Azam Fc vs Yanga mchezo usiotabirika

Jumatatu ya April 29 Azam Fc na Yanga zitachuana katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Huo utakuwa mchezo wa 19 kwa timu hizo kukutana kwenye ligi katika kipindi cha miaka 10

Katika michezo 18 iliyopita, Yanga na Azam Fc zimekuwa na matokeo sawa ambapo Yanga imeshinda michezo sita, Azam Fc ikishinda sita pia huku zikitoka sare mara sita

Hizi hapa takwimu za matokeo ya michezo iliyopita;

2008/09
Azam 1-3 Yanga (Oktoba 15, 2008)
Yanga 2-3 Azam (Aprili 8, 2009)

2009/10
Azam 1-1 Yanga (Oktoba 17, 2009)
Yanga 2-1 Azam (Machi 7,2010)

2010/11
Azam 0-0 (Okt 24, 2010)
Yanga 2-1 Azam (Machi 30, 2011)

2011/12
Azam 1-0 Yanga (Sept 18, 2011)
Yanga 1-3 Azam (Machi 10, 2012)

2012/13
Azam 0-2 Yanga (Nov 4, 2012)
Yanga 1-0 Azam (Feb 23, 2013)

2013/14
Azam 3-2 Yanga (Sept 22, 2013)
Yanga 1-1 Azam (Machi 19, 2014)

2014/15
Yanga 2-2 Azam (Des 28, 2014)
Azam 2-1 Yanga (Mei 5, 2015)

2015/16
Yanga 1-1 Azam (Okt 17,2015)
Azam 2-2 Yanga (Machi 5, 2016)

2017/2018
Azam fc 1-2 Yanga sc (Junuari 27/1/2017
Yanga 1-3 Azam Fc (May 28/5/2018

Katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita, upinzani wa Yanga na Azam Fc umekuwa ukiongezeka hasa baada ya Azam Fc kuanza utamaduni wa kusajili wachezaji kutoka Yanga

Baada ya Azam Fc kuwasajili Didier Kavumbagu na Frank Domayo, mwaka juzi Yanga ilimnyakua Gadiel Michael

Mwaka jana Azam Fc iliwasajili Donald Ngoma aliyeachwa na Yanga na baadae Obrey Chirwa

Ngoma na Chirwa wanatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya Azam Fc kwa mara ya kwanza kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Yanga

Chirwa aliifunga Yanga mapema mwaka huu kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi katika mchezo ambao Azam Fc ilishinda mabao 3-0

Hata hivyo Yanga haikupeleka kikosi chake cha kwanza katika michuano hiyo ambayo Azam Fc iliibuka mabingwa

Ni mchezo ambao Yanga inahitaji kupata ushindi ili kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa huku pia ikiiombea Simba iendelee kupunguzwa kasi katika michezo yake ya viporo

Matokeo tofauti na ushindi kwa Yanga huenda yakafifisha nafasi ya kutwaa ubingwa kwa vinara hao wa ligi kuu msimu huu

Azam Fc haina cha kupoteza kwani tayari imeshajiondoa katika kinyan’ganyiro cha kuwania ubingwa ikiweka mkazo zaidi kwenye michuano ya kombe la FA (ASFC)

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema mchezo huo hautakuwa mwepesi kutokana na ubora wa kikosi cha Azam Fc hata hivyo ni matokeo ya ushindi pekee ambayo yanaweza kuwapa nafasi ya kuwa mabingwa

“Hii ni mechi ngumu kwetu, Azam Fc ni timu nzuri ambayo ina ushindani wa hali ya juu. Tunafanya maandalizi maalum ili tuweze kuwafunga,naamini tukishinda tutajiweka katika mazingira mazuri zaidi ya kuchukua ubingwa,” amesema

Yanga inaongoza ligi ikiwa na alama 74, ikiwa mbele ya Azam Fc inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya alama nane

Faini zaiandama Yanga

Klabu ya Yanga imetozwa faini ya sh. 3,000,000 (milioni tatu) kutokana na timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi dhidi ya Ndanda Fc iliyofanyika Aprili 4, 2019 katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Hilo ni kosa la nne msimu huu kwa timu ya Yanga kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi, na adhabu dhidi yake imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Taratibu za Mchezo.

