Yondani, Kakolanya waikosa Safari ya Shinyanga

Yanga itashuka uwanja wa Kamabarage mkoani Shinyanga keshokutwa Alhamisi, Novemba 22 2018 kumenyana na Mwadui Fc kwenye mchezo wa kiporo wa ligi kuu ya Tanzania Bara.

Kikosi cha Yanga kimeondoka Alfajiri ya leo kwa usafiri wa Ndege mpaka Mwanza ambako kimechukua usafiri wa basi kuelekea mkoani Shinyanga.

Nahodha Kelvin Yondani na Mlinda lango Beno Kakolanya sio miongoni mwa wachezaji waliosafiri baada ya kushindwa kuripoti kambini kwa wakati.

Wachezaji hao waliokuwa na timu ya Taifa nchini Lesotho, walipaswa kuwepo kambini kabla ya safari hiyo licha ya kuwasili na kikosi cha Stars jana saa 12 jioni kutoka Afrika Kusini

Gadiel Michael na Feisal Salum inaelezwa wao waliweza kuwahi na wamesafiri.

Yanga pia itawakosa Ramadhani Kabwili, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Paulo Godfrey ‘Boxer’ ambao wako kwenye kikosi cha timu Taifa ya vijana U23 inayoshuka dimbani leo kumenyana na Burundi

Wengine wanaokosekana kutoka na majeraha ni Papi Tshishimbi na Juma Mahadhi ambaye hata hivyo ameanza mazoezi mepesi baada ya kuwa nje kwa miezi mitatu

STARS Yarejea Nchini Kutoka Lesoth

Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kimewasili leo Jumatatu jioni kutoka nchini Lesotho kwenye mchezo wa kuitafuta tiketi ya kucheza Fainali za Africa 2019.

Stars imerejea ikiwa na majonzi baada ya kupoteza mchezo muhimu dhidi ya Lesotho kwa kukubali kichapo cha bao 1-0 na kufifisha matumaini ya kufuzu fainali za AFCON 2019

Mchezo wa mwisho kundi L unatarajiwa kupiga mwezi March 2019 dhidi ya Uganda.

Ushindi katika mchezo huo unaweza kuipa Stars nafasi ya kufuzu iwapo Lesotho itashindwa kupata ushindi dhidi ya Cape Verde ugenini

Simba Sc yaiwinda Lipuli Fc

Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba wameendelea kujifua kwenye uwanja wa Boko Veterans kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Lipuli Fc.

Mchezo huo ambao awali ulipangwa kufanyika kesho, umesogezwa mbele na sasa utapigwa Ijumaa Novemba 23 kwenye uwanja wa Taifa.

Baada ya mchezo huo Simba itaendelea na maandalizi ya mchezo wa ligi ya mabingwa hatua ya awali dhidi ya Mbabane Swallows unaotarajiwa kupigwa Jumatano ya Novemba 28.

Wachezaji waliokuwa kwenye timu za Taifa wanatarajiwa kuanza kuwasili kikosini leo kuungana na wenzao ambao wamekuwa wakiendelea na mazoezi chini ya kocha Patrick Aussems

Tanzania (U23) va Burundi (U23)

Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania umri chini ya miaka 23, leo saa moja jioni kinashuka uwanja wa Taifa kuikabili Burundi kwenye mchezo wa marudiano kusakata tiketi ya kutinga AFCON 2019 ngazi ya vijana.

Vijana hao wa Tanzania tayari wako nyuma kwa mabao 2-0 kufuatia kuchapwa idadi hiyo ya mabao kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Burundi waiki iliyopita.

Stars U23 inahitaji ushindi wa zaidi ya mabao mawili ili kuweza kutinga raundi ya kwanza.

Kila la kheri vijana wa Stars U23.

SALAMBA kufanya majalibio Ubelgiji

Mshambuliaji wa Simba, Adam Salamba, yupo mbioni kutimkia kwenye Klabu ya Royal Sporting Club Anderlecht inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji.

