BOCCO: Aahidi Kurekebisha Makosa

Nahodha wa kikosi cha Simba John Bocco amesema wanatambua walikosa ufanisi kwenye mchezo wa ligi jana dhidi ya Lipuli Fc na kulazimishwa suluhu ya bila kufungana.

Bocco ameahidi kurekebisha makosa na amesema anaamini watafanya vizuri kwenye mchezo ujao wa ligi ya mabingwa dhidi ya Mbabane Swallows.

“Haikuwa matarajio yetu kwa matokeo tuliyoyapata, tulijitahidi kutengeneza mashambulizi lakini haikuwa bahati yetu. Tunaangalia kipi tulichokosea, tunaenda kujirekebisha ili tufanye vizuri kwa mchezo unaokuja,” amesema

Bocco amekuwa sehemu kubwa ya mjadala miongoni mwa mashabiki wa Simba tangu jana baada ya kukosa nafasi nyingi za wazi kwenye mchezo dhidi ya Lipuli Fc

Kikosi cha Simba kinatarajiwa kuendelea na mazoezi kesho kujiandaa na mchezo wa ligi ya mabingwa utakaopigwa kwenye uwanja wa Taifa Jumatano, Novemba 28 2018.

SIMBA: Mbabane Swallows wametuponza vs Lipuli

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema mawazo ya mchezo wa ligi ya mabingwa kwa wachezaji wake, yamechangia wasifanye vizuri kwenye mchezo wa jana dhidi ya Lipuli fc.

Jana Simba ililazimishwa suluhu ya bila kifungana na Lipuli Fc kwenye mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara uliopigwa uwanja wa Taifa.

Aussems amesema wachezaji wake walitekwa na mawazo ya mchezo wa ligi ya mabingwa utakaopigwa Jumatano ijayo dhidi ya Mbabane Swallows

“Tulipoteza umakini leo, nadhani wachezaji wangu walitekwa zaidi na fikra za mchezo wa ligi ya mabingwa,” amesema Aussems

Aussems anaamini matokeo ya jana hayataathiri morali ya kikosi chake kuelekea mchezo huo muhimu utakaopigwa Jumatano ijayo kwenye uwanja wa Taifa

Simba 0-0 Lipuli FC:

Mabingwa watetezi, ligi kuu ya Tanzania Bara, Simba wamelazimishwa suluhu ya bila ya kufungana na timu ya Lipuli FC kwenye mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Kocha wa Lipuli Fc Selemani Matola ameendeleza ubabe dhidi ya timun yake ya zamani Simba huo ukiwa mchezo wa tatu timu hizo zinatoka sare

Timu zote zilishambuliana kwa zamu lakini washambuliaji walikosa nafasi kadhaa za wazi kutokana na kukosa umakini langoni

Kwa matokeo hayo Simba imefikisha alama 27 ikisalia nafasi ya tatu alama mbili nyuma ya Yanga inayoshika nafasi ya pili

SIMBA : Kocha kuwaandalia Dozi Lipuli FC

Mkufunzi wa klabu ya Simba Patrick Aussems, amesema kikosi chake kimejiandaa vyema na kina matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo dhidi ya lipuli Fc utakaopigwa dimba la Taifa kesho Ijumaa.

Mchezo huo ni mwendelezo wa Ligi Kuu iliyokuwa imesimama kwa muda kupisha Kalenda ya Fifa ya mechi za kimataifa.

Kocha huyo raia wa Ubelgiji kikosi chake kwa mara ya kwanza msimu huu kitamkosa beki mahiri Shomari kapombe aliyeumia akiwa na timu ya Taifa nchini Afrika Kusini.

“Tumejiandaa vizuri, tulikuwa na muda mrefu wa kufanya maandalizi kwa wachezaji ambao hawakuwapo kwenye timu za taifa, naamini bado tutaendeleza makali yetu,” amesema

Mbelgiji huyo amesema anafahamu mashabiki wa timu yake wanataka mwendelezo wa ushindi na ndicho alichokuwa akikifanyia kazi.

“Tutaingia uwanjani kwa lengo la ushindi na nafurahi kuona wachezaji wangu wanahamasa na hata wale waliokuwapo kwenye timu ya taifa nao wanauangalia mchezo huu kwa umakini,” alisema.

Mchezo huo wa kesho awali ulikuwa ufanyike juzi lakini bodi ya ligi iliusogeza mbele ili kuwapa nafasi wachezaji wa Simba waliokuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa kuungana nao na kupata muda kidogo wa kupumzika.

