Ushindi dhidi ya Alliance umetuongezea morali – Niyonzima

Kiungo Haruna Niyinzima amesema ushindi wa mabao 2-0 waliopata jana dhidi ya Alliance Fc umewaongezea morali wachezaji na wataendelea kupambana ili kuhakikisha wanatetea ubingwa waliotwaa msimu uliopita

Niyonzima aliye katika kiwango bora, aliifungia Simba bao la kwanza na baadae Okwi kuongeza la pili katika kipindi cha pili

“Mchezo haukuwa rahisi hasa kutokana na matokeo tuliyopata kwenye mchezo uliopita, tulikuwa na presha ya kupata ushindi,” amesema Niyonzima

“Tunashukuru tumefanikiwa kuondoka na alama zote tatu, matokeo haya yametuongezea morali ya kufanya vizuri kwenye michezo ijayo”

Akizungumzia ugumu wa ratiba, Niyonzima amesema Simba ilisajili wachezaji 30 hivyo anaamini wataweza kukabiliana na changamoto ya kucheza kila baada ya siku mbili au tatu

“Kocha alituambia atakuwa akifanya mabadiliko ya kikosi ili kuhakikisha kila mchezaji anahusika. Hii ndio faida ya kusajili wachezaji wengi”

“Najua haitakuwa kazi rahisi lakini naamini tutafanikiwa kutetea ubingwa”

Simba imebaki jijini Mwanza ambapo kesho itashuka tena kwenye uwanja wa CCM Kirumba kuikabili KMC

Djuma yamkuta Rwanda, atimuliwa As Kigali

Aliyewahi kuwa kocha Msaidizi wa Simba Masudi Djuma ambaye alikuwa kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo, ametimuliwa klabu ya AS Kigali aliyokuwa akiifundisha

Djuma alijiunga na AS Kigali mwezi Oktoba mwaka jana baada ya uongozi wa Simba kuvunja mkataba wake akituhumiwa kumfanyia hujuma kocha Patrick Aussems

Djuma ameinoa AS KIgali kwa muda wa miezi saba tu akitimuliwa baada ya kuiongoza timu hiyo katika michezo mitano iliyopita bila ya kupata ushindi

Faini zaiandama Yanga

Klabu ya Yanga imetozwa faini ya sh. 3,000,000 (milioni tatu) kutokana na timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi dhidi ya Ndanda Fc iliyofanyika Aprili 4, 2019 katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Hilo ni kosa la nne msimu huu kwa timu ya Yanga kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi, na adhabu dhidi yake imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Taratibu za Mchezo.

Aidha, Yanga pia imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuwarushia chupa za maji waamuzi wakati wakirejea vyumbani baada ya mechi dhidi ya Ndanda Fc kumalizika

Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Klabu

Beki wake kisiki mkongwe Kelvin Yondani amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji wa Kagera Sugar FC katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 11, 2019 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 38(9) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji

Yondani tayari amekosa mchezo mmoja dhidi ya Mtibwa Sugar

Zahera aipania Azam Fc

Kikosi cha Yanga leo kimeendelea na mazoezi kwenye uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa April 29 2019 katika uwanja wa Taifa

Muda wa mchezo huo utapigwa saa kumi kamili jioni

Wachezaji wote wa Yanga wako katika hali nzuri ambapo Daktari wa timu hiyo Dk Edward Bavu amesema hakuna majeruhi

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema mchezo dhidi ya Azam Fc hautakuwa mwepesi lakini una umuhimu wa kipekee kwa Yanga kupata ushindi ili kuwa na nafasi ya kutwaa ubingwa

“Najua wazi mechi yetu na Azam FC itakuwa ngumu na ya nguvu kwetu kwa sababu sisi wote tunataka tushinde mechi hiyo ili tuzidi kujiwekea mazingira mazuri katika ligi,” amesema

“Tunajiandaa vizuri ili tushinde tuwaache mbali wapinzani wetu, hii ni mechi ambayo tunahitaji matokeo zaidi na tutapambana kwa ajili ya hilo”

