Aussems asaka dawa ya kupata matokeo ugenini

Droo ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika imefanyika jana nchini Misri Simba ikipangwa kukipiga na TP Mazembe katika hatua hiyo

Simba itaanzia nyumbani kwa kuikaribisha TP Mazembe kwenye dimba la Taifa mchezo utakaopigwa kati ya April 05/06 na mchezo wa marudiano kupigwa Lubumbashi DR Congo kati ya April 12/13 2019

Simba imejipambanua kwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani baada ya kushinda michezo yote ya ligi ya mabingwa iliyocheza kwenye dimba la Taifa msimu huu, hivyo hakuna wasiwasi TP Mazembe hawatatoka salama uwanja wa Taifa

Hata hivyo vijana wa Patrick Aussems wamekuwa na wakati mgumu wanapokwenda ugenini. Wamefanikiwa kushinda mchezo mmoja tu dhidi ya Mbabane Swallows na kupoteza michezo mingine yote

Katika hatua ya makundi Simba iliruhusu mabao 12 ugenini huku pia ikishindwa kufunga bao lolote

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema ili waweze kutinga nusu fainali ni lazima wafanye vizuri nyumbani halafu wahakikishe hawafanyi vibaya ugenini

Amesema wamekuwa wakiyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika michezo ya ugenini na anaamini wataweza kufanya vizuri kwenye mchezo huo wa robo fainali dhidi ya TP Mazembe

Hata hivyo Aussems amesema Simba imevuka malengo iliyojiwekea kwa kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

Amesema michuano ya msimu huu imewasaidia kubaini mapungufu yao hasa kwa michezo ya ugenini na watayafanyia kazi ili msimu ujao wawe imara zaidi

Manara ataka shangwe la Simba lihamie Stars

Afisa Habari wa Simba Haji Manara amewataka mashabiki wa timu hiyo kupeleka shangwe kwa timu ya Taifa siku ya Jumapili itakapochuana na Uganda Cranes katika mchezo wa kusaka tiketi ya kutinga fainali za AFCON 2019

Manara amesema ni zamu ya Stars kufuzu kwa fainali za AFCON 2019 baada ya kujaribu bila ya mafanikio kwa miaka 39.

Amewataka mashabiki wa soka nchini bila ya kujali timu zao, waungane kuipa nguvu Stars ili iweze kupata ushindi dhidi ya Uganda

Naye Mkuu wa Dar es salaam Mh Paul Makonda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya uhamasishaji, amesema jukumu lake kubwa ambalo anaamini amelitekeleza ni kuiweka timu ya Taifa mikononi mwa Watanzania kuelekea mchezo dhidi ya Uganda

Akizungumza na Wanahabari kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere leo, Makonda amesema Watanzania wajitokeze kwa wingi uwanja wa Taifa Jumapili

Amesema atahakikisha usafiri wa kutosha unakuwepo kutoka kila pembe ya jiji la Dar es salaam

“Daladala yoyote kutoka sehemu yoyote ya jiji la Dar es salaam, nawapa ruhusa ya kuendesha route ya kutoka popote walipo kwenda Uwanja wa Taifa. Ukipata shida yoyote njiani nitafute mimi,” amesema Makonda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa jiji la Dar es salaam

“Tukishinda hii mechi nitakahikikisha tunafanya party kubwa sana ndani ya hili jiji la Dar na Tanzania kwa ujumla”

Mgeni rasmi wa mchezo huo atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Kassim Majaliwa

MBAO FC: Yatangaza KOCHA Mpya

Breaking News;
Uongozi wa Mbao Fc umefikia makubaliano na Mr Salum Mayanga kuwa kocha mkuu wa Mbao Fc.

Kabla ya kutua katika Camp la wabishi Kocha Salum Mayanga ameshawahi kufundisha Timu ya Taifa @taifastars_ na Mtibwa kwa mafanikio.

Tunamkaribisha Kocha wetu mpya katika jiji la Miamba Mwanza.

Wachezaji Simba wapewa mapumziko

Baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting juzi, wachezaji wa kikosi cha Simba ambao hawakuitwa katika timu za Taifa walipewa mapumziko ya siku nne kabla ya kuendelea na maandalizi ya michezo inayofuata

Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu amesema baada ya kucheza mechi mfululizo kwa takribani mwezi mzima, wamewapa wachezaji mapumziko hayo ili waweze kuondoa uchovu

Simba inatarajiwa kuerejea mazoezini Jumatatu ijayo kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Mbao Fc ambao huenda ukapigwa dimba la Jamhuri mkoani Morogoro, March 31 2019

Uwanja wa Taifa unatarajiwa kufungwa baada ya mchezo kati ya Tanzania dhidi ya Uganda utakaopigwa Jumapili, March 24 2019

