Taifa STARS : Kupewa Mamilioni Wakiifunga UGANDA | TAIFA

Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kamati yake itatoa shilingi. milioni 10 kwa kila mchezaji wa timu hiyo iwapo timu itafuzu kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika #AFCON2019

Makonda amesema Watanzania wanachokijua kwa sasa ni kwamba AFCON 2019 ni zamu yao, hivyo amewaomba wachezaji wa timu ya Taifa wahakikishe wanawapa furaha kwa kuifunga timu ya Taifa ya Uganda na kwamba wananchi wengi wamehamasika kwenda kuwashangilia.
#zamuyetuafcon2019🇹🇿

Nitakuwepo uwanjani kuiunga mkono Stars – Tshabalala

Nahodha Msaidizi wa kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ amesema ataungana na mashabiki wa soka nchini kwenda uwanjani kesho kuiunga mkono Stars itakapokuwa ikichuana na Uganda Cranes

Tshabalala amesema anaamini kikosi kilichochaguliwa na kocha Emmanuel Amunike ni kizuri na kitaweza kuipa Tanzania matokeo inayohitaji ili iweze kufuzu kwa fainali za AFCON 2019

“Nitakuwepo uwanjani kesho kuwasapoti ndugu zangu, marafiki zangu, kaka zangu kuwapa hamasa ili waweze kupata matokeo chanya katika mchezo huo”

Tshabalala amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa kesho kuhakikisha lengo la kushinda mchezo huo linafanikishwa

Mchezo dhidi ya Uganda umepewa hamasa ya kipekee na wadau wa nyanja zote nchini kutokana na umuhimu wake

Baada ya kukosa kushiriki fainali za AFCON kwa miaka 39, Stars inaweza kupata nafasi ya kushiriki fainali hizo mwaka huu zitakazofanyika nchini Misri kama itaweza kuifunga Uganda

SAMATTA: Kuiongoza STARS Kusaka.Ushindi Kesho

Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Mbwana Samatta kesho Jumapili atabeba matumaini ya Watanzania kuelekea fainali za AFCON 2019 atakapokiongoza kikosi cha Stars katika mchezo dhidi ya Uganda Cranes

Samatta, kinara wa mabao ligi kuu ya Ubelgiji, amewatoa hofu Watanzania kuelekea mchezo huo akiahidi kuwa watafanya kile walichoelekezwa na Kocha Emmanuel Amunike ili waweze kuibuka na ushindi

“Tumefanya maandalizi ya kutosha. Tunafahamu mchezo hautakuwa mwepesi lakini tunayo kila sababu ya kutumia vyema uwanja wetu wa nyumbani kupata ushindi,” amesema Samatta

Matokeo ya ushindi dhidi ya Uganda yanaweza kuipa Stars nafasi ya kufuzu kwa fainali za AFCON 2019 zitakazofanyika mwezi Juni nchini Misri.

Hata hivyo ili Stars iweze kufuzu lazima Cape Verde iifunge au itoke sare na Lesotho. Mchezo baina ya timu hizo utapigwa huko Cape Verde muda sawa na mchezo kati ya Stars dhidi ya Uganda utakaopigwa saa 12 jioni

Wapinzani wa Stars, Uganda Cranes wanatarajiwa kuwasili nchini leo

Uganda iliweka kambi ya wiki moja nchini Misri kujiandaa na mchezo huo

Uganda Cranes kuwasili leo

Kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda ‘Uganda Cranes’ kinatarajiwa kuwasili leo tayari kwa mchezo dhidi ya Taifa Stars utakaopigwa kwenye uwanja wa Taifa kesho Jumapili

Mchezo huo wa kukamilisha ratiba ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za AFCON 2019, unatarajiwa kuanza saa 12 jioni

Uganda ambayo tayari imeshafuzu kushiriki fainali hizo zitakazopigwa nchini Misri mwezi Juni ikiwa kinara wa kundi L, iliweka kambi ya wiki moja jijini Cairo

Kikosi cha timu hiyo kitakachowasili leo, kinajumuisha wachezaji wawili wa Simba, Emmanuel Okwi na Juuko Murshid

MO DEWJI aiombea dua Stars

Mwekezaji wa klabu ya Simba Mohammed Dewji ‘Mo’ amewahamasisha wachezaji wa Taifa Stars kuipigania Tanzania Jumapili, wawaze kushinda mchezo dhidi ya Uganda Cranes