Mshambuliaji huyo mwenye mabao mawili katika ligi ya msimu huu, aliyejiunga Simba akitokea Lipuli msimu huu, amepata nafasi hiyo kutoka kwa wakala wa beki wa Rayon Sport, Abdul Rwatubyaye anayeishi nchini humo.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Simba, zinasema mchezaji huyo anatarajia kuondoka nchini Desemba, mwaka huu kwa ajili ya kufanya majaribio ya wiki moja kwenye timu hiyo inayokamata nafasi ya nne, mbele ya vinara wa ligi hiyo, KRC Genk anayoichezea Mbwana Samatta.

“Salamba anaweza kuondoka mwezi ujao kuelekea Ubelgiji kwenda Anderlecht kwa ajili ya kufanya majaribio ya wiki moja, kuna wakala wa huko ndiyo anafanya hiyo mipango ya kumpeleka baada ya kuvutiwa na uwezo wake kwani ameanza kumfuatilia tangu akiwa na Lipuli.

“Mipango ndiyo ipo kwenye mchakato wa kuweza kuona mambo yanakwenda vipi ila huyo wakala ndiye anajua kila jambo na mambo ya safari ingawa inafahamika kama atakaa huko kwa wiki moja katika majaribio yake,” alisema mtoa taarifa.

Alipoulizwa Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi, akasema: “Bado sijapata taarifa za mchezaji huyo, hayo masuala ya timu yote yanajadiliwa kwanza na C.E.O ambaye ni (Crescentius) Magori pamoja na kocha kabla ya baadaye bodi kukutana na kujadiliana.”

Magori alipotafutwa jana, simu yake ya mkononi haikupokelewa.

Championi

Simba kuharakisha USAJILI wa Beki Wa Kulia

Kuumia kwa Shomari Kapombe kumewafanya mabosi wa Kamati ya usajili ya klabu ya Simba kuharakisha usajili wa mbadala wake imefahamika.

Kapombe alipata majeraha makubwa akiwa kwenye kambi ya timu ya Taifa nchini Afrika Kusini na upo uwezekano akawa nje kwa muda mrefu.

Msimu uliopita Nicolas Gyan alitumika kwenye nafasi hiyo kwa nyakati tofauti, hata hivyo ameshindwa kumshawishi kocha Patrick Aussems.

Gyan hajajumuishwa katika kikosi cha Simba kitakachoshiriki michuano ya ligi ya mabingwa inayoanza mwishoni mwa mwezi huu.

Katika mchezo wa kirafiki kati ya Simba dhidi ya Nyasa Big Bullets uliopigwa Ijumaa iliyopita, Aussems alimtumia Yusufu Mlipili kama beki wa kulia.

Hata hivyo Mlipili alishindwa kuimudu nafasi hiyo.

Wakati Simba ikiendelea na mchakato wa kusajili mlinzi wa kulia, huenda kiraka Erasto Nyoni akarejeshwa kwenye nafasi hiyo.

Nyoni ana uwezo wa kucheza nafasi zote za ulinzi na kiungo.

Simba inahusishwa na beki wa Tanzania Prisons Salum Kimenya ambaye amekiri kuwa katika mazungumzo na uongozi wa Simba

Simba sc Kuwatoa kimasomaso Watanzania Klabu Bingwa

Benchi la ufundi la Simba akili yote kwa sasa limeielekeza Mbabane Swallows kwenye mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mpango mkakati utakamilika mara baada ya wachezaji waliopo na timu zao za taifa kurejea kikosini.

Kalenda ya michuano ya Kimataifa imemalizika jana ambapo wachezaji waliokuwa na majukumu ya timu za Taifa wanatarajiwa kuanza kurejea kikosini kuanzia kesho.

Kocha wa Simba Patrick Aussems amesema zimebaki siku chache kabla ya mchezo huo, hivyo tayari ameanza program za kuwakabili wapinzani wao hao.

Aussems, amesema anaifuatilia Mbabane kujua uwezo na mapungufu yao.

