MKUDE Haendi Popote – MO

Mwenyekiti wa Bodi wa Wakurugenzi ya Simba Mohammed Dewji ‘Mo’ amewatoa hofu wapenzi, wanachama na mashabiki wa timu hiyo juu ya kiungo mkata umeme Jonas Mkude

Mo amesema Mkude ataendelea kubaki Msimbazi

Mkude amekuwa akihusishwa na timu kadhaa ikiwemo klabu ya Yanga inayodaiwa kumuahidi zaidi ya Tsh Milioni 120

Wanasimba msiwe na wasiwasi, Mkude haendi popote! Jumaah Kareem,” ameandika Mo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram

Mkude ni miongoni mwa wachezaji waliomaliza mikataba Simba na alikuwa akisubiri kusaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki Msimbazi

SIMBA vs BIASHARA UNITED TAIFA

Mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Biashara United utakaopigwa kesho Jumamosi, May 25, umehamishiwa uwanja wa Taifa na utaanza saa tisa Alasiri

Mabadiliko hayo yatatoa nafasi kwa Simba kukabidhiwa ubingwa baada mchezo huo kumalizika

Uongozi wa Simba umethibitisha mabadiliko hayo na kuwataka mashabiki wa timu hiyo wajitokeze kwa wingi kesho uwanja wa Taifa kupokea ubingwa wa ligi kuu

“Mchezo wa Ligi Kuu ambao tutacheza kesho dhidi ya Biashara United utachezwa katika Uwanja wa Taifa kuanzia saa 9:00 alasiri. Sababu ya mabadiliko ya muda ni sherehe za kukabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu 2018/2019 ambazo zitafanyika baada ya mechi kuisha,” imesema taarifa ya Simba

NIYONZIMA: Asubiria Mkataba mpya SIMBA

Kiungo fundi Haruna Niyonzima amekuwa kwenye kiwango bora sana. Tangu kuanza kwa mwaka 2019, Niyonzima amekuwa mchezaji wa kutegemewa wa kikosi cha Simba kinachonolewa na Mbelgiji Patraick Aussems

Niyonzima ni miongoni mwa wachezaji ambao mikataba yao inamalizika na tayari mazungumzo ya kumuongezea mkataba yameanza

Akiwa miongoni mwa wachezaji walioisaidia Simba kutwaa ubingwa wa pili mfululizo ligi kuu ya Tanzania Bara, hakuna shaka, ataendelea kubaki Msimbazi

Kiungo huyo wa zamani wa APR, amekiri juu ya kuanza kwa mazungumzo ya mkataba mpya

“Kwa sasa hivi siwezi kuweka kila kitu wazi, muda utakapofika taarifa zitawekwa hadharani, ngoja tumalizie msimu huu kwanza,” alisema Niyonzima

Juzi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Mohammed Dewji ‘Mo’ alisema Bodi hiyo ilikuwa ikisubiri ripoti ya kocha Patrick Aussems ili kuanza michakato ya usajili

Inaelezwa tayari Aussems ameshawasilisha ripoti hiyo

ZANA COULIBALY : Amepoteza Kujiamini

Beki Zana Coulibaly ameshindwa kufikia matarajio ya wengi licha ya kupewa muda wa kutosha kuonyesha makali yake

Beki huyo raia wa Burkina Fasa amepoteza kujiamini, akicheza chini ya kiwango katika michezo ya hivi karibuni

Jana katika mchezo dhidi ya Sevilla, Coulibaly alikumbana na wakati mgumu kutoka kwa baadhi ya mashabiki waliokuwa wakimzomea mara kwa mara kila alipogusa mpira

Kocha Patrick Aussems alimfanyia mabadiliko kwenye kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Nicholas Gyan

Zana alisajiliwa Simba akiwa na matarajio ya kuziba pengo la Shomari Kapombe ambaye bado yuko nje tangu mwishoni mwa mwaka jana alipopata majeraha wakati akiitumikia timu ya Taifa

Beki huyo huenda akawa miongoni mwa wachezaji watakoachwa katika kikosi cha Simba

AUSSEMS: Ataja sababu ya kubadili kikosi kizima mechi ya Sevilla

Jana Simba nusura iondoke na ushindi wa kihistoria dhidi ya Sevilla katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki uliopigwa uwanja wa Taifa ukimalizika kwa Sevilla kushinda mabao 5-4

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems alifanya mabadiliko ya wachezaji tisa kwenye kipindi cha pili, mabadiliko yanayotajwa kupunguza kasi ya Simba na kupoteza uongozi wa mchezo huo baada ya kuruhusu mabao matatu ndani ya dakika 10

Kocha Mkuu wa mabingwa hao wa Tanzania Bara Patrick Aussems ametetea uamuzi wake akisema ilikuwa muhimu kwa kila mchezaji kupata nafasi kwani ulikuwa ni mchezo wa kihistoria kwa wachezaji wa Simba

“Nilitaka kila mchezaji acheze dhidi ya timu bora kama ya Sevilla,” Aussems aliwaambia waandishi wa habari

“Niliona ni fursa ya kila mchezaji kuweza kucheza mchezo huu dhidi ya Sevilla ili kuweza kupata Uzoefu zaidi ndio maana niliwapa nafasi wachezaji karibia wote kucheza mechi hii kubwa na ya kihistoria dhid ya klabu bingwa mara tano ligi ya Europa”

Simba iliongoza mchezo huo kwa muda mrefu lakini ikapoteza mchezo mwishoni

Mabao ya Simba yalifungwa na John Bocco (2) aliyeibuka nyota wa mchezo, Meddie Kagere na Clatous Chama