Nyoni augua ghafla, kuikosa Alliance Fc

Simba imepata pigo baada ya beki kiraka Erasto Nyoni kuugua ghafla hivyo atakosa mchezo wa kesho dhidi ya Alliance Fc

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amethibitisha kuwa Nyoni hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kitakachoshuka dimbani kuikabili Alliance Fc

Nyoni anaungana na beki Paschal Wawa ambaye hakusafiri jijini Mwanza kutokana na majeruhi yanayomkabili

Simba yajifua CCM Kirumba, kamili kuikabili Alliance Fc

Kikosi cha Simba leo jioni kimefanya mazoezi kwenye uwanja wa CCM Kirumba yakiwa ni maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Alliance Fc

Mchezo huo utapigwa kesho Jumanne, April 23 katika uwanja huo

Simba ilitua Mwanza mapema jana ikitokea Kagera ambako ilipoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar kwa kuchapwa mabao 2-1

Katika mazoezi hayo yaliyosimamiwa na kocha Patrick Aussems, Simba iliwaruhusu kukaa jukwaani mashabiki waliofika kuwashuhudia mabingwa hao watetezi

Kuelekea mchezo huo, Aussems amesema wanatarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa Alliance Fc kutokana na ubora wa kikosi cha timu hiyo

Hata hivyo amesema Simba inahitaji kushinda mchezo huo hasa baada ya kupoteza mchezo uliopita

“Tunajua haitakuwa mechi rahisi sababu Alliance ni timu nzuri lakini sisi tumepoteza mchezo Bukoba na kesho tunataka alama tatu,” amesema Aussems

“Tunajua kwanini tulipoteza na tumejiandaa kwa hilo na ninaamini kesho tutakuwa vizuri.”

Simba Queens yaifumua Yanga Princess 5-1

Wanamama wa Simba Queens leo wameendeleza ubabe kwa watani zao Yanga Princess baada ya kuwafumua mabao 5-1 katika mchezo wa ligi kuu ya Wanawake, Serengeti Lite uliopigwa uwanja wa Karume

Magoli ya Simba Queens yalipachikwa na Opah Clement aliyefunga mabao mawili, Mwanahamisi Omary, Joele Bukulu na Amina Ramadhani na goli pekee la Yanga Princess likifungwa na Fausta Thomas

Huu ni ushindi wa pili kwa Simba Queens dhidi ya watani zao, wakipata ushindi wa mabao 7-0 katika mchezo wa duru ya kwanza wa ligi hiyo ya Wanawake

Nyota kibao Simba kumaliza mikataba mwishoni mwa msimu

Bodi ya Wakurugenzi klabu ya Simba imemuagiza kocha Mkuu wa timu hiyo Patrick Aussems kuwasilisha ripoti yake kwa ajili ya usajili wa msimu ujao

Simba imedhamiria kuanza mapema maboresho ya kikosi chake ambapo imebainika mikataba ya nyota zaidi ya 10 inamalizika mwishoni mwa msimu

Baadhi ya wachezaji ambao mikataba yao inaelekea ukiongoni ni pamoja na John Bocco, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni, Aishi Manula, Shomari Kapombe, Paschal Wawa, Paul Bukaba, James Kotei, Asante Kwasi na Nicolas Gyan

Imeelezwa hatma ya wachezaji hao inasubiri mapendekezo ya Aussems ambaye ndiye aliyeachiwa jukumu zima la usajili huku uongozi wa Simba ukibaki katika utekelezaji

Hata hivyo idadi kubwa ya wachezaji hao wataendelea kubaki Msimbazi kutokana na mchango mkubwa waliotoa msimu huu

Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba Crescentius Magori amesema hawatarajii kukivuruga kikosi chao ambacho kimefanya vizuri msimu huu lakini watasikiliza kile kitakachopendekezwa na Aussems kwa ajili ya maboresho

“Masuala yote ya usajili Simba mwenye kauli ya mwisho ni kocha. Tunafahamu baadhi ya nyota wetu mikataba yao inamalizika, hata hivyo mpaka sasa hakuna mchezaji ambaye kocha amesema tumuache, hivyo tutawapa mikataba mipya,” amesema Magori

Baada ya Simba kuondoshwa hatua ya robo fainali michuano ya Ligi ya Mabingwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ alisema msimu ujao wanataka kuwa na kikosi imara zaidi na hawatasita kuachana na wachezaji ambao mchango wao ni mdogo au watovu wa nidhamu

Simba Queens yaiandalia kipigo Yanga Princess leo

Wakinadada wa Simba Queens leo watashuka kwenye uwanja wa Karume kupepetana na watani zao wa jadi Yanga Princess katika mchezo wa ligi kuu ya Wanawake, Serengeti Lite

Simba Queens inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo, imepania kuendeleza umwamba dhidi ya wapinzani wao hao ambao wanashika nafasi ya saba

Katika mchezo wa raundi ya kwanza Simba Queens iliibamiza Yanga Princess mabao 7-0

JKT Queens inaongoza ligi ikiwa imejikusanyia alama 45 ikiwa imeshinda michezo yake yote.

