SIMBA SC: Kuwatoa watatu kwa Mkopo

Kuelekea dirisha dogo la usajili ambalo litafunguliwa wiki ijayo Novemba 15 mastaa watatu wa Simba wamekubali yaishe na muda wowote kuanzia sasa watatolewa kwa mkopo kwenda kuzitumikia klabu nyingine.

Nyota hao ni Mohammed Rashid, ambaye alisajiliwa na Simba msimu huu akitokea klabu ya Tanzania Prison ambapo msimu uliopita alimaliza ligi akiwa amefungia mabao kumi.

Tangu ametua Simba Rashid hajacheza hata mechi moja ya ligi ingawa alianza vizuri kwa kuonesha kiwango katika mashindano ya SportPesa na Kagame Cup, ambapo alifunga bao katika hatua ya makundi.

Marcel Kaheza, ambaye alisajiliwa na Simba mwanzo wa msimu akitokea Majimaji huku alikuwa nyota baada ya kumaliza msimu akiifungia timu yake mabao 12 licha ya kwamba timu hiyo ilishuka daraja.

Said Mohammed ‘Nduda’ naye ni miongoni mwa nyota ambao watatolewa kwa mkopo na kinachosubiliwa ni muda kufika ili kulitimiza hilo kwani, msimu mmoja na nusu aliokuwa katika kikosi cha Simba amecheza mechi moja tu dhidi ya Kagera Sugar msimu uliopita.

Rashid alisema tayari nimekubaliana na kocha kwamba nikatafute nafasi ya kucheza kutokana na ambao nacheza nao hapa katika nafasi moja watanipa muda mdogo wa kucheza.

“Nimekubaliana naye na ameniambia kama nitafanya vizuri huko ambapo nitakwenda nafasi ya kurudi hapa ipo wazi,” alisema Rashid ambaye anawindwa na Alliance, Mwadui, Prison na KMC ambao wanapewa nafasi kubwa ya kumnasa nyota huyo.

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema katika kikosi chake nyota wote wanauwezo ila wale ambao hawajapata nafasi ya kutumika ni kutokana na changamoto ya kuwania nafasi ya kucheza.

“Changamoto ya kuwania nafasi ya kucheza ni kubwa mno katika timu yangu na haswa wale wachezaji ambao, wanapata nafasi ya kucheza kama wapo tayari nitawaruhusu lakini kama watafanya vizuri nafasi ya kurudi ipo wazi,” alisema Aussems.

Mwanaspoti

Aussems Ataka Michezo ya Kirafiki SIMBA SC

Ligi Kuu ya Tanzania Bara itasimama kwa wiki mbili baada ya michezo ya leo kupisha michezo ya Kimataifa iliyo katika kalenda za CAF na FIFA.

Kwa upande wa Simba, Yanga na Azam Fc ligi hiyo ilisimama mapema hadi baada ya michezo ya Kimataifa kutokana na kuwa na wachezaji wengi kwenye kikosi cha timu ya Taifa.

Simba ndio iliyoathirika zaidi kwani imetoa wachezaji 12 kwenye timu za Taifa za wakubwa na U23.

Hata hivyo kocha Mkuu wa timu hiyo Patrick Aussems ameendelea kuwafua vijana wake kuwaandaa na michezo ya baada ya michuano ya Kimataifa kupita.

Aussems ameutaka uongozi wa klabu ya Simba umtafutie michezo miwili ya kirafiki ili kuwaweka vijana wake katika hali ya ushindani.

Aussems ambaye kikosi chake kinakabiliwa na mchezo wa ligi ya mabingwa mwishoni mwa mwezi huu, ametaka atafutiwe mchezo wa kirafiki na timu ya hapa nyumbani na mwingine dhidi ya timu kutoka nje ya nchi.

KADUGUDA: Ataka SIMBA SC iwe klabu kubwa Afrika

Katibu Mkuu wa zamani wa Klabu ya Simba ambaye kwa sasa amechaguliwa kuwa mjumbe wa bodi ya klabu hiyo, Mwina Kaduguda, amesema baada ya kupita uchaguzi sasa wana kazi ya kuitoa Simba kutoka kuwa timu kongwe na kuwa timu kubwa Afrika.