Aidha, Yanga pia imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuwarushia chupa za maji waamuzi wakati wakirejea vyumbani baada ya mechi dhidi ya Ndanda Fc kumalizika

Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Klabu

Beki wake kisiki mkongwe Kelvin Yondani amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji wa Kagera Sugar FC katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 11, 2019 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 38(9) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji

Yondani tayari amekosa mchezo mmoja dhidi ya Mtibwa Sugar

Zahera aipania Azam Fc

Kikosi cha Yanga leo kimeendelea na mazoezi kwenye uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa April 29 2019 katika uwanja wa Taifa

Muda wa mchezo huo utapigwa saa kumi kamili jioni

Wachezaji wote wa Yanga wako katika hali nzuri ambapo Daktari wa timu hiyo Dk Edward Bavu amesema hakuna majeruhi

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema mchezo dhidi ya Azam Fc hautakuwa mwepesi lakini una umuhimu wa kipekee kwa Yanga kupata ushindi ili kuwa na nafasi ya kutwaa ubingwa

“Najua wazi mechi yetu na Azam FC itakuwa ngumu na ya nguvu kwetu kwa sababu sisi wote tunataka tushinde mechi hiyo ili tuzidi kujiwekea mazingira mazuri katika ligi,” amesema

“Tunajiandaa vizuri ili tushinde tuwaache mbali wapinzani wetu, hii ni mechi ambayo tunahitaji matokeo zaidi na tutapambana kwa ajili ya hilo”

Yanga kuanza mawindo ya Azam Fc Jumanne

Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kurejea mazoezini kesho Jumanne kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Azam Fc utakaopigwa Jumatano ijayo April 29 katika uwanja wa Taifa

Kocha Mkuu wa vinara hao wa ligi Mwinyi Zahera aliwapa wachezaji siku tatu za mapumziko ili washeherekee sikukuu ya Pasaka wakiwa na familia zao

Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh amesema baada ya mapumziko hayo, kesho wataanza kujifua uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini kujiandaa na mchezo huo

Yanga bado haijakata tamaa katika mbio za kuwania ubingwa licha ya watani zao Simba kuwa na idadi kubwa ya michezo ya viporo ambayo kama watashinda yote, watatetea ubingwa waliotwaa msimu uliopita

Juzi Zahera alisema hesabu zao ni kushinda michezo yote sita iliyobaki huku akiamini wapinzani wao Simba wataendelea kudondosha pointi hivyo kuwapa mwanya wa kutwaa ubingwa

Yanga iko kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imejukusanyia alama 74 baada ya kushuka dimbani mara 32.

Inafuatiwa na Azam Fc yenye alama 66 ikiwa imeshuka dimbani mara 32 pia. Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 60 ilizovuna katika michezo 24

ZAHERA AMPA ZA USO HAJI MANARA

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amemtaka Ofisa Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara kutofuatilia mambo yasiyomhusu.

Kauli ya Zahera imekuja kufuatia Manara kumsema kocha huyo kuwa amekuwa akiishutumu bodi ya ligi na TFF kuwa inafanya mpango wa kuiwezesha Simba kuchukua ubingwa wa ligi.

Ameeleza kwa kumtaka Manara ni vema akafuatilia mambo yanayomhusu na kuachana na kumzunguzia yeye kwani anaona anachokifanya ni sahihi.

Zahera amesema kamwe hatoweza kukaa kimya kwani kila anachokisema ni sahihi kwake na hataweza kufumbia macho madudu ya TFF.

Amefunguka kwa kusema kama TFF wanaona anakiuka taratibu wamfungie lakini hatoacha kuzungumza mpaka pale uongozi wa Shirikisho hilo utakapobadilika.

Kipigo cha Simba chafufua matumaini ya ubingwa Yanga

Baada ya Simba kupoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar kwa kuchapwa mabao 2-1, matokeo hayo yamefufua matumaini ya ubingwa kwa Yanga ambayo inaomba wapinzani wao hao wapoteze michezo zaidi

Aidha matokeo hayo yametoa taswira kuwa haitakuwa kazi rahisi kwa Simba kushinda michezo yote iliyobaki

Kama Yanga itashinda michezo yote sita iliyobaki itafikisha alama 92 huku wapinzani wao wakiwa na mzigo wa kupata matokeo kwenye michezo 14 ndani ya mwezi mmoja

Yanga imeendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imejikusanyia alama 74 ikifuatiwa na Azam Fc yenye alama 66

Simba ni ya tatu ikiwa na alama 60

Azam na Yanga zimeshuka dimbani mara 32 wakati Simba imeshuka dimbani mara 24

Simba inakabiliwa na ratiba ngumu ya michezo ya viporo ambapo katika kipindi cha siku 15 itashuka dimbani mara sita

Heri ya sikukuu ya Pasaka kwa Wanamsimbazi

Wakristo nchini, leo wanaungana na wenzao duniani kusherehekea Sikukuu ya Pasaka ya kukumbuka ufufuko wa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2,000 iliyopita.

