SIMBA WASHUSHA MAJEMBE MAPYA

MABOSI wa Simba kwa msimu ujao hawataki mchezo kwani wamedhamiria kukisuka hasa kikosi chao kiwe cha ushindani na kwa kuanza hivi karibuni watazishusha sura mpya nne za kigeni, akiwemo mshambuliaji Mzambia, Lazarus Kambole.
Mabosi wa Simba wanataka kukiboresha kikosi chao kwa kuleta wachezaji wenye viwango vikubwa kutokana na aina ya matokeo ambayo walikuwa wanayapata kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya ugenini kwa msimu huu.
Chanzo kutoka Simba kimeliambia Championi Jumatatu, kuwa wachezaji hao wane wanatarajiwa kuingia nchini hivi karibuni ambapo wanaweza kuwemo kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Simba na Sevilla ya Hispania.

“Viongozi wanataka kuboresha kikosi kiwe na uwezo wa hali ya juu kwenye michezo ya kimataifa kuliko msimu huu, ndiyo maana viongozi wanaleta wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu kuliko ambao wapo kwa sasa.

“Wachezaji hao wanaweza kuwepo hapa nchini kwenye mechi na Sevilla kwa ajili ya kuangaliwa na kuongea na viongozi kabla ya kusaini mikataba kwa msimu ujao.
“Huyo Kambole unayesema anaweza kuwemo katika orodha hiyo, lakini ni suala la kusubiri kuona kama ni yeye ambaye atakuja hapa ama la,” kilisema chanzo hicho.

Katibu wa Simba, Anord Kashembe amesema: “Huu siyo wakati wa kufanya usajili, hatuwezi kulizungumzia hilo, ukifika muda wake kila kitu kitakuwa sawa.”

Chanzo: championi & gpl

TETESI ZA USAJILI YANGA: Kifaa kipya Yanga hiki hapa, ni hatari tupu, kutua nchini mwezi ujao

Kwa mujibu wa mtandao wa michezo wa ‘Kawowo Sports’ kutoka nchini Uganda umeripoti kuwa mshambauliaji wa zamani wa klabu ya Onduparaka FC, Agau Rashid ambaye kwa sasa anaichezea timu ya Maroons FC anatarajiwa kuwasili Tanzania mwezi Juni kwa ajili ya majaribio katika miamba ya soka ya ligi kuu Young Africans SC.
Rashid ni mzuri wa kumiliki mipira na mfumaniaji mzuri wa mabao

Kwa mujibu wa wakala wa mchezaji huyo, amesema kuwa Agau amepata mualiko kwaajili ya kwenda kufanya majaribio kufuatia kufanya vizuri zaidi msimu huu.
Nyota huyo wazamani wa Onduparaka, amejiunga na Maroons msimu wa mwaka 2018/19 akiwa kama mchezaji huru kwa mkataba wa miaka mitatu hata hivyo kama atajiunga na Yanga atakuwa amewatumikia waajiri wake hao mwaka mmoja pekee.

Ndani ya msimu huu mmoja, Agau Rashid amefanikiwa kufunga jumla ya mabao saba na kuwaacha mbali baadhi ya wachezaji wenzake kama Pius Obuya na Seif Batte wenye mabao manne kila mmoja ikiwa pamoja na Isaac Otto, Bronson Nsubuga waliyosajiliwa msimu huu mwezi Januari wakiwa na mabao matatu.

Klabu ya Maroons imetoa baraka zote kwa, Agau endapo atafanikiwa kufuzu majaribio yake ndani ya Yanga, hata hivyo kama atafanikuwa atajiunga na baadhi ya Waganda wenzake kama Emmanuel Arnold Okwi na Murushid Jjuuko wanaotumikia klabu ya Simba.

Zahera ataja sababu ya Ngasa kukosekana mchezo dhidi ya Ruvu Shooting

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema winga Mrisho Ngasa hakuweza kucheza jana mchezo dhidi ya Ruvu Shooting baada ya kuugua ghafla

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo, Zahera alisema Daktari wa timu Dk Bavu alishauri mchezaji huyo asitumike kwenye mchezo huo hivyo kuamua kumtumia Paulo Godfrey ‘Boxer’ wingi ya kulia

“Ngasa alipata matatizo muda mfupi baada ya kuwa tumepata kifungua kinywa. Alianza kutapika mfululizo na baada ya kupatiwa huduma na Daktari wa timu Dk Bavu, alishauri asicheze,” alisema Zahera

Akizungumzia mchezo huo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, Zahera aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo huku akifichua hawakuwa wamefanya mazoezi tangu walipocheza na Biashara United May 10

“Tulipata changamoto ya usafiri kutoka Mwanza hali iliyopelekea tuchelewe kurudi jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo. Hata baada ya kurudi tulilazimika kuwapa wachezaji mapumziko kwani walikuwa wamechoka”

“Nilifahamu mchezo wa leo (jana) hautakuwa mwepesi kwetu, lakini nimefurahi tumeweza kutumia moja ya nafasi tulizotengeneza ingawa tulikuwa na uwezo wa kufunga mabao zaidi kwenye kipindi cha kwanza”

TFF yafafanua kutoikabidhi Simba ubingwa mchezo dhidi ya Sevilla

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeamua kumuondoa wasiwasi kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye alikerwa na maneno ya msemaji wa Simba Haji Manara kwamba ubingwa watakabidhiwi wakati wa mechi yao na Sevilla inayoshiriki Ligi Kuu nchini Hispania (La Liga).

