Watatu kuikosa Tanzania Prisons leo

Leo Alhamisi jioni Yanga itakuwa dimba la Uhuru kuikabili Tanzania Prisons katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Yanga itamkosa mlinda lango Klaus Kindoki anayetumikia adhabu ya kadi tatu za njano

Pia beki wa kushoto Gadiel Michael alipata majeraha katika mchezo uliopita dhidi ya Azam Fc anatarajiwa kukosekana pamoja na mkongwe Kelvin Yondani ambaye leo anamaliza adhabu ya kukosa michezo mitatu

Yondani atarejea kikosini kwenye mchezo wa nusu fainali kombe la FA (ASFC) dhidi ya Lipuli Fc utakaopigwa mkoani Iringa, May 06 uwanja wa Samora

Yanga kusaka alama tatu mchezo dhidi ya Prisons leo

Ligi Kuu ya Tanzania Bara inaendelea leo kwa mchezo mmoja kupigwa ambapo vinara wa ligi hiyo Yanga watakuwa uwanja wa Uhuru kuikabili Tanzania Prisons

Yanga inahitaji kushinda mchezo huo ili kuendelea kuipa ‘presha’ Simba kwenye mbio za kuwania ubingwa msimu

Aidha, itakuwa ikisaka rekodi ya kuwa timu kwanza kufikisha alama 80 msimu huu

Wapinzani wao katika mbio za upingwa Simba wao wanaelekea mkoani Mbeya ambapo kesho May 03 watacheza na Mbeya City kisha May 05 watacheza na Tanzania Prisons

Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh amesema wachezaji wote wako katika hali nzuri, tayari kwa mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa kumi kamili jioni

Dk Msolla azindua kampeni Yanga

Mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti katika uchaguzi wa Yanga utakaofanyika May 05, Dk Mshindo Msolla amezindua kampeni zake leo Makao Makuu ya klabu ya Yanga, jijini Dar es salaam

Dk Msolla ambaye kitaalamu ni Mwalimu wa mpira wa miguu (kocha) aliyewahi kuinoa Taifa Stars, ametaja vipaumbele vyake ambavyo atavitekeleza kama atachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Yanga

Baadhi ya vipaumbele hivyo ni pamoja na Kujenga umoja na ushirikiano, Kuendeleza mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji, Kuendeleza miradi yote ya klabu iliyopo pia kuanzisha mipya, Kuweka na kusimamia misingi ya utawala bora pia kuweka misingi ya Yanga kuwa na timu imara

Dk Msolla amesema anataka kuona ushirikiano baina ya timu na mashabiki na wanachama wake unaimarika zaidi na ameunga mkono zoezi la kuichangia Yanga linaloendeshwa

“Nataka kujenga umoja ndani ya klabu kwa maana ya kuirudisha timu kwa wanachi hivyo sio vibaya wenye timu kuichangia klabu yao”

Aidha DK Msolla amesema atabadili mfumo wa uchaguzi wa Yanga unaotoa fursa pekee kwa wanachama wa Dar es salaam kushiriki michakato ya uchaguzi

“Natambua kuwa wanachama wengi wa Yanga ambao hushiriki uchaguzi ni wale ambao wapo Dar, ndani ya uongozi wangu kama nikipewa nafasi basi wa mkoani nao watapata haki hiyo.

“Tutakuwa na mfumo ambao utawawezesha kupiga kura wakiwa kwenye matawi yao”

Kuhusu utawala bora Dk Msolla amesema uongozi wake hautaingilia majukumu ya kocha Mwinyi Zahera

Amesema kocha huyo ni mtu muhimu kwa klabu ya Yanga, ni bahati kuwa nae hasa ikizingatiwa timu inapita katika kipindi kigumu sana

“Mimi ni kocha wengi wananifahamu, akihitaji ushauri wa kiufundi nitampatia lakini nitaingia Yanga kama mwenyekiti hivyo niseme wazi kuwa nitamwacha awe huru kutekeleza majukumu yake.

“Uongozi wangu hautakuwa na mipango ya kuachana naye, mara kadhaa nimekuwa nikisema wazi kuwa Yanga tunabahati ya kupata kocha wa namna hii”

Pia Dk Msolla amesema atahakikisha Yanga inakuwa na misingi mizuri ya kuendeleza vijana wa kikosi B kwa lengo la kuja kuwatumia kikosi cha kwanza

Wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi Yanga wameendelea kuzindua kampeni ambazo zitadumu hadi Jumamosi, May 04 siku moja kabla ya uchaguzi

Sevilla itawajengea wachezaji uzoefu wa Kimataifa

Mafanikio ya Simba kwenye michuano ya SportPesa Super Cup msimu huu yameipelekea mabingwa hao wa Tanzania Bara kuteuliwa kuivaa Sevilla katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki utakaopigwa May 23 jijini Dar es salaam

Uongozi wa Simba umesema mchezo huo ni fursa adimu kwa wachezaji wake kwani utawasaidia kuwajengea uzoefu wa Kimataifa

Aidha Simba imesema itautumia mchezo huo kuitangaza Tanzania Kimataifa kwani wanajua utafuatiliwa na mamilioni ya mashabiki wa soka duniani kwani utarushwa mbashara na runinga mbalimbali kote duniani

Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amesema uteuzi huo ni sahihi kwa Simba kwani ukiachilia mbali mafanikio waliyopata kwenye michuano ya SportPesa ukilinganisha na timu nyingine za Tanzania, Simba iko kwenye kiwango cha juu zaidi kwa sasa hapa nchini

“Simba kwa sasa ipo katika kiwango cha juu na kucheza na Sevilla kutasaidia kujua viwango vya wachezaji wetu katika mechi za kimataifa,” amesema

“Mechi hii inaiweka Tanzania katika historia kubwa sana katika soka. Historia zinaonyesha kuwa miaka ya nyuma, timu mbalimbali kutoka nje ya mipaka ya Afrika zilikuja hapa Tanzania na kucheza na Yanga na Simba, miaka ya hivi karibuni hakukuwa na ujio huo zaidi ya mwaka 2017 ambapo SportPesa iliileta timu ya Everton na kucheza timu ya Gor Mahia ya Kenya”

Sevilla ni moja ya timu kongwe na maarufu nchini Hispania na barani Ulaya. Imewahi kutwaa taji la Europa kwa misimu mitatu mfululizo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita

Simba yaelekea mkoani Mbeya

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Simba wanaondoka asubuhi hii kuelekea mkoani Mbeya tayari nkwa michezo miwili ya ligi dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons

Kesho Ijumaa May 03, Simba itashuka uwanja wa Sokoine kuikabili Mbeya City kisha kurejea tena katika uwanja huo May 05 kuikabili Tanzania Prisons

Ikiwa imesalia na michezo 10, Simba inahitaji kushinda michezo saba tu ili iweze kutetea ubingwa wake kwa msimu wa pili mfululizo

Hii hapa ratiba ya michezo yote iliyobaki

BREAKING NEWS: REGINALD MENGI AFARIKI DUNIA

Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP , Dkt Reginald Abraham Mengi (75) amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.

Dk Mengi amefariki dunia akiwa jijini Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).

Dk Mengi alikuwa ni mfanyabiashara mkubwa barani Afrika, ambapo sehemu ya utajir wake aliuelekeza kwa jamii kwa kutoa misaada mbalimbali.

Kwa mujibu wa jarida la Forbes mwaka 2014, utajiri wa bilione huyo ulitajwa kuwa ni TZS trilioni 1.3 ($560 milioni).

Enzi za uwahi wake na katika shughuli zake aliweza kushinda tuzo mbalimbali za kitaifa na kimataifa, pamoa na kuandika kitabu chake cha I Can, I Must, I will.

Mungu Ailaze Roho yake Mahali Pema Peponi. Amina

Yanga kuikabili Tanzania Prisons uwanja wa Uhuru kesho

Ligi Kuu ya Tanzania Bara inaendelea kesho ambapo vinara wa ligi hiyo Yanga watakuwa uwanja wa Uhuru kupepetana na Tanzania Prisons

Baada ya juzi kuichapa Azam Fc bao 1-0, Yanga itakuwa na nafasi ya kuzidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kama itaibuka na ushindi kwenye mchezo huo

Mabingwa hao wa kihistoria wamesalia na michezo mitano kabla ya kumalizika kwa ligi, kama watashinda yote watafikisha alama 92

Bado Yanga haiwezi kuondolewa katika mbio za ubingwa kwani wapinzani wao Simba bado watahitaji kupata matokeo katika michezo yao10 iliyobaki ili waweze kutete ubingwa

Baada ya mchezo wa kesho Yanga itaelekea mkoani Iringa tayari kwa mchezo wa nusu fainali kombe la FA dhidi ya Lipuli Fc utakaopigwa May 06 2019

Ajib ajumuishwa kikosi cha Stars

Hatimaye kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Emmanuel Amunike amemjumuisha nahodha wa Yanga Ibrahim Ajib kwenye kikosi cha timu ya Taifa kitakachoshiriki michuano ya AFCON itakayofanyika mwezi ujao nchini Misri pamoja na michuano ya CHAN inayohusisha wachezaji wa ndani

Kikosi hicho chenye wachezaji 39 pia kimewajumuisha Gadiel Michael, Kelvin Yondani na Feisal Salum kutoka klabu ya Yanga

Simba kushirikiana na Porto FC

Mwekezaji wa klabu ya Simba Bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’ akiwa nchini Ureno alitembelea kitua cha kulelea vipaji cha klabu ya Porto Fc

Ziara yake hiyo ilikuwa mahsusi kwa ajili ya kutafuta fursa ya ushirikiano baina ya klabu ya Porto Fc na Simba

“Jana nilipata nafasi nzuri ya kujifunza nilipoitembelea @FCPorto ambapo niliweza kujua fursa za ushirikiano kwa kituo cha kukuzia vipaji cha Simba huko mbeleni,” amebainisha Mo

“Tuna mengi ya kujifunza na kupata kutokana na uzoefu wa Porto FC. Natarajia kuimarisha mazungumzo yetu hivi karibuni”

Hii ni habari njema kwa Simba ambayo ina mipango ya kujenga mifumo imara itakayoinufaisha klabu hiyo siku za mbeleni