Simba au Yanga kuchuana na Sevilla May 23

Wadhamini wa vilabu vya Simba na Yanga kampuni ya SportPesa, imetangaza kuileta nchini Sevilla Fc inayoshiriki ligi kuu ya Hispania, La Liga

Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa kampuni ya SportPesa Abbas Tarimba amesema Sevilla itakuja nchini May 23 kuchuana na kati ya Simba au Yanga kwenye mchezo utakaopigwa uwanja wa Taifa

SportPesa pia inadhamini ligi kuu ya Hispania, La Liga

Kagere amfikia Aiyee, afikisha mabao 16 ligi kuu

Mabao mawili aliyofunga Meddie Kagere leo, yamemuwezesha kufikisha mabao 16 na kumfikia Salim Aiyee ambaye amekuwa akiongoza kwa muda mrefu mbio za kuwania kiatu cha dhahabu

Katika kipindi cha wiki mbili hivi Kagere huenda akajiimarisha kileleni katika mbio hizo kwani Simba itacheza michezo saba ya viporo

Leo Kagere ameiongoza Simba kuondoka na ushindi muhimu wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union na kuiweka Simba katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa hasa baada ya Yanga kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar

Simba inaelekea mkoani Kagera tayari kwa mchezo mwingine wa kiporo dhidi ya Kagera Sugar ambao utapigwa Jumamosi, April 20 2019 katika dimba la Kaitaba

Zahera kukamilisha usajili kabla ya ligi kumalizika

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera tayari ameanza michakato ya kuwania sahihi za wachezaji anaowataka kuitumikia Yanga msimu ujao

Zahera ambaye aliasisi zoezi la uchangiaji linaloendelea sasa, ametaka kukamilisha michakato ya usajili kabla hajatimkia kwao DR Congo anakokabiliwa na majukumu ya timu ya Taifa kuelekea fainali za AFCON 2019 zitakazofanyika mwezi Juni nchini Misri

Zahera ataondoka mwanzoni mwa mwezi wa sita hivyo ametaka masuala yote ya usajili yakamilishwe mapema

Yanga inaendelea na mchakato wa kukusanya michango ya wadau wake kupitia Kamati Maalum ya uhamasishaji ambayo imemuhakikishia kocha huyo kuwa atapatiwa kiasi cha fedha alichohitaji ili kukamilisha michakato yote ya usajili

Wakati wa uzinduzi wa zoezi la kuichangia Yanga mkoani Dodoma mwanzoni mwa mwezi huu, Zahera alibainisha kuwa ana orodha ya wachezaji nane ambao wako tayari kutua Yanga

Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji Mh Athony Mavunde amewataka, Wapenzi, mashabiki na wanachama wa Yanga waendelee kuwasilisha michango yao ili kukamilisha michakato yote kwa wakati

Kadi maalum za kuichangia Yanga ambazo zina thamani ya Tsh Milioni moja kwa kila kadi zinaendelea kutolewa, ambapo michango yote imetakiwa kuwasilishwa kabla ya April 25 2019

Simba yasaka alama tatu dhidi ya Coastal Union leo

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba leo wanarejea ‘mzigoni’ kwa kuikabili Coastal Union katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Mkwakwani, saa nane mchana

Simba iko mkoani Tanga tangu juzi ambapo jana jioni ilifanya mazoezi ya mwisho Mkwakwani kuelekea mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu

Baada ya kuondoshwa katika hatua ya robo fainali michuano ya ligi ya mabingwa, Simba imejizatiti kutetea ubingwa iliyotwaa msimu uliopita ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya hiyo msimu ujao

Ikiwa imeshuka dimbani mara 22 na kuvuna alama 57, ushindi katika mchezo wa leo utaifanya Simba ifikishe alama 60 na kuendelea kuzifukuzia Azam Fc (66) na Yanga (74) ambazo hata hivyo zimecheza michezo tisa zaidi

Kocha Patrick Aussems amesema wachezaji wake wanafahamu umuhimu wa mchezo wa leo na baada ya kupoteza mchezo dhidi ya TP Mazembe, leo watakuwa na nafasi ya kufuta makosa waliyofanya kwenye mchezo huo kwa kuibuka na ushindi mnono

Mchezo utapigwa saa nane mchana ili kuwapa nafasi mashabiki kushuhudia mchezo wa michuano ya AFCON U17 kati ya Tanzania dhidi ya Uganda ambao utaanza saa kumi kamili jioni