Kaduguda, ambaye ni miongoni mwa wajumbe watano waliochaguliwa kwenye uchaguzi uliofanyika Dar es Salaam Jumapili iliyopita, alisema Wanasimba wasijidanganye kuwa Simba ni timu kubwa kwa kuwa bado haijafikia kuwa timu kubwa Afrika.

“Simba ni miongoni mwa timu kongwe Afrika na si timu kubwa, haijafikia sifa za kuitwa timu kubwa, sisi viongozi tuliochaguliwa pamoja na wenzetu upande wa pili ndio tuna kazi sasa ya kuitoa Simba hapa ilipo kuelekea kuwa timu kubwa Afrika,” alisema Kaduguda.

Alisema anawashukuru Wanasimba kwa kumrejesha tena kwenye uongozi wa klabu hiyo.

“Wakati naondoka madarakani…, tuliacha Simba ikiwa na eneo la ujenzi wa uwanja Bunju, wazo la kuwa na kiwanja lilitolewa na Hassan Hasanoo kipindi cha uongozi wangu na Mwenyekiti Mzee [Hassan] Dalali, sisi tulilifanyia kazi wazo la kiwanja tukakitafuta,” alisema Kaduguda na kuongeza:

“Tuliacha la uwanja kwa uongozi uliofuata wa Aden Rage ambaye yeye sasa alianza kuulipia fedha ili sasa iwe mali ya klabu, badala yake na yeye akauachia uongozi uliofuata ambao ulikaimiwa na Salim Try Again ambaye wameanza kuujenga, uongozi ni kuachiana kijiti…, sasa tunaenda kuukamilisha na kuanza safari ya kuifanya Simba timu kubwa Afrika,” alisema Kaduguda.

Alisema atautumia uzoefu wake ndani ya Simba na kwa kushirikiana na viongozi wenzake kuipeleka Simba mbele zaidi na kuwa timu ya ushindani kwenye michuano ya Afrika.

Kikosi Cha SIMBA Klabu Bingwa Africa

Klabu ya @simbasctanzania imetuma majina ya Wachezaji 25 wa kunako shirikisho la mpira wa Miguu Afrika CAF kwa ajili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika (Caf Champions League)
Majina hayo ni kama ifuatavyo

Makipa (2)
1-Aishi Manula
2-Deo Munishi Dida
Mabeki (9)
3-Shomary Kapombe
4-Mohammed Hussein
5-Asante Kwasi
6-Paschal Wawa
7-Erasto Nyoni
8-Juuko Murshid
9-Yusufu Mlipili
10-Paul Bukaba
11-Salim Mbonde

Viungo (10)
12-Jonas Mkude
13-James Kotei
14-Clatous Chama
15-Hassan Dilunga
16-Mohammed Ibrahim
17-Said Ndemla
18-Haruna Niyonzima
19-Mzamiru Yassin
20-Shiza Kichuya
21-Rashid Juma

Washambuliaji (4)
22-John Bocco
23-Meddie Kagere
24-Emmanuel Okwi
25-Adam Salamba

#sokaonlineUpdates

NIYONZIMA: Atoswa Timu Ya Taifa RWANDA

Kiungo wa Simba Haruna Niyonzima hajajumuishwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Rwanda kinachojiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za AFCON 2019 dhidi ya Afrika ya Kati.

Mchezo huo utapigwa nchini Rwanda Novemba 18.

Niyonzima amekuwa kwenye mgogoro na uongozi wa Simba uliopelekea afanye migomo ya mara kwa mara na hivyo kuondolewa kwenye kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa Tanzania Bara.

Wakati Niyonzima akiondolewa kwenye kikosi hicho cha Rwanda, Meddie Kagere kinara wa mabao kwenye kikosi cha Simba ameitwa.