Kupitia msemaji wa TFF, Clifford Marion Ndimbo aliliweka sawa jambo hilo kwamba hakuna kanuni ya shirikisho inayoruhusu bingwa akabidhiwa kombe nje na mechi ya Ligi Kuu Bara.

“TFF ina kanuni zake hata Simba wakiandika barua kama alivyosema msemaji wao Manara kwamba endapo wangeshinda mechi zao wakabidhiwe taji la ubingwa kwenye mechi yao na Sevilla hakuna kitu kama hicho na hakitafanyika.

“Kama Zahera ana wasiwasi na hilo basi ajue kabisa kwamba TFF ina kanuni zake hata wakiandika barua hiyo, majibu yao ni rahisi kuwa kanuni haziruhusu mambo hayo”anasema.

Kuna video inayomuonyesha Zahera kwamba Simba watakabidhiwa ubingwa wakati sio mabingwa baada ya kusikia kauli ya msemaji wa Simba, Manara kuwa wataiomba TFF wawakabidhi kombe wakati wa mchezo wao na Sevilla.

Mwanaspoti

Mechi tano za kumaliza msimu Simba

Licha ya kutopata ushindi kwenye michezo miwili iliyopita, hesabu za ubingwa kwa Simba bado ziko salama ikihitaji kushinda angalau michezo mitatu kati ya mitano iliyobaki

Ratiba ya mechi zilizobaki za Wekundu hao wa Msimbazi inaonyesha keshokutwa May 16 watakuwa uwanja wa Uhuru kuikabli Mtibwa Sugar kisha kurejea tena uwanjani hapo May 19 kucheza na Ndanda Fc

May 21 Simba itasafiri kwenda mkoani Singida kuikabili Singida United kisha kurejea jijini Dar es salaam kucheza mchezo wa Kimataifa wa kirafiki dhidi ya Sevilla May 23

May 25 itarudi uwanja wa Uhuru kuikabili Biashara United na itamaliza msimu mkoani Morogoro kwa kuikabili Mtibwa Sugar May 28

YANGA YAUTUMIA UWANJA WA UHURU VIZURI, YAICHAPA RUVU SHOOTING BAO 1-0

Yanga imerejea kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru


Bao pekee la Yanga lilifungwa na Papi Tshishimbi aliyemalizia pasi murua ya Deus Kaseke kwenye dakika ya 16
Hilo lilikuwa bao la nne kwa Tshishimbi kwenye ligi msimu huu

Yanga ilikuwa bora kwenye kipindi cha kwanza na ilistahili kwenda mapumziko na angalau mabao mawili kama Raphael Daud asingekosa nafasi ya wazi
Ushindi huo umeifanya Yanga ifikishe alama 83 na kuiondoa Simba kileleni mwa msimamo wa ligi

Simba itacheza na Mtibwa Sugar keshokutwa Alhamisi katika mchezo ambao kama haitapata ushindi huenda ikafufua matumaini ya Yanga kwenye mbio za ubingwa

Mo Simba awards kutolewa May 30 2019

Hafla ya utoaji Tuzo za Mo Simba 2019 itafanyika siku ya Ijumaa Mei 30, 2019 katika hoteli ya Hyatt Regency, The Kilimanjaro iliyopo Jijini Dar es Salaam

Tuzo za mwaka huu zitahusisha wachezaji na mashabiki wa Simba ambao juhudi zao zimesaidia kupatikana kwa mafanikio makubwa msimu huu

Tuzo hizo zitakuwa na vipengele 11 ambavyo ni Mchezaji Bora, Goli Bora, Golikipa Bora, Beki Bora, Kiungo Bora na Mshambuliaji Bora

Nyingine ni Mchezaji Bora Mwanamke, Mchezaji Bora Mdogo, Shabiki Bora, Tuzo ya Heshima na Mhamasishaji Bora katika mitandao ya kijamii

Simba kurejea dimba la Uhuru Alhamisi, kuikabili Mtibwa Sugar

Baada ya kulazimishwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya Azam Fc jana, Simba itarejea tena uwanja wa Uhuru keshokutwa Alhamisi, May 16 kuikabili Mtibwa Sugar

Katika michezo miwili iliyopita Simba imepoteza alama tano, mabingwa hao watetezi wanahitaji kushinda mchezo huo

Simba haikuwa imecheza na Mtibwa Sugar msimu huu, huo utakuwa mchezo wa duru ya kwanza na timu hizo zitarudiana May 28 siku ya kuhitimisha ligi kuu msimu huu

Katika michezo mitano iliyobaki, miwili ni dhidi ya Mtibwa na mingine mitatu ni dhidi ya Biashara United (nyumbani), Ndanda Fc (nyumbani) na Singida United (ugenini)

Simba inahitaji kukusanya angalau alama nane kuweza kutetea ubingwa wake