Sevilla yaahirisha mchezo dhidi ya Singida United

May 23 2019 Simba itacheza mchezo wa Kimataifa wa kirafiki dhidi ya Sevilla inayoshiriki ligi kuu ya Hispania maarufu kama La Liga

Hata hivyo kulingana na ratiba ya ligi iliyotolea awali na Bodi ya Ligi, May 22 Simba ilipaswa kuwa mkoani Singida kucheza na Singida United

Bodi ya ligi imelazimika kuahirisha mchezo huo dhidi ya Singida United

Huenda Simba ikacheza na Singida United baada ya mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa May 28 kwani baada ya kuikabili Sevilla, May 25 Simba itacheza na Biashara United mchezo utakaopigwa uwanja wa Taifa

Simba yasaka alama tatu dhidi ya Mbeya City leo

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba wako mkoani Mbeya ambapo leo watashuka dimba la Sokoine kuwakabili wenyeji wao Mbeya City

Simba inayoshika nafasi ya pili baada ya kujikusanyia alama 72, inahitaji ushindi katika michezo saba tu ili kuubakisha ubingwa Msimbazi

Msemaji wa Simba Haji Manara amesema wachezaji wa timu hiyo wako katika hali nzuri tayari kwa mchezo huo

“Timu imewasili salama mkoani Mbeya tayari kwa mchezo. Tunafahamu hautakuwa mchezo mwepesi lakini wachezaji wetu watapambana kuhakikisha tunaondoka na alama zote tatu,” amesema

Katika mchezo wa leo, Simba itamkosa nahodha wake John Bocco ambaye aliumia kwenye mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania

Wengine watakaokosekana ni Asante Kwasi, Paschal Wawa na Shomari Kapombe

Baada ya mchezo huo Simba itaendelea kubaki mkoani Mbeya ambapo keshokutwa May 05 itachuana na Tanzania Prisons

Simba yamlilia Dk Mengi

Uongozi wa klabu ya Simba umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Dk Reginald Mengi kilichotokea jana Dubai

Taarifa iliyotolewa na Simba imesema klabu inaungana na familia na Watanzania katika kuomboleza msiba huo mkubwa

Simba yawasili salama Mbeya

Msafara wa kikosi cha Simba umewasili salama mkoani Mbeya tayari kwa michezo miwili ya ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons

Simba iliondoka jijini Dar es salaam mchana wa leo Alhamisi kwa usafiri wa Ndege

Kesho May 03 itacheza mchezo wa kwanza dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wa Sokoine na siku mbili baadae kurudi tena katika uwanja huo kuikabili Tanzania Prisons

Prisons iko jijini Dar es salaam ambapo leo imecheza na Yanga na kufungwa mabao 2-1, itachuana na Simba May 05

FT : Yanga 2-1 Prisons

Yanga imeendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kuichapa Tanzania Prisons mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam

Yanga iliyokuwa bora katika mchezo wa leo, ilifunga mabao yake kupitia kwa Wacongomani Papi Tshishimbi na Heritier Makambo wakati bao la kufutia machozi kwa upande wa Prisons lilifungwa na Ismail Kada

Tshishimbi ndiye aliyeanza kuifungia Yanga bao la kuongoza kwenye dakika ya 23 akimalizia mpira wa adhabu uliochongwa na Ibrahim Ajib

Hilo lilikuwa bao la 16 kutengenezwa na Ajib msimu huu

Dakika tisa baadae Kada aliisawazishia Prisons akiujaza mpira wavuni baada ya walinzi wa Yanga kuzembea kuondoa mpira wa kona

Makambo aliihakikishia Yanga ushindi kwenye dakika ya 66 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Paulo Godfrey ‘Boxer’

Ushindi huo umeifanya Yanga kuwa timu ya kwanza kufikisha alama 80 msimu huu na kuendelea kujikitia kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama nane dhidi ya Simba inayoshika nafasi ya pili ikiwa na alama 72