Mo amesema Watanzania wote tunapaswa kuwa wamoja kuelekea mchezo huo ambao Stars inahitaji kushinda ili iweze kukata tiketi ya kutinga fainali za michuano ya AFCON 2019 itakayofanyika nchini Misri baada ya kukosa michuano hiyo kwa miaka

39

Mo amewahakikishia wachezaji wa Stars kuwa Watanzania wote wako nao kwani wanashauku ya kuiona timu yao ikifuzu kwa fainali za michuano hiyo, hivyo wasiwaangushe

“Watanzania wote tupo nyuma yenu wachezaji wetu wa Taifa Stars kuhakikisha tunashinda dhidi ya Uganda, sababu zote za kufanya hivyo tunazo,” amesema

“Naamini mtashinda na kutufanya Watanzania tutembee kifua mbele. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu mfanye”

Kuelekea mchezo huo utakaopigwa keshokutwa Jumapili saa 12 jioni katika dimba la Taifa, mashabiki wametakiwa kujitokeza kwa wingi ili kuwapa sapoti wachezaji

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi katika mchezo huo ambao kiingilio ni Tsh 2000/- tu

Waziri Mkuu mgeni rasmi mchezo wa Stars vs Uganda

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Kassim Majaliwa keshokutwa Jumapili, March 24 2019 atawaongoza Watanzania kuiunga mkono timu ya Taifa ya Tanzania katika mchezo wa kusaka tiketi ya kutinga fainali za AFCON 2019 akiwa mgeni rasmi katika mcheoz huo dhidi ya Uganda

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mh Paul Makonda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uhamasishaji, amesema Waziri Mkuu amekubali kuwa mgeni rasmi wa mchezo huo na hivyo kuwataka wakazi wa jiji la Dar es salaam na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kwenye uwanja wa Taifa kuungana na Waziri Mkuu katika kuipa sapoti Stars inayohitaji matokeo ya ushindi dhidi ya Uganda

Kikosi cha Stars kimeendelea kujifua katika dimba la Taifa kujiandaa na mchezo huo utakaopigwa saa kumi na mbili jioni

Stars imedhamiria kuvunja rekodi ya miaka 39 ya kukosa nafasi ya kushiriki fainali za michuano ya AFCON. Inaweza kufikia malengo hayo kama itaifunga Uganda huku ikiomba Lesotho ambayo itakuwa ugenini ikichuana na Cape Verde itashindwa kupata ushindi

Uganda tayari imefuzu ikiongoza kundi L ikiwa na alama 13, Lesotho inafuatia nafasi ya pili ikiwa na alama tano sawa na Stars lakini Lesotho imeipiku Stars kutokana na faida ya kupata alama nne katika michezo miwili ambayo timu hizo zilikutana

Cape Verde inashika mkia ikiwa na alama nne lakini pia inaweza kufuzu kama Stars itashindwa kupata ushindi dhidi ya Uganda huku yenyewe ikiichapa Lesotho

Ngasa ashikiria rekodi ya michezo, mabao Stars

Wakati Watanzania wakiusubiri kwa hamu mchezo wa Stars dhidi ya Uganda utakaopigwa keshokutwa Jumapili katika uwanja wa Taifa, winga wa Yanga Mrisho Ngasa ‘Uncle’ ni miongoni mwa wachezaji wenye historia ya kipekee katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania

Ngasa ameichezea Stars michezo 100 na kufanikiwa kufunga mabao 25. Bado rekodi yake hiyo ya michezo na mabao haijavunjwa

Ngasa mwenye umri wa miaka 29 anasema bado hajastaafu kuichezea timu ya Taifa na yuko tayari kuitumikia iwapo ataitwa siku zijazo

“Bado sijatangaza kustaafu kuichezea Stars, bado naamini ninayo nafasi ya kucheza na kuonyesha uwezo kama ilivyokuwa mwanzo,” amesema Ngasa

“Sijakata tamaa nitapambana kuhakikisha wakati wmingine napata nafasi ya kulitumikia taifa langu muda bado ninao na kipaji kipo kwanini nisiitwe hakuna raha kama kucheza katika timu ya taifa”

Ngasa amekuwa na msimu mzuri katika kikosi cha Yanga akijihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Mwinyi Zahera

Ngasa ameifungia Yanga mabao manne katika ligi kuu ya Tanzania Bara