BREAKING NEWS: MAKAMBO ATIMKA YANGA, AJIUNGA HOROYA AC

Mshambuliaji wa Yanga Heritier Makambo ametimkia Guinea kujiunga na klabu ya Horoya Fc

Taarifa za Makambo kusajiliwa na Horoya zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii mapema leo ambapo timu hiyo imemtambulisha rasmi
Makambo ndiye kinara wa mabao katika kikosi cha Yanga msimu huu akitupia kambani mabao 16

Kulingana na mtandao wa Kalonews, Makambo amesaini mkataba wa miaka mitatu

“Horoya AC imemsajili mshambuliaji kutoka DR Congo Heritier Makambo aliyekuwa akiichezea Young Africans ya Tanzania,” imesema taarifa ya mtandao huo

“Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 aliyewahi kuichezea Motema Pembe, amefunga mabao 16 kwenye ligi ya Tanzania”
“Amesaini mkataba wa miaka mitatu”

Kuondoka kwa mshambuliaji huyo ni pigo kwa Yanga ambayo iko kwenye mchakato wa kukiimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao

https://play.app.goo.gl/?link=https://play.google.com/store/apps/details?id=com.chumbani.raha&ddl=1&pcampaignid=web_ddl_1

Yanga italazimika kuingia sokoni kusaka washambuliaji wengine wakali

Hata hivyo Yanga itanufaika na mauzo ya mshambuliaji huyo kwani mkataba wake na Yanga ulikuwa bado haujamalizika
Inaelezwa Makambo ameuzwa kwa dau linalokadiriwa kufikia Milioni 230 za Kitanzania




SIMBA YAIKUNG’UTA MTIBWA SUGAR BAO 3-0 UWANJA WA UHURU YATINGA KILELENI

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba wameendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kutetea taji lao baada ya leo kuichapa Mtibwa Sugar mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru

Simba iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na shauku ya kuondoka na alama zote tatu baada ya kutopata ushindi katika michezo miwili iliyopita
Ilianza kuhesabu bao la kwanza kupitia kwa nahodha John Bocco kwenye dakika ya 32 akiunganisha krosi murua iliyochongwa na Meddie Kagere

Simba iliyotawala mchezo huo, ilikwenda mapumziko ikiwa inaongoza kwa bao 1-0

cut

Kasi waliyomaliza nayo kipindi cha kwanza, waliiendeleza kwenye kipindi cha pili na kufanikiwa kufunga mabao mengine mawili kupitia kwa Emmanuel Okwi(56′) na Clatous Chama (46′)
Mtibwa Sugar ilitumia zaidi mashambulizi ya kushitukiza na ilipoteza nafasi kadhaa kutokana na washambuliaji wake kutokuwa makini
Washambuliaji wa Simba wameendelea kuweka rekodi ya kuzifumania nyvu msimu huu, Simba ikifikisha mabao 72
Kagere, Bocco na Okwi wamefikisha mabao 50
Ushindi huo umeirejesha Simba kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 85
Simba sasa inahitaji alama nne tu kutoka mechi nne zilizobaki ili iweze kutetea ubingwa

Simba yaomba sapoti ya mashabiki mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar

Leo saa kumi jioni Simba itashuka uwanja wa Uhuru kuikabili Mtibwa Sugar katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Uongozi wa timu hiyo umewataka mashabiki wajitokeze kwa wingi kuwapa sapoti wachezaji katika mchezo huo ambao matokeo ya ushindi ni muhimu

Msemaji wa Simba Haji Manara amesema wachezaji wameahidi kupambana ili kupata matokeo lakini uwepo wa mashabiki wengi uwanjani itakuwa chachu ya wao kufanya juhudi zaidi

“Twendeni uwanjani kwa wingi kama ilivyo kawaida yetu. Tunahitaji alama nane tu tuweze kutwaa ubingwa, tujitokeze kwa wingi kwani kwa umoja wetu tutashinda”

Mchezo wa leo ni kwanza kwa Simba na Mtibwa Sugar kukutana msimu huu. Mchezo wa pili baina ya timu hizo utapigwa mkoani Morogoro, May 28

Yanga kukamilisha ukarabati uwanja wa Kaunda

Uongozi wa klabu ya Yanga umeandaa mpango wa muda mfupi ambao utawezesha ukarabati wa uwanja wa Kaunda ili uweze kutumika kwa ajili ya mazoezi

Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema baada ya msimu kumalizika wataanza ukarabati wa sehemu ya kuchezea ‘pitch’ ya uwanja wa Kaunda ili uweze kutumika msimu ujao

“Kwa sasa tutakarabati sehemu ya kuchezea, ni zoezi ambalo litachukua takribani miezi mitatu,” amesema Mwakalebela

“Lengo letu ni kuhakikisha msimu ujao tunakuwa na uwanja wetu wa mazoezi ili kupunguza gharama”

“Gharama tunazotumia kukodi viwanja ni kubwa, pesa hiyo inaweza kutusaidia katika masuala mengine yakiwemo ya usajili”

Kuhusu adha ya mafuriko Jangwani, Mwakalebela amesema kifusi kilichowekwa mwanzo kimepunguza adha hiyo na wanakusudia kuongeza kifusi kingine kabla ya kuanza mchakato wa kupanda nyasi sehemu ya kuchezea

Kadi za njano zamuumiza Fei Toto

Kiungo wa Yanga Feisal Salum ‘Fei Toto’ ni miongoni mwa wachezaji wanaoongoza kwa kupewa kadi za njano msimu huu

Fei Toto tayari amekosa michezo mitatu ya ligi inayotokana na adhabu za kadi za njano

Kiungo huyo aliyesajiliwa na Yanga akitokea JKU ya Zanzibar, hafurahii kadi hizo kwani zinamharibia jina na kumpa sifa mbaya

Fei Toto amesema anachokifanya uwanjani ni kutimiza wajibu na maelekezo anayopewa na Mwalimu.

Anaamini baadhi ya kadi anastahili lakini yapo matukio ambao anadhani hatendewi haki na waamuzi

Aidha kiungo huyo amesema amekuwa akikamiwa na wachezaji wa timu pinzani hali inayomfanya acheze kwa presha kubwa

“Baadhi ya mechi huwa nakamiwa, na kunifanya nicheze kwa presha kubwa. Siwezi kusema uwezo wangu ndio chanzo cha kukamiwa kwani naamini kila timu inaingia uwanjani ikiwa na lengo la kupata alama tatu,” amesema

Simba yapania kuweka sawa hesabu za ubingwa leo

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba leo wanashuka dimba la Uhuru kuwakabili Mtibwa Sugar katika mchezo ambao vijana wa Patrick Aussems wamepania kuchukua alama zote tatu

Baada ya kukosa ushindi katika michezo miwili iliyopita, Simba leo inahitaji ushindi ili kuweka sawa hesabu za ubingwa

Simba inahitaji alama saba kutoka michezo mitano iliyobaki kuweza kutetea ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo

Kama itashinda leo, halafu ikashinda mchezo dhidi ya Ndanda Jumapili, sare au matokeo ya ushindi mchezo dhidi ya Singida United, yatatosha kuipa Simba ubingwa wa pili mfululizo

Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu amesema wachezaji wa timu hiyo wako katika hali nzuri kuelekea mchezo huo ambao wamepania kuondoka na alama zote tatu

Yanga kuunda Kamati ya Usajili

Uongozi wa klabu ya Yanga uko katika mchakato wa kuunda Kamati ya usajili ambayo itashirikiana na Kocha Mwinyi Zahera kusimamia usajili wa timu hiyo

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Yanga jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa timu hiyo Dk Mshindo Msolla amesema tayari uteuzi umeshafanyika kwa sasa wanafanya majadiliano na wajumbe walioteuliwa kabla ya kuwaweka hadharani

“Wajumbe wa Kamati hiyo tumeshawateua lakini hatuwezi kuwatangaza kabla nao hawajaridhia,” amesema Dk Msolla

“Wiki ijayo tutakuwa na kikao na benchi la Ufundi, pengine katika kikao hicho tutaitangaza Kamati”

“Msimu huu tumedhamiria kufanya usajili makini wenye tija”

Aidha Dk Msolla amesema hata hivyo jukumu la kutafuta wachezaji litabaki kwa kocha Zahera na benchi lake la ufundi, Kamati hiyo itakuwa na jukumu la kumsaidia kukamilisha michakato ya usajili baada ya makubaliano kufikiwa

Dk Msolla amesema kuanzia msimu ujao watawatumia wachezaji waliocheza Yanga zamani kutafuta wachezaji

“Msimu ujao kazi kubwa itafanywa na wachezaji wetu wa zamani kwani tutawapa jukumu la kutembea mikoani kutafuta wachezaji wenye vipaji”