Simba ilikuwa na wachezaji 10 kwenye timu za Taifa za Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi

Simba vs Lipuli Fc wasogezwa Mbele

Mchezo wetu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Lipuli ambao ulikuwa umepangwa kuchezwa kesho Jumatano 21/11/2018 umesogezwa mbele na sasa utachezwa siku ya Ijumaa 23/11/2018.

Mabadiliko hayo yamefanywa ili kuwapa nafasi wachezaji wetu waliokuwa kwenye timu zao za Taifa kujiunga na kikosi chetu ili kuwa sehemu ya wachezaji ambao watacheza mchezo huo.

Majeraha Ya Kapombe yamchanganya Aussems

Kiraka wa kimataifa na beki tegemeo wa Simba, Shomary Kapombe ameendelea na mkosi wa kuumia akiwa na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ baada ya kupata majeraha yakayomweka nje ya uwanja wa muda mrefu.

Kuumia kwa Shomary, kumemtibua Kocha Mkuu wa Simba na mabosi wa klabu hiyo hasa ikizingatiwa kuwa Wekundu wa Msimbazi wanakabiliwa na mechi ngumu kwa sasa, hivyo kuilazimisha Simba isake mbadala yake bila matarajio.

Kocha Aussems alisema kuumia kwa Kapombe ni pigo kwa kikosi chake na anawasiliana na viongozi kuona wanafanya nini katika dirisha dogo ili kuziba nafasi yake, ingawa anakiri mbadala wake hatamtumia mechi za CAF.

Beki huyo wa pembeni anayemudu beki ya kati na kiungo, aliumia pia mwaka jana akiwa na Stars katika michuano ya Cosafa na majeraha yake yalimweka nje ya uwanja kwa muda mrefu wakati huo akitua Msimbazi kutoka Azam FC.

Majeraha ya awali yalimfanya Kapombe alijigharamie kujitibu mwenyewe Afrika Kusini na hata sasa akiumia akiwa Lesotho kumembakisha Afrika Kusini na taarifa zinasema atakuwa nje kwa muda wa miezi miwili kutibu jeraha la kifundo cha mguu.

Hata hivyo, kwa sasa Simba imebeba jukumu la kumtibu mchezaji huyo tegemeo kwenye kikosi cha kwanza cha Mbelgiji, Patrick Aussems, ili kuhakikisha anarudi uwanjani haraka.

Jeraha hilo limewatia hofu viongozi wa Simba ambao wanajiandaa na mechi ya kwanza ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland kati ya Novemba 27 na 29 itakayochezwa jijini Dar es Salaam.

Aussems sasa atalazimika kuwatumia wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho ambapo nafasi ya Kapombe ndani ya Simba anayeweza kumudu kuicheza ni Erasto Nyoni kwani Nicholous Gyan hata kama anaweza ila jina lake halijapelekwa CAF kwa ajili ya michuano hiyo.

Kwenye michuano ya ligi, Aussems huenda akasajili beki mpya atakayeendana na kasi ya Kapombe ili pengo lisiwepo hata kama atalazimika kuendelea kumtumia Nyoni basi nafasi ya beki, lakini lazima asajili kama atahitaji kuongeza nguvu ingawa yupo Juuko Murshid na Pascal Wawa.

Tetesi zilizopo ni kwamba beki wa Prisons, Salum Kimenya yupo mawindoni ingawa imeleezwa kwamba hata wakimnasa beki huyo basi itakuwa ni kwa ajili ya ligi na sio michuano ya kimataifa.

Kocha mchambuzi wa soka, Dk Mshindo Msolla alifafanua hilo, “Kimenya ni mzuri lakini kwa Simba hii bado sana, hawezi kuvaa viatu vya Kapombe hata siku moja, ni mzuri kwa timu nyingine kama wanatafuta mrithi wa Kapombe kwa kipindi hiki basi waende nje ya nchi kwa hapa Tanzania hakuna zaidi ya Erasto Nyoni ambaye pia hamudu vyema.

“Kapombe atabaki kuwa Kapombe kwenye ligi hii, kocha akimtoa Nyoni kucheza pale kati basi asajili beki mwingine wa katikati na si vinginevyo,” alisema Msolla Kauli hiyo iliungwa na Joseph Kanakamfumu kwamba Kimenya si mchezaji wa kucheza Simba hii yenye kusaka mafanikio makubwa na imepiga hatua ndefu.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salum Abdallah ‘Try Again’ alielezea hali ya Kapombe huko Afrika Kusini kwamba;

“Anaendelea vizuri na atakuwa nje kwa miezi miwili, ni pigo kwetu na sasa tunamshughulikia ili apone haraka na kurejea kwenye majukumu yake, mapendekezo yatakayoletwa na kocha kuhusu nafasi yake yatashughulikiwa haraka”.

