Serengeti Boyz kuvuna mamilioni wakishinda michezo miwili AFCON U17

Wachezaji wa timu ya taifa ya vijana ya Tanzania, U-17 ‘Serengeti Boys’ wameahidiwa kupewa Sh. 20 milioni kila mchezaji endapo watashinda michezo miwili katika michuano ya AFCON U17 inayoanza kesho jijini Dar es salaam

Ahadi hiyo imetolewa jana na Mlezi wa timu hiyo Dkt.Reginald Mengi pamoja na Kamati ya kuhamasisha ushindi wa timu hiyo inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar, es salaam, Paul Makonda.

Serengeti Boys inahitaji kushinda mechi mbili ili kujikatia tiketi ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17 itakayofanyika nchini Brazil mwaka huu.

Michuano hiyo itafanyika katika viwanja viwili, ambavyo ni Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Timu shiriki zimepangwa katika makundi mawili, ambapo kundi A lina timu za Tanzania, Nigeria, Angola na Uganda, huku kundi B likiwa na timu za Guinea, Cameroon, Morocco na Senegal.

Simba: Tutapigana dakika zote 90

Wakati Simba ikiikabili TP Mazembe kwenye mchezo wa pili wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kocha wake, Patrick Aussems amesema watapambana dakika zote 90. Mchezo huo umepangwa kufanyika Stade TP Mazembe, Lubumbashi DR Congo.
Awali kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wiki moja iliyopita, Simba ambao ni wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano hayo walibanwa mbavu na kwenda suluhu.
Kikosi kamili cha Simba kikiongozwa na nahodha wao, John Bocco kiliondoka jana asubuhi kwa ndege ya kukodi kikiwa na wachezaji 18 tayari kwa mchezo huo wa marudiano.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Aussems alisema wamejiandaa kwa wiki moja kwenda kutafuta matokeo ya ushindi Lumbambashi ili kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika wiki hiyo Simba walianza maandalizi yao kwa kujikita na mazoezi ya kujenga utimamu kwa wachezaji hiyo huku siku chache kabla ya kuondoka wakijinoa pia kwenye upigaji wa mikwaju ya penati.
“Ninaiheshimu TP Mazembe kwa sababu ni timu kubwa yenye rekodi nzuri kwenye mashindano haya lakini hatuiogopi.Tumejiandaa kama tulivyopanga na nina imani kuwa tunakwenda kukitekeleza kile ambacho tumekifanyia kazi kwenye mazoezi.
“Natambua umuhimu wa mashabiki wetu ambao walikuwa wakitupa nguvu kwenye michezo yetu ya nyumbani tunaenda ugenini ambako mazingira yatakuwa tofauti ila niwatoe woga kwa kusema tutapambana kusonga mbele.

“Inawezekana kuingia hatua ya nusu fainali. Tulitengeneza nafasi kwenye mchezo wa kwanza ila tulishindwa kuzitumia hivyo naamini kuwa hata kwenye mchezo huu wa ugenini tunaweza kutengeneza nafasi,” alisema Aussems
Ili Simba isonge mbele kwenye hatua ya nusu fainali, inahitaji ushindi kwenye mchezo huo au sare ya aina yoyote ya mabao.

Kama mchezo huo ukimalizika kwa suluhu kama ilivyokuwa mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam, Simba na TP Mazembe basi mshindi ataamuliwa kwa mikwaju ya penalti.

Aussems alisema mchezaji pekee ambaye atakosekana kwenye kikosi chake ni beki wa kati, Pascal Wawa ambaye ni majeruhi baada ya kuumia kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam.
“Nina wachezaji 24 kwenye kikosi changu hivyo ni rahisi pindi anapoumia mmoja nafasi yake kuzibwa na mwingine, nadhani mliona namna Juuko alivyoziba pengo lake kwenye mchezo wa kwanza,” alisema kocha huyo wa Mbelgiji.

Nahodha wa kikosi hicho, John Bocco alisema wapo kwenye hali nzuri na akatoa ahadi kwa wapenzi na mashabiki wa Simba kuwa lengo lao ni kutinga nusu fainali na sio kitu kingine.
“Tunaenda kupambana. Kushikamana kwetu kwenye mchezo uliopita kama wachezaji kutaendelea ili tuweke historia nyingine ya kutinga hatua ya nusu fainali.
“Kuna mashabiki wetu ambao walitamani kuwa nasi DR Congo lakini kutokana na sababu za kiuchumi pengine wamekwama niwaombe kitu kimoja watuombee ili kila kitu kiende kama tulivyopanga,” alisema Bocco.