“Kila kitu kinaenda sawa, tunaendelea na mazoezi kwa wachezaji tulionao kikosini huku tukiwasubiri waliopo kwenye timu za Taifa,” Aussems amenukuliwa na gazeti la Nipashe

Amesema mikakati yake na mbinu kamili kwa wachezaji wake zitakamilika pindi wachezaji wake waliopo timu za Taifa watakaporejea.

“Wakirejea tunaendelea na maandalizi yetu, kwa sasa naendelea na wachezaji tulionao, nashukuru kila kitu kinaenda sawa,” alisema Aussems.

Mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika umepangwa kuchezwa kati ya Novemba 27 na 28 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana Desemba 4-5, mwaka huu nchini Swaziland.

Timu itakayoibuka mshindi wa jumla itaingia kwenye hatua ya kwanza ya michuano hiyo kusaka nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika kwa ngazi ya klabu.

Amunike Ajitetea kipigo cha lesotho

Baada ya kushushiwa lawama mashabiki kwa kikosi alichopanga kwenye mchezo wa jana, kocha Mkuu wa Taifa Stars Emmanuel Amunike amesema uamuzi wake ulitokana na mwenendo wa wachezaji mazoezini.

Jana Stars ilichapwa bao 1-0 na Lesotho katika mchezo ambao Stars ilihitaji ushindi ili iweze kufuzu kwa fainali za AFCON 2019

Amunike amesema baadhi ya wachezaji hawako katika viwango bora kama wanavyodhani mashabiki.

“Tumefanya mazoezi Afrika Kusini kwa siku 10. Nimepata muda wa kuwatathmini wachezaji wote. Lakini siwezi kutoa maelezo ya ndani zaidi kuhusu wachezaji,” amesema

“Nawapanga wale waliotayari kujitoa kwa ajili ya timu. Bahati mbaya wengine hawako katika ubora wao.

“Sina nia ya kumkosoa mchezaji yeyote. Sina tatizo na John Bocco wala Mkude, tufahamu hii ni timu ya Taifa na sio Simba”

Kocha huyo pia ameomba radhi kwa matokeo hayo ambayo hata hivyo amesema yabidi kuyakubali kwani ni sehemu ya mchezo.

Amesema Stars bado ina nafasi ya kufuzu hivyo watajipanga kuhakikisha wanatumia nafasi hiyo kwenye mchezo dhidi ya Uganda utakaopigwa mwakani

TANZANI 0-1 LESOTHO FULL TIME

Stars imeshindwa kutamba huko Lesotho baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa wenyeji, Lesotho.

Ulikuwa ni mchezo ambao Stars ilihitaji kushinda ili kujihakikishia nafasi ya kutinga fainali za AFCON 2019 zitakazofanyika nchini Cameroon.

Matokeo hayo sasa yanaifanya Stars kulazimika kushinda mchezo wa mwisho dhidi ya Uganda utakaopigwa March 2019 huku ikiomba Lesotho isipate ushindi kwenye mchezo wao wa mwisho dhidi ya Cape Verde ambao watakuwa ugenini.

Lesotho ilitawala mchezo huo kwa muda mwingi huku ikikosa nafasi nyingi kabla ya kufunga kupitia mpira wa kona.

Tanzania iliyocheza kwa kujihami zaidi, ilikosa nafasi kadhaa kupitia mipira miwili ya adhabu iliyopigwa na Aggrey Morris na nafasi nyingine mbili zikikoswa na Shabani Iddi Chilunda.

Lesotho imepanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi L baada ya kufikisha alama tano sawa na Tanzania.

Licha ya Tanzania kuwa na uwiano mzuri wa mabao, Lesotho imenufaika na sheria ya matokeo ya jumla baina ya timu hizo mbili.

Lesotho imevuna alama nne dhidi ya Tanzania iliyopata alama moja kutoka kwao.

Michezo ya raundi ya sita ndio itaamua ni timu ipi inaungana na Uganda kwenda Cameroon huku Lesotho ikiwa mbele ya Tanzania na Cape Verde yenye alama nne