Simba sc Kuwatoa kimasomaso Watanzania Klabu Bingwa

Benchi la ufundi la Simba akili yote kwa sasa limeielekeza Mbabane Swallows kwenye mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mpango mkakati utakamilika mara baada ya wachezaji waliopo na timu zao za taifa kurejea kikosini.

Kalenda ya michuano ya Kimataifa imemalizika jana ambapo wachezaji waliokuwa na majukumu ya timu za Taifa wanatarajiwa kuanza kurejea kikosini kuanzia kesho.

Kocha wa Simba Patrick Aussems amesema zimebaki siku chache kabla ya mchezo huo, hivyo tayari ameanza program za kuwakabili wapinzani wao hao.

Aussems, amesema anaifuatilia Mbabane kujua uwezo na mapungufu yao.

“Kila kitu kinaenda sawa, tunaendelea na mazoezi kwa wachezaji tulionao kikosini huku tukiwasubiri waliopo kwenye timu za Taifa,” Aussems amenukuliwa na gazeti la Nipashe

Amesema mikakati yake na mbinu kamili kwa wachezaji wake zitakamilika pindi wachezaji wake waliopo timu za Taifa watakaporejea.

“Wakirejea tunaendelea na maandalizi yetu, kwa sasa naendelea na wachezaji tulionao, nashukuru kila kitu kinaenda sawa,” alisema Aussems.

Mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika umepangwa kuchezwa kati ya Novemba 27 na 28 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana Desemba 4-5, mwaka huu nchini Swaziland.

Timu itakayoibuka mshindi wa jumla itaingia kwenye hatua ya kwanza ya michuano hiyo kusaka nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika kwa ngazi ya klabu.

Timu Zinazotaka Wachezaji wa SIMBA Zapewa Mashari

Simba haina shida wachezaji kuwatoa kwa mkopo wale ambao hawapati nafasi kwenye kikosi chao lakini timu ambayo inahitaji huduma ya wachezaji hao basi wanapaswa kujipanga kupangua masharti mawili magumu ukiachana na yale madogo madogo.

Sharti la kwanza ambalo limewekwa ni kuhakikisha huko watakakokwenda wanacheza kikosi cha kwanza na sio kukaa benchi ama jukwaani.

Sharti la pili ni kuhakikisha wanawapa huduma zote kwa jinsi watakavyokubaliana ikiwemo, mshahara, posho kuishi maisha mazuri yasiyokuwa ya mawazo hasa suala la kukosa mshahara kwa zaidi ya mwezi.

Kwasasa viongozi wa Simba wanasubiri ripoti ya kocha mkuu Patrick Aussems ili kuona ni wachezaji gani amependekeza waondolewe kwa mkopo na kama atahitaji kuongeza wachezaji na kwa nafasi gani.

Kuna taarifa kwmaba nyota watatu wa Simba Mohamed Rashid ‘Mo Rashid’, Marcel Kaheza na kipa Mohamed Said ‘Nduda’ watatolewa kwa mkopo katika timu ambazo zitahitaji huduma zao na kukubali masharti hayo huku kipa Emmanuel Mseja yeye anasubiri barua pekee ingawa yupo kwenye mazungumzo ya chini chini na Caostal Union ya Tanga.

Aliyekuwa Kaimu Rais wa Simba ambaye sasa ni mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ ambaye ameombwa kuendelea na majukumu yake hadi hapo baadaye Bodi itakapoanza majukumu yake rasmi alisema wamepokea maombi ya timu nyingi zikomba huduma za wachezaji wao.

Try Again amesema kuwa wana maombi mengi lakini hadi sasa hakuna maombi yaliyofanyiwa kazi kwani wanasubiri kocha wao atoe mapendekezo kupitia ripoti yao ila tayari wameweka masharti yao ambapo atakayevuka hayo atapewa mchezaji kama itatokea amependekezwa na kocha.

Simba imepokea maombi mengi ya mshambuliaji wao Mo Rashid ambapo timu tano zimetuma barua ambazo ni Singida United, Lipuli FC, Prisons, Coastal Union na KMC huku Kaheza anasakwa na timu mbili KMC na Alliance upande wa Nduda bado hakuna timu iliyojitokeza hadi sasa.

