Simba yarejea mazoezini kuiwinda Mbao Fc

Baada ya mapumziko ya sikua tano, kikosi cha Simba kimerejea mazoezini leo kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Mbao Fc

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Jumapili, March 31 na huenda ukapigwa kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro

Mazoezi ya leo yalihusisha wachezaji ambao hawakuitwa katika timu za Taifa

Zahera kuiwahi Alliance Fc

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera anatarajiwa kurejea Jumatano kuungana na kikosi cha timu hiyo kinachojiandaa na mchezo wa robo fainali kombe la FA dhidi ya Alliance Fc.

Jana Zahera akiwa kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, alikiongoza kikosi cha timu hiyo kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Liberia na kukata tiketi ya kufuzu fainali za AFCON 2019

Mwishoni mwa wiki hii Yanga itaelekea mkoani Mwanza kuikabili Alliance Fc katika mchezo utakaopigwa dimba la CCM Kirumba, March 30 2019

Kwa sasa Yanga inajifua chini ya kocha msaidizi Noel Mwandila

Serikali kutoa Sh. Bilioni moja kwa timu ya Serengeti Boys

Serikali kutoa Sh. Bilioni moja kwa timu ya Serengeti Boys

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa serikali itatoa shilingi bilioni moja kwaajili ya kuiwezesha Serengeti Boys.

Rais Magufuli amesema kuwa atatoa fedha hizo ili kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri kwenye mashindano ya Afrika kwa vijana AfconU17 yatakayofanyika nchini Tanzania mwezi Aprili mwaka huu.

Rais Magufuli amesema kuwa ataendelea kushirikiana na Wizara ya Michezo kwa kuwa Timu ya Taifa Stars imemfurahisha sana baada ya kuipiga timu ya Uganda 3 bila.

Rais Magufuli awaita wachezaji Stars Ikulu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli amewaalika Ikulu wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ pamoja na Bondia Hassani Mwakinyo aliyemtwanga Muargentina Sergio Eduardo katika pambano lililofanyika juzi nchini Kenya

Kulingana na taarifa iliyotolewa mapema leo na msemaji wa Ikulu Gerson Msigwa, Rais Magufuli atatoa pongezi kwao na kula nao chakula cha mchana

Jana Stars ilifanikiwa kufuzu fainali za AFCON 2019 baada ya kusubiri kwa miaka 39 ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uganda katika mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa

Stars yakata tiketi AFCON 2019 baada ya kuichapa Uganda 3-0

Historia imeandikwa leo katika dimba la Taifa baada ya timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kufuzu kwa fainali za AFCON 2019 kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uganda

Stars imefuzu kwa fainali hizo baada ya kusubiri kwa miaka 39

Matokeo ya suluhu ya bila kufungana kati ya Cape Verde dhidi ya Lesotho yameinufaisha Tanzania kuweza kuwa miongoni mwa timu 24 zitakazochuana nchini Misri mwezi Juni

Stars iliyokuwa katika kiwango bora, iliandika bao la kuongoza kwenye dakika ya 21 kupitia kwa Saimon Msuva aliyemalizia pasi murua ya John Bocco

Erasto Nyoni akaifungia Stars bao la pili kupitia mkwaju wa penati kwenye dakika ya 50 baada ya Samatta kumnawisha mlinzi wa Uganda ndani ya eneo la hatari

Bao lililoizamisha Uganda liliwekwa kimiani na Aggrey Morisi kwenye dakika ya 56 akimalizia krosi iliyochongwa na John Bocco

Ushindi wa Stars ulinogeshwa na idadi kubwa ya mashabiki waliofurika kuujaza uwanja wa Taifa

Kikosi cha Stars kilichoandika historia leo;

Manula, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Agrey Morris, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni , Saimon Msuva, Mudathir Yahya, John Bocco, Mbwana Samatta, Farid Mussa

AKIBA
Metacha Munata, Aron Kalambo, Ally Sonso, Kennedy Juma, Jonas Mkude, Himid Mao, Feisal Salum Fei Toto, Shiza Kichuya, Yahya Zaydi, Thomas Ulimwengu, Rashid Mandawa, ShabaanIddi Chilunda

KAPOMBE: Kurejea Kikosini SIMBA SC

Beki wa pembeni wa Simba Shomari Kapombe ameruhusiwa kuanza mazoezi mepesi tayari kurejea dimbani baada ya kupona majeraha ya goti

Hivi karibuni Kapombe alikwenda Afrika Kusini kufanyiwa uchunguzi wa jeraha alilopata wakati akiitumikia timu ya Taifa mwishoni mwa mwaka jana

Habari njema ni kwamba madaktari wameridhishwa na uponaji wa jeraha hilo hivyo kumruhusu Kapombe kuanza mazoezi mepesi

Kiraka huyo aliyekuwa nje ya dimba kwa takribani miezi mitano, anatarajiwa kuanza mazoezi mepesi wiki ijayo na huenda akarejea kikosini mapema kuwahi mchezo wa marudiano wa robo fainali ligi ya mabingwa dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa April 12 au 13 huko DR Congo

Uganda kumpaisha au kumponza Amunike

Kikosi cha Stars leo kitakuwa katika dimba la Taifa kuikabili Uganda Cranes katika mchezo wa kusaka tiketi ya kutinga fainali za AFCON 2019

Mchezo huo ambao ushindi ni lazima kwa Stars, utapigwa saa 12 jioni

Kocha Mkuu wa Stars Emmanuel Amunike amesema wamefanya maandalizi ya kutosha na anaamini vijana wake watafuata maelekezo na hatimaye kuibuka na ushindi

Ni mchezo ambao umeshikilia hatma ya Amunike kuendelea kuinoa Stars au kurejea kwao Nigeria kama atashindwa kuiongoza Stars kupata matokeo leo

Katika michezo iliyopita Amunike alikumbana na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wadau wa soka nchini kutokana kutofurahishwa na uteuzi wa wachezaji, mbinu pamoja na upangaji wa kikosi chake

Stars ilikuwa na nafasi ya kufuzu mapema kama ingeweza kushinda mchezo uliopita dhidi ya Lesotho. Hata hivyo Amunike alipanga kikosi cha kujihami zaidi katika mchezo huo na kupelekea Stars kuchapwa bao 1-0 ugenini

Wengi wanasubiri kwa hamu kikosi atakachopanga leo dhidi ya Uganda ambapo Stars haihitaji matokeo mengine tofauti na ushindi

Lakini ni dhahiri hatma yake itakuwa mikononi mwake mwenyewe, kwani kama Stars haitashinda nae safari ya kurejea Nigeria itakuwa imewadia