YANGA vs ALLIANCE FC : Robo Fainali ASFC

Droo ya hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la Azam (ASFC) imefanyika leo ambapo vinara wa ligi kuu ya Tanzania Bara Yanga watachuana na Alliance Fc katika mchezo wa robo fainali utakaopigwa kati ya March 25-28 2019
Mchezo huo utapigwa dimba la CCM Kirumba.

Hii itakuwa mara ya tatu kwa Yanga kuchuana na Alliance Fc msimu huu, mara ya pili kwa timu hizo kuchuana uwanja wa CCM Kirumba kwenye mwezi huu wa tatu

Kagera Sugar itakuwa nyumbani kuchuana na Azam Fc katika mchezo mwingine wa robo fainali wakati KMC itakuwa mwenyeji wa African Lyon.

Mchezo mwingine ni kati ya Lipuli Fc itakayokuwa nyumbani kupepetana na Singida United

Michango yamkatisha tamaa Zahera

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema hataendelea kubaki katika klabu hiyo kama Wana Yanga hawatajitoa kuichangia timu kwa ajili ya mipango ya msimu ujao

Akihojiwa na moja ya redio maarufu nchini, Zahera amesema amekuwa akijitoa kuisaidia Yanga na alitarajia Wana Yanga nao watafanya hivyo wakati huu ambao timu inapita katika kipindi kigumu lakini hali imekuwa tofauti

“Wanasema Yanga ni timu ya Wananchi lakini mbona wananchi hao hawaonekani kuisaidia timu?” alihoji Zahera

“Msimu huu hatukuwa na malengo ya kutwaa ubingwa, sababu iko wazi, kikosi chetu hakijakamilisha mahitaji ya kuweza kuwa mabingwa”

“Nilitegemea Wana Yanga watachangia timu kama tulivyopendekeza ili msimu ujao tuweze kuwa na kikosi imara zaidi”

“Lakini kwa hali inavyoendelea mimi sitakuwa tayari kufanya kazi kwenye timu ambayo haina malengo.”

“Sitakuwa tayari kuendelea kuwasaidia watu ambao wenyewe hawajisaidii”

Zahera amefanya kazi kubwa msimu huu ambapo licha ya mapungufu yaliyopo, ameweza kuiweka Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ikipoteza michezo miwili tu

Kocha huyo Mcongomani anataka kuiona Yanga inatoka katika ‘ukata’.

Pendekezo la kuwataka Wana Yanga waichangie timu yao ni moja ya njia za muda mfupi zinazoweza kuifanya Yanga ikasimama wakati ikiendelea kuandaa mikakati ya kuweza kujitegemea kama walivyo watani zao Simba

Hata hivyo muitikio mdogo wa Wana Yanga katika kutoa michango umemfanya kocha huyo akate tamaa na pengine huenda akaondoka mwishoni mwa msimu kama mambo hayatabadilika

Wadau wapendekeza Harambee ya kuichangia Yanga

Ili kuongeza kasi ya uchangiaji wa klabu ya Yanga, baadhi ya wadau wamependekeza uongozi wa Yanga uandae ‘Harambee’ ambayo itakuwa ni siku maalumu kwa Wana Yanga kuichangia timu yao

Harambee hiyo inaweza kuandaliwa na kufanyika katika ukumbi utakaofaa ambapo utaratibu wa kutoa mwaliko kwa wadau wa Yanga unaweza kuandaliwa

Hapa waalikwe wananchi wa kawaida, watu maarufu, wafanyabishara, viongozi wa dini, viongozi wa Serikali kiufupi Yanga ina mtaji mkubwa wa watu, siku hiyo inaweza kutumika kuwaunganisha watu wote

Pia unaweza kuandaliwa utaratibu kwa tukio hilo kurushwa ‘mbashara’ katika runinga na redio mbalimbali ili wadau wengine ambao hawakualikwa waweze kushiriki kwenye Harambee hiyo kupitia vyombo vyao vya habari

Uchangiaji utafanyika ukumbini kwa kuwashirikisha wadau walioalikwa huku pia namba za kuchangia zikiendelea kutangazwa kwa wale wanaofuatilia kupitia vyombo vya habari ili waweze kuchangia

Utaratibu huu sio mgeni umekuwa ukitumiwa na watu binafsi na taasisi mbalimbali katika kuzishirikisha jamii zao linapokuja suala la uchangiaji wa fedha

Michezo 12 kuamua hatma ya ubingwa Yanga

Kimahesabu Yanga bado inayo nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu kama itachanga vyema karata zake

Michezo 12 iliyosalia inaweza kuipa Yanga alama 36 na kuwafanya mabingwa hao wa kihistoria kuweza kufikisha alama 100

Habari njema kwa Yanga ni kuwa haina kibarua kikubwa sana cha michezo ya mikoani ukilinganisha na wapinzani wao katika mbio za ubingwa Simba

Simba iliyoshuka dimbani mara 20 bado ina deni la michezo 18 hivyo kuwafanya bado wawe na kazi kubwa licha ya kuwa na faida ya kimahesabu iwapo wataweza kushinda michezo yao yote