Mlandizi Queens inashika nafasi ya pili ikiwa imejikusanyia alama 32 sawa na Alliance Girls timu hizo zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa

Simba Queens iko nafasi ya nne ikiwa na alama 31 wakati Yanga Princess inashika nafasi ya saba ikiwa na alama 19

Aussems ameipaisha Simba, asubiri kusaini mkataba mpya

Wakati alipokabidhiwajukumu la kuinoa Simba mwanzoni mwa msimu, Patrick Aussems alipewa masharti mawili; moja ni kuipeleka Simba hatua ya makundi michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika na pili ni kutetea ubingwa ligi kuu

Aussems amekamilisha sharti la kwanza na kuvuka malengo baada ya kufanikiwa kuivusha Simba hadi robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa

Sharti lililobaki ni la kutetea ubingwa wa ligi kuu, sharti ambalo nalo anaelekea kulikamilisha

Mbelgiji huyo aliyechukua nafasi ya Pierre Lechantre, hakuna shaka atapewa mkataba mpya kuendelea kuinoa Simba kutokana na mafanikio aliyoipatia timu hiyo msimu huu

Mkataba wake na Simba aliosaini msimu uliopatita utamalizika mwishoni mwa msimu

TETESI ZA USAJILI BARANI ULAYA LEO JUMATATU

Kiwango cha mshahara anachokitaka kiungo wa Manchester United Paul Pogba, 26, kinaweza kikawa kikwazo kwa Real Madrid kumsajili nyota huyo raia wa Ufaransa. (AS)

Chelsea wannapiga hesabu za kumnyakua kiungo wa Brazil na klabu ya Barcelona Philippe Coutinho, 26, kama mbadala wa mshambuliaji wao raia wa Ubelgiji Eden Hazard, 28, ambaye mwisho wa msimu anatarajiwa kuhamia Real Madrid.(Calciomercato)
Klabu ya Manchester United ipo tayari kumpandisha Mike Phelan mpaka kuwa mkurugenzi wa ufundi, na nafasi yake ya meneja msaidizi kupewa kiongo wa zamani wa klabu hiyo Michael Carrick. (Mail)

Mchezaji nyota wa zamani wa Arsenal ambaye pia alitimuliwa kwenye kazi ya ukufunzi na klabu ya Monaco, Thierry Henry, 41, yumo kwenye mazungumzo na klabu ya New York Red Bulls ya ligi ya soka Marekani ili kujiunga nao kama mkufunzi. (Sky Sports)
Mshambuliaji nyota wa Ufaransa na klabu ya PSG Kylian Mbappe, 20, amekanusha uvumi ulioenea kuwa ana mpago wa kuhamia Real Madrid. Mbappe ametoa kauli hiyo baada ya kuifunga goli tatu timu yake ya zamani Monaco. (Goal.com)
Beki raia wa Brazil Marcelo, amesisitiza kuwa hana mpango wa kuihama klabu yake ya Real Madrid mwishoni mwa msimu – licha ya uvumi kuenea kuwa mchezaji huyo alikuwa akitammani kuungana tena na Cristiano Ronaldo, katika klabu ya Juventus. (Bein Sports, via Mirror)

Marcelo
Image captionMarcelo (kulia) ameamua kuuzima uvumi kuwa anajipanga kuhamia Juventus mwishon mwa msimu.
Kocha wa muda mrefu wa wachezaji chipukizi wa Aston Villa Sean Kimberley ameikacha klabu hiyo. (Birmingham Mail)
Bosi wa Newcastle Rafa Benitez amedai kuwa mfumo wa mishahara wa klabu hiyo unaifanya timu isiwe na matokeo mazuri kwenye Ligi ya Premia. (Newcastle Chronicle)
Rafa Benitez
Image captionRafa Benitez amekuwa akihusishwa na mipango ya kuihama Newcastle
Mshambuliaji wa Newcastle raia wa Uhispania Ayoze Perez, 25, ameashiria kuwa anataka kuihama klabu hiyo mwushoni mwa msimu. (Mirror)

Rais wa klabu ya Nice ya Ufaransa Gauthier Ganaye amesema klabu yake huenda ikamsajili mshambuliaji wa Chelsea Olivier Giroud, 32. (Goal.com

Yanga kuanza mawindo ya Azam Fc Jumanne

Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kurejea mazoezini kesho Jumanne kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Azam Fc utakaopigwa Jumatano ijayo April 29 katika uwanja wa Taifa

Kocha Mkuu wa vinara hao wa ligi Mwinyi Zahera aliwapa wachezaji siku tatu za mapumziko ili washeherekee sikukuu ya Pasaka wakiwa na familia zao

Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh amesema baada ya mapumziko hayo, kesho wataanza kujifua uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini kujiandaa na mchezo huo

Yanga bado haijakata tamaa katika mbio za kuwania ubingwa licha ya watani zao Simba kuwa na idadi kubwa ya michezo ya viporo ambayo kama watashinda yote, watatetea ubingwa waliotwaa msimu uliopita

Juzi Zahera alisema hesabu zao ni kushinda michezo yote sita iliyobaki huku akiamini wapinzani wao Simba wataendelea kudondosha pointi hivyo kuwapa mwanya wa kutwaa ubingwa

Yanga iko kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imejukusanyia alama 74 baada ya kushuka dimbani mara 32.

Inafuatiwa na Azam Fc yenye alama 66 ikiwa imeshuka dimbani mara 32 pia. Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 60 ilizovuna katika michezo 24

Simba ilivyojifua Mwanza

Baada ya kuwasili jijini Mwanza mapema leo, jioni kikosi cha Simba kiliendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Alliance Fc

Mchezo huo utapigwa keshokutwa, April 23 2019 katika uwanja wa CCM Kirumba