NINJA : Afungiwa Mechi Tatu

Kamati ya Nidhamu ya TFF imemfungia mchezaji wa timu ya Yanga Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kutocheza mechi tatu mfululizo baada ya kamati hiyo kubaini kuwa mchezaji huyo ametenda kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa timu ya Coastal Union katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania bara uliochezwa mkoani Tanga

Suala la Ninja liliamuliwa juzi katika kikao cha Kamati hiyo kilichoketi jijini Dar es salaam

Ninja atakosa mchezo wake wa kwanza dhidi ya Lipuli Fc, March 16 2019

Kabwili augua Yanga ikijiandaa kuikabili KMC

Kesho Jumapili kikosi cha Yanga kitashuka dimba la Taifa kuikabili KMC katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara unaotarajiwa kuanza saa kumi kamili jioni

Katika mchezo wa kesho Yanga itakosa huduma ya mlinda lango wake kinda Ramadhani Kabwili ambaye ni mgonjwa

Hata hivyo, mkufunzi wa makipa Juma Pondamali amesema hana wasiwasi na kusokena kwa Kabwili kwa kuwa Kindoki na Hamid wapo

Yanga itaingia kwenye mchezo wa kesho ikiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa mzunguuko wa kwanza, bao lililowekwa kimiani na Feisal Salum ‘Fei Toto’ kwa mkwaju wa adhabu kwenye dakika za lala salama

Ligi Kuu ya Tanzania Bara inaendelea leo kwa michezo minne kupigwa kwenye viwanja mbalimbali

Chikupe aongeza nguvu kikosi cha Yanga

Beki kisiki wa Yanga Andrew Vicent Chikupe amerejea katika mazoezi ya mabingwa hao wa kihistoria yanayoendelea uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar es salaam

Chikupe maarufu kama ‘Dente’ alikuwa nje ya dimba tangu alipopata majeraha kwenye mchezo wa kombe la FA dhidi ya Namungo Fc uliofanyika Februari 24 mkoani Lindi

Yanga inajiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya KMC utakaopigwa keshokutwa Jumapili kwenye uwanja wa Taifa

Vinara hao wa ligi watakuwa na nafasi ya kujikita zaidi kileleni mwa msimamo kwani kama wataibuka na ushindi, watafikisha alama 67

Ajib, Tshishimbi waandaliwa mikataba mipya Yanga

Baada ya nyota wake nahodha Ibrahim Ajib na Papi Tshishimbi kuingia kwenye rada za Simba, uongozi wa Yanga umeanza mazungumzo na wachezaji hao ili kuongeza mikataba yao, imefahamika

Mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya usajili ya Yanga amesema wamebaini kama watasubiri mpaka mwishoni mwa msimu ambapo mikataba yao itakuwa imemalizika kabisa, kuna uwezekano mkubwa wa kuwapoteza wachezaji hao ambao wako katika mipango ya kocha Mwinyi Zahera kwa ajili ya msimu ujao

“Ajib na Tshishimbi ni wachezaji muhimu ambao kocha anawahitaji kwa ajili ya msimu ujao. Sio hao tu, kocha ametuagiza tuhakikishe wachezaji wote anaowahitaji kwa ajili ya msimu ujao hawachukuliwi na timu nyingine,” alisema Mjumbe huyo wa Kamati ya usajili ambaye hakutaka jina lake liwekwe hadharani kwa kuwa yeye sio msemaji wa Yanga

Hivi karibu imeripotiwa kuwa Simba imeanza mkakati wa kumrejesha Ajib kunako klabu hiyo aliyoikacha mwaka 2017 huku Tshishimbi akihusishwa na mabingwa hao wa ligi kuu msimu uliopita pamoja na klabu ya Azam Fc

Zahera ameuagiza uongozi wa Yanga kuhakikisha unawapa mikataba mipya wachezaji wote anaowahitaji kabla ya msimu kumalizika

Zahera amesema kusubiri mikataba ya wachezaji hao kumalizika kabisa kutaigharimu zaidi Yanga hasa kama wachezaji hao watakuwa wakiwaniwa na timu nyingine

Jana kwenye Mkutano wa viongozi wa matawi ya Yanga, Zahera alisema anakusudia kusajili wachezaji sita wa kigeni ambao mchakato wa usajili wao anakusudia kuukamilisha kabla ya msimu kumalizika

Amewataka Wana Yanga waendelee kuhamasishana katika kuichangia timu hiyo kwani fedha hizo ndizo zitakazotumika katika usajili wa wachezaji hao na wale ambao mikataba yao inaelekea ukingoni

Zahera amesema msimu ujao anataka kutengeneza kikosi imara ambacho kitaipa mafanikio Yanga kwenye ligi na michuano ya Kimataifa.

Kwa sasa Yanga inapigania kupata moja ya nafasi za kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano CAF msimu ujao

Kutimiza hilo ni lazima itwae taji la ligi kuu au kombe la FA (ASFC)

YANGA: Yaingia Kambini Kuiwinda KMC

Kikosi cha vinara wa ligi kuu ya Tanzania Bara Yanga kinaingia kambini leo katika Hotel ya Nefaland kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya KMC

Mchezo huo utapigwa keshokutwa Jumapili, March 10 2019 saa kumi kamili jioni katika uwanja wa Taifa

Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh amesema wachezaji 20 wanatarajiwa kuingia kambini leo jioni kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo huo

Tangu irejee kutoka Mwanza ambako iliichapa Alliance Fc bao 1-0, Yanga imekuwa ikijifua kwenye uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar es salaam