Yanga imebakiza michezo minne tu ya nje ya jiji la Dar es salaam huku michezo nane ikitarajiwa kupigwa uwanja wa Taifa

Michezo ya ugenini ambayo itapigwa nje ya jiji la Dar es salaam ni dhidi ya Mtibwa Sugar, Lipuli Fc, Ndanda na Biashara wakati michezo dhidi ya Azam Fc na Ruvu Shooting ni ya ugenini lakini itapigwa jijini Dar es salaam

Michezo iliyobaki ambayo Yanga ni mwenyeji ni dhidi ya KMC, African Lyon, Prisons, Mbeya City, Azam Fc na Kagera Sugar

FULL TIME: YANGA 1-0 ALLIANCE FC

Vinara wa ligi kuu ya Tanzania Bara Yanga wameendelea kujikita kileleni katika msimamo wa ligi baada ya kuichapa Alliance Fc bao 1-0 katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa dimba la CCM Kirumba

Ulikuwa ni mchezo wa ushindani kutoka kwa kila upande ambapo kikosi cha Alliance Fc kimeonekana kuimarika sana tofauti na wakati timu hizo zilipokutana kwenye dimba la Taifa mwaka jana

Bao pekee la Yanga liliwekwa kimiani na mshambuliaji mkongwe Amissi Tambwe kwenye dakika ya 75 ya mchezo

Hilo lilikuwa bao la nane kwa Tambwe msimu huu

Katika mchezo huo Heritier Makambo alikosa mkwaju wa penati mapema tu kwenye dakika ya sita baada ya yeye mwenyewe kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari

Matokeo hayo yameifanya Yanga iendelee kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 64

Yanga tayari iko Mwanza, Alliance wajiandae

Kikosi cha mabingwa wa kihistoria Tanzania Yanga kimewasili salama jijini Mwanza tayari kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Alliance Fc

Mchezo huo utapigigwa keshokutwa Jumamosi, March 02 2019 katika uwanja wa CCM Kirumba

Yanga iliondoka jijini Dar es salaam Alfajiri ya leo Alhamisi ikiwa na msafara uliojumuisha wachezaji 20 na viongozi nane wakiwemo wa benchi la ufundi

Baada ya hivi karibuni ‘kuvunja mwiko’ kwa kuchukua alama tatu dhidi ya Mbao Fc katika dimba la CCM Kirumba, Yanga imepania kuchukua alama nyingine tatu mbele ya Alliance Fc

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema anatambua matokeo tofauti na ushindi yatapunguza matumaini ya timu hiyo kutwaa ubingwa hivyo wamejipanga kushinda

Chikupe kuikosa Alliance Fc, Kamusoko arejea

Beki kisiki Andrew Vicent Chikupe ataukosa mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya Alliance dhidi ya Yanga utakaopigwa keshokutwa Jumamosi March 02 katika uwanja wa CCM Kirumba

Chikupe aliumia katika mchezo wa kombe la Azam (ASFC) uliopigwa Jumapili iliyopita mkoani Lindi na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo FC. Matokeo yaliyoipeleka Yanga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo

Nae kiungo Thabani Kamusoko aliyekuwa majeruhi kwa wiki kadhaa amejumuishwa katika kikosi kilichosafiri jijini Mwanza kwa ajili ya mchezo huo

Mbali na Chikupe, mshambuliaji Matheo Anthony na kiungo Pius Buswita nao hawakusafiri na timu

YANGA KUELEJEA MWANZA KESHO

Kikosi cha Yanga Sc kikiwa na wachezaji 20 pamoja na viongozi 8 kutoka bechi la ufundi, kesho asubuhi kitasafiri kwa ndege kuelekea Mwanza, tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya wenyeji @alliancefootballclub2011 utakaopigwa katika uwanja wa #ccmkirumba 2/3/2019 saa 10:00 jioni.
.
Nahodha @ibrahimajibu23 amesema Ni mchezo muhimu na mgumu, lakini maandalizi mazuri yaliyofanyika kikosini yataleta matokeo mazuri baada ya dakika 90 za mchezo.

KABWILI Aruhusiwa kutoka Hospitalini

Mlinda lango wa Yanga Ramadhani Kabwili jana aliruhusiwa kutoka Hospitalini baada ya kufanyiwa vipimo vya jeraha la nyonga alilopata kwenye mchezo dhidi ya African Lyon.

Kabwili alikimbizwa hospitalini baada ya kupata majeraha hayo katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0

“Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu,pili naishukuru klabu yangu kwa kunijali na kuhakikisha napata huduma sahihi,” alisema Kabwili baada ya kuruhusiwa

“Pia awashukuru mashabiki wetu walioungana na mimi hospitalini, mpaka sasa naendelea vizuri.

“Nawapongeza wachezaji wenzangu kwa ushindi wa leo sasa tunaangalia mchezo unaofuata, najisikia vema, Ahsanteni sana”