Pointi 18 kuipa Simba ubingwa

Licha ya Yanga kuongoza ligi kwa tofauti ya alama tano dhidi ya Simba, haitakuwa na ubavu wa kuipoka Simba taji walilotwaa msimu uliopita kama mabingwa hao watetezi watashinda michezo sita tu kati ya tisa ilyobaki

Yanga ina alama 80 na imebakiwa na michezo minne ambayo hata kama wakishinda yote watafikisha alama 92

Simba yenye alama 75 ikishinda michezo sita itafikisha alama 93 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine yoyote

kesho Simba itarejea uwanja wa Sokoine kusaka alama nyingine tatu kati ya 18 zinazohitajika ili kutetea ubingwa katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons

Habari njema ni kwamba baada ya mchezo huo, Simba itarejea jijini Dar es salaam ambako itacheza michezo sita

Ushindi katika michezo hiyo itakayopigwa uwanja wa Taifa/Uhuru, utawahakikishia mabingwa hao kuubakisha ubingwa Msimbazi mapema tu hata kabla ya tarehe ya mwisho ya kufunga msimu

Nyoni aahidi pointi tatu dhidi ya Tanzania Prisons

Beki kiraka wa Simba Erasto Nyoni amesema wamefuata alama sita mkoani Mbeya, alama tatu walizipata jana na kesho watapambana kuhakikisha wanapata alama nyingine tatu dhidi ya Tanzania Prisons

Licha ya changamoto ya ukaribu wa michezo yake, Nyoni amesema wataendelea kujituma ili kupata matokeo yatakayo-wahakikishia kutetea ubingwa waliotwaa msimu uliopita

Baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City jana, kesho Jumapili Simba itarudi tena uwanja wa Sokoine kuikabili Tanzania Prisons

Simba itahitaji kuwa katika ubora wake ili kuondoka na ushindi dhidi ya Prisons iliyoimarisha kiwango chake tangu ilipoanza kunolewa na kocha Adolph Richard

Aidha mazingira ya uwanja wa Sokoine yanaweza kuchangia kuharibu burudani kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo

Hata hivyo Nyoni amesema kama walifanikiwa kupata ushindi dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja huo, basi watahakikisha wanashinda mchezo dhidi ya Prisons

“Hali ya uwanja hatuwezi kuikwepa lakini jambo la msingi kwetu tutahakikisha tunapambana. Tunawaahidi mashabiki wetu kuwa tumedhamiria kushinda mchezo huo,” amesema

Simba iheshimiwe – Manara

Msemaji wa Simba Haji Manara ameeleza kushangazwa na kauli zinazotolewa na baadhi ya makocha wa timu zinazoshiriki ligi kuu kuwa timu hiyo inabebwa

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mbeya leo, Manara amesema uongozi wa timu hiyo uliamua kukaa kimya kwa kuwa haukuona umuhimu wa kuwajibu wanaoropoka

Hata hivyo amesema ukimya huo haumaanishi kuwa wanazifurahia kauli hizo

Amesema Simba ni taasisi kubwa na ametaka taasisi hiyo iheshimiwe, isiingizwe katika tuhuma ambazo hazina ukweli wowote

“Tunawataka wote wanaotuhusisha na masuala ya rushwa waache mara moja na kama wana usahidi wapeleke kwa vyombo husika,” amesema

“Simba sio klabu dhaifu, Simba sio klabu nyonge isifike mahali Simba ikafanywa kuwa ni timu dhaifu. Simba ni taasisi kubwa, tunaomba iheshimiwe”

“Mafanikio tunayopata yanatokana na ubora wa timu yetu. Msimu huu tumefika robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa, mtu anasemaje kuwa kiwango cha soka Tanzania hakijapanda?”

“Huku ni kuikosea heshima nchi yetu”

Azam Fc yaichapa KMC 1-0, yatangulia fainali kombe la FA

Azam Fc imefanikiwa kutinga fainali ya michuano ya kombe la FA (ASFC) baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ambao umechezwa uwanja wa Azam Complex

Bao pekee la Azam lilifungwa na Donald Ngoma katika dakika ya 75

Mchezo wa pili wa nusu fainali kati ya Lipuli Fc dhidi ya Yanga utachezwa Jumatatu, May 06 uwanja wa Samora mkoani Iringa

Mshindi wa mchezo huo atachuana na Azam Fc katika mchezo wa fainali utakaopigwa Juni 02 2019 uwanja wa Ilulu mkoani Lindi