Mwanaspoti

Simba Sc yaiwinda Lipuli Fc

Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba wameendelea kujifua kwenye uwanja wa Boko Veterans kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Lipuli Fc.

Mchezo huo ambao awali ulipangwa kufanyika kesho, umesogezwa mbele na sasa utapigwa Ijumaa Novemba 23 kwenye uwanja wa Taifa.

Baada ya mchezo huo Simba itaendelea na maandalizi ya mchezo wa ligi ya mabingwa hatua ya awali dhidi ya Mbabane Swallows unaotarajiwa kupigwa Jumatano ya Novemba 28.

Wachezaji waliokuwa kwenye timu za Taifa wanatarajiwa kuanza kuwasili kikosini leo kuungana na wenzao ambao wamekuwa wakiendelea na mazoezi chini ya kocha Patrick Aussems

SALAMBA kufanya majalibio Ubelgiji

Mshambuliaji wa Simba, Adam Salamba, yupo mbioni kutimkia kwenye Klabu ya Royal Sporting Club Anderlecht inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji.

Mshambuliaji huyo mwenye mabao mawili katika ligi ya msimu huu, aliyejiunga Simba akitokea Lipuli msimu huu, amepata nafasi hiyo kutoka kwa wakala wa beki wa Rayon Sport, Abdul Rwatubyaye anayeishi nchini humo.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Simba, zinasema mchezaji huyo anatarajia kuondoka nchini Desemba, mwaka huu kwa ajili ya kufanya majaribio ya wiki moja kwenye timu hiyo inayokamata nafasi ya nne, mbele ya vinara wa ligi hiyo, KRC Genk anayoichezea Mbwana Samatta.

“Salamba anaweza kuondoka mwezi ujao kuelekea Ubelgiji kwenda Anderlecht kwa ajili ya kufanya majaribio ya wiki moja, kuna wakala wa huko ndiyo anafanya hiyo mipango ya kumpeleka baada ya kuvutiwa na uwezo wake kwani ameanza kumfuatilia tangu akiwa na Lipuli.

“Mipango ndiyo ipo kwenye mchakato wa kuweza kuona mambo yanakwenda vipi ila huyo wakala ndiye anajua kila jambo na mambo ya safari ingawa inafahamika kama atakaa huko kwa wiki moja katika majaribio yake,” alisema mtoa taarifa.

Alipoulizwa Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi, akasema: “Bado sijapata taarifa za mchezaji huyo, hayo masuala ya timu yote yanajadiliwa kwanza na C.E.O ambaye ni (Crescentius) Magori pamoja na kocha kabla ya baadaye bodi kukutana na kujadiliana.”

Magori alipotafutwa jana, simu yake ya mkononi haikupokelewa.

Championi

Simba kuharakisha USAJILI wa Beki Wa Kulia

Kuumia kwa Shomari Kapombe kumewafanya mabosi wa Kamati ya usajili ya klabu ya Simba kuharakisha usajili wa mbadala wake imefahamika.

Kapombe alipata majeraha makubwa akiwa kwenye kambi ya timu ya Taifa nchini Afrika Kusini na upo uwezekano akawa nje kwa muda mrefu.

Msimu uliopita Nicolas Gyan alitumika kwenye nafasi hiyo kwa nyakati tofauti, hata hivyo ameshindwa kumshawishi kocha Patrick Aussems.

Gyan hajajumuishwa katika kikosi cha Simba kitakachoshiriki michuano ya ligi ya mabingwa inayoanza mwishoni mwa mwezi huu.

Katika mchezo wa kirafiki kati ya Simba dhidi ya Nyasa Big Bullets uliopigwa Ijumaa iliyopita, Aussems alimtumia Yusufu Mlipili kama beki wa kulia.

Hata hivyo Mlipili alishindwa kuimudu nafasi hiyo.

Wakati Simba ikiendelea na mchakato wa kusajili mlinzi wa kulia, huenda kiraka Erasto Nyoni akarejeshwa kwenye nafasi hiyo.

Nyoni ana uwezo wa kucheza nafasi zote za ulinzi na kiungo.

Simba inahusishwa na beki wa Tanzania Prisons Salum Kimenya ambaye amekiri kuwa katika mazungumzo na uongozi wa Simba