Try Again alisema, “Mo Rashid anatafutwa na timu nyingi sana na huenda tukaendelea kupokea maombi, ila hatuwezi kuamua lolote hadi hapo tutakapopata ripoti kutoka kwa kocha mkuu maana kila kitu tumemwachia akifanye yeye.

“Pia hizi timu zinazohitaji wachezaji wetu kiukweli wakubaliane na baadhi ya haya mammbo, apate nafasi ya kucheza kwani hiyo ndiyo maana halisi ya kupelekwa kwa mkopo kwani mchezaji akitolewa kwa mkopo matarajio ni kumrejesha tena kikosi kwetu wakati yupo kwenye kiwango kizuri zaidi.

“Timu hizo zitambue kwamba mchezaji tutakayewapa basi apate huduma zote, asiwe na njaa kabisa ya mshahara na mambo mengine ambayo yanaweza kuchangia kiwango chake kishuke, wamlee kama tunavyowalea sisi wachezaji wetu, vinginevyo itakuwa vigumu kuwapata wachezaji hao kutoka kwetu,” alisema Try Again.

Try Again alifafanua pia kuwa masuala yote ya ufundi yameachwa kwa Aussems ikiwemo kocha msaidizi na mapendekezo mengine ya usajili na mashindano yote ya ndani na nje ya nchi kwamba mahitaji atakayohitaji viongozi watakuwa watekelezaji.

“Kila kitu kipo chini ya kocha mkuu, hatutaki kumwingilia, hivyo akisema anahitaji kocha msaidizi na akimpendekeza basi sisi tutafanya utekelezaji ikiwemo mambo mengine, hivyo kwasasa tunamsubiri yeye tu,” alisema Try Again.

Aussems yeye alisema ataandaa majina ya wachezaji watano hadi sita atakaowasajili ila kati ya hao mchezaji mmoja tu ndiye atapendekeza asajiliwe wakati huu wa dirisha dogo na kufafanua kwamba, “Kati ya hao napendekeza straika mmoja tu mwenye uwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi kwa wenzake,”.

Mpaka sasa kuna majina ya wachezaji wanaotajwa kwenye usajili wa Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu Bara akiwemo Francis Kahata kutoka Gor Mahia ingawa ana mkataba na timu yake, Epharaim Guikan na Philomeno Otieno wote wa Gor Mahia pamoja na Sadam Juma wa KCCA ya Uganda.

Mwanaspoti

Simba 0-0 Nyasa Big Bullets : Full Time

Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba wamelazimishwa suluhu ya bila kufungana na mabingwa wa Malawi, Nyasa Big Bullets katika mchezo wa kirafiki uliopigwa uwanja wa Taifa Ijumaa jioni.

Mchezo huo uliokuwa maalum kuziandaa timu hizo kwa ajili ya michezo ya awali ya ligi ya mabingwa inayopigwa mwishoni mwa mwezi huu, ulishuhudia kosakosa za hapa na pale kutoka kila upande huku Simba ikitawala kwa muda mwingi.

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems aliutumia mchezo huo kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji ambao hawamo kwenye kikosi cha kwanza baada ya idadi kubwa ya wachezaji wa Simba (12) kuitwa kwenye timu za Taifa.

Simba inatarajiwa kucheza mchezo mwingine wa kirafiki kabla ya kuivaa Mbabane Swallows mwishoni mwa mwezi huu.

Usajili: Simba sc Yakanusha Kuhusu Niyonzima kusajiliwa AZAM

Afisa Habari wa Simba Haji Manara amemshukia mwandishi na mchambuzi wa soka nchini Shaffih Dauda baada ya kuweka taarifa kwenye ukurasa wake wa matandao kijamii kuwa kiungo Haruna Niyonzima yuko mbioni kusajiliwa na Azam Fc.

Manara ameshangazwa na taarifa hizo alizodai ni za kiuchonganishi.

“Tunajua Shaffih unatumika na Maadui wa Simba kutaka kutuvuruga kusudi ili kubalance na sisi tuonekane tuna mgogoro na wachezaji wetu,” ameandika Manara.

