Makambo ataja siri ya kufunga mfululizo CCM Kirumba

Kinara wa mabao wa kikosi cha Yanga Heritier Makambo amesema ubora wa uwanja wa CCM Kirumba ni moja ya sababu inayomfanya aendelee ‘kutupia mabao’ kila anashuka katika dimba hilo

Makambo amefunga mabao matano CCM Kirumba, manne akifunga kwenye michezo ya ligi na moja akifunga kwenye michuano ya kombe la FA (ASFC)

Mabao matatu ameyafunga katika michezo miwili iliyopita dhidi ya African Lyon na jana dhidi ya Kagera Sugar

“Najisikia tofauti ninapocheza kwenye uwanja wa CCM Kirumba. Nadhani ubora wa uwanja unachangia mimi kufanya vizuri,” amesema

“Tumekuwa tukipata matokeo mazuri kila tunapocheza hapa, hakuna tofauti na tulivyokuwa tukicheza uwanja wa Taifa”

“Nawapongeza wachezaji wenzangu pia kwani wanachangia mimi kufanya vizuri”

Msimu huu Yanga imeshinda michezo yote ya ligi na kombe la FA iliyocheza katika uwanja wa CCM Kirumba

Aidha akizungumzia mbio za kuwania kiatu cha dhahabu, Makambo amesema ataendelea kufunga kila anapopata nafasi ili kuisaidia Yanga kupata matokeo. Ligi bado inaendelea na lengo lake ni kuendelea kufanya vizuri

Makambo amefunga mabao 15, anashika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora nyuma ya Salim Aiyee wa Mwadui Fc mwenye mabao 16

Ni mchezo wa jasho na damu – Manara

Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amesema kikosi cha timu hiyo kinatarajiwa kuondoka mapema kesho Ijumaa kuelekea DR Congo tayari kwa mchezo wa pili wa robo fainali ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya TP Mazembe

Manara amesema Simba inakwenda Congo kupambana na watahakikisha wanaiwakilisha vyema nchi kwa kupata matokeo mazuri katika mchezo huo utakaopigwa keshokutwa Jumamosi kwenye uwanja wa TP Mazembe

Amesema wachezaji wa Simba wako tayari kuandika historia nje ya nchi

“Tunakwenda kesho kibingwa tukiwa hatuna cha kupoteza ila tunawaahidi jasho jingi litamwagika kuipigania Simba na nchi Jumamosi,” amesema Manara

“Hatuogopi lolote toka Mazembe pamoja na kuwapa heshima yao kama klabu kubwa”

“Wachezaji wetu wapo tayari kuionyesha Afrika ubora wao na ukubwa wa Simba. Tuombeeni tufike salama na turejee salama kifua mbele”

Simba inakwenda Congo kwa usafiri wa ndege maalum ya kukodi na itarejea nchini Jumamosi jioni baada ya mchezo

FT: YANGA 3-2 KAGERA SUGAR

Vinara wa ligi kuu ya Tanzania Bara Yanga wameendeleza ubabe katika uwanja wa CCM Kirumba baada ya kuifumua Kagera Sugar mabao 3-2
Kagera Sugar ilitangulia kufunga bao la kuongoza kwenye dakika ya 30 likiwekwa kambani na Paul Ngalyoma aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona

Dakika nne baadae Yanga ilisawazisha bao hilo baada ya Kassim Khamis kujifunga wakati akijaribu kuokoa mpira wa kichwa uliopigwa na Papi Tshishimbi
Mpaka wakati wa mapumziko matokeo yalikuwa 1-1

Yanga ilihitaji dakika tatu tu za kipindi cha pili kuandika bao la pili lililowekwa kimiani na Heritier Makambo aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa juu uliovushwa na Kelvin Yondani

Kagera Sugar wakasawazisha tena kwenye dakika ya 58 baada ya shuti la Kassim Khamis kumshinda mlinda lango Klaus Kindoki na kutinga kimiani
Kiungo Thabani Kamusoko aliihakikishia Yanga alama tatu muhimu baada ya kufunga bao la tatu kwenye dakika ya 72
Kamusoko aliukwamisha nyavuni mpira wa adhabu kwa ustadi mkubwa

Kwenye dakika ya 82 Yanga ilipata pigo baada ya kelvin Yondani kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia tukio la kumpiga kiwiko mchezaji wa Kagera Sugar

Matokeo hayo yameifanya Yanga ifikishe alama 74 na kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama 11 dhidi ya Azam Fc inayoshika nafasi ya pili

PAUL POGBA

Imeelezwa kuwa Kiungo wa Man United Paul Pogba hana uhusiano mzuri na kocha wake Ole Gunnar Solskjaer huenda sababu hiyo ikarahisisha kiungo huyo kuhamia Real Madrid mwishoni mwa msimu huu (Le Parisien via AS)