Idadi kubwa ya wachezaji wa Simba wameitwa kwenye timu za mataifa yao kwa ajili ya michuano ya AFCON.

Emmanuel Okwi na Juuko Murshidi wao wameitwa timu ya Taifa ya Uganda, wakati Cleotus Chama ‘CCC’ yeye ameitwa timu ya Taifa ya Zambia.

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Shiza Kichuya na John Bocco wao wameitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayotarajiwa kusafiri leo kwenda kuweka kambi nchini Afrika Kusini.

Hawa Hapa VIONGOZI WAPYA SIMBA SC

Jana baada ya Mkutano Mkuu, wanachama wa klabu ya Simba waliingia kwenye zoezi la uchaguzi kuwapata Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.

Zoezi la uchaguzi lilikwenda mpaka usiku na matokeo yake kutangazwa usiku wa kuamkia leo.

Hawa hapa washindi wa nafasi mbalimbali;

MWENYEKITI
Swedi Khamisi Mkwabi

WAJUMBE BODI YA WAKURUGENZI
1. Asha Baraka
2. Hussein Mlinga
3. Dk Zawadi Kadunda
4. Seleman Said
5. Mwina Kaduguda

Mabadiliko SIMBA yavuta wachezaji wakali Msimbazi

Wakati dirisha la usajili Tanzania Bara likitarajiwa kufunguliwa Novemba 15, mwaka huu, imebainika kwamba wachezaji mbalimbali wa kimataifa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wameomba kusajiliwa katika klabu hiyo inayonolewa na Mbelgiji Patrick Aussems.
Wachezaji hao wameomba kusajiliwa Simba kutokana na klabu hiyo kwa sasa kumwaga fedha za usajili kutokana na uwepo wa mwekezaji wake, Mohammed Dewji.
Akizungumza jana kwenye mkutano mkuu wa klabu hiyo, Kaimu Rais aliyemaliza muda wake, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema kwamba wamepokea meseji mbalimbali kutoka kwa wachezaji wa kimataifa wakiomba kusajiliwa katika klabu hiyo.
“Kuna wachezaji mbalimbali ambao wameomba kusajiliwa katika klabu yetu katika kipindi hiki. Nimekuwa nikipokea meseji za wachezaji kutoka sehemu mbalimbali za Afrika wakiomba nafasi ya kusajiliwa ndani ya timu yetu,” alisema Try Again.
Licha ya wachezaji hao kuomba kusajiliwa na Simba klabu hiyo kwa sasa ina wachezaji nane wa kimataifa. Wachezaji hao ni Emmanuel Okwi (Uganda), Claytous Chama (Zambia), Pascal Wawa (Ivory Coast), Meddie Kagere (Rwanda), Nicholaus Gyan (Ghana), Asante Kwasi (Ghana), Juuko Murshid (Uganda) na James Kotei (Ghana).
Wakati huohuo jana Simba walitangaza kutenga kiasi cha milioni 750 kwa ajili ya kufanya usajili kwa ajili ya kukiimarisha kikosi hicho.
Katika hatua nyingine, Try Again amesema kwamba klabu hiyo tayari imekamilika na wanajua watasajili wachezaji gani kwenye dirisha la usajili ambapo usajili huo utasimamiwa na mwekezaji, Mohammed Dewji ‘Mo’.
Pia klabu hiyo imesajili wachezaji 17 kwenye kikosi cha vijana cha klabu hiyo U20 pamoja na kusajili wachezaji 10 wanaocheza kwenye timu ya taifa ya wanawake kwa ajili ya Simba Queens.

SIMBA: Kumtoa kwa mkopo Marcel

Kocha wa klabu ya Simba Sc Patrick Aussems amesema tayari ametoa mapendekezo ya kumtoa kwa mkopo mchezaji wao Marcel Kaheza kwenda klabu atakayopata nafasi ya kucheza kwa kipindi cha miezi 6 tuu.