Maadhimisho hayo yatakwenda sambamba na ibada kwenye makanisa mbalimbali nchini pamoja na burudani zitakazofanyika kumbi tofauti za starehe, fukwe za bahari na sehemu nyingine.

Sherehe hii ambayo kwa Wakristo huwakumbusha upendo, inatakiwa kusherehekewa katika hali ya amani na utulivu.

Tunawatakia Wanamsimbazi na Watanzania wote Pasaka Njema.

Tulishamuondoa Beno kwenye mipango yetu – Kaya

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Omary Kaya amesema mlinda lango Beno Kakolanya alishaondolewa kwenye mipango ya Yanga na suala lake liko katika hatua za kumalizwa kisheria

Kaya amesema baada taratibu zote za kishasheria kukamilishwa, Beno atakuwa huru kuendelea na maisha yake ya soka mahali pengine

“Suala la Beno lipo katika sheria zaidi, Yanga na Beno walishaachana kwa sababu angekuwa bado anahitajiwa kufanya kazi Yanga sidhani mpaka leo kama angekuwa nje ya timu,” Kaya ameiambia UFM

“Sidhani kama ni sawa kulizungumzia suala ambalo tayari limeshapita”

“Taratibu nyingine za kumalizana zipo nyuma ya pazia tutamalizana na ataendelea na maisha yake kama ambavyo sasa hivi anavyoendelea na maisha yake na Yanga inaendelea na maisha yake”

Beno aliondolewa kikosini mwishoni mwa mwaka jana baada ya kufanya mgomo uliosababisha mgogoro baina yake na kocha Mwinyi Zahera

Tutarekebisha makosa – Ninja

Bekiwa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, amewataka mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na wasiwasi, kwani kikosi chao kitarekebisha makosa na kufanya vizuri.

Ninja amesema hayo siku moja baada ya Yanga kuchapwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Ninja amewataka mashabiki wa Yanga kuendelea kuwa wavumilivu, kwani wanapambana kwa ajili ya timu hiyo.

“Naomba mashabiki wetu waendelee kuwa wavumilivu, kwani wenyewe wanaona tunavyopambana na hata wanachotufanyia waamuzi,” Ninja amenukuliwa na Bingwa

Alisema kwa sasa matokeo dhidi ya Mtibwa Sugar wameshayasahau na akili zao wamezielekeza kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Azam, ambao utachezwa Aprili 29, mwaka huu.

“Mpira ni mchezo wa makosa, ukifanya kosa moja wenzako wanakuadhibu, ila naamini benchi la ufundi limeona na tutafanyia kazi, ila kikubwa tunaendelea kuvumilia wakati tunazidi kupambana”

Orodha kamili ya wagombea wa nafasi za uongozi Yanga

Baada ya mchujo uliofanyika mapema wiki hii, wagombea waliopita katika mchujo huo wanaunganishwa na wagombea waliopitishwa kwenye mchakato wa kwanza wa kujaza nafasi zilizowazi. Hivyo orodha kamili ya wagombea wote itakuwa kama inavyoonekana hapa chini;

Mwenyekiti

1. Baraka Igagungula (ME)
2. Dr. Jonas Tiboroha (ME)
3. Elias Mwanjala (ME)
4. Dr. Mbette Mshindo Msola (ME)

Makamu Manyekiti

1. Fredrick Mwakalebela (ME)
2.Jannet Mbene (KE)
3. Titus Osoro (ME)
4. Yono Kevela (ME)

Wajumbe

1. Saady Mohamed Khimji (ME)
2. Hassan H. Yahaya (ME)
3. Arafat Hajji (ME)
4. Suma Mwaitenda (KE)
5. Hamad Islam (ME)
6. Dominick Albinus (ME)
7. Sharifu Amour Makosa (ME)
8. Eng. Bahati F. Mwaseba (ME)
9. Eng. Leonard Marango (ME)
10. Haruna H. Batenga (ME)
11. Athanas Kazinghe (ME)
12. Ramadhan Said (ME)
13. Salim Rupia (ME)
14. Dominick Francis (ME)
15. Sharifu Amir (ME)
16. Benjamin Mwakasendo (ME)
17. Christopha Kashiririka (ME)
18. Ally Msigwa (ME)
19. Frank K. Kamugisha (ME)
20. Said Kambi (ME)
21. Silvester Haule (ME).