za michuano hiyo zilizofanyika Nigeria mwaka 1980

Mchezo dhidi ya Uganda utapigwa saa 12 jioni sambamba na mchezo mwingine wa kundi L kati ya Cape Verde dhidi ya Lesotho

Kila la kheri Stars…!

SAMATTA : Aahidi kuibeba TAIFA STARS

Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Mbwana Samatta amesema wachezaji wa timu hiyo leo wana kazi moja tu ya kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Uganda kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za michuano ya AFCON 2019

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji baada ya kutembelewa na Waziri Mkuu katika kambi ya kikosi cha Stars, Samatta amesema wanajiona kuwa na deni kubwa kwa Watanzania na watahakikisha wanawapa furaha kwa kupata ushindi leo

“Naona naenda kuiongoza nchi siku ya kesho (leo), sitakuwa nahodha kwa ajili ya wachezaji peke yake bali nitakuwa nahodha kwa ajili ya wananchi wote wa Tanzania,” amesema Samatta

“Wachezaji wote wako tayari kwa ajili ya kuitetea nchi yao, lengo kubwa ni kuhakikisha bendera yetu ya Tanzania inasimama, Dunia itambue na Afrika yote ifahamu”

Jana Waziri Mkuu Mh Kassim Majaliwa alitembelea kambi ya wachezaji wa timu ya Taifa na kuwaeleza kwamba Serikali na wananchi wanamatumaini makubwa kwa timu yao, hivyo wahakikishe wanapata ushindi katika mechi yao dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda leo

“Macho yote ya Watanzania yameelekezwa katika mechi ya kesho (leo) na Serikali inamatumaini makubwa na timu ya Taifa, hivyo muelewe kwamba kesho (leo) ni siku muhimu sana. Lengo letu ni kufikia hatua ambayo mataifa mengine yamefikia”

Taifa STARS : Kupewa Mamilioni Wakiifunga UGANDA | TAIFA

Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kamati yake itatoa shilingi. milioni 10 kwa kila mchezaji wa timu hiyo iwapo timu itafuzu kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika #AFCON2019

Makonda amesema Watanzania wanachokijua kwa sasa ni kwamba AFCON 2019 ni zamu yao, hivyo amewaomba wachezaji wa timu ya Taifa wahakikishe wanawapa furaha kwa kuifunga timu ya Taifa ya Uganda na kwamba wananchi wengi wamehamasika kwenda kuwashangilia.
#zamuyetuafcon2019🇹🇿

Nitakuwepo uwanjani kuiunga mkono Stars – Tshabalala

Nahodha Msaidizi wa kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ amesema ataungana na mashabiki wa soka nchini kwenda uwanjani kesho kuiunga mkono Stars itakapokuwa ikichuana na Uganda Cranes

Tshabalala amesema anaamini kikosi kilichochaguliwa na kocha Emmanuel Amunike ni kizuri na kitaweza kuipa Tanzania matokeo inayohitaji ili iweze kufuzu kwa fainali za AFCON 2019

“Nitakuwepo uwanjani kesho kuwasapoti ndugu zangu, marafiki zangu, kaka zangu kuwapa hamasa ili waweze kupata matokeo chanya katika mchezo huo”

Tshabalala amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa kesho kuhakikisha lengo la kushinda mchezo huo linafanikishwa

Mchezo dhidi ya Uganda umepewa hamasa ya kipekee na wadau wa nyanja zote nchini kutokana na umuhimu wake

Baada ya kukosa kushiriki fainali za AFCON kwa miaka 39, Stars inaweza kupata nafasi ya kushiriki fainali hizo mwaka huu zitakazofanyika nchini Misri kama itaweza kuifunga Uganda

SAMATTA: Kuiongoza STARS Kusaka.Ushindi Kesho

Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Mbwana Samatta kesho Jumapili atabeba matumaini ya Watanzania kuelekea fainali za AFCON 2019 atakapokiongoza kikosi cha Stars katika mchezo dhidi ya Uganda Cranes

Samatta, kinara wa mabao ligi kuu ya Ubelgiji, amewatoa hofu Watanzania kuelekea mchezo huo akiahidi kuwa watafanya kile walichoelekezwa na Kocha Emmanuel Amunike ili waweze kuibuka na ushindi

“Tumefanya maandalizi ya kutosha. Tunafahamu mchezo hautakuwa mwepesi lakini tunayo kila sababu ya kutumia vyema uwanja wetu wa nyumbani kupata ushindi,” amesema Samatta

Matokeo ya ushindi dhidi ya Uganda yanaweza kuipa Stars nafasi ya kufuzu kwa fainali za AFCON 2019 zitakazofanyika mwezi Juni nchini Misri.

Hata hivyo ili Stars iweze kufuzu lazima Cape Verde iifunge au itoke sare na Lesotho. Mchezo baina ya timu hizo utapigwa huko Cape Verde muda sawa na mchezo kati ya Stars dhidi ya Uganda utakaopigwa saa 12 jioni

Wapinzani wa Stars, Uganda Cranes wanatarajiwa kuwasili nchini leo

Uganda iliweka kambi ya wiki moja nchini Misri kujiandaa na mchezo huo

Uganda Cranes kuwasili leo

Kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda ‘Uganda Cranes’ kinatarajiwa kuwasili leo tayari kwa mchezo dhidi ya Taifa Stars utakaopigwa kwenye uwanja wa Taifa kesho Jumapili

Mchezo huo wa kukamilisha ratiba ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za AFCON 2019, unatarajiwa kuanza saa 12 jioni

Uganda ambayo tayari imeshafuzu kushiriki fainali hizo zitakazopigwa nchini Misri mwezi Juni ikiwa kinara wa kundi L, iliweka kambi ya wiki moja jijini Cairo

Kikosi cha timu hiyo kitakachowasili leo, kinajumuisha wachezaji wawili wa Simba, Emmanuel Okwi na Juuko Murshid

MO DEWJI aiombea dua Stars

Mwekezaji wa klabu ya Simba Mohammed Dewji ‘Mo’ amewahamasisha wachezaji wa Taifa Stars kuipigania Tanzania Jumapili, wawaze kushinda mchezo dhidi ya Uganda Cranes

Mo amesema Watanzania wote tunapaswa kuwa wamoja kuelekea mchezo huo ambao Stars inahitaji kushinda ili iweze kukata tiketi ya kutinga fainali za michuano ya AFCON 2019 itakayofanyika nchini Misri baada ya kukosa michuano hiyo kwa miaka

39

Mo amewahakikishia wachezaji wa Stars kuwa Watanzania wote wako nao kwani wanashauku ya kuiona timu yao ikifuzu kwa fainali za michuano hiyo, hivyo wasiwaangushe

“Watanzania wote tupo nyuma yenu wachezaji wetu wa Taifa Stars kuhakikisha tunashinda dhidi ya Uganda, sababu zote za kufanya hivyo tunazo,” amesema

“Naamini mtashinda na kutufanya Watanzania tutembee kifua mbele. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu mfanye”

Kuelekea mchezo huo utakaopigwa keshokutwa Jumapili saa 12 jioni katika dimba la Taifa, mashabiki wametakiwa kujitokeza kwa wingi ili kuwapa sapoti wachezaji

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi katika mchezo huo ambao kiingilio ni Tsh 2000/- tu