Yanga kukamilisha ukarabati uwanja wa Kaunda

Uongozi wa klabu ya Yanga umeandaa mpango wa muda mfupi ambao utawezesha ukarabati wa uwanja wa Kaunda ili uweze kutumika kwa ajili ya mazoezi

Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema baada ya msimu kumalizika wataanza ukarabati wa sehemu ya kuchezea ‘pitch’ ya uwanja wa Kaunda ili uweze kutumika msimu ujao

“Kwa sasa tutakarabati sehemu ya kuchezea, ni zoezi ambalo litachukua takribani miezi mitatu,” amesema Mwakalebela

“Lengo letu ni kuhakikisha msimu ujao tunakuwa na uwanja wetu wa mazoezi ili kupunguza gharama”

“Gharama tunazotumia kukodi viwanja ni kubwa, pesa hiyo inaweza kutusaidia katika masuala mengine yakiwemo ya usajili”

Kuhusu adha ya mafuriko Jangwani, Mwakalebela amesema kifusi kilichowekwa mwanzo kimepunguza adha hiyo na wanakusudia kuongeza kifusi kingine kabla ya kuanza mchakato wa kupanda nyasi sehemu ya kuchezea

Kadi za njano zamuumiza Fei Toto

Kiungo wa Yanga Feisal Salum ‘Fei Toto’ ni miongoni mwa wachezaji wanaoongoza kwa kupewa kadi za njano msimu huu

Fei Toto tayari amekosa michezo mitatu ya ligi inayotokana na adhabu za kadi za njano

Kiungo huyo aliyesajiliwa na Yanga akitokea JKU ya Zanzibar, hafurahii kadi hizo kwani zinamharibia jina na kumpa sifa mbaya

Fei Toto amesema anachokifanya uwanjani ni kutimiza wajibu na maelekezo anayopewa na Mwalimu.

Anaamini baadhi ya kadi anastahili lakini yapo matukio ambao anadhani hatendewi haki na waamuzi

Aidha kiungo huyo amesema amekuwa akikamiwa na wachezaji wa timu pinzani hali inayomfanya acheze kwa presha kubwa

“Baadhi ya mechi huwa nakamiwa, na kunifanya nicheze kwa presha kubwa. Siwezi kusema uwezo wangu ndio chanzo cha kukamiwa kwani naamini kila timu inaingia uwanjani ikiwa na lengo la kupata alama tatu,” amesema

Simba yapania kuweka sawa hesabu za ubingwa leo

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba leo wanashuka dimba la Uhuru kuwakabili Mtibwa Sugar katika mchezo ambao vijana wa Patrick Aussems wamepania kuchukua alama zote tatu

Baada ya kukosa ushindi katika michezo miwili iliyopita, Simba leo inahitaji ushindi ili kuweka sawa hesabu za ubingwa

Simba inahitaji alama saba kutoka michezo mitano iliyobaki kuweza kutetea ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo

Kama itashinda leo, halafu ikashinda mchezo dhidi ya Ndanda Jumapili, sare au matokeo ya ushindi mchezo dhidi ya Singida United, yatatosha kuipa Simba ubingwa wa pili mfululizo

Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu amesema wachezaji wa timu hiyo wako katika hali nzuri kuelekea mchezo huo ambao wamepania kuondoka na alama zote tatu

Yanga yatenga Bilioni Mbili kwa ajili ya usajili

Uongozi wa Yanga umetenga kati ya Tsh Bilioni 1.5 hadi Bilioni mbili kwa ajili ya usajili wa msimu ujao

Katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika Makao Makuu ya Yanga jijini Dar es salaam leo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa Lucas Mashauri amesema walikutana na kocha Mwinyi Zahera ambapo aliwapa mchanganuo wa mahitaji yake kwa ajili ya usajili

“Bajeti ya usajili mara nyingi inatolewa baada ya kukamisha zoezi la usajili”

“Lakini kwa sasa tunakuwa na makisio ya Bajeti tunayohitaji ambapo Kamati yetu ilipewa kazi ya kutafuta kati Bilioni 1.5 na Bilioni mbili,” amesema

“lengo letu kubwa ni kuwa na Yanga imara msimu ujao. Kazi tumemuachia kocha Mwinyi Zahera ili atuambie wachezaji anaowahitaji”

“Bajeti halisi itafahamika baada ya kocha kujadiliana na wachezaji anaotaka waje”

“Lakini tumemuhakikishia, hakuna mchezaji ambaye atamuhitaji tutashindwa kumsajili. Awe Tanzania, nje ya Tanzania hata Ulaya akipatikana mchezaji tutamsajili. Yanga imeshawahi kusajili wachezaji kutoka Ulaya”

“Kamati yetu inaendelea na zoezi la kutafuta fedha ili tuweze kutimiza lengo la kusajili timu bora kadiri kocha atavyopendekeza”

Katika hatua nyingine, Mashauri amewataka Wanayanga waendelee kuichangia timu yao waepuke upotoshaji unaosambazwa kwenye mitandao ya kijamii

“Tunawataka wapenzi, wanachama na mashabiki wetu waendelee kuichangia timu wasipotoshwe na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao”

“Taarifa nyingi zinazosambazwa kuwa tumepokea Bilioni mbili hazina ukweli wowote. Wanaoanzisha taarifa hizo wana lengo la kupunguza kasi ya kuichangia timu yetu”

“Yanga ni timu ya Wananchi na safari hii tumeamua kuisimamia sisi wenyewe. Na kama alivyosema Mwenyekiti, zoezi hili la uchangiaji litandelea kwa kuwa ni wajibu kwa kila Mwanchama wa Yanga kuichangia timu kila mwezi Tsh 1000/- ambayo ni ada ya uanachama”

Azam yanyemelea nyota Simba

Wakati klabu ya Simba ikiwa ‘busy’ kuhakikisha inatetea ubingwa wake, baadhi ya nyota wake ambao mikataba yao imemalizika, wameingia kwenye rada za Azam Fc

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni na John Bocco waliotua Simba kutoka Azam Fc misimu miwili iliyopita, wanatajwa kuwaniwa tena na timu hiyo

Baada ya kuachana na mpango wa kubana matumizi, Azam Fc imepanga kufanya usajili mkubwa ili kuwa washindani wa kweli katika kuwania ubingwa wa ligi kuu msimu ujao

Inaelezwa uongozi wa Simba umepanga kuanza michakato ya usajili baada ya kukamilisha mpango wa kutetea ubingwa

Zaidi ya nyota 10 wa kikosi cha Simba mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu

Tiketi Mechi dhidi ya Sevilla zimeanza kuuzwa

Tiketi kwa ajili ya kuushuhudia mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki kati ya Simba dhidi ya Sevilla tayari zimeanza kuuzwa kupitia Selcom

Kiingilio cha chini cha mchezo huo utakaopigwa May 23 saa moja jioni, Mzunguuko ni Tsh 5,000/- wakati majukwaa ya VIP ni Tsh 15,000/-

Pia kutakuwa na tiketi za Platinumambazo zitapatikana kwa Tsh 100,000/-, kwa wanaohitaji tiketi hizi wawasilane na 0745346687

Mchezo huu wa Kimataifa utakuwa wa kihistoria, sio wa kukosa!