Zahera atua, kuiongoza Yanga dhidi ya Alliance Fc

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amewasili usiku wa kuamkia leo Jumatano kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na ataungana na kikosi cha Yanga kinachoondoka kesho kuelekea jijini Mwanza

Zahera alikuwa DR Congo kutimiza majukumu ya timu ya Taifa ambapo wamefanikiwa kukata tiketi ya kutinga fainali za AFCON 2019 kama ilivyo kwa Tanzania

Yanga inatarajiwa ‘kukwea pipa’ kesho Alhamisi kuelekea Mwanza tayari kwa mchezo wa robo fainali kombe la Azam (ASFC) dhidi ya Alliance Fc

Mchezo huo utapigwa katika uwanja wa CCM Kirumba, Jumamosi, March 30 2019

Tambwe, Makambo, Ngasa wanolewa kuibeba Yanga dhidi ya Alliance FC

Mwishoni mwa wiki hii Yanga inakabiliwa na mchezo muhimu wa robo fainali kombe la Azam (ASFC) dhidi ya Alliance Fc utakaopigwa March 30 kwenye uwanja wa CCM Kirumba

Kocha Msaidizi wa Yanga Noel Mwandila amesema ni lazima wajiandae kikamilifu kuhakikisha wanapata matokeo yatakayo-wapeleka hatua ya nusu fainali

Kocha huyo anayekaimu nafasi ya Zahera, amesema wanaufahamu ubora wa Alliance Fc, kupitia michezo miwili ambayo wamekutana nao kwenye ligi, wanafahamu nini wafanye ili waweze kupata matokeo

“Hatuna cha kupoteza kuelekea mchezo huo tupo makini kila idara tunapambana kuhakikisha tunapata matokeo uwanja wa Kirumba, sio kazi rahisi kwetu kwani tunakutana na wapinzani ambao ni bora kila idara,” Mwadila amenukuliwa na Mwanaspoti

“Wana nguvu, wachezaji vijana na wana kasi tunatarajia kukutana na changamoto kubwa kutoka kwao lakini tumejipanga kukabiliana nazo kwasababu tunatambua umuhimu wa mchezo huo, Ngassa na Makambo wanakasi ya kukimbia na mipira Tambwe atakaa tayari kwaajili ya kumalizia mipira mirefu itakayokuwa inapigwa”

Mwandila ameongeza kuwa hawawezi kucheza mchezo sawa na wapinzani wao wanatarajia kutumia mbinu mbadala ambayo itawasaidia wao kupata matokeo kama ilivyokuwa michezo iliyopita na kuweka wazi kuwa lengo lao ni kupata matokeo mapema ili kuwatoa mchezoni wapinzani wao.

Yanga imekutana mara mbili na Alliance Fc katika michezo ya ligi na Yanga kushinda yote

Kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Taifa Yanga ilishinda mabao 3-0 kabla ya kushinda 1-0 katika mchezo wa marudiano uliopigwa dimba la CCM Kirumba

Itarejea mkoani Mwanza tena katika uwanja wa CCM Kirumba dhidi ya vijana hao machachari kuwania tiketi muhimu ya kutinga nusu fainali kombe la FA (ASFC)

Baada ya mchezo huo, Yanga itaendelea kutumia dimba la CCM Kirumba kwa michezo yake yote ya nyumbani wakati uwanja wa Taifa utakapokuwa umefungwa kupisha michuano ya kombe la AFCON ya vijana

Zahera kuiwahi Alliance Fc

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera anatarajiwa kurejea Jumatano kuungana na kikosi cha timu hiyo kinachojiandaa na mchezo wa robo fainali kombe la FA dhidi ya Alliance Fc.

Jana Zahera akiwa kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, alikiongoza kikosi cha timu hiyo kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Liberia na kukata tiketi ya kufuzu fainali za AFCON 2019

Mwishoni mwa wiki hii Yanga itaelekea mkoani Mwanza kuikabili Alliance Fc katika mchezo utakaopigwa dimba la CCM Kirumba, March 30 2019

Kwa sasa Yanga inajifua chini ya kocha msaidizi Noel Mwandila

Yanga yakanusha Zahera, Ajib kuondolewa watia saini akaunti CRDB

Yanga yakanusha Zahera, Ajib kuondolewa watia saini akaunti CRDB

Uongozi wa klabu ya Yanga umewataka wapenzi, wanachama na mashabiki wa timu hiyo kupuuza taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Kamati ya kuhamasisha uchangiaji iliyochini ya Mh Athony Mavunde imependekeza kuondolewa kwa Kocha Mwinyi Zahera na nahodha Ibrahim Ajib katika miongoni mwa watia saini wa akaunti ya kukusanya michango iliyofunguliwa benki ya CRBD

Msemaji wa klabu ya Yanga Dismas Ten ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo amesema hakuna ukweli wowote katika taarifa hiyo na amesisitiza wanaoisambaza ni wenye malengo ya kutaka kuikwamisha Yanga katika mpango wa kujijenga kwa ajili ya msimu ujao