Yanga yatua Iringa kibabe, yaipania Lipuli Fc

Vinara wa ligi kuu Tanzania Bara Yanga waliwasili mkoani Iringa jana jioni tayari kwa mchezo wa nusu fainali kombe la FA dhidi ya Lipuli fc

Mchezo huo utapigwa Jumatatu, May 06 uwanja wa Samora

Yanga inayosaka nafasi ya kurejea kwenye michuano ya Kimataifa msimu ujao, imepania kushinda mchezo huo ili kutinga fainali ambapo kama ikifanikiwa, itachuana na Azam Fc

Msafara wa Yanga umejumuisha wachezaji 24 ambao leo wataanza maandalizi ya mchezo huo mkoani Iringa

MATOKEO MECHI ZA LEO LIGI KUU

MATOKEO YA MECHI ZA LEO

FT: Mbeya City 1-2 Simba SC (Naldo 22’ : Mkude 68’, Kagere 85’)
.
.
FT: Singida United 1-1 Mtibwa Sugar (Habib Kyombo 32’ : Ismail Aidan 45’+1)
.
.
FT: Ruvu Shooting 3-1 JKT Tanzania (Musa Said 48’, Emmanuel Martin 59’, Fully Maganga 79’: Ally Bilaly 44’)
.
.
FT: Alliance FC 2-2 Kagera Sugar (Birimana Blaise 39’, Dickson Ambundo 90’+5 : Ramadhan Kapera 53’, Peter Mwalyanzi 71’)
.
.
#TanzaniaPremierLeague

Yanga yaomboleza kifo cha Mwanachama wake Dk Mengi

TAARIFA

Uongozi wa Yanga, wanachama na mashabiki wamepokea kwa masikitiko makubwa sana kifo cha aliekuwa Mwenyekiti mtendaji wa makampuni ya IPP Dkt Reginald A Mengi kilichotokea jana uko falme za kiarabu

Mzee Mengi alikuwa mwanachama na pia mwanafamilia wa Yanga na tunatambua sana mchango wake kwenye klabu yetu

Tunaungana na Familia pamoja na wa Tanzania wote kwenye kipindi hiki kigumu cha Maombolezo

Bwana ametoa na bwana ametwaa jina lake lihimidiwe

Kesi ya kupinga uchaguzi Yanga yafutwa, kadi zote kutumika

Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi ya TFF Malangwe Mchungahella ambaye Kamati yake inashirikiana na kamati Maalum ya Uchaguzi ya Yanga, amesema kesi iliyokuwa imefunguliwa na Wanachama wawili ya kupinga uchaguzi wa Yanga, imefutwa.

Mchungahella amesema baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuta shauri hilo, uchaguzi utafanyika May 05 kama ulivyopangwa

Aidha amesema mpaka sasa zoezi la kampeni linaendelea vizuri na hakuna malalamiko yoyote ya uvunjwaji wa sheria

Mchungahella amesema wanachama wote wenye kadi za zamani (kitabu) na za ki-elektroniki (posta) wataruhusiwa kushiriki katika mchakato huo

Muhimu ni Mwanachama lazima awe amelipia ada ya mwaka

Yondani aongeza nguvu Yanga

Beki kisiki wa Yanga Kelvin Yondani amejumuishwa kwenye kikosi cha timu hiyo kilichoondoka leo kuelekea mkoani Iringa kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali kombe la FA dhidi ya Lipuli Fc

Mchezo huo utapigwa Jumatatu, May 06 katika uwanja wa Samora

Yondani amemaliza kutumikia adhabu ya kukosa michezo mitatu baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar uliopigwa jijini Mwanza

Amekosa michezo dhidi ya Mtibwa Sugar, Azam Fc na Tanzania Prisons

Wachezaji waliojumuishwa kwenye msafara huo ni pamoja na Klaus Kindoki, Ramadhan Kabwili, Kelvin Yondan, Haji Mwinyi, Juma Abdul, Paul Godfrey, Abdallah Shaibu, Endrew Vicent, Said Makapu, Feisal Salum, Mohammed Issa, Papy Tshishimbi, Thaban Kamusoko, Deus Kaseke, Mrisho Ngasa, Ibrahim Ajib, Raphael Daud, Herieter Makambo, Amiss Tambwe, Haruna Moshi, Jaffar Mohamed, Ibrahim Hamid na Pius Buswita

Mchezo wa kwanza wa nusu fainali kombe la FA unapigwa leo kati ya Azam Fc dhidi ya KMC, saa moja jioni uwanja wa Azam Complex