Ten awapiga ‘dongo’ Simba, ‘vumilieni ndio ukubwa huo’

Afisa Habari wa Yanga Dismas Ten amewataka mashabiki wa Simba wavumilie ‘madongo’ wanayovurumishiwa baada ya jana kufumuliwa mabao 4-1 na TP Mazembe na kuondoshwa katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika hatua ya robo fainali

Kutupwa nje ya michuano hiyo kwa Simba kuliibua shangwe kubwa miongoni mwa mashabiki wa Yanga na hii inatokana na Simba kutumia mafanikio yao msimu huu ‘kuwanyanyasa’ watani zao Yanga ambao wanapita katika kipindi kigumu

Ten amesema Yanga na Simba ni watani wa jadi hivyo ni vyema wakavumilia matani wanayokutana nayo mtaani kwani na wao wamekuwa wakifanya hivyo wakati wote ambao Yanga inakumbwa na changamoto

“Ndiyo Sisi na ninyi ni watani na tunataniana kweli hasa timu zetu zinapokosa matokeo,” ameandika Ten kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram

“Bahati mbaya ni kwamba ninyi mnapenda kutania wenzenu lakini mkitaniwa ninyi ‘Nongwa’ mnahamia kwenye kashfa..! Mkikashifiwa nanyi mnaanza kulialia”

“Hongereni kwa hatua mliyofika, muhimu ni kuangalia wapi mmekosea ili mfanikiwe zaidi siku za usoni”

“Wakati sisi tunajiuliza nanyi mjiulize zaidi. Msimvuruge @moodewji ili aendelee kuwabeba..!”

Aidha Ten amewakaribisha Simba kwenye ligi kuu huku akiwatupia ‘dongo’ kuwa mitandao yao ya simu itakuwa imejaa tayari kwa kufanya miamala

“La huko limeisha, mrudi bongo sasa najua simu zenu zina line mbili mbili yaani full network kama siyo Mpesa basi Tigopesa…!”

Baada ya kutolewa Simba inarejea kwenye ligi ikikumbana na rundo la ‘viporo’ ambavyo watatakiwa wavimalize ndani ya kipindi cha mwezi mmoja

Katika kipindi hicho Simba wanapaswa kucheza michezo 16 kwani ligi imepangwa kumalizika mwishoni mwa mwezi wa tano ili kupisha maandalizi ya timu ya Taifa ambayo mwezi Juni inaelekea Misri kushiriki fainali za AFCON 2019

Njooni mtuunge mkono mchezo dhidi ya Nigeria – Nahodha Serengeti Boyz

Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 17 Serengeti Boyz leo kinashuka dimba la Taifa kuikabili Nigeria kwenye mchezo wa ufunguzi wa michuano ya AFCON U17, mchezo utakaopigwa saa kumi kamili jioni

Tanzania ni mwenyeji wa michuano hiyo inayoanza kutimua vumbi leo katika viwanja vya Azam Complex na Taifa

Nahodha wa kikosi cha Serengeti Boyz Morris Michael amewataka Watanzania wajitokeze kwa wingi uwanja wa Taifa watakapokuwa wakiikabili Nigeria leo

“Nimezungumza na wenzangu na kuwashusha presha kwamba tunaenda kucheza mchezo wa kawaida kama michezo mingine ambayo tumecheza, kwa hiyo tuuone wa kawaida,” amesema

“Ni mechi kubwa lakini hatutakiwi kuwa na presha, tunatakiwa kupambana hadi mwisho kupata ushindi.”

“Tukishinda mchezo huu tutapata picha nzuri ya matarajio yetu hapo mbele tofauti na tukipoteza au kupata sare.”

“Watanzania waje kutuunga mkono kwa sababu tupo nyumbani naamini tutafanya kitu ambacho watanzania hawataamini”

Viingilio vya mchezo huo VIP ni Tsh 5,000/- na upande wa mzunguuko ni Tsh 2,000/-

Tutatetea ubingwa wetu ili tushiriki tena mwakani – Tshabalala

Nahodha Msaidizi wa kikosi cha Simba Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ amesema hatua ya robo fainali waliyofikia kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika imewapa somo na msimu ujao wakipata nafasi anaamini watafanya vizuri zaidi

Aidha Hussein amesema hatua hiyo imewapa nguvu ya kupambana kwenye ligi ili kuhakikisha wanatetea ubingwa wapate nafasi ya kushiriki michuano hiyo mwakani

“Tulianza kwa Kuandika Kitabu cha Historia Mpya ya Soka Letu baada ya Miaka Mingi Kupita Na Tulitegemea Kuendelea Kukiandika Kitabu Hicho Pale LUBUMBASHI Kabla ya Kukifunga Lakini Haikuwa Bahati,” Tshabalala ameandika kwenye ukurasa wa mtandao wa Instagram

“Uzuri na Utamu wa Mashindano Haya ya CAF CHAMPIONS LEAGUEUnatufanya Kama TEAM Na Mimi binafsi Kupambana Kuhakikisha Mwakani Tunarudi Tena INSHAALLAH”

Simba tayari imerejea nchini kuanza ‘mchakamchaka’ wa kula viporo katika kampeni ya kubakisha ubingwa Msimbazi

FT: Simba 1-4 TP Mazembe

Mchezo wa pili wa robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika kati ya TP Mazembe dhidi ya Simba umemalizika kwa wenyeji kusonga mbele hatua ya nusu fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1

Licha ya kutangulia kufunga bao la kuongoza kwenye dakika ya pili kupitia kwa Emmanuel Okwi, Simba ilishindwa kulinda bao hilo huku mfumo wa kujihami zaidi uliotumiwa na kocha Patrick Aussems ukitajwa kuigharimu Simba katika kipindi cha kwanza na kujikuta ikiruhusu mabao mawili mpaka wakati wa mapumziko

TP Mazembe ilitawala zaidi mchezo kwenye kipindi cha pili kwa kutengeneza nafasi nyingi huku ikifanikiwa kutumia nafasi nyingine mbili kujihakikishia ushindi wa mabao 4-1

Licha ya kuondoshwa katika hatua ya robo fainali, mafanikio ya kufika hatua hiyo ni ya kujivunia kwa Simba

Aidha bila shaka Simba itaendeleza hapa ilipoishia kwa kuimarisha zaidi kikosi chake ili kuwa cha ushindani zaidi msimu ujao

Rais Congo kushuhudia mchezo wa TP Mazembe vs Simba

Klabu ya TP Mazembe iimemualika Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi kushuhudia mchezo wa pili wa robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Simba

Ikulu ya DR Congo imethibitisha kuwa Tshisekedi atakuwepo uwanjani kushuhudia mchezo huo unaopigwa leo saa kumi kamili jioni

Mchezo huo utapigwa katika uwanja wa Stade TP Mazembe