Simba vs TP Mazembe robo fainali ligi ya mabingwa

Droo ya hatua ya robo fainali michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika imefanyika leo nchini Misri ambao mabingwa wa soka Tanzania Simba wamepangwa kucheza na TP Mazembe katika hatua hiyo ya robo fainali

Mchezo wa kwanza utapigwa jijini Dar es salaam April 05 huku mchezo wa marudiano ukitarajiwa kupigwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, April 12 2019

Simba itasafiri kwenda nCongo kwa mara ya pili katika michuano ya mwaka huu mara ya kwanza ikicheza na AS Vita katika hatua ya makundi

Mamelodi Sundowns mabingwa wa mwaka 2016 wao wamepangwa kuchuana na Al Ahly, Horoya ikipangwa kuchuana na Wydad Casablanca wakati CS Constantine imepangwa kuchuana na Esperance

Katika droo hiyo Simba iliwakilishwa na Afisa Mtendaji Mkuu Crescentius Magori na Mwenyekiti Swedi Mkwabi

Simba kucheza na Wydad, TP Mazembe au Esperance robo fainali ligi ya mabingwa

Droo ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika inafanyika leo huko Misri, saa 12 jioni kwa saa za Afrika Mashariki

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba ni miongoni mwa timu nane zinazosubiri kuwafahamu wapinzani wao katika hatua hiyo

Miongoni mwa kanuni zitakazotumika katika upangaji wa droo hiyo, timu zilizotoka kundi moja haziwezi kukutana katika hatua ya robo fainali

Kwa maana hiyo Simba haiwezi kukutana na Al Ahly kwenye hatua ya robo fainali

Pia timu zilizomaliza nafasi ya pili hatua ya makundi zitapangwa na timu zilizomaliza katika nafasi ya kwanza

Al Ahly, Wydad Casablanca, TP Mazembe na Esperance zimemaliza katika nafasi ya kwanza kwenye makundi yao hivyo ukiondoa Al Ahly, Simba itapangiwa miongoni mwa timu tatu zitakazokuwa zimesalia

YANGA : MICHANGO

Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Yanga Mh Anthony Mavunde amesema nahodha Ibrahim Ajib na Kocha Mwinyi Zahera hawajaondolewa kutia saini katika Akaunti Maalum iliyofunguliwa kukusanya fedha kwa ajili ya kuboresha kikosi cha timu hiyo

Mavunde ameiambia Yanga TV kuwa Ajib na Zahera watabaki kuwa watia saini kutokana na umuhimu wao

“Lazima kapteni na kocha waendelee kubaki kuwa watia saini sababu hawa ni watu muhimu sana,” amesema Mavunde

Aidha ili kuongeza uaminifu na kuwahakikishia Wanayanga kuwa fedha wanazochangia ziko salama, Mavunde amesema Kamati imependekeza kuongeza watia saini wengine ambao ni Mhasibu wa klabu na kiongozi mmoja wa Yanga

Pia Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamati maalum ambao ndio wanaongoza zoezi la kutafuta fedha nao watakuwa miongoni mwa watia saini

“Lakini pia viongozi waliopo, kwa maana mtaalamu wetu ambaye ni mhasibu na kiongozi mmoja wa Yanga nao watakuwepo sehemu ya watia saini”

“La tatu ni kundi la Kamati yenyewe ambao kimsingi ndio watafuta fedha, Mwenyekiti nitakuwepo miongoni mwa watia saini na Makamu Mwenyekiti”

“Hii yote tunaifanya katika kuongeza uwajibikaji na vilevile tuishi kwenye misingi ya uadilifu mkubwa ili fedha inayochangwa na Mwanayanga iende kufanya kazi iliyokusudiwa”

Mpinzani wa Simba robo fainali ligi ya mabingwa kujulikana leo

Droo ya hatua ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika inafanyika leo huko Misri

Simba ikiwa miongoni mwa timu nane zilizotinga hatua hiyo, baadae leo itaweza kumfahamu mpinzani wake kati ya Esperance ya Tunisia, Wydad Casablanca ya Morocco, TP Mazembe ya Congo, Mamelodi ya Afrika Kusini, Horoya ya Guinea, Asec Mimosa ya Ivory Coast na Al Ahly ya Misri.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba Crescentius Magori na Mwenyekiti wa klabu hiyo Swedi Mkwabi wataiwakilisha Simba katika droo hiyo inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini

Kuelekea droo hiyo, kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema baada ya kufanikiwa kutinga robo fainali, hawaihofii timu yoyote watakayopangwa nayo katika hatua inayofuata

Michezo ya duru ya kwanza ya hatua ya robo fainali itapigwa April 05 2019 huku michezo ya marudiano ikitarajiwa kupigwa April 12