FT : Alliance 0-2 Simba

Simba imeendeleza mawindo yake ya ubingwa wa pili mfululizo ambapo leo imefanikiwa kuibomoa Alliance Fc mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa CCM Kirumba

Simba iliyokuwa na mabadiliko katika kikosi kilichoanza, ilijipatia bao la kuongoza kwenye dakika ya 21 kupitia kwa kiungo fundi Haruna Niyonzima

Bao la pili liliwekwa kambani na Emmanuel Okwi kwenye dakika ya 75

Okwi alianzia benchi kwenye mchezo huo ambapo aliingia katika dakika ya 64 kuchukua nafasi ya Adam Salamba

Hilo lilikuwa bao la tisa kwa Okwi msimu huu sasa akiwa amefunga katika michezo yote miwili iliyopita

Matokeo hayo yameifanya Simba ifikishe alama 63 sasa ikiwa nyuma ya Azam Fc kwa tofauti ya alama tatu

Ushindi katika mchezo unaofuata dhidi ya KMC utaipaisha Simba hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi

Simba itaendelea kubaki jijini Mwanza kusubiri mchezo dhidi ya KMC ambao utapigwa keshokutwa Alhamisi, katika uwanja wa CCM Kirumba

Tunahitaji ushindi dhidi ya Alliance Fc – Mkude

Kiungo Jonas Mkude amesema wanafahamu hawana nafasi ya kufanya makosa zaidi kwani wanahitaji kutetea ubingwa waliotwaa msimu uliopita

Simba iko mkoani Mwanza ambapo leo itachuana na Alliance Fc katika mchezo utakaopigwa uwanja wa CCM Kirumba

Akizungumza baada ya mazoezi ya jana jioni, Mkude alisema baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar, wanahitaji kupata matokeo dhidi ya Alliance Fc leo

“Hakuna mechi rahisi katika Ligi Kuu, lakini timu itakayokuwa na nidhamu uwanjani ndiyo yenye asilimia kubwa ya kupata pointi tatu muhimu. Tunahitaji kuwa kwenye ubora wetu ili tuweze kushinda kesho (leo)” amesema

Aidha, Mkude alisema hakuna timu inayoingia uwanjani kwa ajili ya kufungwa, ila anayeruhusu kufanya makosa ndiyo yanaweza kuwagharimu na hatimaye kupoteza mchezo.

“Tumekuja kupambana, mechi zetu hizi zimekuwa zinatizamwa sana na wapinzani wetu, tukifanya vizuri itatusaidia kutetea ubingwa tunaoushikilia na hiyo ndiyo mipango yetu”

Baada ya mechi ya leo, Simba itaendelea kubaki jijini Mwanza kusubiri mchezo dhidi ya KMC FC utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba pia.

Simba yapania kufuta makosa CCM Kirumba leo

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba leo wanashuka kwenye uwanja wa CCM Kirumba kuikabili Alliance Fc katika mchezo unaotarajiwa kupigwa saa kumi kamili jioni

Kikosi cha Simba kiko jijini Mwanza tangu juzi kikiendelea na maandalizi ya mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka

Baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar, Simba imepania kusahihisha makosa yake na kuibuka na ushindi dhidi ya Alliance Fc leo

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema anafahamu mchezo hautakuwa mwepesi lakini wanahitaji kuondoka na alama zote tatu

Katika mchezo wa leo Simba itamkosa beki kiraka Erasto Nyoni ambaye ni mgonjwa

Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu amewataja Nyoni, Paschal Wawa na Shomari Kapombe kuwa wachezaji pekee watakaokosekana kwenye mchezo huo

Simba iliyoshuka dimbani mara 24 inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa imejikusanyia alama 60

Bado mabingwa hao watetezi wana michezo nane ya viporo ambayo kama watashinda yote watajikita kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama 10 dhidi ya Yanga inayoongoza