Yanga yakanusha Zahera, Ajib kuondolewa watia saini akaunti CRDB

Yanga yakanusha Zahera, Ajib kuondolewa watia saini akaunti CRDB

Uongozi wa klabu ya Yanga umewataka wapenzi, wanachama na mashabiki wa timu hiyo kupuuza taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Kamati ya kuhamasisha uchangiaji iliyochini ya Mh Athony Mavunde imependekeza kuondolewa kwa Kocha Mwinyi Zahera na nahodha Ibrahim Ajib katika miongoni mwa watia saini wa akaunti ya kukusanya michango iliyofunguliwa benki ya CRBD

Msemaji wa klabu ya Yanga Dismas Ten ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo amesema hakuna ukweli wowote katika taarifa hiyo na amesisitiza wanaoisambaza ni wenye malengo ya kutaka kuikwamisha Yanga katika mpango wa kujijenga kwa ajili ya msimu ujao

“Hakuna sehemu hata moja kamati imekaa na kuzungumza haya. Huu ni uzushi upuuzwe na apuuzwe aliyeuandika,” amesema Ten

“Uongozi kupitia kamati hii ya Mh Mavunde ipo kwenye mikakati mizuri kuhakikisha klabu inavuka kwenye kipindi hiki kifupi wakati ikielekea kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi na mabadiliko mengine”

“Tukumbuke fedha hizi zinakusanywa maaalumu kwa ajili ya usajili na mambo mengine yenye manufaa kwa klabu”

Jana Kamati ya Uhamasishaji ilikutana kwa mara ya kwanza ambapo mpango wa kuchangisha kiasi cha Bil 1.5 uliandaliwa mkakati wa utekelezaji katika kila mkoa

FT : Simba 2-0 Ruvu Shooting

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba wameendeleza wimbi la ushindi katika ligi baada ya leo kuibamiza Ruvu Shooting mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa

Mabao ya Simba yalipatikana kwenye kipindi cha pili yakiwekwa kambani na beki Paul Bukaba (51′) huku bao la pili likifungwa na Meddie Kagere kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 55 baada ya Adam Salamba kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems alifanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake leo akiwapumzisha baadhi ya nyota waliocheza mchezo wa ligi ya mabingwa mwishoni mwa wiki

Aidha bao alilofunga Kagere leo limemfanya afikishe mabao 13 sasa akishika nafasi ya pili nyuma ya Salim Aiyee wa Mwadui Fc mwenye mabao 16

Simba inaendelea kushika nafasi ya tatu ikiwa imefikisha alama 54, alama tano nyuma ya Azam Fc inayoshika nafasi ya pili huku Yanga ikiongoza ikiwa na alama 67

Hata hivyo Azam Fc na Yanga zimecheza michezo saba zaidi ya Simba

Kikosi cha Simba vs Ruvu Shooting Leo

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba mda mchache ujao watashuka katika dimba la Taifa kuikabili Ruvu Shooting kwenye mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amekifanyia mabadiliko kikosi kinachoshuka dimbani leo, akiwapa mapumziko baadhi ya wachezaji huku wengine wakikosekana kutokana na kukabiliwa na majukumu ya timu za Taifa

Habari njema ni kujumuishwa kwa kiungo Jonas Mkude na Meddie Kagere ambao watajiunga na majukumu ya timu za Taifa baada ya mchezo wa leo

NIYONZIMA: Tutacheza fainali ya ligi ya mabingwa

Kiungo Haruna Niyonzima amesema Jumamosi ya March 16 2019 ilikuwa siku ya kipekee kwake na klabu ya Simba baada ya kufanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika

Niyonzima anayetajwa kuwa nyota wa mchezo wa siku hiyo ambao Simba iliilaza AS Vita Club mabao 2-1, amefichua kuwa licha ya kupata majeraha punde tu baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Emmanuel Okwi katika dakika ya 58, amesema alilazimika kuvumilia na kuhakikisha anaitumia vyema nafasi aliyopewa na kocha Patrick Aussems

“Nilijipa moyo na kusema siwezi kuruhusu majeraha haya yakanifanya nitoke nje. Nimekuwa nikijituma ili nipate nafasi kama hii,” amesema Niyonzima

“Tangu nikiwa mdogo nimekuwa na ndoto ya kucheza fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika. Hakuna kitakachonizuia kutimiza ndoto hiyo na pia sikuwa tayari kuwaangusha mashabiki wa Simba na Watanzania pamoja na ndugu zangu Wanyarwanda”

“Tuna nafasi ya kucheza fainali ya ligi ya mabingwa mwaka huu, bila shaka tutaweza kwani tuna kikosi cha kufanikisha hilo pamoja na mashabiki wanaotuunga mkono muda wote”

Aussems alia na mazoezi ya Stars

Kocha Mkuu wa timu ya Simba Patrick Aussems ameingiwa na hofu kutokana mazoezi wanayopewa wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kuwa yanaweza kupelekea majeruhi

Aussems ametoa tahadhari hiyo hasa ikizingatiwa kwenye kikosi cha Stars Simba ina wachezaji wanne

Wachezaji wa Simba walioitwa kikosi cha Stars ni Aishi Manula, Jonas Mkude, John Bocco na Erasto Nyon

Ikumbukwe mwishoni mwa mwaka jana Simba ilimpoteza beki wake Shomari Kapombe ambaye yuko nje kwa zaidi ya miezi mitano akiuguza majeraha aliyopata akiwa katika kambi ya Stars Afrika Kusini

Simba inakabiliwa na michezo ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa, droo ya hatua hiyo ikiatarajiwa kufanyika nchini Misri kesho

Kocha Mkuu wa Stars Emannel Amunike ameanza kukinoa kikosi cha Stars jana, wachezaji wakifanya mazoezi mara mbili kwa siku

Stars inajiandaa kuikabili Uganda Jumapili, March 24 2019

Simba kuivaa Ruvu Shooting bila nyota kibao

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba leo jioni watashuka katika dimba la Taifa kuikabili Ruvu Shooting kwenye mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Katika mchezo huo utakaopigwa saa moja jioni, Simba itawakosa baadhi ya nyota wake ambao wameitwa kujiunga na timu za Taifa

Nahodha John Bocco, Jonas Mkude, Erasto Nyoni na Aishi Manula wameitwa katika kikosi cha timu ya Taifa kinachojiandaa na mchezo dhidi ya Uganda Cranes utakaopigwa mwishoni mwa wiki

Meddie Kagere ameitwa kikosi cha Rwanda wakati Emannuel Okwi na Juuko Murshid wao wameitwa kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema atafanya mabadiliko madogo ya kikosi chake kitakachoshuka dimbani leo

Amewatoa wasiwasi Wanamsimbazi kuwa watafanya vizuri katika mchezo huo lengo likiwa ni kuondoka na alama zote tatu