Aussems anataka ushindi mechi zote zilizobaki

Kikosi cha Simba tayari kimerejea jijini Dar es salaam baada ya kumaliza ratiba ya michezo ya kanda ya ziwa

Simba kesho Jumanne itashuka uwanja wa Uhuru kuikabili JKT Tanzania katika mchezo mwingine wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Kocha Mkuu wa mabingwa hao watetezi Patrick Aussems amesema licha ya timu yake kukusanya alama tisa kutoka kanda ya ziwa, bado kazi haijamalizika na wanahitaji kushinda michezo yote iliyobaki waweze kutetea ubingwa wao

Aidha Aussem amesema ushindani kwenye ligi umeongezeka katika kipindi hiki cha lala salama hivyo wanahitaji kupambana kila mara wanaposhuka dimbani

“Bado tuna kazi ya kufanya, mechi zote ni ngumu, ligi bado ina ushindani, hakuna mechi rahisi, kila timu inahitaji ushindi ndio maana hakuna anayekata tamaa mpaka filimbi ya mwisho inapopigwa, tunataka kushinda kila mechi iliyopo mbele, ” amesema

Baada ya mchezo dhidi ya JKT Tanzania kesho, kikosi cha Simba kitaelekea mkoani Mbeya ambako kitacheza michezo miwili dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons

Kimahesabu, Simba inahitaji kushinda michezo nane kati ya 11 iliyobaki ili kujihakikishia ubingwa bila ya kujali matokeo ya mpinzani wake Yanga ambaye leo huenda akadondosha pointi zaidi dhidi ya Azam Fc

Kapombe anakaribia kurejea kisosini Simba

Uongozi wa Simba umethibitisha kuwa beki wake kiraka Shomari Kapombe anakaribia kurejea kikosini baada ya kuanza mazoezi mepesi

Msemaji wa Simba Haji Manara amesema Kapombe amepona majeraha ya goti na tayari ameanza mazoezi ya gym ikiwa ni hatua ya mwanzo kabla ya kurejea dimbani

“Tunashukuru beki wetu Shomari Kapombe amepona majeraha ya goti yaliyomuweka nje kwa muda mrefu. Hivi sasa anafanya mazoezi ya Gym ili kuurejesha mwili katika hali yake kabla ya kuanza mazoezi ya mpira,” amesema

Kapombe amekuwa nje kwa zaidi ya miezi mitano akiuguza majeraha ya goti aliyopata nchini Afrika Kusini wakati akiitumikia timu ya Taifa

Licha ya beki huyo kuanza kujifua, kuna uwezekano mdogo kwake kucheza mechi zilizobaki

Wagombea Yanga kuanza kampeni Jumanne

Wagombea waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika klabu ya Yanga, wanatarajiwa kuanza rasmi kampeni kesho Jumanne, April 30 2019

Kampeni zitaanza baada ya muda wa rufaa kwa wagombea walioenguliwa kupita huku mgombea mmoja kati ya 15 ambao majina yao yalienguliwa, amekata rufaa

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF Malangwe Mchungahella amesema rufaa ya mgombea huyo wa nafasi ya Ujumbe, Rodgers Gumbo itasikilizwa kesho

Uchaguzi Mkuu wa Yanga kuwapata viongozi wapya watakoiongoza timu hiyo kwa kipindi cha miaka minne utafanyika Jumapili, May 05 2019

Hii hapa orodha ya wagombea wote waliopitishwa;

Mwenyekiti

1. Baraka Igagungula (ME)
2. Dr. Jonas Tiboroha (ME)
3. Elias Mwanjala (ME)
4. Dr. Mbette Mshindo Msola (ME)

Makamu Manyekiti

1. Fredrick Mwakalebela (ME)
2.Jannet Mbene (KE)
3. Titus Osoro (ME)
4. Yono Kevela (ME)

Wajumbe

1. Saady Mohamed Khimji (ME)
2. Hassan H. Yahaya (ME)
3. Arafat Hajji (ME)
4. Suma Mwaitenda (KE)
5. Hamad Islam (ME)
6. Dominick Albinus (ME)
7. Sharifu Amour Makosa (ME)
8. Eng. Bahati F. Mwaseba (ME)
9. Eng. Leonard Marango (ME)
10. Haruna H. Batenga (ME)
11. Athanas Kazinghe (ME)
12. Ramadhan Said (ME)
13. Salim Rupia (ME)
14. Dominick Francis (ME)
15. Sharifu Amir (ME)
16. Benjamin Mwakasendo (ME)
17. Christopha Kashiririka (ME)
18. Ally Msigwa (ME)
19. Frank K. Kamugisha (ME)
20. Said Kambi (ME)
21. Silvester Haule (ME)

NB : Rufaa ya mgombea mmoja wa nafasi ya Ujumbe Rodgers Gumbo itasikilizwa kesho Jumanne April 30 2019

Yanga yasaka alama tatu dhidi ya Azam Fc leo

Vinara wa ligi kuu ya Tanzania Bara Yanga leo wanashuka kwenye uwanja wa Uhuru kuikabili Azam Fc katika mchezo wa ligi hiyo

Mchezo unatarajiwa kuanza saa kumi kamili jioni

Yanga iliyojikusanyia alama 74, iko mbele ya Azam Fc kwa tofauti ya alama nane, inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kuendelea kuweka hai mbio za kuwania ubingwa msimu huu

Hata hivyo, mchezo hautakuwa mwepesi kutokana na uimara wa kikosi cha Azam ambacho tangu kimtimue kocha Hans van Pluijm kimepoteza mchezo mmoja tu

Kocha Mwinyi Zahera amesema amewaandaa wachezaji wake kikamilifu lengo lao likiwa kushinda

Amesema ni mchezo ambao wanahitaji kupambana na kuwa makini zaidi, hawapaswi kufanya makosa mengi na lazima watumie nafasi

Timu zote zitawakosa wachezaji wake waandamizi Kelvin Yondani na Aggrey Morris wanaotumikia adhabu ya kukosa michezo mitatu

Yanga yataka sapoti ya mashabiki mchezo dhidi ya Azam Fc

Mashabiki wa Yanga wameaswa kujitokeza kwa wingi uwanja wa Uhuru kesho kuiunga mkono timu yao ikichuana na Azam Fc

Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh amesema wamefanya maandalizi ya kutosha na wana matumaini makubwa ya kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo

“Tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kutuunga mkono. Timu iko tayari kwa ajili ya mchezo huo na lengo letu ni kupata ushindi ambao utaendelea kutuimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi”

Azam Fc itakuwa mwenyeji wa mchezo huo wa kwanza kwa timu hizo kukutana msimu huu

Viingilio kwa majukwaa ya VIP A ni Tsh 15,000/- na VIP B ni Tsh 10,000/- wakati Mzunguuko ikiwa Tsh 5,000/-

Mchezo huo pia utakuwa mbashara kupitia Azam Sport 2 ambapo mtangazaji Baraka Mpenja ndiye atakayeongoza matangazo hayo

Simba yaondoka Mwanza kurejea Dar

Kikosi cha Simba kimeondoka leo jijini Mwanza kurejea jijini Dar es salaam kuendelea na ratiba ya michezo ya ligi kuu ambapo keshokutwa Jumanne itachuana na JKT Tanzania katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Uhuru

Simba imemaliza salama ratiba ya michezo ya kanda ya ziwa ikifanikiwa kushinda michezo mitatu na kufungwa mchezo mmoja

Baada ya mchezo dhidi ya JKT Tanzania, kikosi cha Simba kitaelekea mkoani Mbeya kuzifuata Mbeya City na Tanzania Prisons

Simba yaondoka Mwanza kurejea Dar

Kikosi cha Simba kimeondoka leo jijini Mwanza kurejea jijini Dar es salaam kuendelea na ratiba ya michezo ya ligi kuu ambapo keshokutwa Jumanne itachuana na JKT Tanzania katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Uhuru

Simba imemaliza salama ratiba ya michezo ya kanda ya ziwa ikifanikiwa kushinda michezo mitatu na kufungwa mchezo mmoja

Baada ya mchezo dhidi ya JKT Tanzania, kikosi cha Simba kitaelekea mkoani Mbeya kuzifuata Mbeya City na Tanzania Prisons

Wanaosema Simba ‘inabebwa’ wajitafakari

Afisa Habari wa Simba Haji Manara amewashangaa mashabiki wanaosema klabu hiyo inabebwa na waamuzi wakati timu hiyo imepata mafanikio nje na ndani ya Tanzania kutokana na ubora wa kikosi chake

Manara amesema Simba imekuwa ikicheza kila baada ya siku mbili na inapata matokeo kutokana na ubora wake na si vinginevyo

“Tumefika robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa tulibebwa na nani?” alihoji Manara

“Hata hao Yanga ambao mashabiki wao wanalalamika kuwa tunabebwa nao tuliwafunga, je tulibebwa?”

“Kwa sasa Simba ndio timu yenye kikosi bora Tanzania, ndio mabingwa watetezi na baada ya wiki moja tutakuwa kileleni mwa msimamo wa ligi tayari kurejesha ubingwa Msimbazi”

Simba imebakisha michezo 11, lakini inahitaji kushinda michezo nane tu ili iweze kutwaa ubingwa

Aidha kama Yanga itashindwa kuifunga Azam Fc kesho, Simba itahitaji kushinda michezo miwili tu ili kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi

Aussems ashangazwa na mzuka wa mashabiki Musoma

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amewashukuru mashabiki wa timu hiyo mkoani Mara kwa sapoti waliyotoa kwa mabingwa hao watarajiwa wa ligi kuu kwa msimu wa pili mfululizo

Aussems amesema amefarijika kuona mashabiki wakijitokeza kwa wingi uwanjani jana lakini zaidi juzi Simba ilipotua mkoani Mara

“Tumefarijika na mapokezi waliyotupa mashabiki wa hapa ikiwa ni muda mrefu umepita tangu Simba ije kucheza hapa,” amesema

“Tumewaachia zawadi ya ushindi, sisi tunaelekea Dar ambako tutacheza mchezo mmoja Jumanne (na JKT Tanzania) kisha tutaelekea mkoani Mbeya kuzikabili Mbeya City na Tanzania Prisons”

Msafara wa Simba ulilala jijini Mwanza ambapo leo wanarejea jijini Dar es salaam kwa usafiri wa ndege