Katika mchezo huo Simba itawategemea zaidi wachezaji wake wanne ambao wana mabao mengi katika mashindano hayo wakiongozwa na Meddie Kagere mwenye mabao sita, Clatous Chama(5),John Bocco (3) na Emmanuel Okwi mwenye mabao mawili katika safu ya ushambuliaji.
Wapinzani woa TP Mazembe wanawategemea Tressor Mputu mwenye mabao manne sawa na Jackosn Muleka, Kelvin Mondeko mwenye mabao matatu na Meshack Elia aliyefunga mawili.
Kikosi kamili cha wachezaji wa Simba ambacho kimekwenda DR Congo ni Aishi Manula, Deogratius Munishi ‘Dida’, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Erasto Nyoni, Paul Bukaba, James Kotei, Jonas Mkude.
Nyota wengine ni Mzamiru Yassin, Said Ndemla, Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga, Clatous Chama, John Bocco, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na Rashid Juma.

Kila kheri Simba, kila la kheri wawakilishi wa nchi

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba leo wanashuka katika dimba la Stade De Mazembe huko Lubumbashi DR Congo kuikabili TP Mazembe kwenye mchezo wa pili wa robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika

Simba ina nafasi ya kutinga nusu fainali ya michuano hiyo kama itaibuka na ushindi au kutoka sare yoyote ya mabao

Simba ilitua Lubumbashi mapema jana Ijumaa na jioni kupata nafasi ya kufanya mazoezi katika uwanja wa Mazembe ambao utatumika baadae

Kocha Patrick Aussems amesema kikosi chake kiko tayari kuelekea mchezo huo na amewataka wapenzi, mashabiki wa Simba na Watanzania wote kwa ujumla kuwaombea dua ili waweze kuibuka na ushindi

Ushindi wa Simba leo ni faida kwa Tanzania kwani matokeo hayo yataisaidia Tanzania kuongezewa timu za kushiriki michuano ya CAF kuanzia msimu ujao

Simba tayari imedhihirisha kuwa inaweza kupambana na timu yoyote barani Afrika, mchezo wa leo utadhihirisha mara dufu uimara wa Simba

Kila la kheri Simba, kila la kheri mabingwa wa nchi, kila la kheri wawakilishi wa Tanzania..

MAKUNDI AFCON 2019

MAKUNDI YOTE SITA: #AFCON2019

Kundi A
Misri
DR Congo
Uganda
Zimbabwe

Kundi B
Nigeria
Guinea
Madagascar
Burundi

Kundi C
Senegal
Algeria
Kenya
Tanzania

Kundi D
Morocco
Ivory Coast
South Africa,
Namibia

Kundi E
Tunisia
Mali
Mauritania,
Angola

Kundi F
Cameroon
Ghana
Benin,
Guinea-Bissau

Simba yawasili Lubumbashi

Msafara wa kikosi cha Simba uliondoka mapema leo jijini Dar es salaam kuelekea DR Congo, umewasili salama katika mji wa Lubumbashi yalipo makazi ya klabu ya TP Mazembe

Kesho Jumamosi Simba itashuka dimba la Mazembe kuwakabili wenyeji wao katika mchezo wa pili wa robo fainali michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika

Simba imetumia usafiri wa Ndege Maalum ya kukodi na wataitumia Ndege hiyo kurejea nchini kesho baada ya mchezo

Mabingwa hao wa Tanzania leo jioni wanatarajia kujifua katika uwanja wa Mazembe ambao utatumika kwenye mchezo wa kesho

Stars yawekwa chungu cha nne, upangaji makundi AFCON 2019

Droo ya makundi ya michuano ya AFCON 2019 inafanyika leo saa tatu usiku huko Misri ambapo Tanzania iliyofuzu baada ya kusubiri miaka 39, itakuwa miongoni mwa timu 24 zitakazoshiriki michuano hiyo mwaka huu

Katika droo hiyo, timu zitapangwa kwenye makundi sita ya timu nne nne

Droo ya makundi itafanyika kwa kuchagua timu kutoka kila chungu miongoni mwa vyungu vinne vyenye timu sita sita ambazo zimewekwa kwa kufuata ubora

Tanzania imewekwa kwenye chungu cha nne sambamba na Namibia, Guinea Bissau, Angola, Burundi na Zimbabwe

Timu zinazokuwa kwenye chungu kimoja haziwezi kupangwa kundi moja hivyo Stars haiwezi kupangwa na timu zilizotajwa hapo juu