“Hakuna sehemu hata moja kamati imekaa na kuzungumza haya. Huu ni uzushi upuuzwe na apuuzwe aliyeuandika,” amesema Ten

“Uongozi kupitia kamati hii ya Mh Mavunde ipo kwenye mikakati mizuri kuhakikisha klabu inavuka kwenye kipindi hiki kifupi wakati ikielekea kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi na mabadiliko mengine”

“Tukumbuke fedha hizi zinakusanywa maaalumu kwa ajili ya usajili na mambo mengine yenye manufaa kwa klabu”

Jana Kamati ya Uhamasishaji ilikutana kwa mara ya kwanza ambapo mpango wa kuchangisha kiasi cha Bil 1.5 uliandaliwa mkakati wa utekelezaji katika kila mkoa

Mzee Akilimali augua Bagamoyo

Hali ya Mwanachama maarufu wa klabu ya Yanga Mzee Ibrahim Akilimali inaelezwa sio nzuri ambapo amelazwa Hospitali ya Baobab akiendelea na matibabu ya ugonjwa kisukari

Mzee Akilimali amewaomba wadau wa Yanga na Watanzania wote kwa ujumla wamuombee ili aweze kupona maradhi yanayomsumbua

“Hali yangu sio nzuri. Niko huku Bagamoyo najiuguza maradhi ya kisukari. Mniombee kwani kisukari kinanitesa sana,” Mzee Akilimali amenukuliwa na Spoti Xtra

Mzee Akilimali ni miongoni mwa wanachama wa Yanga vinara wa kutoa maoni juu ya masuala mbalimbali ya klabu hiyo

Wakati mwingine hujikuta akiingia katika mgogoro na wanachama wenzake, wakimtuhumu kuwa ni mpinga maendeleo.

Ajib mgonjwa, kuikosa Lipuli Fc

Nahodha wa Yanga Ibrahim Ajib ameondolewa katika kikosi kinachosafiri kwenda mkoani Iringa baada ya kuugua

Yanga itaikabili Lipuli Fc bila ya kuwa na mpishi wake huyo wa mabao aliyehusika katika mabao 21 kati ya 45 yaliyofungwa kwenye ligi

Hata hivyo kukosekana kwake hakuwezi kuwa tatizo kwa kikosi cha Mwinyi Zahera kilichosheheni viungo wengi

Mohammed Issa ‘Banka’, Thabani Kamusoko na Haruna Moshi ‘Boban’ wote wanaweza kucheza nafasi yake.

Kwa michezo ya hivi karibuni, Ajib amekuwa akitokea benchi kuongeza nguvu kwenye kipindi cha pili

Changamoto pekee inayoikabili Yanga huenda ikabaki kwenye safu ya ulinzi baada ya kukosekana kwa Andrew Vicent ambaye ni majeruhi na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ aliyefungiwa michezo mitatu

Kocha Noel Mwandila huenda akalazimika kumtumia kiraka Said Juma Makapu kwenye nafasi ya ulinzi sambamba na mkongwe Kelvin Yondani.

Pia yupo beki aliyepandishwa kutoka Yanga B Cleosaf Sospeter

SABABU Za AJIBU Kuanzia BENCHI

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amewataka wanaohoji kwa nini nahodha wa kikosi cha timu hiyo Ibrahim Ajib haanzi katika michezo ya hivi karibuni kuwa watulie kwani yeye ndiye anayefahamu mahitaji ya kila mechi

Katika mahojiano na Radio UFM, Zahera amesema huwa anapanga kikosi chake kufuatana na mahitaji ya mpinzani anayekutana nae

“Kwa wanaofuatilia wanafahamu, sio Ajib tu ambaye huwa anapumzika, nimekuwa nikibadili wachezaji mara kwa mara kufuatana na mahitaji ya mchezo,” alisema Zahera

“Mabadiliko haya ni ya kawaida, haimaanishi kwamba Ajib kashuka kiwango au nina ugomvi nae”

“Wapo watu ambao kazi yao ni kufanya uchonganishi Yanga, nawashauri wafanye mambo mengine yenye faida kwao”

Baada ya kuwa na mwenendo mzuri tangu akabidhiwe kitambaa cha unahodha, Ajib amehusika kwa kucheza michezo mingi ya Yanga kabla ya michezo mitatu iliyopita ambayo yote hakuanza

Ajib amefunga mabao sita msimu huu na kutoa pasi za mabao 15.

Mpaka sasa ndiye mchezaji mwenye mafanikio zaidi kwenye ligi kwani kati ya mabao 45 ayliyofungwa na Yanga, Ajib amehusika katika mabao 21

YANGA: Yapigwa FAINI 6 Million

🤗Klabu ya Yanga imetozwa faini ya jumla ya sh. 6,000,000 (milioni sita) kwa kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi kutoingia vyumbani na kusababisha wachezaji wakaguliwe kwenye korido, na pia kutotumia njia maalum iliyowekwa kwa ajili ya kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch) katika mechi hiyo iliyochezwa Februari 16, 2019 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Adhabu imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
.
.
Nini maoni yetu?