Mabingwa wa kihistoria Tanzania, Yanga wameendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa African Lyon bao 1-0 katika mchezo uliopigwa dimba la Sheikh AMri Abeid mkoani Arusha.
Bao pekee la Yanga lilipatikana kwenye dakika ya 64 likiwekwa kimiani na beki ‘mbishi’ Abdallah Shaibu ‘Ninja’ aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Ibrahim Ajib ‘Miguu ya dhahabu’
Hilo lilikuwa bao la pili kwa Shaibu msimu huu huku Ajib akiendelea kujiongezea ‘assists’ sasa zikifika 12
Licha ya kukabiliwa na changamoto ya uwanja, Yanga ilicheza vizuri hasa katika kipindi cha pili.
Mabingwa hao wa kihistoria walipata pigo katika mchezo huo baada ya kuwapoteza wachezaji wake wawili kutokana na majeruhi.
Jaffard Mohammed alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia katika dakika ya 14 na nafasi yake kuchukuliwa na Deus Kaseke.
Mlinda lango tegemeo Ramadhani Kabwili nae aliumia nyonga na kushindwa kuendelea na mchezo katika dakika ya 38 na nafasi yake kuchukuliwa na Klaus Kindoki
Kabwili alikimbizwa Hospitalini kupatiwa matibabu zaidi
Ushindi huo umeikita Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama saba baada ya kufikisha alama 47














