KICHUYA: Arejeshwa TAIFA STARS

Shirikisho la soka nchini (TFF) limeweka hadharani Kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinachotarajia kucheza mchezo wa kufuzu AFCON dhidi ya Lesotho Novemba 18,2018 Mjini Maseru,Lesotho.

Kiungo wa Simba Shiza Kichuya amerejeshwa katika kikosi hicho na kocha Emmanuel Amunike baada ya kukosa mchezo uliopita

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Jonas Mkude na John Bocco pia wameitwa.

LIGI: Ya mabingwa AFRICA kuanza mwezi huu

Mchezo wa fainali wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika kwa msimu uliopita utapigwa kesho Ijumaa kati ya Al Ahly dhidi ya Esperance.

Kufuatia mabadiliko ya kalenda ya michuano hiyo yaliyofanywa na CAF, Novemba 28 michezo ya hatua ya awali ya michuano hiyo kwa ajili ya msimu huu inaanza

Ratiba ya michezo ya awali inatarajiwa kupangwa wiki ijayo jiji la Cairo nchini Misri.

Simba, mabingwa wa soka Tanzania Bara ndio wawakilishi wa nchi kwenye michuano hiyo msimu huu.

Wanatarajiwa kuanza kampeni yao kati ya tarehe 27 na 28 mwezi huu wakisubiri kumfahamu mpinzani wao wiki ijayo.

Michezo ya marudiano kwa hatua ya awali itapigwa baada ya wiki moja

Timu zitakazofuzu hatua ya awali zitatinga raundi ya kwanza na kama zitashinda kwenye hatua hiyo zitafuzu kwa hatua ya makundi.

Kwa zile zitakazotolewa kwenye raundi ya kwanza zitahamishiwa kwenye raundi ya pili ya michuano ya kombe la Shirikisho

Kuanzia msimu huu michuano hiyo itakuwa inamalizika mwishoni mwa mwezi wa tano.

SIMBA 2- JKT TANZANIA

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba leo wametakata uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga baada ya kuilaza JKT Tanzania mabao 2-0.

Alikuwa ni mshambuliaji hatari Meddie Kagere ‘MK14’ aliyepeleka kilio kwa maafande wa JKT baada ya kuifungia Simba mabao yote mawili.

Alifunga bao la kwanza kwenye dakika ya 12 kwa shuti kali akiwa ndani ya 18 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Emmanuel Okwi.

Mpira wa adhabu uliopigwa na Okwi kwenye dakika ya 38 uligonga mwamba kabla ya kukutana na guu la Kagere kwa mara nyingine na kuiandikia Simba bao la pili.

Licha ya changamoto ya uwanja, kikosi cha Simba kilicheza kandanda safi muhimu zaidi ikiwa ni kufanikiwa kuondoka na alama zote tatu dhidi ya JKT Tanzania, moja ya timu ngumu kabisa kwenye ligi msimu huu.

Ushindi huo umeirejesha Simba kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 26.

Kagere amefikisha mabao saba sawa na Okwi wote wakiwa nyuma ya Eliudi Ambokile wa Mbeya City aliyefunga mabao nane.

Matokeo ya michezo ya leo

MLIPILI: Akanusha Kutoweka Kikosini

Beki wa Simba Yusufu Mlipili amesema hakuna ukweli wowote juu ya taarifa kwamba alikuwa ameikacha timu na kuelekea ‘kusikojulikana’.

Mlipili aliyesajiliwa na Simba kutoka Toto Africans misimu miwili iliyopita, hakuonekana kwenye kikosi cha Simba kwa siku kadhaa huku viongozi wa timu hiyo wakisema hawajui alipo.

“Nipo na nitaendelea kuwepo ondoeni hofu watu wangu ni uzushi tu mimi kutokuwepo mazoezini. Simba Nguvu moja kila hatua duaaa,” amesema

Hivi karibuni Mlipili alikiri kuwa na wakati mgumu kumshawishi kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems ameweze kumjumuisha kwenye kikosi cha kwanza.

Juuko Murshidi, Erasto Nyoni, Paul Bukaba na Paschal Wawa ndio waliocheza mechi nyingi za Simba msimu huu

OKWI: Afurahishwa na Ushirikiano Wa wachezaji SIMBA SC

Mshambuliaji kinara wa mabao katika kikosi cha Simba Emmanuel Okwi, amesema moja ya sababu inayomfanya kuwa kwenye kiwango cha juu ni ushirikiano na mapenzi anayoyapata kutoka kwa wachezaji wenzake.

Mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Uganda amesema mbali na kufuata maelekezo ya kocha na kujituma uwanjani, lakini amekuwa na wakati mzuri kwenye kikosi hicho kutokana na ushirikiano uliopo kati yake na wachezaji wenzake kikosini.

Jumapili iliyopita alickeka na nyavu mara tatu kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ambao Simba iliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0.

Aidha Okwi amesema mashabiki wa timu hiyo waendelee kusubiri furaha kutoka kwa wachezaji katika kila mchezo watakaocheza.

“Sehemu yoyote kukiwapo na umoja, mafanikio yanapatikana, nipo kwenye kiwango kizuri kwa sababu ya ushirikiano uliopo ndani ya Simba, lakini pia kufuata maelekezo ya kocha na kujituma uwanjani,” alisema Okwi.

Alisema ligi ni ngumu na kila timu imejipanga kufanya vizuri na wanachokifanya wao ni kujituma uwanjani na kuweka malengo ya kupata pointi tatu kwenye kila mchezo.

“Ushindi tunaoupata kwenye mechi zetu si rahisi kuupata, kila timu imejipanga na kinachotokea ni kujituma uwanjani na kufuata maelekezo ya kocha ili kupata ushindi,” alisema Okwi.

Okwi sasa amefikisha jumla ya mabao saba katika michezo 10 aliyoichezea Simba msimu huu huku akionekana kuwa na kasi kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Msimu uliopita, Okwi aliibuka mfungaji bora kufuatia kufikisha jumla ya mabao 20.

Simba, wiki hii itashuka tena uwanjani kuumana na JKT Tanzania kwenye mfululizo wa michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga baada ya JKT kuhamishia mechi hiyo mkoani humo.

Nipashe

ADAM SALAMBA: Aahidi kuendeleza motto wa mabao simba Sc

Mshambuliaji Adam Salamba, amesema kitendo cha kufunga kwenye michezo miwili iliyopita kimemuongezea hamu ya kuendelea kufanya vizuri zaidi msimu huu.

Salamba amesema ameongeza kujiamini na sasa anataka kutumia vema kila nafasi atakayopewa na kocha wake kuitumikia timu hiyo.

“Nafurahi kwa sababu napata nafasi ya kucheza na nimeanza kuonyesha kile ambacho Wanasimba wanakitaka kutoka kwangu…, ingawa muhimu ni ushindi kwa timu lakini pia ninapopata nafasi ya kufunga kwangu ni furaha zaidi,” alisema Salamba.

Salamba ambaye alijiunga na Simba msimu huu akitokea Lipuli ya Iringa, amefunga mara mbili mfululizo kwenye michezo iliyopita dhidi ya Alliance ya Mwanza na Ruvu Shooting.

Katika michezo hiyo, Simba ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 (dhidi ya Alliance) na baadaye 5-0 (dhidi ya Ruvu Shooting).

Kikosi hicho cha kocha Patrick Aussems, kitashuka tena dimbani wiki hii kuumana na JKT Tanzania ambao wameamishia mechi hiyo kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Simba imefikisha pointi 23 baada ya kucheza michezo 10 ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Azam fc

Simba Sc Kuivaa JKT Tanzania

Kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba Jumamosi ijayo Novemba 03 kitakuwa mkoani Tanga kupepetana na maafande wa JKT Tanzania kwenye mchezo wa ligi kuu.

Awali TFF ilitangaza kufuta michezo ya Simba, Yanga na Azam iliyokuwa ipigwe wiki ya kwanza ya mwezi Novemba ili kutoa nafasi kwa wachezaji wa timu hizo walio kwenye kikosi cha Stars kujuishwa kambini nchini Afrika Kusini.