“Haruna Niyonzima yupo kambini na leo atacheza ikimpendeza kocha dhidhi ya Bata Bullets.

“Hivi mtu muungwana kabisa unawezaje kuandika uongo na kufikia kumvalisha jezi ya timu nyingine mchezaji aliye na mkataba na klabu yetu kama si uchochezi na uhuni wa kishamba?,” amehojia Manara

OKWI: Anavyomuumiza kichwa Kocha wa Mbabane Swallows

Licha ya mbwembwe zake na uzoefu wake, Kocha wa Mbabane Swallows ya Swaziland, Thabo ‘Koki’ Vilakati akisikia jina la Mohammed Dewji ‘Mo’ na Emmanuel Okwi wa Simba anashtuka paap!

Kocha huyo mzawa anayesi­fika kwa staili ya uchezaji ya 4-3-2-1 na uwezo mkubwa wa kuhamasisha, timu yake itacheza na Simba Novemba 27 jijini Dar es Salaam katika mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mbabane ambayo ni timu ya zamani ya Papy Tshishimbi wa Yanga na Asante Kwasi wa Simba, iliwaondoa Azam kwenye Kombe la Shirikisho msimu uliopita. Kama Simba ikiwaondoa Mbabane itaingia raundi ya kwanza kucheza na mshindi kati ya Nkana ya Zam­bia na UD Songo ya Msumbiji.

Thabo ambaye amekimbiwa na wachezaji kadhaa nyota waliokwenda kusaka masilahi nje, amesema kwamba anajua mambo kadhaa kuhu­siana na Simba lakini tishio kubwa akataja ni ufundi wa Okwi na uwekezaji wa Mo.

Anasema kuwa anaelewa kuna ma­badiliko makubwa Simba am­bayo yametokana na uwekezaji wa Mo ambaye ana shauku ya mabadiliko na amefuatilia na kugundua anataka kufanya sapraizi msimu huu.

Kocha huyo ambaye yupo klabuni hapo tangu msimu wa 2016, ameweka wazi kwamba mchezaji anayemuumiza sana kichwa ni Okwi ambaye ame­kuwa kwenye fomu muda mre­fu huku akimtaja kama mche­zaji asiyekubali kushindwa.

Lakini akadadisi kujua nini kimemtokea au wapi alipo win­ga machachari ndani ya Simba, Shiza Kichuya kama ilivyokuwa msimu uliopita.

“Tunawafahamu. Tunajua nini wanafanya na kila kitu kinachoendelea kwao tumekuwa tukikifahamu,” Koki amenukuliwa na gazeti la Championi

“Tunafahamu kuwa Simba ni timu kubwa Afrika, na inatupa hofu zaidi sasa kwa kuwa ina mwekezaji bilionea Afrika, Mohammed Dewji, huyu amewekeza fedha nyingi na ni mtu maarufu sana.

“Tunafahamu anataka ma­fanikio makubwa kwenye timu yake, hivyo watakuja kamili sana, lakini pia Simba wanaye mmoja kati ya wachezaji mahiri Afrika Mashariki, Emmanuel Okwi, huyu kila mtu anaujua uwezo wake, hivyo lazima tuwe makini tunapocheza nao.

“Ila jambo moja ambalo si­jaelewa ni kwamba walikuwa na winga wao wa msimu uliopita (Shiza Kichuya) huyu alikuwa hatari sana lakini sasa haonekani, hivi yupo?” alisema kocha huyo mwenye mbwembwe nyingi.

Mpaka sasa kwenye ligi ya ndani, Mbabane wamecheza mechi nane na wako kwenye nafasi ya nne na pointi zao 16. Wameshapoteza mechi mbili, wakati msimu uliopita walitwaa ubingwa bila kupoteza mchezo hata mmoja zaidi ya sare tisa kwenye michezo 26 kwani ligi yao ina timu 14.

Kwa mujibu wa Mwenyeki­ti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Swedy Mkwabi wana­choangalia ni kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mab­ingwa tu na si vinginevyo na tayari wameanza kusaka video za Mbabane.