DISMAS TEN: Afunguka kuhusu Usajili wa NDEMLA

Kwa siku za karibuni kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Msemaji wa klabu ya Yanga Dismas Ten amekuwa akimposti kiungo wa Simba Said Khamis Ndemla huku akiweka jumbe zinazoashiria kuwa huenda mabingwa hao wa kihistoria wanaiwania sahihi ya kiungo huyo kwa ajili ya msimu ujao

Ndemla nusura asajiliwe na Yanga katika usajili wa mwanzoni mwa msimu huu kabla hajaamua kubaki Simba kwa kuongeza mkataba wa mwaka mmoja

Jana Ten alifunguka kuhusu tetesi za Yanga kumuwania Ndemla ambapo amekiri kuwa kiungo huyo ana uwezo mkubwa lakini ana bahati mbaya hapati nafasi katika klabu yake ya Simba

“Ndemla ni mchezaji mzuri sana. Mtu yeyote ukimuuliza katika wachezaji wa Tanzania wenye vipaji hawezi kukosa kumtaja Ndemla,” amesema Ten

“Ndemla mimi ni rafiki yangu, suala la kusajili au kutosajiliwa na Yanga hilo linahusu benchi la ufundi na Kamati yetu ya usajili. “

“Yote yanaweza kusemwa mwisho wa msimu lakini kwa sasa hivi huwezi kuzungumza lolote lakini anabaki kuwa ni mchezaji mwenye kipaji na kila mtu anaona”

“Amekuwa ni mchezaji mwenye mwenendo mzuri licha ya kuwa sasa hapati nafasi kwenye timu yake”

Wakati msimu ukielekea ukingoni tayari timu zimeanza ‘kupigana vikumbo’ kuwania wachezajia ambao mikataba yao inaelekea ukingoni

ZAHERA: Michango ya Wanayanga Ipo SALAMA

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amewahakikishia wapenzi, mashabiki na Wanachama wa klabu ya Yanga kuwa pesa wanazoichangia timu yao ziko salama na wapuuze taarifa zinazosambazwa zinazodai kuwa kuna fedha zimetolewa ‘kinyemela’

Akizungumza mapema leo katika mazoezi ya Yanga yanayofanyika uwanja wa chuo cha Polisi, Kurasini jijini Dar es salaam, Zahera amesema wanaotoa taarifa hizo wana lengo la kuwavunja moyo Wana Yanga ili wasiendelee kuichangia timu yao

“Nawaambia watu wengi wanapenda timu yetu iharibike. Kuna watu wanafanya matangazo mengi ya kusema kama mchango unaofanyika viongozi wanakula pesa”

“Wanasema kuna viongozi wanakula milioni tatu, ni uongo. Hakuna hata elfu moja, senti moja ambayo inatoka katika pesa hiyo ambayo watu wanachangia.” amesema Zahera

“Hakuna hata kiongozi mmoja ambaye ana ruhusa ya kugusa iyo pesa”

Naye nahodha wa Yanga Ibrahim Ajib amesema hakuna namna yoyote ambayo fedha hiyo inaweza kutolewa bila kuidhinishwa na watia saini watatu ambao ni yeye(Ajib), Kocha Mwinyi Zahera na Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh

“Kama fedha inatakiwa kutolewa ni lazima wote watatu tusaini, hivyo taarifa inayosambazwa ni uongo kwani jambo hilo haliwezekani”

Jana kupitia Redio One, mtu aliyejitambulisha kama mwanachama wa Yanga Suleiman Kato alidai kiasi cha pesa milioni tatu zilizochangwa na mashabiki wa Yanga kupitia mitandao ya simu zilitolewa kwenye mtandao husika na kuhamishiwa kwenye Bank moja iliyopo Kariakoo ambapo aliwatuhumu Kaimu katibu Omary Kaaya pamoja na Mhasibu na baadhi ya viongozi kushirikiana katika hujuma hiyo

Hatuwahofii Alliance Fc, tukutane Mwanza -Dismas Ten

Misimu miwili iliyopita Yanga ilitolewa kwenye michuano ya kombe la Azam (ASFC) na Mbao Fc katika hatua ya nusu fainali ambapo mchezo ulipigwa dimba la CCM Kirumba

Yanga itarudi tena Mwanza katika uwanja huohuo kuikabili Alliance Fc lakini ikiwa ni mchezo wa hatua ya robo fainali

Afisa Habari wa Yanga Dismas Ten amesema hawana hofu ya kuikabili Alliance Fc kwa mara nyingine na watajiandaa kikamilifu ili waweze kushinda mchezo huo na kutinga hatua ya nusu fainali

Baada ya kukosa ushindi kwa misimu kadhaa kwenye dimba la CCM Kirumba, msimu huu Yanga imetakata katika dimba hilo kwa kufanikiwa kuzifunga Mbao Fc na Alliance

“Tunafahamu Mwanza ni pagumu, ili kupata ushindi kwenye uwanja wa CCM Kirumba unapaswa kuwa umejiandaa kwelikweli,” amesema Ten

“Msimu huu tumefanya vizuri katika michezo yote miwili tuliocheza Mwanza, naamini tunao uwezo wa kupata matokeo kwa mara nyingine”

“Tunaiheshimu Alliance, tunafahamu ni timu nzuri lakini kucheza na Yanga ni kitu tofauti”

Kama Yanga itashinda mchezo huo utakaopigwa kati ya March 25-28, kwenye hatua ya nusu fainali itachuana na mshindi kati ya Lipuli Fc dhidi ya Singida United, mchezo ambao utakuwa wa ugenini

Mchezo wa fainali utapigwa uwanja wa Ilulu mkoani Lindi mwishoni mwa msimu