Okwi, Chama hawakugoma – Manara

Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amesema wachezaji Emmanuel Okwi na Clatous Chama walichelewa kujiunga na kambi ya Simba mkoani Morogoro kutokana na sababu maalum na sio kweli kuwa wachezaji hao walifanya mgomo

Akizungumza na waandishi wa habari leo Makao Makuu ya klabu ya Simba yaliyopo mtaa wa Msimbazi, Manara amesema klabu iliwapa ruhusa wachezaji hao kushughulikia masuala yao ya kifamilia na tayari wamesharipoti mkoani Morogoro kujiunga na wenzao

“Hakuna mchezaji aliyegoma kama taarifa zinavyoenezwa huko mitandaoni hivi timu inayocheza klabu bingwa Africa kuna mchezaji anaweza kugoma?”, amehoji Manara

“Okwi na Chama walipewa ruhusa maalum na tayari wapo kambini toka jana”

“Sisi kwa sasa tunaweza chukua mchezaji yeyote hata Tp Mazembe sio kama kipindi kile kwa sasa simba ni giant inabeba yeyote”

“Tuna barua zaidi ya 100 za wachezaji mbalimbali wameomba kuchezea Simba msimu ujao tena wengine wametoka vilabu vikubwa hapa Tanzania wanahitaji kucheza hata bure”

Kipenga kimepulizwa, fomu za uchaguzi Yanga zaanza kutolewa

Baada ya ‘figisu’ za uchaguzi kumalizika, hatimaye Wanayanga wana uhakika sasa kuwa mwezi ujao uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo utafanyika na viongozi wapya watapatikana katika nafasi zote

Jana Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF Malangwe Mchungahela aliweka wazi kuwa uchaguzi utafanyika May 05 badala ya April 28 kutokana na siku hiyo kutakuwa na mchezo wa fainali za AFCON U17. Uchaguzi huo utasimamiwa na Yanga, wao TFF watakuwa waangalizi tu

Tayari kipenga kimepulizwa na leo fomu zinaanza kutolewa Makao Makuu ya klabu Mtaa wa Twiga na Jangwani jijini Dar es salaam

Hii ni nafasi adhimu kwa Wanayanga kuijenga timu yao upya baada ya mateso ya takribani misimu miwili

Ni wakati kwa Wanachama wenye sifa na uwezo wa kuipeleka Yanga mbele kujitokeza kuchukua fomu

Aidha si vibaya kwa wanachama wengine kushawishiwa wachukue fomu kugombea pale tunapoona wanazo sifa na tuna imani nao

Huu ni wakati wa kuijenga Yanga imara ambayo itakuwa na mafanikio zaidi

Wanachama wajitokeze kwa wingi kuchukua fomu na siku ya uchaguzi, haipaswi kufanya makosa kwa wapiga kura.

Wanachama watumie muda wao kuwasikiliza wagombea wote wakati wa kampeni ili waweze kuchagua viongozi ambao wataweza kuitoa Yanga hapa ilipo

Wasauzi wampagawisha Okwi,aanza mbwembwe

Simba huenda ikalazimika kufanya kazi ya ziada kumbakisha mshambuliaji wake hatari Emmanuel Okwi ambaye timu nyingi zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili

Mkataba wa Okwi unatarajiwa kumalizika ndani ya siku 60 huku mchezaji huyo raia wa Uganda akionyesha dalili zote za kutaka kuondoka Msimbazi

Okwi anahusishwa na vilabu kadhaa vinavyoshiriki ligi kuu ya Afrika Kusini, Orlando Pirates na Kaizer Chiefs

Kocha Patrick Aussems alimuondoa Okwi katika kikosi kilichokwenda mkoani Morogoro baada ya mchezaji huyo kuchelewa kuripoti kambini

Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu amesema hana taarifa kuhusu mshambuliaji huyo ambaye alikuja nchini na kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda Cranes na alicheza mchezo dhidi ya Stars

“Mimi sijui chochote kuhusiana na Okwi labda waulizwe viongozi wangu wa juu, hayupo kwenye msafara wetu huu unaoelekea Morogoro, hivyo waulizwe viongozi wa juu suala lake,”Rweyemamu alinukuliwa na Championi jana

Hata hivyo Okwi amekuwa na kawaida ya kuchelewa kuripoti kambini kila anapotoka kutimiza majukumu ya timu ya Taifa

Hali ni tofauti kwa Juuko Murshid ambaye tangu aliporejeshwa kikosini, amekuwa akiwajibika ipasavyo

Juuko alikuwa miongoni mwa wachezaji waliowahi kuripoti kambini baada ya kumalizika michezo ya AFCON

Taarifa zilizopatikana mapema leo zimebainisha Okwi amerejea na ameshatua mkoani Morogoro kuungana na wenzake

Okwi, Chama waongeza nguvu Simba ikijiandaa kuikabili JKT Tanzania

Mshambuliaji Mganda Emannuel Okwi na kiungo Mzambia Clatous Chama tayari wamejiunga kwenye kambi ya Simba mkoani Morogoro kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya JKT Tanzania

Okwi na Chama hawakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kilichoifumua Mbao Fc mabao 3-0 baada ya wachezaji hao kuchelewa kurudi kutoka nchini kwao walikokwenda kutimiza majukumu ya timu ya Taifa

Baada ya mchezo wa kesho, Simba itaendelea kubaki mkoani Morogoro kuendelea na maandalizi ya mchezo wa robo fainali ligi ya mabingwa dhidi ya TP Mazembe

Mchezo huo utapigwa Jumamosi, April 06 kwenye uwanja wa Taifa

Simba vs JKT Tanzania kupigwa Jumatano

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba keshokutwa Jumatano watashuka uwanja wa Jamhuri kuikabili JKT Tanzania katika mchezo wa ligi hiyo

Licha ya kukabiliwa na mchezo wa robo fainali ligi ya mabingwa siku ya Jumamosi, April 06 dhidi ya TP Mazembe, TFF imegoma kusogeza mbele mchezo dhidi ya JKT Tanzania ambao utapigwa April 03 2019 kama ulivyopangwa

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema kwa sasa wanaelekeza nguvu zao kuelekea mchezo huo kabla ya kuanza maandalizi ya mchezo dhidi ya TP Mazembe

“Nitalazimika kubadili kikosi ili kila mchezaji apate nafasi kwani baada ya mchezo huo tutakuwa na siku mbili tu za kujiandaa kabla ya kuivaa TP Mazembe,” amesema

Akizungumzia ushindi wa mabao 3-0 ambao Simba ilipata jana dhidi ya Mbao Fc, Aussems alisema mipango yao ni kuhakikisha wanashinda kila mchezo ili waweze kutetea ubingwa hivyo ushindi huo unaendelea kuweka hai mipango yao

“Kila mechi tunacheza kushinda, hata huu mchezo tulistahili kushinda, tulianza kushambulia tangu mwanzo hadi mwisho, mchezo ulikuwa mgumu lakini tulitengeneza nafasi”

Wachezaji Yanga wapewa mapumziko ya siku moja

Kikosi cha Yanga kimewasili salama jijini Dar es salaam wakitokea mkoani Mwanza ambako jana walitinga nusu fainali ya kombe la FA (ASFC) baada ya kuifunga Alliance Fc kwa mikwaju ya penati 4-3 kufuatia matokeo ya sare ya bao 1-1

Kocha Mkuu wa vinara hao wa ligi kuu Mwinyi Zahera, amewapa wachezaji mapumziko ya siku moja kabla ya kuendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ndanda Fc

Mchezo huo utapigwa Alhamisi April 04 mkoani Mtwara kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona