Mastaa kibao waalikwa ‘Gala Dinner’ May 11

Siku ya Jumamosi ya May 11 2019 Yanga imepanga kuandika historia jijini Dar es salaam katika hafla maalum ya chakula cha jioni iliyoandaliwa Kamati ya Uhamishaji wa michango inayoongozwa na Mh Anthony Mavunde

Hafla hiyo ambayo itatumika ‘kuijaza Yanga mapesa’, itawashirikisha wadau wake mbalimbali ambao kwa umoja wao wamedhamiria kuirejesha heshima ya timu hiyo

Mwanamuziki Ali Kiba ni miongoni mwa watu maarufu watakaohudhuria hafla hiyo itakayofanyika Hoteli ya Serena kuanzia saa 12 jioni

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mh Jokate Mwegelo, Wema Sepetu, Jackline Wolper, Batuli, Vicent Kigosi na Steve Nyerere nao watakuwepo

Rekodi ya mabao Simba inatisha

Simba imeendelea ‘kuzikimbiza’ timu nyingine zinazoshiriki ligi kuu ya Tanzania Bara, ikiongoza kwa kufunga mabao

Mabao mawili yaliyoiwezesha Simba kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya Mbeya City leo, yameifanya timu hiyo iwe imefunga mabao 60

Meddie Kagere sasa ndiye kinara wa kuzifumania nyavu akiwa ametupia kambani mabao 17 akiwaacha washindani wake Salum Aiyee (16) na Heritier Makambo (16)

Katika mabao 60 yaliyofungwa mpaka sasa, Kagere, Okwi na Bocco wamechangia mabao 41

Kagere (17), Okwi (10) na Bocco (14)

Lakini pia Simba ndio timu iliyoruhusu mabao machache zaidi mpaka sasa ikiwa imefungwa mabao 12 tu. Azam Fc inafuatia ikiwa imeruhusu mabao 19

Simba inakaribia kutetea ubingwa wake ikihitaji kushinda michezo sita kati ya tisa iliyobaki

Baada ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons keshokutwa, Simba itarejea jijini Dar es salaam ambako itacheza michezo sita katika dimba la Taifa/Uhuru

Huenda ikatangaza ubingwa kupitia michezo hiyo

FT : Mbeya City 1-2 Simba

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba wameendelea kuukaribia ubingwa wa pili mfululizo baada ya leo kuichapa Mbeya City mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya

Mchezo huo uliathiriwa na mazingira ya uwanja uliojaa maji baada ya mvua kunyesha muda mchache kabla ya mchezo kuanza

Mbeya City ilitangulia kufunga bao katika dakika ya 22 kupitia kwa Iddi Selemani Naddo

Hata hivyo Simba ilirejea ikiwa imara kwenye kipindi cha pili na kusawazisha bao hilo kupitia kwa Jonas Mkude kwenye dakika ya 68 kabla Meddie Kagere hajaihakikishia Simba alama tatu muhimu kwa kufunga bao la ushindi kwenye dakika ya 85

Ushindi huo umeifanya Simba ifikishe alama 75, ikiendelea kushika nafasi ya pili kwa tofauti ya alama tano dhidi ya Yanga

Itacheza mchezo mwingine dhidi ya Tanzania Prisons keshokutwa Jumapili hapohapo dimba la Sokoine

Sevilla yaahirisha mchezo dhidi ya Singida United

May 23 2019 Simba itacheza mchezo wa Kimataifa wa kirafiki dhidi ya Sevilla inayoshiriki ligi kuu ya Hispania maarufu kama La Liga

Hata hivyo kulingana na ratiba ya ligi iliyotolea awali na Bodi ya Ligi, May 22 Simba ilipaswa kuwa mkoani Singida kucheza na Singida United

Bodi ya ligi imelazimika kuahirisha mchezo huo dhidi ya Singida United

Huenda Simba ikacheza na Singida United baada ya mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa May 28 kwani baada ya kuikabili Sevilla, May 25 Simba itacheza na Biashara United mchezo utakaopigwa uwanja wa Taifa

Simba yasaka alama tatu dhidi ya Mbeya City leo

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba wako mkoani Mbeya ambapo leo watashuka dimba la Sokoine kuwakabili wenyeji wao Mbeya City

Simba inayoshika nafasi ya pili baada ya kujikusanyia alama 72, inahitaji ushindi katika michezo saba tu ili kuubakisha ubingwa Msimbazi

Msemaji wa Simba Haji Manara amesema wachezaji wa timu hiyo wako katika hali nzuri tayari kwa mchezo huo

“Timu imewasili salama mkoani Mbeya tayari kwa mchezo. Tunafahamu hautakuwa mchezo mwepesi lakini wachezaji wetu watapambana kuhakikisha tunaondoka na alama zote tatu,” amesema

Katika mchezo wa leo, Simba itamkosa nahodha wake John Bocco ambaye aliumia kwenye mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania

Wengine watakaokosekana ni Asante Kwasi, Paschal Wawa na Shomari Kapombe

Baada ya mchezo huo Simba itaendelea kubaki mkoani Mbeya ambapo keshokutwa May 05 itachuana na Tanzania Prisons

Simba yamlilia Dk Mengi

Uongozi wa klabu ya Simba umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Dk Reginald Mengi kilichotokea jana Dubai

Taarifa iliyotolewa na Simba imesema klabu inaungana na familia na Watanzania katika kuomboleza msiba huo mkubwa