Baada ya ushindi huo, Yanga itaelekea mkoani Iringa tayari kwa mchezo wa nusu fainali kombe la FA (ASFC) dhidi ya Lipuli, mchezo ukitarajiwa kupigwa Jumapili, May 05

Makambo awafikia Aiyee, Kagere

Bao alilofunga Heritier Makambo katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons limemfanya mshambuliaji huyo afikishe mabao 16 na kuwafikia Salum Aiyee wa Mwadui Fc na Meddie Kagere wa Simba

Leo Makambo ameiongoza Yanga kuibuka na ushindi muhimu wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons

Mshambuliaji huyo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, anayo nafasi ya kuibuka mfungaji bora msimu huu kama ataweza kuitumia vyema michezo minne iliyobaki kujiongezea mabao

Michezo iliyobaki ni dhidi ya Ruvu Shooting, Mbeya City, Biashara United na Azam Fc

Ni mchezo mmoja tu dhidi ya Biashara United ambao utapigwa nje ya jiji la Dar es salaam

Wawa aanza mazoezi, kurejea kikosini karibuni

Beki kisiki wa Simba Paschal Serge Wawa ameanza mazoezi mepesi tayari kurejea dimbani baada ya kuwa nje kwa zaidi ya wiki tatu

Wawa aliumia kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika kati ya Simba dhidi ya TP Mazembe uliopigwa uwanja wa Taifa

Wawa ameanza mazoezi binafsi na huenda akajumuishwa kwenye kikosi cha Simba kitakaporudi kutoka mkoani Mbeya

Mwenyewe amethibitisha kuwa hali yake inaendelea vizuri na tayari ameshaanza mazoezi binafsi

“Ninaendelea vizuri kwa sasa tofauti na awali na nimeanza mazoezi binafsi na sasa hivi ninafanya mazoezi ya Gmy,” amesema

Simba imecheza michezo sita ya ligi bila ya Wawa na imefanikiwa kushinda michezo mitano

Walinzi Juuko Murshidi, Paul Bukaba na Yusufu Mlipili wameweza kutimiza ipasavyo majukumu ya ulinzi wa kati wakishirikiana na mkongwe kiraka Erasto Nyoni

Igangula kuanza na uwanja wa Kaunda

Mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Baraka Igangula amesema kama atachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, atahitaji miezi mitatu tu kukamilisha ukarabati wa uwanja wa Kaunda ambao unamilikiwa na Yanga

Aidha Igangula anayechuana na Dk Mshindo Msolla, Dr Jonas Tiboroha na Elias Mwanjala kuwania uwenyekiti wa Yanga, amesema kutokana na uzoefu mkubwa aliyokuwa nao kwenye uongozi wa Yanga, ana lengo la kuifanyia timu hiyo mambo makubwa na kamwe hataweka mbele maslahi binafsi

“Tutakuwa na mpango wa muda mfupi ambao tutaukarabati uwanja wetu pale klabuni, huku tukiwa na mpango wa muda mrefu wa kujenga uwanja nje ya mji, hata ikiwezekana Kibaha, Pwani ambao utakuwa na hosteli, maduka na ofisi mbalimbali,” amesema Igangula

Igangula pia ameunga mkono mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa Yanga akiahidi kulikamilisha zoezi hilo haraka

“Nitasimamia mchakato wa mabadiliko na kuhakikisha unakamiliki punde tu nitakapoingia madarakani. Nitaajiri wataalamu wenye ujuzi wa masuala ya kampuni ili tuachane na utaratibu huu wa kuendesha klabu kwa mazoea”

Ahadi nyingine alizotoa Igangula ni kuanzisha bima ya afya itakayowalenga wanachama, saccos, vicoba na mfuko wa kufa na kuzikana, kama sehemu ya kuimarisha umoja, upendo na mshikamano baina ya wanachama na viongozi wa Yanga

Pia atahakikisha wachezaji na benchi la ufundi wanalipwa mishahara kwa wakati, kusimamia mikataba na mapato ili kudhibiti ufisadi

Uchaguzi wa Yanga utafanyika Jumapili, May 05 ukumbi wa bwalo la Polisi, Osterbay jijini Dar es salaam