Bao la Dilunga lawavuruga mashabiki Yanga

Bao la dakika za lala salama lililowekwa kambani na kiungo Hassani Dilung ‘HD’ na kuihakikishia Simba ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania, limewavuruga mashabiki wa Yanga ambao wanalalamikia dakika saba za nyongeza zilizoongezwa na mwamuzi Elie Sasie

Mashabiki wa Yanga wamekuwa wakiiombea ‘dua mbaya’ Simba isishinde michezo yake na pengine wao kuwa na nafasi ya kutwaa ubingwa

Msemaji wa Simba Haji Manara amewataka mashabiki hao waache kuingilia kazi za waamuzi

“Ni jambo la ajabu kusema Simba imependelewa kisa mchezo kuongezwa dakika saba. Dakika hufidiwa pale mwamuzi anapoona muda ulipotezwa isivyo uwanjani,” amesema Manara

Aidha Manara amewakumbusha mashabiki wa timu hiyo kuwa hata wao walipocheza na Lipuli Fc na kukubali kipigo cha bao 1-0 mkoani Iringa, waliongezwa dakika saba

Hesabu za Simba zimeendelea kukaa vizuri kuelekea ubingwa wa pili mfululizo baada ya ushindi wa leo

Simba imefikisha alama 72 ikitofautiana na Yanga kwa alama tano tu huku mabingwa hao watetezi wakiwa na michezo mitano ya viporo

Simba iko katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wake

FT : Simba 1-0 JKT Tanzania

Simba imeendeleza rekodi yake ya ushindi kwenye ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa JKT Tanzania bao 1-0 katika mchezo mgumu uliopigwa dimba la Uhuru

Simba ililazimika kusubiri hadi dakika za nyongeza kujipatia bao la ushindi lililowekwa kambani na Hassani Dilunga huku pasi ya bao ikitotewa na Emmanuel Okwi

JKT Tanzania walitoa upinzani mkali kwa mabingwa hao watetezi lakini uzoefu na kujitolea kwa wachezaji kulifanikisha Simba kuchukua alama zote tatu dakika za majeruhi

Ushindi huo unaifanya Simba izidi kuikaribia Yanga baada ya kufikisha alama 72 ikitofautiana kwa alama tano tu na Yanga inayoongoza ligi

Kituo kinachofuata ni Mbeya ambapo May 03 Simba itashuka dimba la Sokoine kuikabili Mbeya City

Nimepata maumivu ya kawaida – Gadiel

Beki wa kushoto wa Yanga Gadiel Michael Mbaga amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuwa hali yake inaendelea vizuri

Gadiel alishindwa kuendelea na mchezo leo dhidi ya Azam Fc baada ya kuumia kwenye kipindi cha kwanza na nafasi yake kuchukuliwa na Jaffar Mohammed

Gadiel amesema alipata mshtuko uliosababisha maumivu ya misuli. Amesema akipata mapumziko ya siku tatu hadi nne atakuwa sawa

“Nimepata maumivu ya kawaida ya misuli, mapumziko ya siku tatu hadi nne yatanisaidia kurejea katika hali yangu ya kawaida,” amesema

Yanga inakabiliwa na mchezo mwingine wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons ambao utapigwa Alhamisi, May 02 kwenye uwanja wa Taifa

Ninja, Chikupe wawatuliza Chirwa na Ngoma

Washambuliaji wa zamani wa Yanga Obrey Chirwa na Donald Ngoma ambao wanakipiga katika klabu ya Azam Fc leo wameshindwa kufurukuta mbele ya waajiri wao wa zamani wakikubali kipigo cha bao 1-0

Walinzi wawili wa kati wa Yanga Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Andrew Vicent ‘Dante’ leo walikuwa na kazi maalum ya kuhakikisha washambuliaji hao hawasababishi madhara

Hakika kazi hiyo wameifanya kwa ustadi mkubwa kwani walifanikiwa ‘kuwaweka mifukoni’ washambuliaji hao

