Zahera akerwa na waamuzi ligi kuu

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema kumekuwa na makosa mengi yanafanywa na waamuzi hasa kuionea Yanga lakini anasikitishwa kuona wanaondesha mpira nchini hawachukui hatua yoyote

Zahera aliyazungumza hayo jana baada ya mchezo kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga, mchezo ambao wenyeji waliondoka na ushindi wa bao 1-0

Zahera amesema kwa mfumo huu wa kuzibeba dhahiri baadhi ya timu, ana mashaka na hatma ya mpira wa Tanzania kuwa utaendelea kubaki chini

Marefa wa Tanzania watoswa AFCON 2019

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetoa orodha ya marefa 27 na marefa wasaidizi 29 kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu nchini Misri, lakini hakuna Mtanzania hata mmoja.

Waamuzi hao wameteuliwa kushiriki kozi maalum kuanzia Aprili 28 hadi Mei 5 mwaka huu mjini Rabat, Morocco kunolewa kwa ajili ya Fainali za Misri mwezi Juni.

Marefa hao wanatoka nchi 33 na wataingia kwenye kambi maalum ya mafunzo itakayosaidia uteuzi wa orodha ya mwisho ya marefa watakaochezesha fainali za mwaka huu zitakazoanza Juni 21 hadi Julai 19 katika miji ya Alexandria, Cairo, Ismailia na Suez

Kabwili kutimkia Arabuni

Mlinda lango wa Yanga Ramadhani Kabwili huenda akatimkia Saudi Arabia mwishoni mwa msimu baada ya timu ya Aladalah Fc inayoshiriki ligi kuu nchini humo kumuhitaji

Kabwili aliyejiunga na Yanga mwaka juzi baada ya kufanya vizuri kwenye michuano ya AFCON U17 iliyofanyika Gabon, mkataba wake na Yanga uko ukingoni na atakuwa huru ifikapo mwezi Juni

Kabwili amepata nafasi ya kucheza zaidi msimu huu baada ya aliyekuwa mlinda lango namba moja Beno Kakolanya kuingia kwenye mgogoro na kocha Mwinyi Zahera

Kwa sasa hapati nafasi mara kwa mara baada ya mlinda lango aliyeimarisha kiwango chake Klaus Kindoki kumpiku

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amepania kukijenga upya kikosi cha Yanga kwa ajili ya msimu ujao na inaelezwa amewaruhusu wachezaji wote wanaotaka kuondoka, waondoke

Yanga huenda ikamsajili mlinda lango wa Bandari Fc, Farouk Shikalo ambaye usajili wake ulipaswa kukamilishwa mwezi Disemba wakati wa dirisha dogo la usajili kabla ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Yanga Hussein Nyika kushindwa kwenye dakika za majeruhi

Shikalo ni miongoni mwa wachezaji wanne ambao Zahera alisikitika kuwakosa katika usajili huo

Zahera azipigia hesabu Azam Fc, Lipuli Fc

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema licha ya changamoto za waamuzi wanazokabiliana nazo kwenye ligi, hawatakata tamaa na watafanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo unaofuata dhidi ya Azam Fc utakaopigwa uwanja wa Taifa April 29 2019

Yanga imesalia na michezo sita kumaliza msimu huku imchezo mmoja dhidi ya Biashara United ukitarajiwa kupigwa nje ya Dar

Yanga itarejea jijini Dar es salaam kutumia uwanja wa Taifa baada ya kumalizika fainali za AFCON U17 April 28 2019

Zahera amesema watahakikisha wanashinda michezo yote iliyobaki pamoja na kuweka msisitizo zaidi kwenye michuano ya kombe la FA (ASFC) wakitarajia kucheza na Lipuli Fc mwanzoni mwa mwezi wa tano katika mchezo wa nusu fainali

“Unajua mimi nimezunguka nchi nyingi sana Afrika lakini sijawahi kuona maamuzi ya hovyo kama ya waamuzi wa Ligi ya Tanzania, Hakuna haki na kungekuwa na haki nina uhakika sasaivi tungekuwa tushajihakikishia ubingwa”

“Kwa sasa tumesahau yote, tunajipanga kuelekea michezo inayofuata ukiwemo wa Azam Fc ili kuhakikisha tunashinda mechi zote zilizosalia huku tukihakikisha tunatwaa ubingwa wa Kombe la ASFC ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani”

Yanga, Azam Fc zairahisishia Simba mbio za ubingwa

Azam Fc imeangukia pua mkoani Mtwara baada ya kuchapwa bao 1-0 na Ndanda Fc katika mchezo uliopigwa uwanja wa Nangwanda Sijaona

Ndanda Fc pia ilipata alama moja moja kwenye michezo dhidi ya Yanga na Simba iliyopigwa katika uwanja huo