Simba Sc: Kocha Afunguka Kuelekea Mechi Dhidi ya Big Bullet

Licha ya kuwakosa wachezaji wake 12 wa kikosi cha kwanza, kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wamejiandaa kikamilifu kuikabili Nyasa Big Bullets kwenye mchezo wa kimtaifa wa kirafiki.

Kesho Ijumaa saa 12 jioni Simba itashuka kwenye uwanja wa Taifa kuchuana na mabingwa hao wa Malawi.

Aussems amesema atautumia mchezo huo kuwapa nafasi wachezaji wake ambao wamekuwa hawatumiki mara kwa mara kutokana na ushindani wa namba uliopo kwenye kikosi chake.

“Msimu huu tunakabiliwa na michuano mingi. Tunawahitaji wachezaji wetu wote wawe katika kiwango bora na tayari kuipa matokeo timu wanapohitajika,” amesema Aussems

“Mchezo wa kesho tutawakosa wachezaji wanaozitumikia timu za Taifa lakini itakuwa ni nafasi nzuri kwa wachezaji waliobaki kuonyesha uwezo wao.”

“Pia mchezo huo utawapa uzoefu wa michezo ya Kimataifa kwani tunacheza na timu ambayo ni bingwa wa nchi kama sisi”

Simba vs Big Bullet Haji Manara Aweka wazi Viingilio

Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba keshokutwa Ijumaa, Novemba 16 2018 watashuka kwenye uwanja wa Taifa kuwakabili mabingwa wenzao Nyasa Big bullets kutoka nchini Malawi katika mchezo wa kirafiki.

Mchezo huo wa Kimataifa wa kirafiki unatarajiwa kuanza saa 12 jioni.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Afisa Habari wa Simba Haji Manara amesema watautumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Mbabane Swallows utakaopigwa Novemba 27.

Manara ametaja viingilio vya mchezo huo kuwa ni;
VIP A : 10,000/-
VIP B na C : 7,000/-
Mzunguuko : 3,000/-

Manara amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa keshokutwa ili kuiunga mkono timu yao.

Uongozi SIMBA SC Kuzungumza na waandishi Wa Habari Jumatano Nov 14

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kesho tarehe 14/11/2017 Siku ya Jumatano Saa Sita kamili mchana ,Mabingwa wa Soka nchini Simba SC itazungumza na Wanahabari kwenye Makao Makuu ya klabu yaliyopo Mtaa wa Msimbazi jijini Dar es salaam

Mkutano huo muhimu unatarajiwa kurushwa live kama kawaida na Channel maarufu ya Azam kupitia Azam sports two pamoja na kurasa za Mitandao ya kijamii ya klabu pamoja na ya Msemaji wa klabu.

IMETOLEWA NA
Haji S Manara
Mkuu wa Habari na Mawasiliano
Simba SC

Simba sc Kumsajili kiungo huyu Rayon Sport

#TetesiZaUsajili Imeripotiwa kuwa klabu ya Simba Sc tayari imeanza mazungumzo na mshambuliaji wa Rayon Sports Bonfils Caleb Bimenyimana (20) ili kumsajili katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.
Caleb ni moja ya washambuliaji hatari katika kikosi hicho chenye maskani yake nchini Rwanda ambapo alishwahi kuifunga Yanga Sc bao safi katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika msimu uliopita.
#sokaonlineUpdates

SIMBA : kujipima na Timu ya MALAWI

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba Ijumaa, Novemba 16 2018 watashuka kwenye uwanja wa Taifa kuikabili Big Bullets kutoka Malawi katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki.

Mchezo huo utapigwa kuanzia saa 12 jioni na utarushwa mbashara na Azam Sport 2.

Mchezo huo uliombwa na kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems ili kukipima kikosi chake ambacho mwishoni mwa mwezi huu kitacheza mchezo wa kwanza wa ligi ya mabingwa dhidi ya Mbabane Swallows.

Hata hivyo katika mchezo huo Simba itawakosa wachezaji wake 12 walioitwa kwenye vikosi vya timu za Taifa