Wakati Ngoma alipata mwanya wa kufunga bao lililokataliwa na mwamuzi baada ya kumfanyia madhambi Chikupe, nafasi pekee aliyopata Chirwa kwenye kipindi cha kwanza iliokolewa kwa ustadi mkubwa na kipa Klaus Kindoki

Ushindi wa Yanga leo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na umakini wa walinzi hao na wachezaji wote kwa ujumla ambao walikuwa na nidhamu ya hali ya juu katika ulinzi

Licha ya kumiliki mpira kwa muda mwingi, Azam Fc ilikosa mbinu ya kuipenya ngome ya Yanga

FT : Azam Fc 0-1 Yanga

Mabingwa wa kihistoria wa Tanzania Yanga wameendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kuu baada ya kuichapa Azam Fc bao 1-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam

Ikicheza kwa nidhamu na tahadhari kubwa, Yanga ilifunga bao lake pekee kwenye dakika ya 13 kupitia kwa winga Mrisho Ngasa aliyeunganisha mpira wa krosi uliochongwa na Ibrahim Ajib kutoka winga ya kulia

Krosi hiyo ya Ajib ilikuwa zao la shambulizi la kushitukizwa lililofanywa na Yanga

Ngasa sasa amefikisha mabao 5 msimu huu wakati Ajib ametengeneza bao la 16

Azam Fc ilitawala mchezo huo kwa muda mwingi hata hivyo mbinu ya mahiri ya kujilinda ya kocha Zahera iliwapa wakati mgumu wana ‘rambaramba’ hao kuipenya ngome ngumu ya Yanga iliyokuwa chini ya Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Andrew Vicent ‘Dante’

Azam ilipoteza nafasi pekee adimu kwenye dakika ya 84 baada ya Dani Lyanga kushindwa kuutumbukiza mpira kimiani akiwa amebaki na kipa Klaus Kindoki

Ushindi huo umeendelea kuiweka Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imefikisha alama 77, ikiongoza kwa tofauti ya alama 8 dhidi ya Simba na alama 11 dhidi ya Azam Fc

Mchezo unaofuata ni dhidi ya Tanzania Prisons na utapigwa May 02 kwenye uwanja wa Taifa/Uhuru

KIkosi : Azam Fc vs Yanga, TPL April 29

1. Klaus Kindoki

2. Paulo Godfrey

3. Gadiel Michael

4. Abdallah Shaibu

5. Andrew Vicent

6. Feisal Salum

7. Mrisho Ngasa

8. Mohammed Issa

9. Heritier Makambo

10. Ibrahim Ajib (C)

11. Raphael Daudi

SUB

Ramadhani Kabwili

Juma Abdul

Said Juma

Jaffar Mohammed

Papi Tshishimbi

Amissi Tambwe

Haruna Moshi

Misimu miwili, mabao 35 huyu ndio John Bocco

Nahodha wa Simba John Bocco amefikisha mabao 35 katika misimu miwili aliyoitumikia Simba kwenye mashindano yote

Bocco aliyetua Simba akitokea klabu ya Azam Fc ambayo aliitumikia kwa takribani miaka 10, nidye kinara wa muda wote wa upachikaji mabao katika ligi ya Tanzania akiwa amefunga mabao zaidi ya 100

Licha ya umri kusonga, Bocco ‘hachuji’, ameendelea kuwa katika ubora uleule wa kupachika mabao

Msimu huu ameifungia Simba mabao 14 kwenye ligi akishika nafasi ya nne katika orodha ya vinara wa upachikaji mabao nyuma ya Meddie Kagere (16), Salim Aiyee (16) na Heritier Makambo (15)

Msimu uliopita Bocco aliifungia Simba mabao 14 na kushika nafasi ya pili nyuma ya Emmanuel Okwi ambaye msimu huu kasi yake ya kuzifumania nyavu imepungua akiwa amefunga mabao 10

Bocco kwa kushirikiana na Kagere na Okwi, wamefungia Simba jumla ya mabao 40 kwenye ligi msimu huu na kuifanya Simba kuwa moto wa kuotea mbali katika kuzifumania nyavu ikiwa imefunga jumla ya mabao 57