Matokeo hayo yameipandisha Ndanda Fc mpaka nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia alama 43

Yanga yenye alama 74, imeendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama nane dhidi ya Azam Fc inayoshika nafasi ya pili ikijikusanyia alama 66

Simba yenye michezo mingi ya viporo, inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 60

Bodi ya ligi yatahadharishwa mechi za saa nane

Mtaalamu wa misuli ya mwili wa binadamu Dk Kitambi Mganga ameishauri Bodi ya ligi kuu kuwa makini na utaratibu wa kupanga michezo ya ligi kuu saa nane mchana wakati wa jua kali

Dk Mganga amesema kitaalam, muda huo sio mzuri kwani unaweza ukasababisha madhara makubwa kwa wachezaji yakiwemo matukio ya vifo

“Wachezaji wanapocheza wakati wa jua kali wanakuwa katika hali ya kukausha maji mwilini kwa haraka na hivyo kuwepo na hatari ya kupatwa na shambulio la moyo au kuziba moyo na misuli kukakamaa,” amesema

“Shambulio la moyo linatokana na mwili kulazimishwa kufanya kazi ngumu wakati wa jua kali, moyo unaziba, ulimi unatoka nje, misuri inashindwa kufanya kazi ni hatari kubwa mchezaji anaweza kupoteza maisha uwanjani kama hakutakuwa na mtaalamu mwenye kujua atoe huduma gani”

Dk Mganga ambaye ni Daktari wa Coastal Union, amesema kama kuna ulazima wa kuchezesha mechi hizo katika muda huo basi mwamuzi anaweza kutenga hata dakika moja ya kuwapa nafasi wachezaji kunywa maji utaratibu ambao hutumika kote duniani ambapo mchezo husimamishwa kwenye dakika ya 25-30 kuwapa nafasi wachezaji kunywa maji

Msimu huu baadhi ya michezo ya ligi kuu imekuwa ikipigwa saa nane mchana ili kutoa nafasi kwa michezo mingi kuonyeshwa ‘mbashara’ na Azam TV

Michezo ya ligi iliyopigwa jana ambayo ilihusisha Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga na Coastal Union dhidi ya Simba, ilipigwa saa nane mchana ili kuepusha muingiliano wa ratiba na michuano ya AFCON U17 inayoendelea jijini Dar es salaam

Simba kurudi ‘machinjioni’ baada ya AFCON U17 kumalizika

Michuano ya vijana ya AFCON U17 inayoendelea jijini Dar es salaam, inatarajiwa kumalizika April 28 2019 kwa mchezo wa fainali kupigwa ambapo baada ya mchezo huo, uwanja wa Taifa utaruhusiwa kwa matumizi ya michezo ya ligi

Hii ni taarifa njema sana kwa Simba ambayo katika kipindi cha wiki mbili zijazo inakabiliwa na michezo mingi ya viporo inayopigwa ugenini

Mwanzoni mwa mwezi wa tano Simba itarejea kumalizia michezo iliyobaki katika uwanja wa Taifa ambao umepachikwa jina la ‘machinjioni’

Msimu huu Simba imeweka rekodi ya kipekee uwanja wa Taifa kwa kushinda michezo yote iliyocheza kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika na kulazimishwa sare michezo miwili tu kwenye ligi

Simba yarejea Dar usiku kwa usiku, tayari kwa safari ya Kanda ya Ziwa

Kikosi cha Simba kimerejea jijini Dar es salaam usiku kikitokea Tanga ambapo jana kilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union

Kutokana na ukaribu wa michezo yake Simba imelazimika kusafiri usiku na mchana ili kwendana na ratiba ya viporo iliyopangwa na Bodi ya Ligi

Simba inaelekea Kanda ya Ziwa ambapo keshokutwa Jumamosi, April 20 2019 itakuwa dimba la Kaitaba kuikabili Kagera Sugar

Baada ya ushindi Tanga, Simba kurejea Dar

Baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union leo, kikosi cha Simba kinarejea jijini Dar es salaam tayari kuifuata Kagera Sugar

Simba itacheza na Kagera Sugar Jumamosi April 20 katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Kaitaba

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema licha ya kukabiliwa na ratiba isiyo rafiki watapambana kuhakikisha wanapata matokeo

Akizungumzia matokeo ya mchezo wa leo, Aussems amewapongeza wachezaji kwa kupata ushindi licha ya mazingira yasiyo rafiki ya uwanja wa Mkwakwani

“Haikuwa rahisi sababu uwanja haukuwa mzuri lakini tulifanikiwa kumiliki mchezo na baadae tulifanya mabadiliko ambayo yametuletea magoli. Kubwa zaidi nawapongeza wachezaji kwa kuibuka na ushindi”