Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema baada ya kupoteza mchezo wa nusu fainali kombe la FA kwa kufungwa mabao 2-0 na Lipuli Fc leo, wanahamishia nguvu zao kwenye ligi kuhakikisha wanashinda michezo minne iliyobaki
Zahera amesema licha ya kutofanikiwa kutinga fainali, msimu huu wamevuka malengo na matarajio ya awali
“Hakuna kitu kitabadilika juu ya mipango yetu, tunahitaji kushinda mechi nne zilizobakia ligi kuu,” amesema Zahera
“Ukiangalia mpaka hapa tumefanikiwa kuliko matarajio. Mwaka huu tulianza ligi tukiomba mungu atusaidie japo tumalize nafasi ya sita au ya saba”
“Tulipaswa kumaliza nafasi ya sita au saba kutokana na changamoto tulizopitia msimu huu. Tulikubaliana tufanye nguvu tusimalize chini ya nafasi ya kumi”
“Mkiangalia tunaongoza ligi tokea mwanzo wa msimu mpaka leo. Malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi na hata kombe la FA yalikuja baada ya kuona tumeweza kufanya vizuri licha ya changamoto zilizokuwa zinatukabili”
“Kazi waliyofanya wachezaji wangu ni nzuri sana. Tutaendelea kupambana kwenye ligi ili tuweze kushinda michezo yote minne iliyobaki”
Aidha akizungumzia mabadiliko aliyofanya kwenye kipindi cha pili amesema ilikuwa ni kazima kuwatoa Ajib na Mohammed Issa na kuwaingiza Tambwe na Juma Abdul ili kwendana na aina ya uchezaji wa Lipuli Fc
“Lipuli walikuwa wengi katikati hivyo nililazimika kumuingiza Tambwe na Abdul ili kutumia mipira ya krosi kupitia pembeni kujaribu kusaka mabao ya kusawazisha”
“Mfumo huo ulitusaidia kwani tulipata karibu nafasi tatu za kuweza kufunga lakini tulikosa bahati”