Hata hivyo michezo hiyo itapigwa kama kawaida.

Hivi karibuni TFF iliiruhusu JKT Tanzania kutumia uwanja wa Mkwakwani kwa ajili ya michezo yake dhidi ya Simba na Yanga.

MLIPILI: Atoweka Kikosini Simba sc

Inaelezwa beki chipukizi wa Simba Yusufu Mlipili ameondoka kikosini na viongozi wa timu hiyo hawajui alipo.

Mlipili aliyekuwa mmoja wa wachezaji wa kutegemewa kwenye kikosi cha Simba msimu uliopita, amekumbana na wakati mgumu wa kupata namba msimu huu.

Inaelezwa beki huyo aliyesajiliwa kutoka klabu ya Toto Africans hajaonekana kwenye mazoezi ya Simba kwa takribani wiki moja sasa.

“Hatujui alipo, kwa sababu hatuna taarifa rasmi juu ya kukosekana kwake,” kimesema chanzo

Usajili wa Paschal Wawa na kurejea kwa Juuko Murshidi kumemuweka kwenye wakati mgumu beki hiyo ambaye alitabiriwa kuwa na mafanikio makubwa siku za baadae

NIYONZIMA: Aitwa kamati ya Nidhamu SIMBA SC

Kiungo wa Simba, Mnyarwanda Haruna Niyonzima amewekwa kikaangoni baada ya kuhojiwa na Kamati ya Nidhamu ya klabu hiyo kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali.

Kwa muda mrefu Niyonzima amekuwa kwenye sintofahamu na mabosi wake huku tangu alipojiunga na wenzake mazoezini hajacheza.

Niyonzima amehojiwa na Kamati hiyo iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Suleiman Kova.

Kova, ambaye amepata kuwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, aliongoza kikao hicho akiwa na wajumbe wengine wanne kwenye ukumbi wa hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kuwa Niyonzima aliitwa na kamati hiyo kwa ajili ya kuzungumza masuala ya nidhamu yake huku ikielezwa kuwa pande zote zimeshindwa kufikia mwafaka.

MKWABI: aahidi SIMBA ya Kisasa

Mgombea pekee wa nafasi ya urais wa Simba, Swedy Mkwabi amesema kama akifanikiwa kushinda nafasi hiyo, basi ataanza kwa kupitia mikataba upya ya wadhamini huku akiahidi kusimamia vizuri mfumo wa mabadiliko ya uendeleshaji ya klabu hiyo kwa kufuata katiba ya mwaka 2018 iliyopitishwa na wanachama.

Kauli hiyo aliitoa jana kwenye ufunguzi wa kampeni zake zilizofanyika Southern Sun Hotel, Posta jijini Dar es Salaam huku akisindikizwa na wenyeviti wa matawi wa wilaya ya Dar.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mkwabi alisema ataipitia mikataba hiyo ya wadhamini kwa ajili kuangalia kama kuna sehemu ya kuboreshwa, basi iboreshwe, hiyo yote katika kuhakikisha klabu hiyo inakuwa na vyanzo vingi vya fedha.

“Ninafahamu klabu ina wadhamini, hivyo baada ya kuingia madarakani nitahakikisha ninaipitia upya mikataba hiyo pamoja na kukutana na wadhamini kwa ajili ya kujadili baadhi ya vitu.

“Hicho ni kitu cha kwanza nitakachoanza nacho, pia nitahakikisha kunakuwepo na ushirikiano wa karibu kati ya uongozi wa makao makuu na uongozi wa matawi, wilaya na mikoa ili kuleta ufanisi na umoja ndani ya klabu ya Simba.

“Katika kuhakikisha kwamba maslahi ya wanachama wa Simbakatika Simba Sports Club Limited yanalindwa vizuri kwa kushirikiana na muwekezaji mkuu wa klabu ya Simba.

“Pia, nitaondoa makundi ya wanachama ndani ya klabu ya Simba kwa kutengeneza umoja wenye nguvu ndani ya Simba kwa kuifuata na kuheshimu katiba ya klabu,”alisema Mkwabi mwenye Stashahada ya juu ya Biashara na Utawala Chuo ya CBE.