Kocha huyo amefika mbali zaidi na kusema hawezi akaruhusu nyota huyo wa zamani wa MajiMaji Fc kuuzwa kwa kuwa ana uwezo wa hali ya juu, kutokana na upana wa kikosi cha Simba Sc ndio maana hapati nafasi ya kucheza na kuonyesha ubora wake #sokaonlineUpdates

Nyota Wailili wa GorMahia Mikononi mwa Aussems

Uongozi wa Simba umeanza kuichokoza Gor Mahia ya Kenya baada ya kukabidhi majina mawili ya Philemon Otien na Ephrem Guikan kwa kocha Mbelgiji Patrick Aussems.
Aussems anataka kuimalisha kikosi chake kwa kusajili wachezaji kutoka nje wakati wa dirisha dogo litakapofunguliwa Novemba 15.
Aussems amekabidhiwa majina ya nyota hao wawili wa Gor Mahia, Mkenya Otien (26) anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji au mshambuliaji wakati Guikan anacheza katika nafasi ya ushambuliaji tangu alivyotua hapo msimu mmoja uliopita akitokea katika klabu ya AS Port Louis ya nchini Mauritius.
Guikan (24) raia wa Ivory Coast ailijiunga na Gor Mahia mwanzo wa msimu uliopita kwa maana hiyo mkataba wake umebaki mwaka mmoja na ameweza kuifungia timu yake mabao 17 msimu mzima katika mashindano yote.
Simba wanaingia katika vita ya kumuania Guikan dhidi ya timu mbili kubwa Afrika ambazo ni Free State Stars ya Afrika Kusini na Nkana Fc inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Zambia.
Wakala wa Guikan, George Bwana aliweka wazi kuwa amezungumza na uongozi wa Simba na kweli wameonesha nia ya kumtaka nyota wake huyo ambaye amebakisha mwaka mmoja wa kuitumia klabu ya Gor Mahia ambayo kesho Jumanne inacheza na Everton nchini Uingereza.
Bwana alisema aliwasiliana na kiongozi wa juu wa Simba ambaye hakutaka jina lake liwekwe wazi kuwa wanamuhitaji Guikan, lakini bado hawajafikia uamuzi ya mwisho ya kumchukua kwani bado wapo katika majadiliano.
“Kiongozi huyo wa Simba aliniambia wanamtaka mchezaji wangu Guikan, lakini anasubiri wa kufanya uamuzi wamalizana naye,” alisema.
“Kwangu sina shida nawasubiri Simba maana ni timu nzuri, lakini hapa mkononi nipo na ofa kutoka Nkana na Free State zinamtaka mchezaji wangu nimewambia wasubili kwanza nioni hili la Simba tutalimaliza vipi,” alisema Bwana.
Kocha wa Simba, Aussems awali aliweka wazi kwamba yupo na orodha ya wachezaji watano mpaka sita ambayo atawapatia kamati ya usajili ili waweze kumsajili nyota mmoja na kama wao watapenda kumuongeza mwingine mwenye uwezo halitakuwa na shida kwake.
“Nataka straika mwenye uwezo wa kufunga kama waliokuwa sasa au zaidi yao lakini awe na uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga kwa wenzake,” alisema Aussems.
Sifa hizo ambazo Aussems ameziweka hapo kwa straika ambaye anamuhitaji zinapatikana kwa Guikan na huenda Simba wakaingia miguu miwili kumalizana na straika huyo.

Crescentiua Magori: CEO Simba SC

Klabu ya Simba ambayo imeingia rasmi kwenye mfumo mpya wa uendeshaji wa kampuni, imemtangaza Crescentius Magori kuwa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa kampuni ya Simba Sports Club.

Magori ametangazwa kuwa CEO wa SSC katika Mkutano Mkuu wa klabu hiyo unaoendelea Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Posta jijini Dar es salaam.

Magori amewaahidi wanachama wa klabu ya Simba kuwa ataifanya klabu hiyo kuwa ya kisasa

Amesema ataifanya Simba kuwa klabu yenye mafanikio sio Tanzania tu, bali Afrika nzima