Aussems aahidi Simba tofauti Lubumbashi

Kikosi cha Simba tayari kimeondoka nchini kuelekea Lubumbashi DR Congo kwa ajili ya mchezo wa marudiano robo fainali ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya TP Mazembe


Simba itashuka katika dimba la Mazembe kesho kuumana na wenyeji wao hao ambao mchezo wa raundi ya kwanza uliopigwa uwanja wa Taifa waliwalazimisha suluhu ya bila kufungana
Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Simba kushindwa kupata ushindi katika dimba la Taifa kwenye michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu
Hata hivyo licha ya matokeo hayo kocha Mkuu wa mabingwa hao wa Tanzania Patrick Aussems amesema wana nafasi kubwa ya kupata matokeo yatakayowapeleka nusu fainali huko Lubumbashi

Aussems amesema mchezo waliocheza Dar umemsaidia kutambua udhaifu wa wapinzani wao na amerekebisha makosa yaliyosababisha wakose ushindi nyumbani
Amewataka mashabiki wa Simba na Watanzania wote kuwaombea huku akiahidi kuwa wataishuhudia Simba tofauti kabisa na ile ambayo ilipoteza michezo yote ya ugenini katika hatua ya makundi
Aussems amesema mbinu atakazotumia kwenye mchezo huo wa marudiano zitawashangaza Wakongo nyumbani kwao, licha ya kukiri ni pambano gumu.

Kocha huyo alisema wamegundua kwenye mchezo wa kwanza viungo wao walishindwa kumiliki mpira na washambuliaji kupoteza nafasi nyingi kizembe na kuwapa nafasi Mazembe kuwatawala, lakini wanapoenda kuwafuata kwao viungo wake na washambuliaji watakuwa na kazi maalum Lubumbashi.

“Hatutakiwi kufanya makosa ya kupoteza mpira katika sehemu ya kiungo, pia tukienda mbele tutatakiwa kuwa na malengo makubwa tutawalazimisha wafanye makosa, tuko katika utofauti mkubwa ukilinganisha na mechi za nyuma tulizocheza ugenini,” amesema

Simba imeondoka na kikosi cha wachezaji 18 ikitumia usafiri wa ndege ya kukodi. Itarejea jijini Dar es salaam kesho baada ya mchezo huo

Makambo amuwashia taa nyekundu Aiyee

Bao alilofunga Heritier Makambo leo limemfanya mshambuliaji huyo Mcongoman afikishe mabao 15 akimuacha Meddie Kagere wa Simba mwenye mabao 14.

Leo Makambo aliisaidia Yanga kuibuka na ushindi muhimu wa mabao 3-2 dhidi ya Kagera Sugar

Makambo sasa anahitaji kufunga bao moja zaidi ili aweze kumfikia Salim Aiyee wa Mwadui Fc anayeongoza kwa ufungaji akiwa na mabao 16

Katika michezo miwili iliyopita, Makambo ameifungia Yanga mabao matatu

Waziri Mkuu aichangia Yanga Milioni moja, kupewa cheti Maalum

KAMATI YA HAMASA YA KUCHANGIA YANGA 2019

Kamati ya Hamasa ya Kuchangia Klabu ya Yanga inatoa shukurani kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa (MB) Kwa kuwa mchangiaji wa Kwanza kuichangia Klabu ya Yanga ambayo ina historia kubwa ya upatikanaji wa Uhuru wa Nchi yetu ya Tanzania.

Waziri Mkuu ameichangia Klabu ya Yanga kiasi cha shilingi milioni moja (1,000,000/=).

Kamati ya Hamasa kwa niaba ya Wanachama, Mashabiki na Wapenzi wa Klabu ya Yanga ina imani kubwa kuwa, mchango huu utakuwa chachu kwa Viongozi wengine wa ngazi zote kwa Taasisi za Umma na Binafsi bila kujali Itikadi, Jinsia na hata Ushabiki wa kijadi wa Yanga na Simba na hatimaye kuunga mkono jitihada hizi za Kiukombozi za KLABU YA YANGAzenye kauli mbiu ya Timu ya Wananchi Wawekezaji ni Wananchi Wenyewe

Cheti Maalumu kitatolewa kwa Mh. Waziri Mkuu na Mwenyekiti wa Kamati Mh. Anthony Peter Mavunde (MB) wakati wa kuhitimisha zoezi hili Maalumu

Deo Mutta
KNY – Kamati ya Hamasa ya Kuchangia