Kagere apania kumpiku Aiyee

Licha ya Mwadui Fc kubamizwa mabao 6-2 na Ruvu Shooting jana, mshambuliaji wa timu hiyo Salim Aiyee alifunga moja ya mabao na kumfanya afikishe mabao 14

Leo Meddie Kagere anatarajiwa kuiongoza safu ya ushambuliaji ya Simba kwenye mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Stand United utakaopigwa uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga

Kagere mwenye mabao 12, yuko katika kiwango bora cha upachikaji mabao, akifunga mfululizo kwenye michezo mitano iliyopita

“Kazi yangu mimi ni kufunga, hivyo nitaendelea kufanya hivyo kila ninapopata nafasi ili niisaidie timu yangu iweze kupata ushindi,” alisema Kagere baada ya mazoezi ya jana

Kagere ndiye mchezaji hatari zaidi katika ligi kuu ya Tanzania Bara kwa sasa kutokana na kuwa na wastani mzuri wa kufunga kulingana na uwiano wa michezo aliyocheza

Simba kuelekea Shinyanga leo, Okwi arudi Dar

Mshambuliaji wa Simba Emmanuel Okwi alipata majeraha kwenye mchezo dhidi ya Lipuli Fc na kulazimika kurejea jijini Dar es salaam kwa ajili ya matibabu zaidi

Hata hivyo Okwi bado anaweza kuungana na kikosi cha Simba kwa ajili ya mchezo dhidi ya Stand United utakaopigwa keshokutwa katika uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga

Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amesema hatma yake itategemea na ripoti ya Daktari wa timu hiyo Dk Yassin Gembe

Wakati huo huo Simba inaondoka mkoani Singida leo kuelekea Shinyanga tayari kwa mchezo dhidi ya Stand United utakaopigwa Jumapili

HIMID MAO ACHEZA MECHI YOTE TIMU YAKE YACHAPWA 4-0 NA AL AHLY LIGI YA MISRI

KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Himid Mao Mkami jana amecheza kwa dakika zote 90, timu yake, Petrojet FC ikichapwa mabao 4-0 na Al Ahly katika mchezo wa Ligi Kuu ya Misri Uwanja wa Petrosport mjini Cairo.
Mabao ya Al Ahly yamefungwa na Junior Ajayi dakika ya nane akimalizia pasi ya Nasser Maher, Marwan Mohsen dakika ya 31 akimalizia pasi ya Geraldo aliyefunga la tatu dakika ya 69 kwa pasi ya Ali Maaloul na Karim Nedved aliyefunga la tano dakika ya 75.
Nedved aliyefunga akimalizia pasi ya mfungaji wa bao la pili la Al Ahly, Marwan Mohsen angeweza kufunga mabao zaidi kama angetumia vyema nafasi nyingine alizopata.
Kwa ushindi huo, Al Ahly inafikisha pointi 51 baada ya kucheza mechi 22, ikipanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Zamalek inayoongoza kwa pointi zake 52 za mechi 21

Zahera amjumuisha Makambo kikosi cha DR Congo

Mshambuliaji wa Yanga kinara wa mabao Heritier Makambo amejumuishwa kwenye kikosi cha awali cha timu ya Taifa ya DR Congo chenye wachezaji 40 ambao baadae watachujwa na kubaki 23

DR Congo mwishoni mwa mwezi huu itachuana na Liberia katika mchezo wa kusaka tiketi ya kutinga fainali za michuano ya AFCON 2019 itakayofanyika nchini Misri mwezi Juni

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera ndiye kocha msaidizi wa DR Congo akimsaidia Florente Ibenge ambaye pia anainoa Vita Club

Bila shaka, Zahera amechangia kwa kiasi kukubwa Makambo kujumuishwa katika kikosi hicho ambacho kimesheheni wachezaji wengi wanaocheza soka barani Ulaya

Serengeti Boyz yaalikwa Ulaya

Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 17, Serengeti Boyz kinaondoka nchini leo kwenda Uturuki kushiriki michuano ya Kimataifa ya UEFA ASSIST

Serengeti Boyz ni timu alikwa kwenye michunao hiyo ambayo itaitumia kama sehemu ya maandalizi kuelekea fainali za vijana za AFCON 2019 zitakazofanyika nchini kuanzia Apri 14 hadi April 28 Tanzania ikiwa mwenyeji

Jana vijana hao walifanyiwa vipimo vya kuhakiki umri (MRI), vipimo vilivyofanyika kwenye hospitali ya Muhimbili

MWILI WA RUGE Kuwasili Kesho

Mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba unatarajiwa kuwasili nchini kesho Ijumaa Machi mosi 2019 na utazikwa Bukoba, mkoani Kagera Jumatatu ijayo

Msemaji wa famili Annik Kashasha amesema taratibu za kuuleta mwili zinafanyika nchini Afrika Kusini ambako marehemu alifariki juzi wakati akiendelea na matibabu.

“Mwili wa marehemu utarejeshwa hapa nchini siku ya Ijumaa (Machi 1) na siku ya Jumapili (Machi 3) utasafirishwa kwenda Bukoba kwaajili ya mazishi,” alisema Kashasha

Kifo cha Ruge kimewashtua Watanzania kutokana na mchango wake hasa katika kuwasaidia vijana kutimiza ndoto zao

Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera ni miongoni mwa walioguswa na kifo cha Ruge ambapo amebainisha licha ya kutokumfahamu kabla, amebaini alikuwa ni mtu wa kipekee kwa Watanzania

Chikupe kuikosa Alliance Fc, Kamusoko arejea

Beki kisiki Andrew Vicent Chikupe ataukosa mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya Alliance dhidi ya Yanga utakaopigwa keshokutwa Jumamosi March 02 katika uwanja wa CCM Kirumba

Chikupe aliumia katika mchezo wa kombe la Azam (ASFC) uliopigwa Jumapili iliyopita mkoani Lindi na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo FC. Matokeo yaliyoipeleka Yanga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo

Nae kiungo Thabani Kamusoko aliyekuwa majeruhi kwa wiki kadhaa amejumuishwa katika kikosi kilichosafiri jijini Mwanza kwa ajili ya mchezo huo

Mbali na Chikupe, mshambuliaji Matheo Anthony na kiungo Pius Buswita nao hawakusafiri na timu

Uwanja wa Taifa, Uhuru na Azam Complex kufungwa wakati wowote

Timu zinazotumia Uwanja wa Uhuru, Taifa na Azam Complex kwaajili ya michezo ya ligi mbalimbali zimeshauriwa kutafuta viwanja vingine kwa ajili ya michezo yao kutokana na viwanja hivyo kukaribia kufungwa kupisha ukarabati kuelekea kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana.

Wito huo umetolewa jana na Meneja wa Uwanja wa Taifa Nsajigwa Gordon ambaye amesema hatua hiyo inatokana na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kuagiza viwanja hivyo kufungwa ili kupisha marekebisho.

Viwanja hivyo vinatarajiwa kufungwa ili kupisha ukarabati tayari kwa michuano ya AFCON 19 ngazi ya vijana chini ya umri wa miaka 17 inayotarajiwa kuanza April 14-28 Tanzania ikiwa mwenyeji wa michuano hiyo

Sima imekuwa ikitumia uwanja wa Taifa kama uwanja wake wa nyumbani hivyo italazimika kutafuta uwanja mwingine kwa ajili ya michezo yake ya nyumbani kwa kipindi chote ambacho uwanja huo utakuwa umefungwa